Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Showing posts with label Lugha yetu Kiswahili. Show all posts
Showing posts with label Lugha yetu Kiswahili. Show all posts

Tuesday, December 13, 2016

Lugha yetu Kiswahili

Kiswahili lugha nzuri, lakini hutatanisha wengi.

Siku moja nikiwa safarini nilijikuta kwenye mgahawa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Nilikuwa nimewahi asubuhi mapema siku hiyo nikaondoka Arusha bila kupata staftahi, au kifungua kinywa.

Nilipovuka eneo la ukaguzi la maafisa usalama na kuingia kwenye ukumbi wa abiria wanaojiandaa kupanda ndege nikawahi kwenye mgahawa na kuagiza kahawa. Aidha, hupendelea kula mayai asubuhi, kwa hiyo nikamuita mhudumu ili nimuagize mayai kuwahi kabla ya abiria kutangaziwa kuingia ndani ya ndege.

Mazungumzo yakawa hivi:

Mimi: Nitapata mayai?
Yeye: Ndiyo.
Mimi: Naomba jicho la ng'ombe.
Yeye: Hapa hatuna jicho la ng'ombe.

Sikumuelewa. Huyo huyo aliyekubali kuwa mayai yapo akaniambia hawana jicho la ng'ombe. Nilibaini naongea na mtu ambaye Kiswahili kinampiga chenga. Nilihisi alikuwa mwenyeji wa Kenya. Nikamwambia anipeleke kwa mpishi niongee naye, na huko kwa mpishi nikaagiza mayai jicho la ng'ombe na yakakaangwa vizuri tu.
Jicho la ng'ombe.
Nilivyoelewa mimi, mhudumu alidhani nimeagiza nipikiwe jicho hasa la ng'ombe.

Taarifa inayofanana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/10/msiofahamu-vyema-kiingereza-zungumzeni.html

Wednesday, August 12, 2015

Lugha yetu Kiswahili: Kiswahili kinasambaa toka Scotland mpaka Butiama

Wanafunzi 12 toka Chuo Kikuu cha Edinburgh wapo kijijini Butiama kujifunza Kiswahili kwa mwezi mmoja.

Mafunzo yao ni sehemu ya mpango wa Chuo Kikuu cha Edinburgh kuvutia wanafunzi kutoka nje ya Scotland kujiunga na masomo mbalimbali katika chuo hicho maarufu, ambacho mmoja wa wanafunzi wake mashuhuri ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wanafundishwa Kiswahili na walimu Watanzania watatu.
Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh wakiwa Butiama, pamoja na walimu wao wa lugha ya Kiswahili.
Kuwepo kwa wanafunzi wa lugha ya Kiswahili kutoka Edinburgh hapa Butiama kwa Mwalimu Nyerere, ambaye pia anatambuliwa kama mmoja wa viongozi wa Tanzania ambao walitoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ni suala la fahari kubwa kwa mmoja wa waratibu wa mafunzo haya ya Kiswahili, Dk. Thomas Molony, ambaye mwaka jana alichapisha kitabu juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere kinachoitwa Nyerere: The Early Years.

Akiwa Butiama wakati akifanya utafiti wa kitabu chake, nilipata fursa ya kuchangia kwa kiwango kidogo taarifa ambazo hatimaye alizitumia kwenye kitabu hicho.

Na mimi nakubaliana naye. Naamini kuwa Mwalimu Nyerere angekuwa hai angefurahi sana kushuhudia wanafunzi kutoka chuo chake cha zamani wakiwa Butiama kujifunza lugha ambayo yeye mwenyewe aliipenda na aliyoshiriki kuiimarisha.

Wednesday, December 18, 2013

Lugha Yetu Kiswahili

Hivi karibuni, wakati nikisikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili la Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mtangazaji alisoma taarifa za majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuanza kutumia ndege zinazosemekana kuruka bila rubani, kwa Kiingereza zikijulikana kama drones.

Ukweli ni kuwa ndege hizo zinaongozwa na marubani ambao wako ardhini kwenye vituo maalum.

Mtangazaji alitumia neno "drone" lakini akauliza iwapo lipo neno la Kiswahili lenye kutoa maana hiyo hiyo. Mimi haraka haraka niliangalia kwenye kamusi ya Kiingereza kwa Kiswahili ya Taasisi ya Uchungizi wa Kiswahili (TUKI), toleo la mwaka 2006, na nikatuma ujumbe mfupi wa maandishi BBC: "drone ni nyuki dume."

Wasikilizaji wengine nao wakatuma majibu yao, mmoja akipendekeza kuwa tafsiri sahihi iwe "ndege tiara." Hayakuwa mashindano na hakuna aliyepewa zawadi yoyote, lakini nakiri kuwa "ndege tiara" inasikika vizuri zaidi kuliko "nyuki dume."

Habari inayozungumzia shambulizi la nyuki dume dhidi ya wapiganaji itachukuliwa na maana kuwa ni nyuki ndiyo waliofanya shambulio hilo na siyo ndege inayoruka angani.

Wataalamu wa lugha ya Kiswahili mnasemaje?

Friday, October 25, 2013

Msiofahamu vyema Kiingereza zungumzeni na andikeni kwa Kiswahili, mtafanya makosa machache zaidi

Hili nimeshalisema sana lakini naona kuna umuhimu kulirudia: tofauti na Watanzania wengi tunavyoamini, kufahamu vyema lugha ya Kiingereza siyo ishara kuwa anayeifahamu vyema lugha hiyo ni mtu aliyesoma kwa kiwango cha juu. Inasemekana kuwa John Major, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, alikuwa na elimu ndogo sana lakini hatuna shaka kuwa alifahamu Kiingereza vizuri sana.

Tunang’ang'ania lugha ya Kiingereza tunapoongea au kuandika kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo tutaonekana ni wasomi sana. Kiingereza ni lugha kama lugha nyingine: Kichina, Kijapani, Kifaransa, na hata Kizanaki.
Ni kweli mtu anapoongea au kuandika lugha vyema inaashiria kuwa yeye ni msomi kwa maana ya kwamba yawezekana amekaa kwenye mfumo wa elimu kwa miaka mingi na bila shaka amejifunza misingi ya hiyo lugha anayoongea. Lakini ukweli unabaki kuwa hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja kati ya kuongea na kuandika lugha yoyote kwa ufahasaha na kiwango cha elimu cha mhusika.

Naona mara kadhaa mwenye mitandao ya jamii watu wakijaribu kujipambanua kuwa waandikaji wazuri wa lugha ya Kiingereza lakini kinachojitokeza ni kuwa hawana uwezo huo.

Unaweza kujiuliza: kwanini baadhi ya hawa wanaoamini kuwa kufahamu vyema matumizi ya lugha ya Kiingereza ni ishara ya usomi wasitumie lugha yao mama, Kiswahili, kwa sababu wengi wanaowaandikia wanafahamu lugha hiyo? Kama jamii nzima inaamini kuwa kufahamu Kiingereza ndiyo hali ya kujivunia basi ni vigumu kuona mabadiliko.

Jambo la msingi ingekuwa kwa wale wasiofahamu lugha vyema – siyo Kiingereza tu – wajifunze hizo lugha vyema ili pale wanapoongea au kuandika basi wafanye hivyo kwa ufasaha na kuweza kuwa walimu wa wengine. Ukweli ni kuwa kama hufahamu lugha ya Kiswahili vyema ni vigumu kujifunza lugha nyingine kwa ufasaha.

Lakini kuna suala moja la msingi linajitokeza: iwapo hufahamu kuwa hufahamu basi tatizo ni kubwa zaidi. Kuna mwanahabari mmoja mwandamizi aliwahi kuandika makala akisema kuwa ili mtu apate uwezo wa kufahamu kuwa hafahamu anahitaji kiwango fulani cha elimu. Kwa maana nyingine, inahitaji kuwa msomi kidogo kubaini kuwa huna uwezo na jambo fulani.

Inawezekana kuwa mfumo wetu wa elimu umekuwa duni kwa muda mrefu sana kiasi ambapo limejengeka tabaka kubwa la Watanzania ambao wako kwenye kundi hilo la kuwa watu wasiofahamu kuwa hawafahamu na basi hujikuta wakiandika na kusema vitu ambavyo siyo sahihi kwa Kiingereza wala Kiswahili.

Jambo lingine ambalo linatuangamiza kabisa ni kuwa Watanzania ni wagumu sana kusahihisha wenzao pale wanapokosea kwenye matamshi na maandishi. Mkosoaji anaonekana siyo mstaarabu au huonekana anataka kujipambanua kuwa yeye anafahamu zaidi ya wenzake. Matokeo yake ni kuwa matumizi yasiyo sahihi ya lugha yanaendelea kushamiri kwenye jamii.

Nimesikiliza mara nyingi tangazo linalosikika hivi karibuni kwenye vyombo vya habari ambapo binti anatamka namba za simu na anataja “zilo zilo” akimaanisha “ziro ziro” au “sifuri sifuri.” Hilo tangazo limepitiwa na wahusika na hawakuona kasoro yake. Matokeo yake mamilioni ya watoto wanalisikiliza na kuamini kuwa kutamka “zilo” ni sahihi. Najiuliza: hawa wahusika ndiyo wale wale waliopoteza uwezo wa kutofahamu kuwa hawafahamu, au ndiyo ule ustaarabu wetu wa kutosahihisha makosa?


Maoni yangu ni kuwa tujifunze Kiswahili vyema kwanza kabla ya kujaribu kujifunza lugha nyingine. Ni kazi ndogo zaidi kumfundisha Kiswahili mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama kuliko kumfundisha Kiingereza (au lugha nyingine) mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama. Na hili ni kweli hata kwa yule ambaye Kiswahili ni lugha yake mama na anayetamka “zilo zilo.”

Taarifa zinazofanana na hii:

Friday, June 7, 2013

Lugha yetu Kiswahili: Ulemavu wa ngozi?

Imezuka desturi ya miaka ya hivi karibuni ya kubadilisha baadhi ya matumizi ya lugha na kutunga matumizi ambayo yanakuwa mbadala ya mazoea yaliyopo. Mojawapo wa mabadiliko ya lugha ya aina hii ni kuacha kutumia neno "zeruzeru" na badala yake kutumia "mlemavu wa ngozi."

Mabadiliko haya yanaiga desturi iliyoanzia Marekani ya kuacha kutumia maneno, misemo, au majina ambayo matumizi yake yalionekana kudhalilisha au kuudhi makundi kadhaa ya jamii ambayo yalibaguliwa kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na jinsia, dini, rangi ya ngozi, na kadhalika.

Mathalani, kwa mantiki hiyo, baadhi ya Wamarekani hutumia physically challenged (mwenye changamoto za kimaumbile) badala ya maneno invalid (asiyejiweza), handicapped (kilema), au disabled (mlemavu).

Mimi naafiki ubunifu wa misemo mipya mbadala na kuacha matumizi ya misemo ambayo inadhalilisha. Lakini bado sijaona mantiki ya matumizi ya "mlemavu wa ngozi" badala ya "zeruzeru." Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford, toleo la pili 2004) inaeleza zeruzeru kuwa ni "...mtu ambaye nywele na ngozi yake imekosa rangi yake kamili na badala yake kuwa nyeupe sana na ambaye macho yake hayawezi kuvumilia mwangaza mwingi; albino."

Haya maelezo yanadhalilisha?

Monday, May 6, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Neno jipya nililojifunza leo ni ajari. Siyo ajali, bali ajari.

Ajari ni muda wa ziada ambao mfanyakazi anabaki kazini akifanya kazi kwa muda wa ziada, zaidi ya muda aliopangiwa kwa mujibu wa mkataba wake wa kazi. Ajali ni ni tukio lenye athari mbaya linalotokea ghafla; ni neno ambalo linafahamika kwa watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili, hata wale ambao ni mbumbumbu wa lugha hiyo.

Sunday, April 14, 2013

Jifunze Kiswahili kwa njia ya mtandao

Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Georgia inatoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa njia ya mtandao.

Maelezo yaliyopo kwenye tovuti inayoitwa Kiswahili kwa Komputa yanaonyesha kuwa kozi hiyo ya Kiswahili inaendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu na inaelekea kuwa hufundishwa darasani pamoja na nyongeza ya masomo yaliyopo kwenye tovuti hiyo.

Mbali na kuwa Kiswahili sahihi ni "kompyuta" na siyo "komputa" na kuwa baadhi ya matamshi yaliyorekodiwa kwa njia ya sauti yanatofautiana na matamshi niliyozowea kusikia (mfano "redio" inatamkwa "radio"), tovuti hiyo bado inaweza kuwa ya manufaa makubwa na inaweza kumsaidia mwanafunzi yoyote wa lugha ya Kiswahili ambaye anafahamu vyema Kiingereza na anaweza kujifunza mwenyewe kutokana na maelezo yaliyopo.

Anwani ya tovuti hii hapa: http://www.africa.uga.edu/Kiswahili/doe/index.html

Kila mwaka wa masomo una sura sita, na kozi inakamilika kwa sura 18. Mwisho wa kila sura mwanafunzi anapaswa kufanya mtihani ambao unaweza kutumwa kwa njia ya mtandao kwa mwalimu kwa masahihisho.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/02/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2013/01/lugha-yetu-kiswahili.html

Tuesday, February 26, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Hivi majuzi katika sherehe mojawapo niliandaa mtiririko wa nyimbo mbalimbali za muziki wa dansi za kusikiliza kwenye sherehe hiyo kwa kutumia kompyuta yangu ambayo inahifadhi mkusanyiko wa nyimbo nyingi ambazo nimezikusanya kwa miaka mingi. Baada ya hapo kompyuta inaunganishwa na vipaza sauti na nyimbo zilizochaguliwa zinaanza kusikika moja baada ya nyingine kwa muda mrefu tu.

Nyingi ya nyimbo hizo ni za wanamuziki wa zamani, wengi ambao hawako hai kwa sasa. Baadhi ya hizo Watanzania tunaziita "zilipendwa" au nyimbo za zamani ambazo vijana wengi wa siku hizi hawasikilizi.

Mmoja wa waliohudhuria sherehe hiyo alizipenda nyimbo zile sana na hakutulia sana kwenye kiti chake, akiinuka mara kwa mara kwenda kucheza muziki mmoja baada ya mwingine.

Nilivyotambua jinsi nilivyomsumbua huyo mtu nikajisifia kwa kumuuliza: Umenikubali? Na hapo nikazua mjadala na mtu mwingine aliyehudhuria sherehe hiyo akihoji iwapo ilikuwa sahihi kwangu kutumia neno hilo. Alisisitiza kuwa hawezi kunikubali mimi bali anaweza kukubali nyimbo ambazo nilizichagua kusikilizwa kwenye sherehe hiyo.

Mimi nilisisitiza kuwa "kunikubali" ulikuwa ni msemo tu lakini ukimaanisha alikubali uwezo wangu wa kuchagua nyimbo nzuri na siyo kunikubali mimi binafsi. Hoja yangu ilikuwa hata asingefahamu ni nani aliyechagua zile nyimbo angeweza kusema: "namkubali aliyepanga hizo nyimbo."

Ni kweli kuwa msemo wa "kumkubali" mtu umeibuka kwenye matumizi yasiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili, hasa kwa vijana wa Tanzania, ukimaanisha kutoa sifa isiyo ya kawaida kwa mtu kwa uwezo wake wa kufanya jambo fulani.

Lakini siyo kweli pia kuwa tunaweza kuzungumzia kuwa wapiga kura "wamemkubali" mgombea mmoja na kumchagua kuwa kiongozi wao na kwa maana hiyo matumizi hayo yakaleta maana rasmi?

Wewe unasemaje?

Tuesday, January 8, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Miaka mingi iliyopita wakati nafanya kazi Dar es Salaam nilikuwa natoa huduma ya kufasiri lugha ya Kitaliani kutoka kwenye nyaraka mbalimbali zenye maandishi ya Kiingereza na Kiswahili. Nilipata kusoma nchini Italia miaka mingi iliyopita ambako nilijifunza lugha ya huko.

Kwa kuwa mimi siyo mtaalamu wa lugha mara kadhaa nilitembelea ofisi ya Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ambayo ilikuwa jirani na ofisi yangu ili kupata ufafanuzi wa maneno ambayo sikuwa na hakika niliyatumia kwa usahihi kwenye ile kazi ya tafsiri.

Wakati mmoja mtaalamu mmoja wa lugha huko BAKITA alinifahamisha kuwa maana sahihi kwa Kiingereza ya neno "tafsiri" ni translation na kuwa "kufasiri" ilikuwa na maana to translate. Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa maelezo yake, haikuwa sahihi kutamka: "Leo nimetafsiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza. Ilikuwa sahihi kusema: "Leo nimefasiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza. Hii ndiyo hoja yangu niliyokusudia kuiwasilisha leo hapa ambayo nimelazimika kuibadili baada ya kufungua kamusi ili kuhakikisha kuwa ninayotaka kuandika ni sahihi.
Nilichogundua ni tofauti kidogo na yale niliyoambiwa kule BAKITA. Ni kweli kuwa neno lina maana ile niliyofafanuliwa na yule mtaalamu. Lakini nimegundua sasa, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza toleo la 2001 iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni sahihi pia kusema: "Leo nimetafsiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza."

Hisia zangi ni kuwa matumizi yasiyo sahihi yaliendelea kwa muda mrefu na kwa watumiaji wengi sana wa lugha ya Kiswahili na kuwafanya waandaaji wa Kamusi kuhalalisha matumizi mapya ya neno hilo.

Taarifa zinazohusiana na taarifa hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2012/11/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/04/lugha-yetu-kiswahili.html

Friday, December 28, 2012

Lugha yetu Kiswahili: Kamusi ya Kiswahili kwenye mtandao

Hivi karibuni nililazimika kutafuta maana ya Kiswahili ya neno la Kiingereza dilemma na tafsiri iliyopo kwenye Kamusi ya Kiingereza - Kiswahili iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tole la 2006, imetoa neno "mtanziko."

Lakini TUKI hao hao kwenye Kamusi yao ya Kiswahili - Kiingereza, toleo la 2001, hawajatoa maana ya neno hilo kwa lugha ya Kiingereza. Inawezekana kuna toleo lijalo ambalo litaweka maana ya "mtanziko" kwa lugha ya Kiingereza.
Hali kadhalika toleo la mwaka 2004 la Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Oxford University Press nalo halina neno hilo.

Nilifanya utafiti kidogo kwenye mtandao na kugundua wavuti inayoitwa The Kamusi Project ambayo inayo kamusi ya Kiingereza - Kiswahili - Kiingereza inayoruhusu watumiaji kutafuta maana ya maneno na inaruhusu pia hata mtumiaji kuongeza maneno ambayo hayapo kwenye kamusi hiyo. Nyongeza ya maneno hupitiwa na mtaalamu na inapoonekana ni sahihi basi inaorodheshwa rasmi kwa matumizi na watumiaji wengine.

Sunday, November 4, 2012

Lugha yetu Kiswahili

Jana kwenye redio nimesikia marudio ya majadiliano kutoka kwenye vikao vya Bunge la Muungano vinavyoendelea sasa hivi. Alisikika mbunge mmoja, akiwa anatetea hoja kuwa lugha ya Kiswahili itumike kwenye uendeshaji wa shughuli za mahakama, akisema yafuatayo (siyo nukuu halisi kwa maana ya neno kwa neno lakini ni sahihi kwa maana ya nukuu yenyewe):

"...mienendo yote ya shughuli za mahakama iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili tu, na kusiwe na option ya Kiswahili au Kiingereza, iwe ni Kiswahili tu."

Anayesisitiza matumizi ya Kiswahili pekee kwenye shughuli za mahakama za Tanzania anajenga hoja yake kwa kutumia neno la Kiingereza.

Ni kazi kweli kweli.

Kwenye kamusi neno option lina maana kadhaa, ikiwa ni pamoja na: uchaguzi, na hiari.

Tuesday, October 23, 2012

Huduma ya bure kufasiri Kiswahili kwa Kiingereza*

*Vigezo na viwango kuzingatiwa: kutokana na kuwa na majukumu mengine naweza kupokea kazi kidogo tu kwa siku.

Nimechunguza kiwango cha watu wengi kumudu uandishi wa lugha ya Kiingereza - na hata lugha yetu ya Kiswahili - na, kwa maoni yangu, picha inayojitokeza ni kuwa kiwango hakiridhishi. Hapa nazungumzia Watanzania wa kada mbali mbali, kuanzia wasomi na wale ambao hawakupata fursa ya kupata elimu ya juu.

Kwa bahati mbaya imejengeka tabia inayohusisha uongo kuwa mtu anayeongea au kuandika kwa lugha ya Kiingereza ndiyo anadhihirisha kuwa ana elimu nzuri. Kwa sababu hii, watu wengi ambao wangeweza kufanya mawasiliano kwa lugha ya Kiswahili hung'ang'ana kuongea au kuandika kwa Kiingereza pasipo kuwepo uwezo mzuri wa kufanya hivyo. Kama ambavyo kutofahamu Kichina haihusiani na kutokuwa na elimu, vivyo hivyo kutofahamu Kiingereza hakuashirii kutokuwa na elimu.

Hata hivyo kuna ukweli kuwa yapo mazingira yanayolazimu mtu kuandika au kuwasilisha mada kwa lugha ya Kiingereza. Hapa naamini naweza kusaidia kutokana na uwezo wangu wa zaidi ya miaka 20 wa uandishi kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili na uandishi kwa ujumla.

Najitolea kufasiri maandishi kutoka lugha ya Kiswahili kwenda kwenye lugha ya Kiingereza iwapo maandishi hayo hayatazidi kurasa moja ya ukubwa wa A-4. Lakini nikiri kuwa nikiona dalili kuwa kazi ni kubwa nitatoza ada kuanzia kurasa ya pili na kuendelea.

Mimi si mtaalamu wa lugha kwa hiyo siwezi kutoa tafsiri rasmi, ila nina uzoefu wa kutosha wa uandishi katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kiasi cha kuweza kutoa tafsiri zinazokidhi viwango vya kuridhisha vya uandishi.

Nitumie maandishi yako kwa barua pepe na nitakurudishia tafsiri siku inayofuata:

kiswahilikwakiingereza@gmail.com

Tuesday, September 4, 2012

Katiba mpya itamke lugha rasmi ya bunge kuwa Kiswahili

Kama kuna kundi liliojijengea utaalamu wa kuvuruga lugha ya Kiswahili, kundi hilo ni la viongozi wa kada mbalimbali hapa Tanzania. Na vinara zaidi wa kuivuruga lugha ya Taifa ni wabunge wetu.

Ukisikiliza mjadala wa Bunge la Muungano ni vigumu kupita dakika kumi bila anayeongea kutumia neno la Kiingereza ndani ya mjadala unaoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya watu wameipachika jina tabia hii ya kuchanganya lugha za Kiingereza na Kiswahili kuwa ni kuongea kiswanglish, neno lisilo rasmi kwenye lugha zote mbili.

Kuna dhana potofu miongoni mwa viongozi wetu wa sasa kuwa unapochanganya mazungumzo kwa kutumia maneno ya Kiingereza kwenye mazungumzo yako, basi wewe unaonekana kuwa ni mtu msomi. Na utakuta viongozi hawa hawa hata kwenye maandishi yao wanaweza kutumia neno la Kiswahili halafu kwenye mabano wanatoa fasili ya neno hilo hilo kwa lugha ya Kiingereza, kama vile kuwakumbusha wale wanaosoma maelezo yao kuwa wasisahau kuwa wao ni wasomi.

Jambo moja dhahiri ni kuwa ni Watanzania wachache sana wanaoelewa hayo maneno ambayo viongozi wetu, katika jitihada za kukogana wao kwa wao, wanayoyatumia kwenye maandishi na matamshi ikiwa ni pamoja na kwenye mijadala, mikutano, na kwenye vyombo vya habari.

Naamini umewadia wakati kwa lugha ya Kiswahili kutamkwa kuwa ndiyo lugha rasmi ya kutumika ndani ya Bunge la Muungano. Haileti mantiki kwa mwananchi aliyepiga kura kumchagua mbunge asielewe anachojadili mbunge wake.

Wednesday, May 9, 2012

Lugha yetu Kiswahili

Kwa Kiswahili sanifu, kofia ya rangi nyekundu anayovaa Mhe. Nimrod Mkono, mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, inaitwa tarabushi. Aidha, huitwa pia tarbushi.
Bango la barabarani lenye picha ya Mhe. Nimrod Mkono akiwa amevaa tarabushi, akiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kulia.
Asili ya tarabushi ni eneo la Ugiriki ya kale lakini ni kofia ambayo huvaliwa sana na Waislamu wa eneo la mashariki la Bahari ya Mediterenia. Mpaka mwaka 1925 kofia hii ilikuwa sehemu ya vazi rasmi nchini Uturuki.

Wednesday, March 21, 2012

Lugha yetu Kiswahili

Hii ni sehemu ya hotuba niliyotoa kwenye mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto, Mwanza, tarehe 18 Februrai 2012.
***********************************
Napenda kugusia pia matumizi sahihi ya lugha kwa sababu kama tukirejea kwenye ile nukuu ya Mwalimu Nyerere kuwa shabaha ya elimu ni:

 “...kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine maarifa na mila za taifa, na kuwaandaa vijana wawe tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza taifa.”

basi utakuta kuwa lugha ni kipengele muhimu sana cha mila za Taifa. Lakini kinachotokea kwenye lugha siku hizi kinatisha. Mifano ni mingi lakini nitataja mfano toka kwenye sanaa.

Kuna msanii mmoja wa siku hizi anaimba wimbo mmoja na kutumia neno “hakunaga”. Sasa sitaki kuanzisha ubishi kati yangu na nyinyi kuhusu kama huyu ni msanii mzuri au siyo kwa sababu tunaweza tusifikie muafaka. Lakini kuna mtu nimesikia akisema kuwa katika masuala ya sanaa siyo muhimu kuzungumza lugha sahihi kwa sababu ukilazimisha hivyo unaua kipaji cha ubunifu, au utunzi.

Inawezekana haya ninayosema yanapingana na mliyofundishwa na walimu zenu, lakini kwa maoni yangu ni afadhali tuache kusikia nyimbo kama “hakunaga” lakini tuzungumze lugha ambayo ni sahihi. Huyu msanii anasikilizwa na watoto ambao baada ya miaka ishirini wataamini kuwa “hakunaga” ni neno sahihi la lugha ya Kiswahili.

Hapa sizungumzii Kiswahili tu, ila lugha yoyote ile ambayo wewe umejifunza au ambayo utajifunza. Hakuna lugha ambayo ni muhimu kuliko lugha nyingine. Mimi naongea Kiswahili, Kiingereza, na Kitaliani, lakini nafahamu Kizanaki kidogo sana. Kwa wazee wa Kizanaki ambao hawaongei Kiswahili hizo lugha nyingine hazinisaidii kitu chochote. Kwanza ni aibu kuwa kuna wakati mwingine nalazimika kutumia mkalimani kuongea na mzee wa Kizanaki.

Kwa hiyo ushauri wangu ni kuwa jiufunzeni lugha kwa kadiri inavyowezekana lakini jifunzeni hizo lugha vizuri.

Labda ni vyema kuanza kuzungumza Kiswahili vizuri kwanza, halafu kuendelea na lugha nyingine. Nyie ndiyo wazazi wa kesho, ndiyo viongozi wa kesho. Na mnao wajibu wa kulinda na kuhifadhi Kiswahili kama urithi wetu.

Siku hizi, kwa bahati mbaya, wale wanoongea Kiswahili kwa kuchanganya na maneno ya Kiingereza ndiyo wanaonekana wafahamu zaidi kuliko wale wanaoongea Kiswahili peke yake. Wengine wanachanganya lugha kwa kufikiria wataonekana bora zaidi ya wengine, lakini kuna wengine wanafanya hivyo kwa sababu baadhi ya maneno wamejifunza kwa Kiingereza halafu ndiyo wanatafuta maana yake katika Kiswahili.

Ninawaomba nyinyi mjifunze lugha vizuri kwa sababu nyinyi ndiyo mtakuwa mnaotazamwa na watoto wenu kama walimu wao. Msipojifunza vizuri lugha yenu mtachangia kupoteza kabisa lugha yetu au kuibadilisha.

Naomba niwape mfano mmoja. Zamani wakati Watanzania tukisafiri kwenda Kenya tulikuwa tunaagiza “nyama ya kuchoma” ; Wakenya walivyokuja Tanzania waliagiza “nyama choma”. Sasa naogopa kuanza mjadala na Sr. Judy kuhusu usemi upi ni sahihi lakini ukweli ni kuwa naamini sasa hivi ni Watanzania wachache sana wanaotumia msemo “nyama ya kuchoma”. Karibu kila mtu anasema ”nyama choma”, na hii naamini imechochewa na matumizi na hasa matangazo kwenye vyombo vya habari.

Maana yake ni kuwa jambo linalorudiwa mara kwa mara linaweza kubadilisha matumizi kwenye lugha.

Na huu ndiyo aina ya mfano wa mabadiliko ya matumizi ambayo tunaweza kuona baada ya miaka kadhaa kwa watoto wanaoendelea  kusikiliza “hakunaga”.

Tuesday, September 6, 2011

Lugha yetu Kiswahili


Taswira ya lugha ya Kiswahili na ya wale wanaotumia lugha hiyo ni masuala ambayo yanaleta mitazamo na maana mbalimbali.

Nina rafiki yangu toka Kagera alinisimulia kuwa kwa baadhi ya Wahaya katika nyakati ambazo wenye uwezo wa kuongea Kiswahili fasaha walikuwa wachache, hasa kwenye maeneo ya vijijini, mtu yoyote aliyeongea lugha Kiswahili vizuri alionekana ni mtu mmoja mjanja mjanja ambaye hakuwa mtu wa kuaminika kwa urahisi.

Nakumbuka simulizi nyingine pia toka Uganda zinazoeleza kuwa kwa sababu lugha ya Kiswahili ilikuwa inatumika na wanajeshi (na inaendelea kutumika mpaka sasa) basi lugha hiyo imehusishwa katika historia ya Uganda na nyakati ambapo jeshi lilionekana kama kinara wa ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Katika matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili, mtu anayeitwa Mswahili, pamoja na kuwa na maana nyingine, ni mtu mwenye maneno mengi, na mjanja.

Friday, July 22, 2011

Maana sahihi ya neno 'fisadi'

Leo hii wakati nikisikiliza kipindi cha Kipima Joto cha ITV kinachoongozwa na Rainfred Masako, nimemsikia Profesa Tigiti Sengo akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi sahihi ya neno 'fisadi'. Alisema:
Fisidi ndiyo mwizi; fisadi ni malaya na mlevi.
Huyu ni gwiji wa lugha ya Kiswahili. Natabiri kuwa miaka 20 tangu leo hii, Watanzania wataendelea kutumia neno ‘fisadi’ kama ambavyo linavyotumika sasa hivi kwa makosa. Au inawezekana mafisidi hawatakuwepo wakati huo.

Monday, July 4, 2011

Lugha Yetu Kiswahili: Kwa matumizi haya, Kiswahili kitaangamia


Suala moja ambalo linajidhihirisha mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni ni matumizi mabaya ya lugha ambayo yamejikita katika mazungumzo na hata maandishi ya kila siku ya lugha ya Kiswahili.

Mimi naamini mtu yoyote anayefahamu lugha yake, au anayetaka kulinda matumizi sahihi ya lugha yake hawezi kupuuza matumizi sahihi ya lugha, lakini kwa mwenendo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ulivyo siku hizi, hasa kwa vijana, Kiswahili kina wakati mgumu na uwepo wake uko hatarini.

Mimi nakubaliana na wanaosema kuwa kuna ulazima wa lugha kubadilika na msamiati kuongezeka kila muda unavyozidi kupita. Lakini siyo kwa mtindo huu wa sasa ambapo maneno sahihi yanageuzwa kuwa maneno yasiyo sahihi, na misemo isiyofaa kutumika hata kwenye vyombo vya habari. Nitoe mifano michache:

Vijimambo: Hili neno nimewahi kusikia watu wazima wakilizungumza. Ni afadhali ingekuwa vijana peke yao kwa kuwa wao wanajulikana kwa kutunga maneno mapya. Kwa uelewa wangu mimi lina maana ya mambo kadha wa kadha ambayo msemaji hawezi kuyaweka bayana na hutumia neno hilo kufunika hayo asiyoweza au asiyotaka kuyasema kwa wakati ule. Ushauri wangu ni kuwa kama huwezi kulisema inawezekana halistahili kusemwa.

Ndivyo sivyo: Huu msemo nimeusikia ukitumika na baadhi ya wanahabari na nashindwa kabisa kuelewa mwanahabari anawezaje kuacha kutumia lugha ambayo inaweka wazi maana anayokusudia badala ya msemo unaomlazimu msikilizaji kukisia maana inayokusudiwa.

Kudadeki: Kwa kadiri ninavyofahamu mimi chimbuko la hili neno ni tusi la nguoni na limeingia katika matumizi ili kuepuka mtumiaji kusema lile tusi lenyewe. Cha ajabu ni kuwa nimeshasikia tangazo kwenye redio la kampuni moja ya simu wakitumia neno hilo. Kama linatumika kwenye tangazo muda si mrefu litakuwa kwenye matumizi ya kawaida ya lugha. Ukiuliza maana yake sidhani kama wengi wa wanalolitumia wanafahamu kwa uhakika, lakini mimi naamini kuwa hili neno linatokana na tusi zito tu.

Kwa mtindo huu, Kiswahili kitapona?

Monday, October 18, 2010

Lugha yetu Kiswahili

Nilitembelewa Butiama hivi karibuni na Andrea Wobmann, raia wa Uswisi, ambaye alikuwa Tanzania kwa miezi kadhaa akifanya kazi ya kujitolea katika kuendeleza shughuli za utalii jijini Mwanza.

Alisindikizwa na mwenyeji wake toka Mwanza (ambaye jina lake nitaliweka hapa baada ya muda kwa sababu silikumbuki kwa sasa) aliyevaa fulana iliyoandikwa "mzungu."

Awali nilihisi kuwa ile fulana angeivaa Andrea, lakini nilivyopekuwa kwenye kamusi nikagundua kuwa yawezekana sifahamu vizuri tu Kiswahili. Neno hilo, kama lilivyoandikwa kwenye fulana lina maana nyingine zifuatazo, zaidi ya ile maana ambayo wazungumzaji wengi wa Kiswahili tunaifahamu:

1. jambo lisilo la kawaida
2. mafunzo yanayotolewa kwa wanafunzi wa ngazi ya awali
3. ujanja; uerevu

Ingekuwa maandishi ya kwenye fulana yalikuwa "Mzungu", yaani na herufi kubwa ya mwanzo, basi ile maana niliyoidhania mimi ndiyo ingekuwa sahihi, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya mwaka 2001.

Thursday, May 20, 2010

Lugha yetu Kiswahili


Picha hii inaonyesha pikipiki ambayo haijapata namba ya usajili yenye maandishi ya lugha isiyokuwepo duniani. Neno "chassis" ni la asili ya lugha ya Kifaransa. Lakini mwenye pikipiki hii, au mwandika namba, ameandika "chasess" neno ambalo haliko kwenye Kiingereza, Kifaransa, wala Kiswahili.

Neno sahihi la Kiswahili lingekuwa "chesisi" kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza, toleo la pili la mwaka 2000, iliyochapishwa na Taasisi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa vile msamiati wa Kiswahili unakuwa kila mara, inawezekana limejitokeza neno jingine mbadala linalofanana na lugha yetu. "Chesisi" bado ni neno linalofanana kimatamshi na asili ya lile la Kifaransa.

Ukweli unabaki kuwa katika maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, kuendeleza ushabiki wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye maandishi na mazungumzo ni jambo linalokuwa gumu kila siku zinavyozidi kupita.

Lakini pamoja na hayo bado ni muhimu kuunga mkono jitihada za Serikali kuamua kutumia lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zote rasmi za Serikali. Matumaini ni kuwa huu utaratibu utatumika pia bungeni ambapo tabia ya kuchanganya Kiingereza na Kiswahili imekuwa jambo la kawaida.