Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, June 5, 2011

Mada yangu ya leo: Umaskini mbaya

Mojawapo ya habari ambazo zimeandikwa kwa kina sana kwenye kipindi cha hivi karibuni ni nia ya Serikali ya kujenga Barabara ya lami kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara kupitia mbuga ya Serengeti.

Ni habari ambayo pia imeleta mvutano mkubwa baina ya pande mbili. Upande moja ina wale wanaopinga kuwepo kwa barabara hiyo, wakidai kuwa ujenzi wake utaathiri majaliwa ya wanyamapori waliyopo Serengeti. Upande wa pili ni wale ambao wanadai kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wakazi wa mkoa wa Mara na mkoa wa Arusha na kuwa umefika wakati kwao pia kufaidikia ni ujenzi wa barabara kama maeneo mewngine ya Tanzania.

Wanamazingira wa ndani ya nchi na nje ya nchi wameungana kupinga kwa nguvu kabisa ujenzi wa barabara hiyo wakidai kuwa Serikali ya Tanzania imeweka sahihi mikataba ya kimataifa ya kutunza na kulinda mazingira na kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakiuka mikataba hiyo. Aidha hifadhi ya Serengeti imeorodheshwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kama eneo la urithi wa Dunia na ujenzi wa barabara hiyo unaweza kusababisha kufutwa hadhi hiyo na kuleta athari mbalimbali kwa nchi, ikiwa ni pamoja na kupunguka kwa watalii watakaotembelea Serengeti na hivyo kuathiri biashara ya utalii na mapato yanayotokana na utalii. Na vitisho siyo vidogo, ikiwa ni pamoja na tishio la Tanzania kunyimwa misaada mbalimbali kutoka nje.

Hoja ya kwamba kwa kujenga barabara hiyo Tanzania itakuwa inakiuka mikataba ya kimataifa ambayo imeweka sahihi ni hoja yenye nguvu. Lakini tunayo mifano mingi ya nchi ambazo zinafanya maamuzi yanayokiuka sheria za kimataifa kwa misingi ya kulinda maslahi ya nchi hizo. Sisi tunaathirika na tatizo la kuwa omba omba. Maslahi ya nchi yetu tunapangiwa na nchi nyingine kwa hiyo hatuna ubavu wa kujenga hoja kuwa jambo fulani linaathiri maslahi yetu, na hivyo basi kudai mapitio ya vipengele ambavyo vitazingatia mahitaji yetu kwenye mikataba ya Kimataifa ya aina hiyo.

Hoja kuwa barabara ya lami inaweza kufuta misafara ya msimu ya wanyama kuhama kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine nina wasiwasi nayo. Kwamba nyumbu na pundamilia wanaovuka  mbuga zenye wanyama hatari kama simba, na chui, na wanaovuka mto Grumeti uliyojaa mamba watashindwa kuvuka barabara ya lami ni mojawapo ya yale masuala ambayo wengine tunayakubali kwa shingo upande kwa sababu tu wanayoyasema ni watu ambao wanasemekana ni wataalamu wa wanyamapori na mazingira. Lakini ni hoja ya kitoto, kwa maoni yangu. Inawezekana ipo athari ya kiasi fulani itakayosababishwa na barabara ya lami, lakini siamini kuwa athari hiyo itafuta kabisa uwepo wa wanyama hao kwenye sura ya dunia kama inavyodaiwa na hawa wataalamu.

Umaskini ni tatizo, lakini wenye hoja inayounga mkono ujenzi wa barabara ya lami kupita ndani ya mbuga ya Serengeti tungekuwa na uwezo wa kifedha ingewezekana kabisa kupata wataalamu wetu wakatufanyia utafiti utakaoonyesha kuwa athari ya barabara ya lami kwa nyumbu na pundamlia siyo ya kutisha. Huu ndiyo utaratibu uliyopo nchi zilizoendelea pande zinazokinzana zinapotaka kuvunja hoja ya upande mwingine. Umesikia hivi karibuni kuna tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya simu za kiganja yanaweza kuleta ugonjwa wa saratani, wakati miaka yote tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya simu hizo hayana athari zozote?

Barabara zilizopo kwenye hifadhi za wanyama katika mataifa mengi yaliyoendelea kunakotoka shinikizo kubwa dhidi ya ujenzi wa hii barabara zimewekwa lami. Tungekuwa tuna uwezo wa kuweka msimamo tungeomba wale wote wanaopinga barabara za lami kwenye mbuga za wanyama kwanza wafumue lami zilizopo kwenye barabara zinazopita kwenye mbuga zao halafu ndiyo waje tukae meza moja kupanga namna ya kuepusha kuweka lami ndani ya mbuga ya Serengeti.

Sishabikii kumaliza wanyama, lakini naamini mahitaji ya binadamu yanawekwa nyuma ya mahitaji ya wanyama. Tatizo ni kuwa wanaharakati wa mazingira hawaambiliki, na hawana muafaka. Tunaamrishwa kusikiliza wanaosema wao, na hawasikilizi hoja nyingine zozote. Ni baadhi ya hao ambao katika jitihada za kuzuwia kuuwawa kwa baadhi ya wanyama kwa ajili ya kutengeneza makoti ya baridi kwa ajili ya binadamu, wako tayari kuua binadamu hao hao wanaovaa hayo makoti.

Hakuna tusi kubwa kwa Watanzania kama kusema kuwa mnyama ni muhimu kuliko mwanadamu. Ni kweli kwa baadhi ya wenzetu, wanyama ni muhimu sana hata kuliko binadamu. Na tumeshuhudia wanyama kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa kuwatibu maradhi wakati binadamu wenzao wanalala nje bila kufahamu wapi watakula, wacha kupata huduma ya matibabu.

Hoja yangu ya leo ni kuwa umasikini si sifa nzuri, na ina athari kubwa kwa nchi ambayo inajaribu kuwahudumia raia wake lakini inapata shinikizo kutoka kwa wahisani ambao kauli yao ina nguvu kuliko ile ya raia Watanzania.

Wednesday, June 1, 2011

Wageni wa Butiama: Profesa Mbilinyi na Profesa Mbilinyi

Muda si mrefu uliyopita nilipokea simu ikiniarifu kuwa kuna mgeni amefika nyumbani. Nilipouliza ni nani, niliambiwa: "Profesa Mbilinyi."
Profesa Simon Mbilinyi (kulia) akijaza kitabu cha wageni kwenye maktaba ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere, Butiama. Katikati ni Profesa Marjorie Mbilinyi.
Nikielekea kuonana na mgeni nikawa najiuliza: "Huyu atakuwa Profesa Mbilinyi yupi? Hakuwa mmoja, walikuwa wawili: Profesa Marjorie Mbilinyi, na Profesa Simon Mbilinyi (ambaye ni mume wake) ambao walikuwa wamepita Butiama wakielekea Ukiliguru ambapo waliwahi kufanya kazi zamani.

Profesa Marjorie Mbilinyi ni mwanaharakati wa masuala ya jinsia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Profesa Simon Mbilinyi amewahi kuwa waziri wa Serikali ya Tanzania.

Saturday, May 28, 2011

Habari Njema Kwa Watu Wote

Siku chache zilizopita nilipokea barua pepe yenye kichwa cha habari, “Habari Njema Kwa Watu Wote” kutoka kwa mtu ambaye jina lake ninahifadhi kwa sababu nitakazofafanua, ambaye amejitambulisha kama mtaalamu wa tiba za jadi. Anadai kuwa na utaalamu wa tiba za jadi na uwezo wa “kutibu matatizo mbali mbali kwa kutumia makarama ya kiuchawi, kutatua matatizo yanayosumbua mwanadamu na yakaisha kabisa…”

Sababu moja ya msingi inayonisukuma kuhifadhi jina la 'mtaalamu' huyu ni kuwa shughuli za uchawi haziruhusiwi kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, kwa hiyo ili kutupunguzia yeye na mimi uwezekano wa kujikuta tunasaidia polisi kwenye uchunguzi nimeona ni bora abaki bila jina.

Katika barua pepe hiyo ameorodhesha matatizo 43 ambayo ana uwezo wa kuyamaliza. Nasema anayamaliza kwa sababu siyo yote ni maradhi. Mfano, anaweza “kutatua matatizo ya sehemu yako ya kazi, kama kutoelewana na bosi.” Kama hupandi cheo kazini anao uwezo wa kukupandisha. Jambo la hatari ambalo ana uwezo wa kufanya ni “kulipa kisasi kwa mbaya wako.”

Anaonekana kuwa na uwezo wa kipolisi na wa kimahakama kwa mpigo. Mfano, anaweza kurejesha mali iliyoibiwa. Aidha, anaweza kumaliza kesi mahakamani. Ni mshauri wa mavazi pia: anaweza "kutabiri nyota na nguo za kuvaa kuanzia Jumatatu hadi Jumapili." Mengine ni pamoja na uwezo wa kuwanasa wanga na wachawi, na uwezo wa "kutengeneza jini wa shari na kumtuma katika mambo ya shari."

Pamoja na mambo hayo anajitangaza kuwa na uwezo wa kutibu pia matatizo ya kiafya, mfano, matatizo ya uzazi kwa kina mama, kupungua nguvu za kiume, maradhi ya masikio, pumu, kichwa, tumbo, n.k.

Hivi karibuni, baada ya kuandamwa kwa Babu wa Loliondo kuwa anadanganya na kuwa hatibu ila anadanganya, niliandika makala kumtetea nikeleza jinsi gani watafiti wa nchi moja ya Ulaya walibaini katika utafiti kuwa inawezekana kumdanganya mgonjwa kuwa anapata dawa ya kutibu ugonjwa fulani, naye akapona akiamini kuwa amepewa dawa kumbe kapewa peremende tu inayofanana na dawa halisi. Katika mazingira hayo mgonjwa anapona kwa sababu anamuamini daktari anayempa ile dawa feki, na kuamini kuwa ni kweli anapewa dawa.

Katika makala niliyoandika nilihoji kama ni kweli kuwa Babu wa Loliondo anadanganya lakini watu wanapona kwa imani kuwa wanapewa dawa inayoponyesha basi hilo lisiwe tatizo la mtu yoyote ambaye hana mpango wa kwenda Loliondo. Kwa mantiki hiyo, ningemtetea hata huyu ‘mtaalamu’ wa kutibu zaidi ya 43, lakini nasita.

Labda tofauti ya msingi hapa kati ya huyu mtaalamu na Babu wa Loliondo ni kuwa Babu hakutangaza kama anatumia nguvu za uchawi – ingawa kuna baadhi ya watu wanasema kuwa anafanya hivyo.

Tuesday, April 26, 2011

Mwalimu wangu, Gordian Mukiza

Mwaka jana, wakati vuguvugu za kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea nchini kote, nilifunga safari kwenda Muleba, Kagera, kumtembelea rafiki yangu Hamisi Millanga, aliyekuwa kwenye mikakati ya kutetea kiti chake cha udiwani wa kata ya Muleba kupitia Chama cha Wananchi (CUF). Safari yangu ilikuwa na nia ya kupata muelekeo wa harakati za kampeni kwenye maeneo hayo.
Mwalimu Gordian Mukiza, kushoto, na mimi.
Siku moja katika pitapita zangu mjini Muleba nilikutana na mwalimu wangu wa siku nyingi nilivyokuwa mwanafunzi wa Shycom (Shinyanga Commercial Institute) kati ya mwaka 1977 – 1979, Mwalimu Gordian Mukiza. Aliyenitambua ni yeye, pamoja na kuwa nimesheheni mvi kibao kichwani na pengine sifanani hata kidogo na nilivyokuwa Shycom.

Aliniambia kuwa alikuwa mgombea wa udiwani wa kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Alishinda uchaguzi huo kwa kishindo, na matokeo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wapiga kura waliyoandikishwa: 2,553
Waliyopiga kura: 1,685
Kura zilizoharibika: 64

Kura za Wagombea:
CHADEMA - Amri Kalizabona Hamisi : 254
CUF - Felician Rutwaza:                   400
CCM - Gordian Joseph Mukiza:          967

Wednesday, March 9, 2011

Msanii Hardman ateuliwa katika Tuzo za Muziki za Kilimanjaro

Kwa mujibu wa taarifa iliyopokelewa toka kampuni ya Maisha Music, msanii wake, Hardman, ameteuliwa kushindania Tuzo ya Muziki ya Kilimanjaro Kilimanjaro,
Bango la Hardman la uzinduzi wa album yake, Imebaki Stori, uliyofanyika Desemba 2010
Taarifa hiyo pia inatoa wito na maelekezo kwa mashabiki wa Hardman kumpigia kura ili aweze kushinda.
Taarifa kamili hii hapa: 
Toleo hili la barua taarifa limejikita zaidi juu ya uteuzi wa Hardmad ni msanii wa reggae na dancehall ambaye kwa sasa anasimamiwa na kampuni ya Maisha Music. Katika tuzo za mwaka huu amefanikiwa kuteuliwa katika vipengele viwili navyo ni; kipengele cha wimbo bora wa reggae ambapo ameingiza ameingiza nyimbo mbili, na kipengele kingine ni kile cha wimbo bora wa kushirikishwa, na ni kutokana na kushirikishwa kwake katika wimbo wa Mwana FA na AY “Dakika Moja”.  

Haya ni mafanikio makubwa kwetu pamoja na Hardmad, na tunaamini kuwa hii imetokana na kujituma kwake kwa bidii pamoja na ushirikiano baina yetu. Sisi tunamtakia kila la heri katika tukio hili muhimu kwa maisha yake kama msanii. Maisha Music inapenda pia kuwatakia mafanikio marafiki zetu wengine ambao wamo katika kinyangányiro hiki mwaka huu, baadhi yao ni Jhikoman, Warriors From The East, Ras Rwanda, Lamar, Fid Q, Ray C na Chidi Beenz.

Washindi wa tuzo za Kilimanjaro wanapatikana kwa kupiga kura. Hii inamaanisha kwamba wimbo utakaopata kura nyingi kutoka kwa mashabiki na wapenzi ndiyo utakoshinda. Tafadhali mpigieni Hardmad kura zenu kwa wingi ili aweze kufanikiwa kuibuka kidedea kwani tunaamini anastahili na unaweza kuthibitisha kwa kusikiliza kazi zake kupitia katika linki zilizowekwa hapo chini.

Unaweza kumpigia kura kwa njia mbili tofauti ambazo ni; kwa kubonyeza katika linki iliyoonyeshwa hapo chini na pili ni kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu. Iwapo utaweza basi unayo ruhusa ya kutumia njia zote mbili. Angalizo: Kwa kuwa Hardmad ana nyimbo mbili katika kipengele kimoja tunapendda kuwashauri wadau wetu kuupigia kura wimbo wa Ujio Mpya ambao amemshirikisha Enika. Vinginevyo kunaweza kuwa na uwezekano wa kura kugawanyika katika nyimbo mbili.

Katika wimbo wa Ujio mpya tumeshangaa kuona kuwa limeongezwa jina geni la msanii ambaye hatumfahamu (BNV). Tunadhani kuna makosa
yamefanyika na tunajaribu kuwasiliana na wahusika ili kuona namna ya kuliondoa.

Namna ya kupiga kura:

KWA MTANDAO (rahisi sana): 

Gonga kwenye linki hii: http://www.kilitime.co.tz/awards/2009/nominees_2007.php (Na ni kwa mwaka 2011), na ikifunguka gonga kwenye nyimbo unazotaka kuzipigia kura, andika anuani yako ya barua pepe na bonyeza “VOTE”. Kumbuka kubonyeza katika linki ya kuhakiki na utatumiwa barua pepe ya kutoka KTMA (Kilimanjaro Tanzanian Music Awards), vinginevyo kura yako haitasajiliwa! Unaweza kupiga kura moja tu kwa anuani moja ya barua

SIMU:

"Wimbo bora wa Reggae":

Andika K179 katika ujumbe mfupi na tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "Ujio Mpya - Hardmad Feat. Enika" 
Andika K186 katika ujumbe mfupi na tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "What you feel inside - Hardmad"

(Unaweza kupiga kura moja tu katika kila kipengele kwa kila namba ya simu).

"Wimbo bora wa kushirikishwa:

Andika W137 kwa ujumbe mfupi na kisha tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "Dakika Moja - Mwana FA & AY feat. Hardmad" 

Tunakushukuru sana kwa ushirikiano wako na msaada ambao tunaamini utaweza kumfikisha Hardmad katika kilele cha mafanikio anayostahili. Tuna matarajio ya mengi mazuri katika harakati za kimuziki kwetu pamoja na wasanii tunaoshirikiana nao. Kwa ufafanuzi zaidi unaweza kusikiliza na kuangalia baadhi ya nyimbo katika Myspace au Youtube au kwenye kurasa za Hardmad katika mitandao ya Facebook na Myspace. Albamu mpya ya Hardmad “Imebaki Story” kwa sasa inapatikana pia kwa njia ya mtandao, na unaweza kuipata kwa kubonyeza hapa kwa Itunes pamoja na maduka mengine ya kwenye mtandaoni. 

Hivi sasa Maisha Music ipo katika maandalizi ya maonyesho kadhaa ya utambulisho wa albamu ya Hardmad katika miji mbalimbali hapa Tanzania pamoja na Kenya mwezi wa Aprili. Taarifa sahihi pamoja na tarehe zitatangazwa muda si mrefu.

Tafadhali tusaidie kusambaza taarifa hii kwa wapendwa, marafiki pamoja na wadau wengiine wa muziki!

Kila la heri na asante sana kutoka
Timu ya MAISHA MUSIC