Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, May 28, 2011

Habari Njema Kwa Watu Wote

Siku chache zilizopita nilipokea barua pepe yenye kichwa cha habari, “Habari Njema Kwa Watu Wote” kutoka kwa mtu ambaye jina lake ninahifadhi kwa sababu nitakazofafanua, ambaye amejitambulisha kama mtaalamu wa tiba za jadi. Anadai kuwa na utaalamu wa tiba za jadi na uwezo wa “kutibu matatizo mbali mbali kwa kutumia makarama ya kiuchawi, kutatua matatizo yanayosumbua mwanadamu na yakaisha kabisa…”

Sababu moja ya msingi inayonisukuma kuhifadhi jina la 'mtaalamu' huyu ni kuwa shughuli za uchawi haziruhusiwi kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, kwa hiyo ili kutupunguzia yeye na mimi uwezekano wa kujikuta tunasaidia polisi kwenye uchunguzi nimeona ni bora abaki bila jina.

Katika barua pepe hiyo ameorodhesha matatizo 43 ambayo ana uwezo wa kuyamaliza. Nasema anayamaliza kwa sababu siyo yote ni maradhi. Mfano, anaweza “kutatua matatizo ya sehemu yako ya kazi, kama kutoelewana na bosi.” Kama hupandi cheo kazini anao uwezo wa kukupandisha. Jambo la hatari ambalo ana uwezo wa kufanya ni “kulipa kisasi kwa mbaya wako.”

Anaonekana kuwa na uwezo wa kipolisi na wa kimahakama kwa mpigo. Mfano, anaweza kurejesha mali iliyoibiwa. Aidha, anaweza kumaliza kesi mahakamani. Ni mshauri wa mavazi pia: anaweza "kutabiri nyota na nguo za kuvaa kuanzia Jumatatu hadi Jumapili." Mengine ni pamoja na uwezo wa kuwanasa wanga na wachawi, na uwezo wa "kutengeneza jini wa shari na kumtuma katika mambo ya shari."

Pamoja na mambo hayo anajitangaza kuwa na uwezo wa kutibu pia matatizo ya kiafya, mfano, matatizo ya uzazi kwa kina mama, kupungua nguvu za kiume, maradhi ya masikio, pumu, kichwa, tumbo, n.k.

Hivi karibuni, baada ya kuandamwa kwa Babu wa Loliondo kuwa anadanganya na kuwa hatibu ila anadanganya, niliandika makala kumtetea nikeleza jinsi gani watafiti wa nchi moja ya Ulaya walibaini katika utafiti kuwa inawezekana kumdanganya mgonjwa kuwa anapata dawa ya kutibu ugonjwa fulani, naye akapona akiamini kuwa amepewa dawa kumbe kapewa peremende tu inayofanana na dawa halisi. Katika mazingira hayo mgonjwa anapona kwa sababu anamuamini daktari anayempa ile dawa feki, na kuamini kuwa ni kweli anapewa dawa.

Katika makala niliyoandika nilihoji kama ni kweli kuwa Babu wa Loliondo anadanganya lakini watu wanapona kwa imani kuwa wanapewa dawa inayoponyesha basi hilo lisiwe tatizo la mtu yoyote ambaye hana mpango wa kwenda Loliondo. Kwa mantiki hiyo, ningemtetea hata huyu ‘mtaalamu’ wa kutibu zaidi ya 43, lakini nasita.

Labda tofauti ya msingi hapa kati ya huyu mtaalamu na Babu wa Loliondo ni kuwa Babu hakutangaza kama anatumia nguvu za uchawi – ingawa kuna baadhi ya watu wanasema kuwa anafanya hivyo.

Tuesday, April 26, 2011

Mwalimu wangu, Gordian Mukiza

Mwaka jana, wakati vuguvugu za kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea nchini kote, nilifunga safari kwenda Muleba, Kagera, kumtembelea rafiki yangu Hamisi Millanga, aliyekuwa kwenye mikakati ya kutetea kiti chake cha udiwani wa kata ya Muleba kupitia Chama cha Wananchi (CUF). Safari yangu ilikuwa na nia ya kupata muelekeo wa harakati za kampeni kwenye maeneo hayo.
Mwalimu Gordian Mukiza, kushoto, na mimi.
Siku moja katika pitapita zangu mjini Muleba nilikutana na mwalimu wangu wa siku nyingi nilivyokuwa mwanafunzi wa Shycom (Shinyanga Commercial Institute) kati ya mwaka 1977 – 1979, Mwalimu Gordian Mukiza. Aliyenitambua ni yeye, pamoja na kuwa nimesheheni mvi kibao kichwani na pengine sifanani hata kidogo na nilivyokuwa Shycom.

Aliniambia kuwa alikuwa mgombea wa udiwani wa kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Alishinda uchaguzi huo kwa kishindo, na matokeo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wapiga kura waliyoandikishwa: 2,553
Waliyopiga kura: 1,685
Kura zilizoharibika: 64

Kura za Wagombea:
CHADEMA - Amri Kalizabona Hamisi : 254
CUF - Felician Rutwaza:                   400
CCM - Gordian Joseph Mukiza:          967

Wednesday, March 9, 2011

Msanii Hardman ateuliwa katika Tuzo za Muziki za Kilimanjaro

Kwa mujibu wa taarifa iliyopokelewa toka kampuni ya Maisha Music, msanii wake, Hardman, ameteuliwa kushindania Tuzo ya Muziki ya Kilimanjaro Kilimanjaro,
Bango la Hardman la uzinduzi wa album yake, Imebaki Stori, uliyofanyika Desemba 2010
Taarifa hiyo pia inatoa wito na maelekezo kwa mashabiki wa Hardman kumpigia kura ili aweze kushinda.
Taarifa kamili hii hapa: 
Toleo hili la barua taarifa limejikita zaidi juu ya uteuzi wa Hardmad ni msanii wa reggae na dancehall ambaye kwa sasa anasimamiwa na kampuni ya Maisha Music. Katika tuzo za mwaka huu amefanikiwa kuteuliwa katika vipengele viwili navyo ni; kipengele cha wimbo bora wa reggae ambapo ameingiza ameingiza nyimbo mbili, na kipengele kingine ni kile cha wimbo bora wa kushirikishwa, na ni kutokana na kushirikishwa kwake katika wimbo wa Mwana FA na AY “Dakika Moja”.  

Haya ni mafanikio makubwa kwetu pamoja na Hardmad, na tunaamini kuwa hii imetokana na kujituma kwake kwa bidii pamoja na ushirikiano baina yetu. Sisi tunamtakia kila la heri katika tukio hili muhimu kwa maisha yake kama msanii. Maisha Music inapenda pia kuwatakia mafanikio marafiki zetu wengine ambao wamo katika kinyangányiro hiki mwaka huu, baadhi yao ni Jhikoman, Warriors From The East, Ras Rwanda, Lamar, Fid Q, Ray C na Chidi Beenz.

Washindi wa tuzo za Kilimanjaro wanapatikana kwa kupiga kura. Hii inamaanisha kwamba wimbo utakaopata kura nyingi kutoka kwa mashabiki na wapenzi ndiyo utakoshinda. Tafadhali mpigieni Hardmad kura zenu kwa wingi ili aweze kufanikiwa kuibuka kidedea kwani tunaamini anastahili na unaweza kuthibitisha kwa kusikiliza kazi zake kupitia katika linki zilizowekwa hapo chini.

Unaweza kumpigia kura kwa njia mbili tofauti ambazo ni; kwa kubonyeza katika linki iliyoonyeshwa hapo chini na pili ni kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu. Iwapo utaweza basi unayo ruhusa ya kutumia njia zote mbili. Angalizo: Kwa kuwa Hardmad ana nyimbo mbili katika kipengele kimoja tunapendda kuwashauri wadau wetu kuupigia kura wimbo wa Ujio Mpya ambao amemshirikisha Enika. Vinginevyo kunaweza kuwa na uwezekano wa kura kugawanyika katika nyimbo mbili.

Katika wimbo wa Ujio mpya tumeshangaa kuona kuwa limeongezwa jina geni la msanii ambaye hatumfahamu (BNV). Tunadhani kuna makosa
yamefanyika na tunajaribu kuwasiliana na wahusika ili kuona namna ya kuliondoa.

Namna ya kupiga kura:

KWA MTANDAO (rahisi sana): 

Gonga kwenye linki hii: http://www.kilitime.co.tz/awards/2009/nominees_2007.php (Na ni kwa mwaka 2011), na ikifunguka gonga kwenye nyimbo unazotaka kuzipigia kura, andika anuani yako ya barua pepe na bonyeza “VOTE”. Kumbuka kubonyeza katika linki ya kuhakiki na utatumiwa barua pepe ya kutoka KTMA (Kilimanjaro Tanzanian Music Awards), vinginevyo kura yako haitasajiliwa! Unaweza kupiga kura moja tu kwa anuani moja ya barua

SIMU:

"Wimbo bora wa Reggae":

Andika K179 katika ujumbe mfupi na tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "Ujio Mpya - Hardmad Feat. Enika" 
Andika K186 katika ujumbe mfupi na tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "What you feel inside - Hardmad"

(Unaweza kupiga kura moja tu katika kila kipengele kwa kila namba ya simu).

"Wimbo bora wa kushirikishwa:

Andika W137 kwa ujumbe mfupi na kisha tuma kwa namba 15747 ili kuupigia kura wimbo wa "Dakika Moja - Mwana FA & AY feat. Hardmad" 

Tunakushukuru sana kwa ushirikiano wako na msaada ambao tunaamini utaweza kumfikisha Hardmad katika kilele cha mafanikio anayostahili. Tuna matarajio ya mengi mazuri katika harakati za kimuziki kwetu pamoja na wasanii tunaoshirikiana nao. Kwa ufafanuzi zaidi unaweza kusikiliza na kuangalia baadhi ya nyimbo katika Myspace au Youtube au kwenye kurasa za Hardmad katika mitandao ya Facebook na Myspace. Albamu mpya ya Hardmad “Imebaki Story” kwa sasa inapatikana pia kwa njia ya mtandao, na unaweza kuipata kwa kubonyeza hapa kwa Itunes pamoja na maduka mengine ya kwenye mtandaoni. 

Hivi sasa Maisha Music ipo katika maandalizi ya maonyesho kadhaa ya utambulisho wa albamu ya Hardmad katika miji mbalimbali hapa Tanzania pamoja na Kenya mwezi wa Aprili. Taarifa sahihi pamoja na tarehe zitatangazwa muda si mrefu.

Tafadhali tusaidie kusambaza taarifa hii kwa wapendwa, marafiki pamoja na wadau wengiine wa muziki!

Kila la heri na asante sana kutoka
Timu ya MAISHA MUSIC

Saturday, February 5, 2011

Kuahirishwa kwa Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha

Taarifa iliyotolewa na Sabatho Nyamsenda, Mwenyekiti wa Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA) inaeleza kuwa kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha lililokuwa lifanyike leo asubuhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam limeahirishwa.

Sababu ya kuahirishwa imeelezwa kuwa ni "kukosekana kwa hali ya utulivu katika mazingira ya chuo." Taarifa katika vyombo vya habari zinaeleza kuwa jana wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipambana na polisi baada ya kujaribu kuandamana kuelekea Ikulu Dar es Salaam kupeleka madai ya kuongezewa posho.

Taarifa ya Nyamsenda haijaeleza ni lini hilo kongamano litafanyika. Taarfia zaidi zinaweza kupatikana kwa Sabatho Nyamsenda 0717 34070/0784 641031.

Wednesday, February 2, 2011

Kongamano la Azimio la Arusha Jumamosi tarehe 5 Februari 2011

Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha

Siku: 
Jumamosi tarehe 5 Februari 2011

Muda: 
Saa 3:30 Asubuhi mpaka saa 8:00 Mchana

Mahali: 
Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Kauli Mbiu: 
"Tafakuri ya kina juu ya Azimio la Arusha. Je, lina nafasi katika mjadala wa katiba mpya?"

Mtoa mada: Prof. Issa G. Shivji

Waandaaji: 
Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA - UDSM) & Philosophy Club

Mawasiliano: 
0717 34070/0784 641031 (Sabatho Nyamsenda), na 0713 415001 (Hatib Yusuph)