Mojawapo ya habari ambazo zimeandikwa kwa kina sana kwenye kipindi cha hivi karibuni ni nia ya Serikali ya kujenga Barabara ya lami kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara kupitia mbuga ya Serengeti.
Ni habari ambayo pia imeleta mvutano mkubwa baina ya pande mbili. Upande moja ina wale wanaopinga kuwepo kwa barabara hiyo, wakidai kuwa ujenzi wake utaathiri majaliwa ya wanyamapori waliyopo Serengeti. Upande wa pili ni wale ambao wanadai kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wakazi wa mkoa wa Mara na mkoa wa Arusha na kuwa umefika wakati kwao pia kufaidikia ni ujenzi wa barabara kama maeneo mewngine ya Tanzania.
Wanamazingira wa ndani ya nchi na nje ya nchi wameungana kupinga kwa nguvu kabisa ujenzi wa barabara hiyo wakidai kuwa Serikali ya Tanzania imeweka sahihi mikataba ya kimataifa ya kutunza na kulinda mazingira na kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakiuka mikataba hiyo. Aidha hifadhi ya Serengeti imeorodheshwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kama eneo la urithi wa Dunia na ujenzi wa barabara hiyo unaweza kusababisha kufutwa hadhi hiyo na kuleta athari mbalimbali kwa nchi, ikiwa ni pamoja na kupunguka kwa watalii watakaotembelea Serengeti na hivyo kuathiri biashara ya utalii na mapato yanayotokana na utalii. Na vitisho siyo vidogo, ikiwa ni pamoja na tishio la Tanzania kunyimwa misaada mbalimbali kutoka nje.
Hoja ya kwamba kwa kujenga barabara hiyo Tanzania itakuwa inakiuka mikataba ya kimataifa ambayo imeweka sahihi ni hoja yenye nguvu. Lakini tunayo mifano mingi ya nchi ambazo zinafanya maamuzi yanayokiuka sheria za kimataifa kwa misingi ya kulinda maslahi ya nchi hizo. Sisi tunaathirika na tatizo la kuwa omba omba. Maslahi ya nchi yetu tunapangiwa na nchi nyingine kwa hiyo hatuna ubavu wa kujenga hoja kuwa jambo fulani linaathiri maslahi yetu, na hivyo basi kudai mapitio ya vipengele ambavyo vitazingatia mahitaji yetu kwenye mikataba ya Kimataifa ya aina hiyo.
Hoja kuwa barabara ya lami inaweza kufuta misafara ya msimu ya wanyama kuhama kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine nina wasiwasi nayo. Kwamba nyumbu na pundamilia wanaovuka mbuga zenye wanyama hatari kama simba, na chui, na wanaovuka mto Grumeti uliyojaa mamba watashindwa kuvuka barabara ya lami ni mojawapo ya yale masuala ambayo wengine tunayakubali kwa shingo upande kwa sababu tu wanayoyasema ni watu ambao wanasemekana ni wataalamu wa wanyamapori na mazingira. Lakini ni hoja ya kitoto, kwa maoni yangu. Inawezekana ipo athari ya kiasi fulani itakayosababishwa na barabara ya lami, lakini siamini kuwa athari hiyo itafuta kabisa uwepo wa wanyama hao kwenye sura ya dunia kama inavyodaiwa na hawa wataalamu.
Umaskini ni tatizo, lakini wenye hoja inayounga mkono ujenzi wa barabara ya lami kupita ndani ya mbuga ya Serengeti tungekuwa na uwezo wa kifedha ingewezekana kabisa kupata wataalamu wetu wakatufanyia utafiti utakaoonyesha kuwa athari ya barabara ya lami kwa nyumbu na pundamlia siyo ya kutisha. Huu ndiyo utaratibu uliyopo nchi zilizoendelea pande zinazokinzana zinapotaka kuvunja hoja ya upande mwingine. Umesikia hivi karibuni kuna tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya simu za kiganja yanaweza kuleta ugonjwa wa saratani, wakati miaka yote tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya simu hizo hayana athari zozote?
Barabara zilizopo kwenye hifadhi za wanyama katika mataifa mengi yaliyoendelea kunakotoka shinikizo kubwa dhidi ya ujenzi wa hii barabara zimewekwa lami. Tungekuwa tuna uwezo wa kuweka msimamo tungeomba wale wote wanaopinga barabara za lami kwenye mbuga za wanyama kwanza wafumue lami zilizopo kwenye barabara zinazopita kwenye mbuga zao halafu ndiyo waje tukae meza moja kupanga namna ya kuepusha kuweka lami ndani ya mbuga ya Serengeti.
Sishabikii kumaliza wanyama, lakini naamini mahitaji ya binadamu yanawekwa nyuma ya mahitaji ya wanyama. Tatizo ni kuwa wanaharakati wa mazingira hawaambiliki, na hawana muafaka. Tunaamrishwa kusikiliza wanaosema wao, na hawasikilizi hoja nyingine zozote. Ni baadhi ya hao ambao katika jitihada za kuzuwia kuuwawa kwa baadhi ya wanyama kwa ajili ya kutengeneza makoti ya baridi kwa ajili ya binadamu, wako tayari kuua binadamu hao hao wanaovaa hayo makoti.
Hakuna tusi kubwa kwa Watanzania kama kusema kuwa mnyama ni muhimu kuliko mwanadamu. Ni kweli kwa baadhi ya wenzetu, wanyama ni muhimu sana hata kuliko binadamu. Na tumeshuhudia wanyama kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa kuwatibu maradhi wakati binadamu wenzao wanalala nje bila kufahamu wapi watakula, wacha kupata huduma ya matibabu.
Hoja yangu ya leo ni kuwa umasikini si sifa nzuri, na ina athari kubwa kwa nchi ambayo inajaribu kuwahudumia raia wake lakini inapata shinikizo kutoka kwa wahisani ambao kauli yao ina nguvu kuliko ile ya raia Watanzania.