Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, September 4, 2012

Katiba mpya itamke lugha rasmi ya bunge kuwa Kiswahili

Kama kuna kundi liliojijengea utaalamu wa kuvuruga lugha ya Kiswahili, kundi hilo ni la viongozi wa kada mbalimbali hapa Tanzania. Na vinara zaidi wa kuivuruga lugha ya Taifa ni wabunge wetu.

Ukisikiliza mjadala wa Bunge la Muungano ni vigumu kupita dakika kumi bila anayeongea kutumia neno la Kiingereza ndani ya mjadala unaoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya watu wameipachika jina tabia hii ya kuchanganya lugha za Kiingereza na Kiswahili kuwa ni kuongea kiswanglish, neno lisilo rasmi kwenye lugha zote mbili.

Kuna dhana potofu miongoni mwa viongozi wetu wa sasa kuwa unapochanganya mazungumzo kwa kutumia maneno ya Kiingereza kwenye mazungumzo yako, basi wewe unaonekana kuwa ni mtu msomi. Na utakuta viongozi hawa hawa hata kwenye maandishi yao wanaweza kutumia neno la Kiswahili halafu kwenye mabano wanatoa fasili ya neno hilo hilo kwa lugha ya Kiingereza, kama vile kuwakumbusha wale wanaosoma maelezo yao kuwa wasisahau kuwa wao ni wasomi.

Jambo moja dhahiri ni kuwa ni Watanzania wachache sana wanaoelewa hayo maneno ambayo viongozi wetu, katika jitihada za kukogana wao kwa wao, wanayoyatumia kwenye maandishi na matamshi ikiwa ni pamoja na kwenye mijadala, mikutano, na kwenye vyombo vya habari.

Naamini umewadia wakati kwa lugha ya Kiswahili kutamkwa kuwa ndiyo lugha rasmi ya kutumika ndani ya Bunge la Muungano. Haileti mantiki kwa mwananchi aliyepiga kura kumchagua mbunge asielewe anachojadili mbunge wake.

Sunday, September 2, 2012

Dk. Kenneth Kaunda, rais mstaafu wa Zambia

Mwezi Juni 2007 nilialikwa jijini London, Uingereza, kwenye uzinduzi mpya wa Azimio la Arusha na nikafikia kwa wenyeji wangu, Selma James na Nina Lopez, wote ambao hawali nyama. Nikiwa natokea kwenye kabila ambalo ukizungumzia "chakula" ni sawa sawa na kutamka "nyama" na ambapo mboga za majani zinaliwa na mifugo peke yake, zile siku kumi nilizokaa London nikila mboga za majani zilikuwa ni mtihani mkubwa kwangu.

Nilimudu kwa jitihada kubwa kuishi hizo siku kumi bila kula nyama na niliporudi Tanzania watu walioniona walisema kuwa nilionekana kijana kuliko ninavyostahili. Nilihisi kuwa yawezekana kuwa kulishwa mboga za majani kwa siku kumi bila hiari yangu nikiwa London ndiyo kulisababisha mimi kuonekana kijana.

Imani yangu kuwa ulaji wa mboga za majani kwa siku kumi ndiko kulisababisha kupunguza kuzeeka kwangu ilinisukuma kuacha kula nyama na nikaanza jitihada ya kuwa mlaji mboga za majani tu na kuacha kula aina zote za nyama.

Mwaka mmoja baada ya hapo, nikiwa kwenye mkutano jijini Maputo, Msumbiji, nilipata fursa ya kuonana na  Dk. Kenneth Kaunda, rais mstaafu wa Zambia ambaye ni maarufu pia kuwa mtu ambaye hali nyama.
Rais mstaafu wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, kulia.
Aliniambia aliacha kula nyama mwaka 1952 kupinga sera za kibaguzi za serikali ya kikoloni ya Waingereza iloyoelekeza wamiliki wa bucha kuweka madirisha mawili tofauti ya kuwauzia nyama Waafrika na wazungu. Yeye hanywi pombe, kahawa, wala chai lakini anakunywa maji ya matunda kila siku.

Kitendo hicho cha upinzani wa kisiasa kinaelekea kufanikisha kupunguza idadi kubwa ya miaka ya huyu rais mstaafu mwenye umri wa miaka 88. Ni mwingi wa nguvu na mchangamfu sana. Kwenye mkutano Maputo kila alipoitwa kwenye jukwaa alienda kwa mchakamchaka.

Mtanziko mkubwa unaonikabili, mkubwa zaidi kuliko uamuzi wa kuacha kula nyama, ni kipi kitakachofuata kuacha kula kati ya samaki na kuku.

Tuesday, August 28, 2012

Hatimaye, watu wa sensa hawa hapa

Jumapili, tarehe 26 Agosti, nilikaa nyumbani siku nzima nikisubiri kuhesabiwa kwenye Sensa ya Taifa lakini sikuona mtu hata mmoja kuja kuniuliza swali. Hatimaye leo maafisa wa sensa ya Taifa wamefika kunihoji maswali yao 62, ambayo kila mshiriki anapaswa kuyajibu.

Wengi wetu hatukukumbuka kuwa ni zoezi la juma zima.
Mimi, kushoto, nikijibu maswali ya Sensa ya Taifa leo asubuhi. 
Ndani ya muda wa dakika kumi zoezi lilimalizika na wakaondoka.

Pamoja na kwamba wengine tulikuwa na shauku kubwa ya kukamilisha kazi hii kuna Watanznia wenzetu ambao kabla ya zoezi hili kuanza wamekuwa wakiendesha kampeni ya wazi kuhimiza Waislamu wasishiriki kwenye sensa kwa sababu maswali yale 62 hayaulizi dini ya anayehesabiwa.

Nimejaribu kuuliza hili swali lakini mpaka leo sijasikia jibu lake: tunataka kujua kuna Watanzania wangapi wa dini mbalimbali ili tutumie hizo takwimu kufanya nini? Mwenye jibu naomba anifahamishe.

Sunday, August 26, 2012

Wageni wa Butiama: Agustino Lyatonga Mrema

Butiama inatembelewa na wageni wengi, baadhi yao mashuhuri, lakini wengi ambao siyo mashuhuri. Wengi wa wageni mashuhuri waliowahi kutembelea Butiama walifika hapo kwa sababu ya kumtembelea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mmojawapo wa hao wageni ni Mhe. Agustino Mrema ambaye amewahi kufika Butiama mara kadhaa. Katika picha hii anaonekana akisalimiana na Mwalimu Nyerere mwaka 1997 wakati wa msiba wa Bibi Mugaya wa Nyang'ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere.

Friday, August 24, 2012

Mada yangu ya leo: Muungano una manufaa

Pamoja na kuwepo malalamiko mengi juu ya muungano uliounganisha Unguja na Tanganyika na kutoa Tanzania, tushukuru kuwepo kwa muungano huu kwa kutuepusha na majanga mengi.

Na wanaopaswa kushukuru zaidi ni Watanzania wa upande ulioitwa Tanganyika kabla ya tarehe 26 Aprili 1964, siku ulipozaliwa Muungano.

Bila Muungano kusingekuwepo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Bila shaka ingekuwepo JWTZ lakini labda ingekuwa ni Jeshi la Wananchi wa Tanganyika.

Leo hii, makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanganyika wangekuwa wakikuna vichwa kutafakari namna ya kupambana na nchi mbili: Malawi na Zanzibar. Yote hii kutokana na kutokuafikiana kwa pande mbili za Muungano kuhusu mgawanyo wa mapato yatakayotokana na mafuta yanayokisiwa kuwepo ndani ya mipaka ya Tanzania kwenye eneo la Bahari ya Hindi, na pia kutokana na madai ya Malawi kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa ni mali ya Malawi, ikiwa ni suala linaloibuliwa na kuwepo kwa uwezekano kuwa kuna shehena kubwa ya mafuta chini ya Ziwa Nyasa. Tanzania haitambui madai hayo ya Malawi na kubainisha kuwa mpaka kati yao upo katikati ya Ziwa Nyasa.

Kwa bahati nzuri Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, ametamka hivi karibuni kuwa mgogoro kati ya Malawi na Tanzania juu ya mpaka wa Ziwa Nyasa hautahusisha vita na kuwa utamalizwa kwa njia za kidiplomasia.

Lakini hapa tusisahau kuwa hata majeshi ya Idi Amin yalipovamia maeneo ya Tanzania mwaka 1978 Serikali ya Tanzania ilifanya jitihada kubwa za kutatua ule mgogoro kwa njia za kidiplomasia. Zile jitihada hazikufaulu kumaliza mgogoro na matokeo yake Tanzania na Uganda zikaingia kwenye vita ambayo ilileta madhara makubwa kwa pande zote mbili.

Hasara ya Uganda: gari la kijeshi lililoteketezwa na majeshi ya Tanzania ndani ya eneo la Tanzania kwenye mji mdogo wa Mutukula.
Na kwa uhakika kwa sababu ya Muungano, mgogoro kati ya Tanzania Visiwani na Tanzania Bara hautahusisha vita. Bila hivyo zingepigwa mpaka mmoja aelewe hoja ya mwenzake. Anaesema Muungano hauna faida yoyote atafakari tena.