Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, August 29, 2010

Vicent Nyerere: mgombea ubunge wa CHADEMA jimbo la Musoma Mjini

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2010, nitajitahidi kuhudhuria mikutano ya wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea na kuzileta habari hapa.

Jana nilihudhuria mkutano wa uzinduzi wa Vincent Josephat Nyerere wa kuwania kiti cha ubunge, Musoma Mjini, kupitia Chama cha Demokrasia na Mandeleo (CHADEMA).

Katika hotuba yake alisema:
"Nimejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kwa sababu ndiyo chama pekee kinachoweza kumtetea mwananchi mwenye maisha ya chini, na mlalahoi. Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, na mbunge aliyemaliza muda wake, hawaambiliki."
Vincent Nyerere akihutubia mkutano jana mjini Musoma.
Mkutano huo ulifanyika kwenye kiwanja cha Mukendo, Musoma. Aliongeza:
"Nyinyi ni mashahadi wa kutosha kwamba afya ya wakazi wa Musoma Mjini imedorora. Tunayo magari na wagonjwa mengi na mnayaona. Niambie ni nani ambaye ni mgonjwa na akabebwa na gari lile akapelekwa hospitali? ...Gari ya wagonjwa inabeba diwani wa CCM anakwenda kufuata ndizi Tarime."

Vincent Nyerere akihutubia mkutano Musoma mjini.
Aliendelea:
"Shule za kata nyinyi mmezichangia. Lakini huwezi kusema shule ya kata ni maendeleo. Shule inakuwaje maendeleo kama haitowi watoto wanaopasi; kama hakuna watoto waliopasi, siyo maendeleo. Mimi sijaridhika. Chama changu pia hakijaridhika.

Elimu inayotolewa Tanzania haimsaidiii mtoto wa Kitanzania, hasa shule ya msingi....Sisi CHADEMA tunaamini kwamba lazima mtoto huyu asome sekondari. Shule ya msingi iishie kidato cha nne. Ndiyo maana Tarime watoto walikuwa wanasoma mpaka kidato cha nne bila kulipa.* Na Musoma Mjini, inawezekana."

Na kusema:

"Mji huu umezungukwa na ziwa kwa asilimia karibu ya sabini, na kazi kubwa tunazozifanya katika ziwa hili ni uvuvi. Tumemchagua mbunge, anakwenda bungeni hajuwi thamani ya wavuvi na ni wapiga kura wake. Anaacha wabunge wa Morogoro wanachangia hoja za Ziwa Viktoria: wanasema kokoro ni marufuku.

Bila kokoro haiwezekani. Alitakiwa aweke hoja, ajenge hoja na aitetee kwamba kokoro liwepo, tuwe na maendeleo maalum ya kuvua, tuwafundishe vijana wetu wanaovua, wapi ni mazalia ya samaki, na wapi siyo mazalia ya samaki, na uvue kwa kutumia kokoro."
Vincent Nyerere akihutubia mkutano Musoma mjini.
Mengine haya:

"Bungeni nitajenga na kusimamia hoja. Mimi siyo muoga. Ukiona natetemeka, ni baridi. Na mimi nitafanya kazi zangu za ubunge bila chuki, bila uwoga, bila ubaguzi."
.............

"Lazima tutengeneze miradi mipya ya maendeleo, kwa kutumia mfuko wa Jimbo na marafiki tuliyonao, wawasaidie kina mama kwa sababu wakina mama ndiyo jamii inayoteseka kuliko sisi wanaume. Mama wa Musoma mjini ndiyo anakwenda kulala na mtoto hospitali, baba yuko nyumbani. Anaomba mama mwingine amshikie mtoto arudi kumpikia baba."
*Halmashauri ya Tarime Mjini inayomaliza muda wake likuwa inaongozwa na CHADEMA.

Thursday, August 26, 2010

Michuzi kupanda Mlima Kilimanjaro

Mwamablogu mashuhuri. Muhiddin Issa Michuzi, ameniarifu kuwa ataungana nami mwezi Novemba 2010 kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha pesa za hisani

Michuzi, akiwa na Simba
Tangu mwaka 2008 nimekuwa napanda Mlima Kilimanjaro kwenye tukio linalojulikana kama The Mwalimu Nyerere Charity Climb kwa madhumuni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya hisani. Mwaka 2008 nilichangisha zaidi ya dola za Marekani 20,000 kuchangia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Edward Wanzagi iliyopo Buturu, Mkoa wa Mara.

Mwaka 2009 nilichangisha pesa kwa ajili ya asasi ya Mjini Musoma, Community Alive, inayosaidia watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kwa UKIMWI. Ahadi na michango vilifikia kiwango kidogo, kulinganisha na mwaka 2009. Ingawa ahadi zilifikia zaidi ya Sh.2 milioni ni sehemu ndogo sana ya ahadi hizo zilitolewa.

Pesa zinazotolewa zinatumwa moja kwa moja kwa walengwa kwenye akaunti zao, na hamna sehemu yoyote inayopunguzwa.

Monday, August 23, 2010

Ujumbe toka kwa mwanablogu Sarah

Ujumbe huu unatoka kwa mwanablogu anaitwa Sarah:
Natatumaini kuwa mnaendelea vyema na shughuli za kila siku za kujenga taifa..Jambo la msingi tu kuhusu email hii hi kuwaomba wana blog wenzangu kuweza kunisaidia kuwataarifu wasomaji kupitia blog zenu kuhusu mabadiliko ya blog yangu kutoka www.angaliabongo.co.tz na sasa kuwa www.angalia-bongo.com
Natumaini mtaweza kunisaidia kwa hilo.
NATANGULIZA SHUKRANI ZA DHATI.
SARAH.

Wednesday, August 4, 2010

Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA ametembelea Butiama leo

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafirishaji, SUMATRA, Israel Sekirasa, leo ametembelea Butiama, akiongozana na Tumaini Silaa, Meneja wa Huduma za Sheria wa SUMATRA.

Israel Sekirasa, kushoto, akiweka sahihi kitabu cha wageni kwenye Maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Akiwa Butiama alitembelea vivution mbalimbali vya Butiama, ikiwa ni pamoja na maktaba ya Mwalimu Nyerere, Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, pamoja na kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere.
Tumaini Silaa (kushoto), na Israel Sekirasa, wakiangalia sehemu ya vitabu zaidi ya 8,000 vilivyo ndani ya maktaba ya Rais mstaafu Mwalimu Nyerere, ambayo inajulikana rasmi kama Maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere