Nimepiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 1985. Ningeweza
kupiga kura mwaka 1980 lakini sikuwa nchini wakati huo, nilikuwa masomoni.
Naamini kuna vijana wengi ambao watakuwa wanapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka
huu na naomba nitoe ushauri mdogo kwao.
Nikiwa na Mwalimu wangu, Godian Muikza (kushoto) ambaye ni diwani anayemaliza muda wake wa Kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini. |
Hata mwaka huu naamini kuna wapiga kura wengi watajitokeza
wa aina yangu, kama nilivyokuwa mimi mwaka 1985 na kupiga kura kwa kufurahishwa
na jina la mtu tu bila hata kuchambua kwa makini sera anazowakilisha mgombea
huyo. Mwaka 1985 hatukuwa na vyama vingi, lakini sasa vipo. Kwa hiyo, hakuna
sababu ya msingi ya mpiga kura yoyote kuacha kuweka sera za vyama kwenye
mizania na kuamua chama kipi kitapata kura yake. Hatuna uhakika kuwa
yanayoahidiwa yatatekelezwa, lakini bado ni muhimu kuchambua sera tofauti. Akishinda
mtu wako na asipotekeleza ilani yake angalau unayo sehemu ya kuanzia kumhoji.
Kama ulimchagua kwa mkumbo tu hutakuwa na kigezo cha kuamua kuwa hajatimiza
ahadi zake.
Wapiga kura wa Butiama wakipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 |
Pili, nazungumzia wale ambao wana uhakika mkubwa wa matokeo
ya ushindi kwa wanaowaunga mkono, ikiwa ni vyama vya siasa au mgombea mmoja
mmoja. Kusikiliza na kuamini na kauli kama “ushindi ni lazima” ni mwanzo wa kukaribisha
vurugu. Kama kiongozi anatumia kauli hiyo kuhamasisha tu wafuasi wake ili
waweke juhudi kubwa kwenye kampeni inaweza kuwa haina madhara. Lakini kauli hiyo
inaweza kufasiriwa kuwa “tumeshashinda hata kabla ya kupiga kura na mtu yoyote
atakayesema kuwa hatujashinda ni muongo na ametuibia kura.” Hapo tunakaribisha
vurugu.
Mwaka 2010 niliteuliwa wakala wa mgombea ubunge na nilijifunza
kitu kimoja cha msingi. Kama wakala wa mgombea yuko makini, siyo rahisi kuibiwa
kura. Sikulala siku hiyo mpaka matokeo yalipothibitishwa na msimamizi wa
uchaguzi alfajiri ya siku iliyofuata. Wanaoibiwa kura ni wale ambao wameweka
mawakala ambao siyo waaminifu au ambao hawakuwa makini. Mtu akitaka kuibiwa,
ataibiwa.
Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi tumesikia shutuma kuwa
Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo wataalamu wa kuiba kura. Kama hizo shutuma ni
za kweli, sioni sababu yoyote ya kutoana roho kwa sababu sasa hivi Mhe. Edward
Lowassa amehamia upande wa pili. Yeye amekulia na kujifunza siasa ndani ya CCM na,
kwa vyovyote vile, atakuwa amehama na uelewa uliobobea wa mbinu zinazotumika
kuiba kura na atakuwa anafahamu mbinu za kutumika kuzuwia wizi huo. Mwizi
hawezi kumuibia mwizi.
Mwanachama wa Chama cha wananchi (CUF) akielekea kwenye mkutano wa kampeni jijini Mwanza mwaka 2010. |
Kwa sababu hii sioni kabisa busara ya mtu yoyote kutamka
kuwa kaibiwa kura kama yeye mwenyewe hataki kuibiwa kura. Labda atumie kauli hiyo
kama kisingizio cha kupinga matokeo. Tunao wajibu wa kujenga mazingira yenye kulinda
amani, lakini tunao pia uwezo wa kuweka mazingira yanayobomoa amani.
Uchaguzi huu umeibua ushindani mkubwa kati ya CCM na vyama
vinavyowakilishwa na UKAWA. Kwa bahati mbaya, ushindani unaonyesha dalili za
uhasama na muelekeo kuwa kipindi hiki cha kampeni kitaibua matukio ya kuvunjika
kwa amani. Lakini amani itavunjika tu iwapo wapiga kura tutakubali ivunjike. Na
amani inapovunjika hutasikia hata siku moja kuwa Mhe. John Magufuli au Mhe.
Edward Lowassa kavunjika mguu kwa sababu ya vurugu za kisiasa.
Bado sijaona sababu ya msingi ya kuvunjika kwa amani
kutokana na uchaguzi. Usikubali kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani.