Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, July 5, 2011

Machinga wa Dar es Salaam


Kabla ya mwaka 1999 niliishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam, halafu baada ya hapo nikahamia kijijini Butiama.

Kuna mabadiliko makubwa yanaonekana jijini Dar es Salaam kwa mtu ambaye anakuwa nje ya jiji hilo kwa muda. Siyo rahisi kwa wakazi wa Dar kuona hayo mabadiliko kulinganisha na anayetokea nje ya Dar. Nakiri huwa “nashangaa” kwa mabadiliko makubwa ninayoyaona Dar kila ninapotembelea huko. Mfano, hivi karibuni nilienda sehemu ambapo ilikuwepo Sno Cream, jirani na Shule ya Forodhani, nikakuta jengo lile ilipokuwa Sno Cream limebomolewa na kuna jengo jipya linajengwa. Niliambiwa Sno Cream walishahama pale siku nyingi.

Kundi la watu wenye uzoefu wa kuwasoma watu “wanaoshangaa” ni machinga wanaorandaranda jijni Dar es Salaam wakiuza bidhaa mbalimbali. Miaka kadhaa iliyopita nilitembelea Dar es Salaam na nilikuwa nimekaa na rafiki zangu wa siku nyingi sehemu ya vinywaji na chakula inayoitwa George’s Grill. Machinga aliingia pale akiuza vitu na alikuja moja kwa moja kwangu akijaribu kuniuzia bidhaa. Nilimuuliza: ‘”Mimi fala? Katika watu wote waliokaa hapa umeona mimi ndiyo nafaa kuwa mteja wako?”

Yule machinga alijibu: “Hapana, siyo hivyo mzee”, akionekana kujizuwia kucheka.

Baada ya kuondoka Dar na kuisha kijijini kwa muda mrefu ni dhahiri kuwa nina mueleko ambao ni tofauti na wa wakazi wa Dar es Salaam, hasa  wale niliokaa nao meza moja. Yule machinga aliiona hiyo tofauti (labda kwa mavazi yangu) na akanilenga mimi moja kwa moja. Hainisumbuwi, lakini ndiyo hali halisi.

Mwanzoni mwa mwaka huu nilionana na mwanafunzi mwenzangu wa siku nyingi tuliyesoma naye Chuo cha Elimu ya Biashara (Shycom) miaka iliyopita. Anasema enzi hizo, miaka 33 iliyopita, sisi wanafunzi wa Shycom kutoka Dar tulionekana wajanja sana kuliko wanafunzi wengine ambao walitokea maeneo mengine ya Tanzania. Leo nimegeuka mawindo ya machinga.

Monday, July 4, 2011

"Wagumu" wa Mlima Kilimanjaro

Mgeni yoyote anayepanda mlima Kilimanjaro anahitaji huduma ya waongoza msafara, wapishi, na wabeba mizigo. Hili kundi la mwisho wanajulikana kama “wagumu” kwa sababu ya ugumu wa kazi wanayofanya ya kumbebea mgeni vitu muhimu vinavyohitajika: mahema, chakula, maji, na vifaa vingine vya lazima.
Mgumu (kushoto) akiwa na mzigo wake baada ya kumpita Muongoza Msafara (mwenye kofia nyekundu) anayeongoza mgeni aliye nyuma yake.
Asubuhi wao huamka mapema kuandaa kifungua kinywa kwa wageni wakishirikiana na mpishi. Baada ya kifungua kinywa Muongoza Msafara (ambaye naye huanza kazi kama mbeba mizigo kwa miaka kadhaa) huongoza msafara wa wageni kuelekea kwenye kambi inayofuata. Msafara wa kukwea Mlima Kilimanjaro unaweza kuchukuwa kati ya siku 5 hadi 12, kutegemea na njia inayotumika.

Baada ya msafara kuondoka kambini, wagumu huvunja kambi na kufungasha mahema na mizigo mingine yote na kuanza safari ya kuelekea kambi inayofuata. Kwa kuwa ni wazoefu wa kubebea mzigo, huupita msafara wa wageni na Muongoza Msafara na msafara unapofika kwenye kambi wageni wanakuta wagumu wameshasimika upya mahema yote, na mpishi anakuwa tayari ameshapika chakula cha wageni. Wanafanya hivi kila siku ya msafara.
 
Wagumu wanayo sifa ya kutumia pesa inayotokana na kazi yao ya kusindikiza wageni kupanda Mlima Kilimanjaro kwa fujo. Dada mmoja mhudumu wa baa moja ya mjini Moshi aliniambia baadhi yao wanapolipwa pesa yao huhamia baa mpaka pesa iishe. Pesa inapoishia kwenye pombe, wengine hujisababishia majeraha ya mwili na kudanganywa wake zao kuwa wameporwa malipo yao na vibaka.
Wagumu wa Kilimanjaro wakifurahia siku ya mwisho ya msafara katika Kambi ya Mweka.
 Hii ndiyo baadhi ya mikasa ya wagumu wa Kilimanjaro.
Wagumu wa Kilimanjaro wakifurahia siku ya mwisho ya msafara katika Kambi ya Mweka.

Wageni wa Butiama: Ujumbe wa VETA - Shinyanga wamtembelea Mama Maria Nyerere

Hivi karibu walimu wa VETA Shinyanga walitembelea Butiama na kufika kumsalimia Mama Maria Nyerere. Ujumbe wa watu watatu ulijumuisha Machumu K. Machumu (Mratibu wa Mafunzo), Miharano M. Ismail (Mwalimu wa Udereva), na Edwin Tahani (Mwalimu wa Mitambo).
Kwenye picha, kutoka kushoto, ni Miharano Ismail, Machumu K. Machumu, Mama Maria Nyerere, na aliyesimama ni Edward Tahani ambaye ni baba mzazi wa Edwin Tahani ambaye haonekani kwenye picha. Edward Tahani anafanya kazi Butiama.

Mtanzania Mohamed Sakara aliyedhaniwa amekufa nchini Blugaria yu hai, anatafuta ndugu zake

Miezi michache iliyopita nilipokea barua pepe kutoka Bulgaria ikiniarifu kuwa kuna Mtanzania anaitwa Mohamed Sakara aliyedhaniwa amekufa lakini ilibainika kuwa yu hai na habari zake zikaandikwa kwenye gazeti moja la huko Bulgaria. 

Picha za hivi karibuni za Mohamed Sakara, akiwa jijini Sophia, nchini Bulgaria.
Raia wa Bulgaria aliyesoma hizo habari aliniandikia barua pepe kuniomba nijaribu kuwatafuta ndugu zake Sakara huku Tanzania. Nilituma hizo taarifa kwa mwanablogu Muhidini Michuzi lakini sina hakika kama zilitoka kwenye blogu yake.

Kwa kifupi Sakara alienda nchini Bulgaria kwenye miaka ya 1980 kusomea uhandisi, lakini hali ilimuendea vibaya mpaka kujikuta hana uwezo kabisa wa fedha na akiishi kwa shida mitaani. Angependa kurudi Tanzania lakini hana uwezo wa kujilipia nauli. Inasemekana baada ya kutangazwa amekufa, ndugu zake hawakuendelea kumtafuta, lakini ukweli ni kuwa yuko hai. Taarifa zake nyingine ni:
  • Amezaliwa mwaka 1961
  • Inakisiwa alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1982 - 1984 halafu akaenda Bulgaria ambako alikuwepo mpaka kipindi napata taarifa hizi
  • Anatoka kwenye familia ya watoto 8
  • Taarifa za kaka yake Abeid Hassan Sakara ni: amezaliwa mwaka 1954; ameandika kitabu "Jizoeze Kiswahili", na "Rashid Mfaume Kawawa"; alikuwa mkuu wa kitengo cha uchapishaji cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (Dar es Salaam); alikuwa akiishi Upanga Mashariki, Mtaa wa Maweni, Na.244, lakini hajulikani alipo kwa sasa.
Yoyote anayemfahamu Mohamed Sakara au ndugu zake awasiliane na mimi ili nimpe anwani ya aliyenitumia taarifa hizi toka Bulgaria.

Lugha Yetu Kiswahili: Kwa matumizi haya, Kiswahili kitaangamia


Suala moja ambalo linajidhihirisha mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni ni matumizi mabaya ya lugha ambayo yamejikita katika mazungumzo na hata maandishi ya kila siku ya lugha ya Kiswahili.

Mimi naamini mtu yoyote anayefahamu lugha yake, au anayetaka kulinda matumizi sahihi ya lugha yake hawezi kupuuza matumizi sahihi ya lugha, lakini kwa mwenendo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ulivyo siku hizi, hasa kwa vijana, Kiswahili kina wakati mgumu na uwepo wake uko hatarini.

Mimi nakubaliana na wanaosema kuwa kuna ulazima wa lugha kubadilika na msamiati kuongezeka kila muda unavyozidi kupita. Lakini siyo kwa mtindo huu wa sasa ambapo maneno sahihi yanageuzwa kuwa maneno yasiyo sahihi, na misemo isiyofaa kutumika hata kwenye vyombo vya habari. Nitoe mifano michache:

Vijimambo: Hili neno nimewahi kusikia watu wazima wakilizungumza. Ni afadhali ingekuwa vijana peke yao kwa kuwa wao wanajulikana kwa kutunga maneno mapya. Kwa uelewa wangu mimi lina maana ya mambo kadha wa kadha ambayo msemaji hawezi kuyaweka bayana na hutumia neno hilo kufunika hayo asiyoweza au asiyotaka kuyasema kwa wakati ule. Ushauri wangu ni kuwa kama huwezi kulisema inawezekana halistahili kusemwa.

Ndivyo sivyo: Huu msemo nimeusikia ukitumika na baadhi ya wanahabari na nashindwa kabisa kuelewa mwanahabari anawezaje kuacha kutumia lugha ambayo inaweka wazi maana anayokusudia badala ya msemo unaomlazimu msikilizaji kukisia maana inayokusudiwa.

Kudadeki: Kwa kadiri ninavyofahamu mimi chimbuko la hili neno ni tusi la nguoni na limeingia katika matumizi ili kuepuka mtumiaji kusema lile tusi lenyewe. Cha ajabu ni kuwa nimeshasikia tangazo kwenye redio la kampuni moja ya simu wakitumia neno hilo. Kama linatumika kwenye tangazo muda si mrefu litakuwa kwenye matumizi ya kawaida ya lugha. Ukiuliza maana yake sidhani kama wengi wa wanalolitumia wanafahamu kwa uhakika, lakini mimi naamini kuwa hili neno linatokana na tusi zito tu.

Kwa mtindo huu, Kiswahili kitapona?