Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Showing posts with label Wageni wa Butiama. Show all posts
Showing posts with label Wageni wa Butiama. Show all posts

Saturday, August 5, 2017

Baraka Elias, Mtanzania mrefu kuliko Watanzania wote

Nimewahi kuonana na Baraka Elias, Mtanzania mrefu kuliko Watanzania wote, alipotembelea Butiama mwaka 2012. Ana urefu wa mita 2.20 na umri wa miaka 27.
Kwenye picha juu ni yeye pamoja na Notburga Maskini anayeongea naye, kushoto. Notburga tumewahi kuongozana naye kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro.

Taarifa nyingine za Baraka Elias hizi hapa (kwa Kiingereza):

Taarifa nyingine za Notburga Maskini hizi hapa (kwa Kiingereza):

Friday, July 14, 2017

Simulizi za Jaffar Idi Amin

Hii simulizi nilipewa na Jaffar Idi Amin, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Uganda kati ya mwaka 1971 hadi 1979, Idi Amin Dada.

Anasema kuna siku alikuwa kwenye matembezi kwenye jiji la Kampala akakuta gari aina ya Volkswagen imeegeshwa na akasimama kwa muda mrefu akiiangalia kwa sababu aliitambua kuwa ilikuwa gari ya zamani ya baba yake.

Akiwa anaiangalia akatokea mtu na kumsalimia na kumuuliza sababu za kukaa muda pale akiangalia ile gari. Mazungumzo yakawa hivi:

"Mbona unaishangaa sana hiyo gari?"
"Ilikuwa gari ya baba yangu."
"Baba yako nani?"
"Idi Amin."

Anasema alivyotamka jina la baba yake yule aliyekuwa anamhoji akashangaa sana na kusema: "Baba yako ndiyo alimuondoa baba yangu nchini!"

Aliyekuwa anaongea naye alikuwa mmoja wa watoto wa Milton Obote, Eddy Engena-Maitum. Serikali ya Rais Obote ilipinduliwa na Idi Amin, wakati huo akiwa kamanda wa jeshi la Uganda, tarehe 25 Januari 1971 wakati Obote akiwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Idi Amin alishika madaraka mpaka mwaka 1979 baada ya Rais Nyerere kutangaza vita dhidi ya Uganda kufuatia uvamizi wa eneo la Kagera na majeshi ya Idi Amin. Baada ya kukomboa eneo lililovamiwa vita iliendelea ndani ya ardhi ya Uganda na kuhitimishwa kwa kuangushwa kwa serikali ya Amin.

Jaffar akamwambia Eddy: "Mimi nitakutambulisha kwa mtu ambaye baba yake alimuondoa baba yangu hapa Uganda." Alimaanisha mimi.

Mwalimu Nyerere akiwa na mwenyeji wake, Rais Milton Obote, wakati wa moja ya ziara zake nchini Uganda. Wa pili kutoka kulia ni Idi Amin, na kulia ni Philemon Mgaya, aliyekuwa mpambe wa Rais Nyerere.
Kabla ya siku hiyo Jaffar alipokutana na Eddy jijini Kampala, mimi na Jaffar tulikwa tumeonana kijijini Butiama katika tukio lililoandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuadhimisha miaka 30 ya vita vya Kagera, vita vilivomuondoa Idi Amin nchini Uganda.

***********************************
Bofya hapo chini kusoma maelezo yangu (kwa lugha ya Kiingereza) juu ya ziara ya Butiama ya Jaffar:

***********************************

Idi Amin na familia yake walikimbilia nchini Libya, na baadaye kuhamia Saudia Arabia. Milton Obote na familia yake walihamia Tanzania na wakawa majirani zetu Msasani kwa muda mrefu.

Saturday, July 12, 2014

Wageni wa Butiama: Urmila Jhaveri

Ni Watanzania wachache wa kizazi kipya wanatambua mchango wa baadhi ya Watanzania wenye asili ya Kiasia kwenye harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Mmoja wa wanaharakati hawa ni Urmila Jhaveri ambaye hivi karibuni alitembelea Butiama.
Mama Urmila Jhaveri akiwa Butiama kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere. 
Mama Jhaveri, mwenye umri wa miaka 83 na ambaye alizaliwa kwenye kisiwa cha Pemba, ni mjane wa Kantilal Jhaveri aliyekuwa miongoni mwa wanasheria watatu wa upande wa utetezi kwenye kesi ya kashfa ya jinai ya mwaka 1958 iliyomkabili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa harakati za kudai uhuru iliyofunguliwa dhidi yake na serikali ya kikoloni ya Uingereza. Kantilal Jhaveri alifariki nchini India Januari 2014.

Wakati wa kudai uhuru wakati mume wake akiwa mmoja wa viongozi wa chama cha Waasia, Indian Association, kilichoshirikiana na kuunga mkono sera za Tanganyika African National Union (TANU), Urmila alishiriki kwenye harakati hizo akiwa mwanachama wa kitengo cha wanawake cha TANU ambacho kilijulikana kama TANU Women's Section.

Hivi karibuni amechapisha kitabu juu ya maisha yake kiitwacho Dancing with Destiny ambacho atakizindua tarehe 19 Julai  2014 jijini Dar es Salaam.

Itakuwa fursa nzuri kwa wote kukumbuka mchango muhimu wa makundi mbali mbali ya Watanzania kwenye harakati za kudai uhuru.

Sunday, October 27, 2013

Wageni toka Kagera wamtembelea Mama Maria Nyerere

Viongozi wa kikundi cha wajane na yatima kutoka mkoa wa Kagera walimtembelea Mama Maria Nyerere, kijijini Butiama hivi karibuni.
Grace Mahambuka, mwenyekiti wa kikundi cha Wajane na Yatima Kagera akitoa zawadi ya "akamwani" (kahawa ya kutafuna) kwa Mama Maria Nyerere (kushoto) Mwitongo, Butiama.
Msafara uliongozwa na mwenyekiti wao, Mama Grace Mahambuka, ambaye aliongozana na Mama Agnes Paulo Mukuta ambaye ni mdau wa maendeleo anayeunga mkono kikundi hicho. Mwingine katika msafara huo alikuwa Sittiwarth Mugasha ambaye ni yatima na msanii muimbaji wa kikundi cha Umoja wa Wanawake Wajane na Yatima Band.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/kumbukumbu-ya-siku-ya-kufariki-mwalimu.html

Thursday, April 25, 2013

Wageni wa Butiama: Selma James

Miaka kadhaa iliyopita, Selma James, mkazi wa London Uingereza, alitembelea Tanzania. Yeye na wenzake walipofika Butiama niliwauliza sababu iliyowafanya waamue kutembelea Butiama. Walisema walisoma maandishi mablimbali ya viongozi wa dunia lakini hawakuwahi kusikia kiongozi hata mmoja akitamka umuhimu wa wanawake katika maendeleo ya nchi, kwa hiyo walikuwa na shauku kubwa ya kutembelea sehemu alikotoka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwenye Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere alisema haya kuhusu wanawake:
Ingefaa kuwauliza wakulima wetu, hasa wanaume, ni saa ngapi za juma na majuma mangapi kwa mwaka wanafanya kazi. Wengi hawafanyi kazi hata kwa nusu ya saa ambazo mpokea mshahara anafanya. Ukweli ni kuwa kwenye vijiji wanawake wanafanya kazi ngumu sana. Nyakati nyingine wanafanya kazi kwa saa 12 au 14 kwa siku. Wanafanya kazi hata siku za Jumapili na za sikukuu. Wanawake wanaoishi vijijini wanafanya kazi ngumu kuliko mtu mwingine yeyote Tanzania.  Lakini wanaume wanaoishi vijijini (na baadhi ya wanawake mijini) wako likizo kwa nusu ya maisha yao. Nguvu ya mamilioni ya wanaume kwenye vijiji na maelfu ya wanawake mijini ambazo kwa sasa zinapotezwa kwenye udaku, dansi na kunywa, ni hazina kubwa ya nchi ambayo inaweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu zaidi ya ambavyo tunaweza kupata kutoka mataifa tajiri.
Haya ndiyo maneno yaliyomvutia Selma na wenzake kutembelea Butiama.

Selma James ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake, ni mwandishi mwenza wa kitabu The Power of Women and the Subversion of the Community, ni mmoja wa waasisi wa International Wages for Housework Campaign, na ni mratibu wa Global Women's Strike.

Selma ni mke wa mwanaharakati mashuhuri kutoka Trinidad, C.L.R. James, ambaye aliandika vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na The Black Jacobins.

Baada ya ziara yao ya Butiama, mwaka 2007, nilipata mualiko kutoka kwao kuhudhuria hafla jijini London ya uzinduzi wa Azimio la Arusha, tukio lililohusisha pia kuchapishwa kijitabu kidogo kuhusu Azimio la Arusha kikiwa na makala yangu na ya Selma James, pamoja na Azimio la Arusha lenyewe.
Selma James, kushoto, na mimi jijini London, Uingereza, mwaka 2007.
Baada ya kustaafu urais Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa inahitaji wendawazimu kidogo kulizungumzia Azimio la Arusha kwa wale wanaoamini kuwa bado lina manufaa. Selma na kundi lake waliamini kuwa Azimio la Arusha bado lina umuhimu mkubwa na linapaswa kufahamika kwa walimwengu.

Na kwa machache niliyoyasikia kutoka kwenye Tamasha la Tano la Kigoda cha Taalum cha Mwalimu Nyerere mapema mwezi huu, yaelekea kuwa kuna wengi ambao wanaamini kuwa Azimio linayo misingi muhimu ambayo yapaswa kuzingatiwa leo hii.

Saturday, March 9, 2013

Mwenyekiti wa ABETO atembelea Butiama

Moses Musana, mwenyekiti wa Always Be Tolerant Organisation (ABETO), azaki ya nchini Uganda, amefanya ziara kijijini Butiama hivi karibuni.

ABETO iliundwa mwaka 1966 ikiwa na madhumuni ya kuhimiza jamii katika bara la Afrika kutumia njia za amani kutatua migogoro, kuishi kwa amani, kudumisha uvumilivu, demokrasia, na utawala bora.
Mwenyekiti wa ABETO, Moses Musana (kushoto), akisalimiana na Mama Maria Nyerere wakati wa ziara aliyofanya kijijini Butiama hivi karibuni
Katika hafla iliyofanyika jijini Kampala tarehe 11 Agosti 2012, ABETO ilitoa tuzo ya amani kwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo ilipokelewa na Mama Maria Nyerere.

Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2012/12/mkutano-wangu-na-jaffar-idi-amin.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/09/wageni-toka-jkt-wamtembelea-mama-maria.html

Sunday, February 17, 2013

Wageni wa Butiama: mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC

Hizi ni habari za zamani kidogo ambazo nilizitoa kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza. Nazirudia hapa kwa manufaa ya wale ambao hawakuzisoma.
******************************************
Kabla ya kufika kwa Jaffar Amin kijijini Butiama mwezi Aprili [2009] ziara yake, ambayo iliandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya shirika la utangazaji la BBC, ilitanguliwa na kufika Butiama kwa baadhi ya miamba ya utangazaji ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikiwa ni pamoja na Solomon Mugera, mkuu wa Idhaa hiyo, na Vicky Ntetema, kiongozi wa ofisi ya BBC iliyopo Tanzania.
Wengine toka BBC waliyofika Butiama walikuwa ni muongozaji vipindi Charles Hilary ambaye kwa desturi hutangaza akiwa London, Caroline Karobia anayefanya kazi kutokea Nairobi, na jina lenye kufahamika na wengi wa wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Eric David Nampesya, mtangazaji wa BBC wa eneo la Maziwa Makuu, ambaye anaonekana hapo juu, kulia, pamoja na Solomon Mugera. 

Nikiwa mmoja wa wasikilizaji wa mara kwa mara wa BBC nilijisikia mwenye furaha kuwa miongoni mwa watu mashuhuri kama hawa toka Idhaa ya Kiswahili ya BBC.

Tuesday, January 29, 2013

Wageni wa Butiama: Jaji Augustino Ramadhani

Kati ya wageni ambao wametembelea Butiama ni pamoja na aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani. Alitembelea Butiama wakati akiwa Jaji Mkuu.
Jaji Augustino Ramadhani akipata maelezo toka kwa muongozaji wageni wa Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere ya Butiama wakati wa ziara yake ya Butiama.
Mapema mwaka 2012 Jaji Ramadhani aliteuliwa kuongoza jopo la majaji waliochunguza tukio la Naibu Jaji Mkuu wa Kenya, Nancy Baraza, aliyetuhumiwa kumtishia kwa silaha mlinzi mmoja wa duka moja la jijini Nairobi.

Wednesday, January 9, 2013

Wageni wa Butiama: Mhe. Benjamin William Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ametembelea Butiama mara nyingi, kabla na baada ya kustaafu kwake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Kwenye picha hii ilikuwa mara yake ya mwisho kutembelea Butiama alipohudhuria mazishi ya Mzee Josephat Kiboko Nyerere, mdogo wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mzee Kiboko ni baba mzazi wa mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA).

Tuesday, December 25, 2012

Mkutano wangu na Jaffar Idi Amin

Taarifa ifuatayo ni ya siku nyingi kidogo, na awali niliitoa kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza From Butiama and Beyond tarehe 15 Mei 2009. Nairudia hapa katika mfululizo wa taarifa ambazo niliwahi kuzitoa kwenye From Butiama and Beyond na ambazo naamini wasomanji wangependa kuzirudia kusoma na vilevile kutoa fursa kwa wale ambao bado hawajazisoma kuweza kutafakari niliyoyaandika wakati huo.
***************************************
Mapema mwezi Aprili mimi pamoja na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tulikuwa wenyeji kijijini Butiama wa Jaffar Amin, mmojawapo wa watoto wa kiume wa zaidi ya watoto 50 wa kiongozi wa zamani wa Uganda Idi Amin Dada.

Nakiri kuwa kabla ya ujio wake nilijikuta kwenye mtanziko mkubwa ambao ulinifanya nisite kwa muda kuendelea kuandikia kwenye blogu yangu. Sikuwa na hakika wasomaji wangu wangechukuliaje mkutano wangu na Jaffar. Unapotamka tu 'Idi Amin' basi siku zote utaibua hisia kali, na mimi niligundua hizo hisia zilikinzana na sababu nilizoona zinaafikiana na uamuzi wangu wa kukubali wazo la BBC la kuonana na Jaffar.
Karibu Butiama: Jaffar Amin (kushoto), pamoja na mimi tukiwa Butiama ndani ya nyumba ambayo Mwalimu Nyerere alijengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kumalizika kwa vita kati ya Uganda na Tanzania.
 Nilieleza sababu zangu kwenye makala niliyoandika kwenye safu yangu iitwayo Letter from Butiama. Kwa kifupi niliwjenga hoja kuwa matukio ya kale tuyaache yabakie ya kale na umuhimu wa matukio hayo unajitokeza pale tu ambapo tunahitaji kijufunza jambo kutokana na matukio yaliyopita ili tusirudie makosa ya zamani. Matukio yaliyopita yasitumike kama rungu la kuwapiga wale wa sasa ambao hawahusiki kabisa na matukio ya zamani.

Mkutano wetu na Jaffar ulijikita kwenye wazo la BBC la kuadhimisha, kwa kupitia vipindi kadhaa vya redio vilivyorushwa mwezi Aprili, kumbukumbu ya miaka 30 ya vita vya Kagera, vita kati ya Uganda na Tanzania vya 1979 - 1980. Solomon Mugera, mkuu wa Idara ya Kiswahili ya BBC, alieleza kuwa awali wazo lilikuwa mkutano wetu ufanyike Nairobi. Alibainisha ni Jaffar aliyependekeza kuwa mkutano uhamishiwe Butiama, badala ya Nairobi.

Kwa hiyo katikati ya mwezi Machi nlijiandaa kuonana na Jaffar jijini Nairobi lakini nikafahamu mwishoni kabisa kuwa mkutano ulihamishiwa Butiama pasipo kufahamishwa mapema hayo mabadiliko. Ninahisi kuwa BBC waliendelea na mipango ya kukutana Butiama bila kunifahamisha kwa kuhofu kuwa ningakataa wazo lao.

Nilipata shida kubwa sana kuorodhesha waalikwa. Ilikuwa rahisi kuamua nani kati ya marafiki zangu kuwaalika. Baadhi yao walinirahisishia kazi kwa kuniomba niwaalike. Orodha ngumu ilikuwa ile ya viongozi wa serikali wa mkoa. Sikuwa na hakika iwapo wangehudhuria ingawa hutembelea Butiama mara kwa mara. Niliwatumia mialiko na baadhi yao walihudhuria mkutano ule pamoja na Jaffar.

Mwisho wa yote inaelekea kuwa wale waliofuatilia matangazo ya maadhimisho yaliyorushwa na BBC pamoja na mkutano na Jaffar walibaki na maoni chanya tu kuhusu mkutano wangu na Jaffar. Mtoa maoni mmoja alipendekeza kuwa mtu aliyeibua wazo la kuwakutanisha watoto wa Idi Amin na Julius Nyerere alipaswa kupendekezwa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.
Solomon Mugera wa BBC akihutubia waalikwa.
Ni matumaini yangu kuwa siku Solomon Mugera atakapoinuka akiwa amevalia vazi rasmi kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mjini Oslo (pamoja na kupokea hundi ya dola milioni moja) basi atakumbuka kuniorodhesha mimi pia kwenye orodha yake ya waalikwa.w

Thursday, December 20, 2012

Naibu Waziri atembelea Butiama, achangia utalii wa utamaduni

Naibu Waziri wa Viwanda na Bisahara, Mhe. Gregory Teu, ametembelea Butiama hivi karibuni na kutoa Shs.160,000/- kuchangia shughuli za utalii wa utamaduni zinazoratibiwa na Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE).
Kutoka kushoto kwenda kulia: Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Gregory Teu, msaidizi wake ambaye jina lake haliweza kupatikana mara moja, na mimi, wakati nilipokuwa natoa maelezo ndani ya Maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo kwenye nyumba ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), eneo la Mwitongo, Butiama.
Katika ziara yake fupi aliyofanya akiwa safarini kutoka Tarime kuelekea Mwanza, Mhe. Teu alizuru eneo la Mwitongo ambalo lenye makazi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kaburi la Mwalimu Nyerere, maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, na vivutio vingine vilivyopo Mwitongo.

Saturday, November 24, 2012

Jimmy ChangChuu, msanii toka Bagamoyo atembelea Butiama

Jimmy ChangChuu, ni msanii anayeishi na kufanya kazi Bagamoyo. Baadhi ya kazi anazofanya ni pamoja na kuchonga vinyago, kufinyanga, kuandaa michoro ya grafiti (michoro ya ukutani) na ni mwanamitindo.

Aidha hushiriki kwenye matangazo ya televisheni na anafahamisha kuwa ameshiriki kwenye kipindi televisheni cha cha Dume Challenge. Hivi karibuni alitembelea Butiama na yafuatayo ni maoni yake kuhusu Butiama.
***************************************************

"Naishi hizi sehemu mbili, Dar es Salaam na Bagamoyo, kwa sababu Bagamoyo ni sehemu yangu ambayo napata msukumo, ni sehemu iliyotulia. Mizunguko ya Dar es Salaam kidogo inakuwa inanishinda lakini ninapohitajika Dar es Salaam nakuwepo na familia.

Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Butiama. Mara ya kwanza nilipokuja tu ile mandhari ilinifanya nijisikie kama niko na amani, nilipata amani kwenye moyo. Mazingira yametulia, yaani hakuna kitu ambacho kinaweza kikajiingiza wakati unafikiria kufanya kitu fulani au wakati uanataka kufanya kitu. Kwa hiyo ni sehemu ambayo imetulia ambayo inaweza kukupa msukumo.

Ni ngumu sana kupata msukumo kwenye sehemu ambapo kuna vitu vinapita ambavyo vinakuvuruga lakini hapa unaona hali asili ya mazingira, unaona ndege, yaani vitu ambavyo vinakufanya unaona kuwa kuna Muumba ambaye ametengeneza hivi vitu. Ni vitu ambavyo vinavutia kweli.

Kitu ambacho kinaweza kufanya niwaambie watu waje Butiama ni mazingira na hali ya utulivu halafu nikiangalia chimbuko la kabila la Wazanaki kuna vitu ambavyo nilikuwa nikiviangalia ambavyo vina nguvu kubwa ambavyo ukiviangalia kwa juu juu huwezi kuviona, lakini kuna vitu ambavyo vipo ambavyo vimemfanya Mwalimu Nyerere akawa ana nguvu kwenye maamuzi yake, vitu ambavyo vinaendana na tamaduni yetu ya Kitanzania na ambavyo Mwalimu aliviweka kwenye siasa yake na kwenye mila na hakutoka nje ya mila yake kusikiliza mila za kigeni. Alisimama yeye pale aliposimama kutoka kwenye chimbuko la tamaduni yake.

Kwa hiyo unakuta sasa hata katika utawala wake hakutoka nje sana kwa sababu hata nikiangalia nilivyokwenda makumbusho [Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere] kule kuna vitu ambavyo nimesoma na Nyerere mwenyewe alikuwa anakwambia elimu ya wakoloni ilikuwa inawaandaa wao kuwatumikia wakoloni siyo kuwaandaa kuweza kujiendeleza wao wenyewe.

Kitu kizuri kama watu wanataka kuwa kwenye siasa na kuwa viongozi wazuri wanapaswa kujifunza kutoka kwa Nyerere na aliyoyafanya. Tangu akiwa shuleni alianza kuwa kiongozi na alichaguliwa na watu. Watu waliona Mwalimu alikuwa na kitu fulani wakamchagua. Siyo kwamba yeye alipendekeza 'mimi nataka kuwa kwenye nafasi hii.' Watu walimuona kuwa ana kitu ambacho anaweza kuchangia kwa wengine na pia alikuwa na uwezo wa kushawishi wengine."

Sunday, October 28, 2012

Kwaya ya Mt. Cecilia ya mjini Singida yatembelea Butiama

Leo jioni wanakwaya wa Kwaya ya Mt. Cecilia ya Kanisa Katoliki mjini Singida wametembelea Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


Wanakwaya hao ambao wako kwenye ziara ya Mkoa wa Mara walipita Butiama wakitokea Musoma na wakiwa njiani kwenda Isenye.

Monday, September 10, 2012

Wageni wa Butiama

Bi Victoria Gilago Bache kutoka Makumbusho ya Taifa alitembelea Butiama hivi karibuni akifanya utafiti juu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Bi Victoria ni msimamizi wa nyumba aliyoishi Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni, Dar es salaa, Mtaa wa Ifunda.
Bi Victoria akiwa ndani ya maktaba yenye mkusanyiko wa vitabu zaidi ya 8,000 vya Mwalimu Nyerere kwenye nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Mwitongo, Butiama.
Utafiti wake ulijikita juu ya maisha ya Mwalimu na familia yake wakati wanaishi kwenye nyumba hiyo ya Magomeni kabla ya uhuru, mwaka 1961.

Sunday, August 26, 2012

Wageni wa Butiama: Agustino Lyatonga Mrema

Butiama inatembelewa na wageni wengi, baadhi yao mashuhuri, lakini wengi ambao siyo mashuhuri. Wengi wa wageni mashuhuri waliowahi kutembelea Butiama walifika hapo kwa sababu ya kumtembelea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mmojawapo wa hao wageni ni Mhe. Agustino Mrema ambaye amewahi kufika Butiama mara kadhaa. Katika picha hii anaonekana akisalimiana na Mwalimu Nyerere mwaka 1997 wakati wa msiba wa Bibi Mugaya wa Nyang'ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere.

Sunday, April 1, 2012

Wageni wa Butiama

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Rwamkoma, kijiji kilichopo jirani na Butiama, walitembela Butiama hivi karibuni na kuzuru kaburi la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililopo kwenye makazi yake eneo la Mwitongo.
Picha inaonyesha wanafunzi hao wakiwa mbele ya hilo kaburi.

Wednesday, September 14, 2011

Wageni wa Butiama: Kelvin Bernard


Muda si mrefu uliyopita, Kelvin Bernard, wa pili toka kulia kwenye picha hii hapa chini,
pamoja na wanafunzi wenzake Benedicto David, Raphael Nenebwa, and Kelvin Ryoba toka Mwanza walitembelea Butiama kwa ajili ya kukamilisha somo lao kuhusu Mwalimu Nyerere.

Walifanya utafiti wao kwenye Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, kwenye maktaba ya Mwalimu Nyerere, na kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Mwitongo, Butiama.

Friday, July 15, 2011

Wageni wa Butiama: Dk. Thomas Molony


Mtafiti mwandamizi wa Kituo cha Masomo ya Afrika kilichopo Chuo Kikuu cha Edinburgh, Dk. Thomas Molony, yuko kijijini Butiama mwezi huu wa Julai akiandika kitabu juu ya muasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922 – 1999).
Dk. Thomas Molony
Kitabu hicho kitahusu sehemu ya maisha ya Mwalimu kati ya mwaka 1922 alipozaliwa hadi mwaka 1952, baada tu ya kuhitimu masomo yake kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh na kabla hajajitupa kwenye harakati za kudai uhuru toka kwa Waingereza. 

Kwa kujiandaa na uandishi wa kitabu hiki, Dk. Molony amefanya utafiti nchini Uingereza na Tanzania na ni mara yake ya pili kutembelea Butiama. Anatarajia kitabu chake kitachapishwa kabla ya mwisho wa mwaka, kuwahi maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru tarehe 9 Desemba.

Saturday, July 9, 2011

Wageni wa Butiama: Kwaya ya Uamsho ya Musoma yafika Mwitongo kutengeneza video


Kwaya ya Uamsho ya Dayosisi ya Musoma ya Kanisa la Anglikana ilizuru Mwitongo juzi kuandaa video ya nyimbo ambazo inakusudia kutoa katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa. 
 Katika ya miaka ya hivi karibuni kwaya kadhaa zimetembelea Butiama kwa madhumuni ya kutengeneza video kutokana na mandhari murua iliyopo kwenye eneo la Mwitongo.

Monday, July 4, 2011

Wageni wa Butiama: Ujumbe wa VETA - Shinyanga wamtembelea Mama Maria Nyerere

Hivi karibu walimu wa VETA Shinyanga walitembelea Butiama na kufika kumsalimia Mama Maria Nyerere. Ujumbe wa watu watatu ulijumuisha Machumu K. Machumu (Mratibu wa Mafunzo), Miharano M. Ismail (Mwalimu wa Udereva), na Edwin Tahani (Mwalimu wa Mitambo).
Kwenye picha, kutoka kushoto, ni Miharano Ismail, Machumu K. Machumu, Mama Maria Nyerere, na aliyesimama ni Edward Tahani ambaye ni baba mzazi wa Edwin Tahani ambaye haonekani kwenye picha. Edward Tahani anafanya kazi Butiama.