Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, October 1, 2012

Mwanafunzi wa kidato cha nne afika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Mwanafunzi Placidia Prudence wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto ya jijini Mwanza ambaye alikuwa kwenye msafara wa kukwea Mlima Kilimanjaro amefanikiwa kufika kilele cha mlima huo tarehe 28 Septemba 2012.

Nami nilikuwa kwenye msafara huo ambao ulishirikisha wanafunzi wengine 15 toka shule hiyo pamoja na walimu watatu. Katika wote tulioshiriki ni yeye peke yake alifanikiwa kufika kileleni ambako alifika akiongozana na muongozaji Entold Mpunga.
Placidia Prudence akiwa kwenye kambi ya Horombo baada ya kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Kushoto, juu, unaonekana Mlima Kilimanjaro.
Mwanafunzi Nusra Alkarim, mwalimu wa michezo Isack Katambi, na mimi tulifanikiwa kufika Gillman's Point, mita 5,685 juu ya usawa wa bahari na kiasi cha mwendo wa kama saa moja na nusu toka kilele cha Uhuru alikofika Placidia. Kilele cha Mlima Kilimanjaro kina urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari.

Msafara huo ulipangwa kwa madhumuni ya kuchangisha pesa za mradi wa kuboresha na kufikisha maji safi na salama kwenye shule ya Loreto.

Placidia ana umri wa miaka 20 na ameniarifu anakusudia kuwa mhandisi.

Sunday, September 23, 2012

Pambano la ndondi Oktoba 14 kumuenzi Mwalimu Nyerere

Mabingwa wa uzito wa kati (kilo 72.5) wa Uganda na Tanzania wanaotambuliwa na Tanzania Professional Boxing Organization (TPBO) watapambana tarehe 14 Oktoba mwaka huu Friends Corner Bar, Manzese, Dar es Salaam katika pambano lilioandaliwa kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki zaidi ya miaka 12 iliyopita.

Pambano hilo litawapambanisha bingwa wa Tanzania Thomas Mashali, juu, na bingwa wa Uganda, Med Sebyala, chini.


Mchezo huo utakuwa wa kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki.

Bondia Sebyala ameshawahi kupambana na kushindwa kwa pointi na bondia Francis Cheka, bingwa wa mabara wa Afrika anayetambuliwa na International Boxing Federation (IBF). Aidha, ameshawahi kupambana na Rashidi Matumla na ingawa mapambano yote alishindwa kwa pointi, alitoa upinzani mkali kwa mabondia hao Watanzania.

Bondia Mashali anayo sifa ya kutoa vichapo vikali kwa wapinzani wake na kuwapumzisha kwa knock-out za mapema.

Taarifa kutoka TPBO zinaeleza kuwa kwa kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuthamini juhudi zake za kuendeleza michezo TPBO itaandaa mapambano ya ngumi kwenye kila maadhimisho ya kifo chake tarehe 14 Oktoba.

Friday, September 21, 2012

Twist mpaka chini: harusi za Tanzania zinafanana sana

Sijui ni hisia zangu tu, lakini nahisi kama mtiririko wa ratiba za harusi ninazohudhuria siku hizi zinafanana sana.

Kwenye harusi nilizohudhuria hivi karibuni nimeshuhudia kuna wakati wa kuita kamati iliyoandaa harusi na kila mwanakamati hujitambulisha. Salama ipo kama wanakamati bado hawajachangamka kwa vinywaji vinavyoondoa aibu mbele ya kadamnasi. Lakini kama wanakamati wameshachagamka mambo huwa hayatabiriki.
Mara wanapomaliza kujitambulisha na kueleza mambo waliyofanya kufanikisha harusi, basi muongozaji wa sherehe anaagiza DJ aweke twist ya uhakika.

Na mara zote nimeshuhudia kuwa wimbo unaopigwa ni ule ule. Uchezaji nao ni ule ule, haujabadilika tangu miaka ya hamsini ingawa silalamikii uchezaji nao ubadilike.

Monday, September 17, 2012

Msondo Ngoma bado wanatamba

Wapiga gitaa wa bendi ya Msondo Ngoma Abdul Ridhiwani, kushoto, na Zahoro Bangwe, kulia,
wakiburudisha mashabiki wao hivi karibuni wakati bendi hiyo ilipotumbuiza kwenye ukumbi wa Max Bar, Ilala Bungoni, Dar es Salaam.

Msondo Ngoma ni moja ya bendi kongwe za muziki wa dansi za Tanzania. Zamani ilikuwa inaitwa NUTA Jazz.

Picha na habari zimetolewa na Rajabu Mhamila.

Sunday, September 16, 2012

Mada yangu ya leo: polisi na waandamanaji

Kuna mambo mawili muhimu yanajitokeza baada ya kuuwawa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten wa Iringa, Daudi Mwangosi, tarehe 2 Septemba 2012. Kwanza, Jeshi la Polisi, ambalo mmoja wa askari wake ameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, linahitaji kutoa mafunzo maalum ya namna polisi waliyopo kwenye eneo la maandamano wanavyopaswa kusimamia suala la amani katika maandamano.

Siyo kila tukio la mkusanyiko wa watu linahatarisha mali au maisha ya raia, kwa hiyo ni dhahiri pia kuwa siyo lazima kila mara kutumia nguvu zisizokuwa za lazima dhidi ya raia. Polisi wanafunzi wanapaswa kupewa elimu inayojenga taswira kuwa anaepinga serikali iliyoko madarakani siyo lazima pia awe ni adui wa Taifa au anaetishia usalama wa Taifa.

Picha inayojitokeza baada ya baadhi ya matukio ambapo polisi wameua raia ni kama vile kazi kuu ya polisi ni kuhakikisha kuwa upinzani halali wa kisiasa unaminywa kiasi cha kutosha na kuondoa kabisa uwezekano wa serikali iliyopo madarakani kuondolewa madarakani kwa njia za kidemokrasia.

Polisi wapate mafunzo kuwaelimisha kuwa kazi yao siyo kulinda maslahi ya kisiasa ya serikali iliyopo madarakani, na wafunzwe kukubali uwezekano kuwa chama chochote kilichopo upande wa upinzani kinaweza hatimaye kushinda uchaguzi na kuongoza serikali.

Jambo la pili na ambalo ni muhimu sana ni kuwa sasa waandishi wa habari wapate mafunzo ya namna ya kukusanya habari kwenye maeneo yenye usalama mdogo ili kupunguza tishio kwa usalama na maisha yao. Polisi anafanya kazi kwa amri, na kuna mazingira mengi ya kisheria yanayomruhusu polisi kutumia silaha kwa jinsi ambavyo anaona ni sawa kutokana na mazingira yanayomkabili. Polisi anayefukuzwa na kundi la waandamanaji ambao anaamini wanakusudia kumuua hatasita kutumia silaha yake dhidi ya kundi hilo. Huu ni mfano tu; haya sidhani kama ni mazingira yaliyotokea kwenye tukio lilisobabisha kifo cha Daudi Mwangosi.

Jambo la msingi ni kuwa, hata pale ambapo tunajua tunayo haki, si busara hata kidogo kubishana na mtu ambaye ameshika silaha na anaamini kuwa anatekeleza amri halali aliyopewa na mkubwa wake. Na hili haliwezi kubadilika mpaka itolewe elimu ambayo itambadilisha polisi Mtanzania ili atumie mbinu tofauti kukabiliana na waandamanaji.