Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, July 14, 2011

Mbio za Mwenge wa Uhuru kuanzia Butiama mwaka huu

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa muda mrefu kidogo uliyopita, mbio za Mwenge wa Uhuru zitaanza kijijini Butiama tarehe 14 Oktoba mwaka huu, na kumalizika Dar es Salaam. Tarehe 14 Oktoba ni maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Nyerere, siku aliyofariki Mwalimu Nyerere mwaka 1999.
Dk. Nassoro Matuzya, kiongozi wa mbio za mwenge 2010 akipandisha Mwenge wa Uhuru eneo la Mwitongo wakati wa mbio za mwenge mwaka jana.
Vyanzo vyangu vya habari vinaniambia kuwa awali sherehe hizi zilikuwa zifanyike Mbeya na pesa za maandalizi zilishatumwa huko. Baada ya uamuzi wa kuhamishia sherehe kuja Butiama taarifa zinaeleza kuwa pesa zilizokwishatumwa Mbeya hazikuweza kupatikana kwa sababu, kwa mujibu wa Serikali mkoani Mbeya, pesa hizo tayari zilikuwa zimeshatumika kwa maandalizi. Hii imeilazimu Serikali kutafuta upya pesa za kugharamia sherehe za Butiama.

'Muhunda' aonekana Butiama


Hivi karibuni, siku chache baada ya mazishi ya mwanafamilia, alionekana nyani mkubwa akikatisha kwenye baadhi ya maeneo ya kijiji cha Butiama.

Nilipata taarifa za kuonekana kwa nyani huyo baada ya kuulizwa: “Umemuona Muhunda?”

“Muhunda?”

“Ndiyo, ametutembelea.”

Wakati napokea taarifa hiyo, mbwa walikuwa wakibweka ovyo, mithili ya mbwa mwitu.

Kuna Muhunda wawili tu ninaowafahamu. Mmoja ni baba yangu mdogo, Joseph Muhunda. Na mwingine ni mzimu wa kabila la Wazanaki, kiumbe asiye wa kawaida anayeaminika kuishi ndani ya msitu wa nasaba wa Muhunda uliyopo jirani na Mwitongo, sehemu yalipokuwa makazi ya babu yangu. Ni marufuku kuingia ndani ya msitu huo ila kwa watu maalumu tu, kwa mfano rika la wazee, au wanyikura ambao ndiyo wasimamizi wa msitu. Aidha kukata miti ya huo msitu pia ni marufuku ingawa kuokota matawi makavu yalioanguka inaruhusiwa.

Mwalimu mstaafu, Jack Nyamwaga, anakumbuka kuwa wakati wa utoto wake kuna nyani mkubwa alifika kwenye makazi ya babu yangu, Mtemi Nyerere Burito. Yule nyani alisogelea na kuanza kula mihogo iliyokuwa imeanikwa nje, na watoto walipojaribu kumfukuza Mtemi Nyerere aliwazuwia na kusema wamwache yule nyani aendelee kula ile mihogo.

Inaaminika kuwa mzimu huu hujibadilisha katika maumbile mbalimbali ikiwa ni pamoja na chui, nyoka, mbuzi, au nyani. Ni nadra kuona nyani Butiama na ingawa nimewahi kuwaona kwenye milima ya jirani na Butiama huwa hawafiki eneo la Butiama. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 11 kwa nyani kuonekana hapa Butiama.

Wanaoamini kuwepo kwa mzimu huu wanaamini kuwa umefika kufuatia msiba tuliyopata hivi karibuni. Mashuhuda wanasema kuwa huyu nyani aliyeonekana hivi karibuni alitokea upande wa kaskazini, akavuka eneo lenye makazi, akipuuzia watoto waliokuwa wanamrushia mawe, na alifika kwenye kaburi la ndugu tuliyemzika hivi karibuni na akabaki pale kwa dakika chache halafu akaelekea Mwitongo.
Wakati wa msiba wa ndugu yangu, Mazembe Joseph Nyerere.
Siyo mbwa tu walikuwa wamekosa amani, inasemekana kuwa hata tumbili ‘waliingia mitini’ na hawakuonekana kabisa, ingawa kwa kawaida eneo la Mwitongo lina makundi mengi ya tumbili.
Tumbili 'waliingia mitini.'
Katika miaka iliyopita kila nyani mkubwa alipojitokeza eneo la Butiama wanyikura walikutana na kutuma wawakilishi kwa mpiga ramli mashuhuri aliye eneo la Mto Kirumi kupata ufafanuzi juu ya ujumbe au tafsiri ya kuonekana ‘Muhunda’. Iwapo ‘Muhunda’ alikuwa amekasirishwa na tukio fulani ndani ya jamii, basi ujumbe uliwasilishwa kwa jamii na tambiko lilifanyika.

Tuesday, July 12, 2011

Siasa ya Tanzania: chama na sera zake, au mtu?


Kwenye picha ya hapa chini anaonekana diwani wa kata ya Muleba, Hassan Milanga wa Chama cha Wananchi (CUF), mwenye fulana nyekundu, akiteta jambo na wapiga kura wake wa mjini Muleba, ambao pia ni wafanyabiashara wa samaki. Milanga aliingia kwenye siasa mwaka 2000 na akachaguliwa kuwa diwani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na kile anachokieleza kuwa ‘mizengwe’ilizomzuwia kubaki CCM wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 alihamia CUF, na wapiga kura wakahama naye na kumchagua kwa mara ya pili kuwaongoza kama diwani wao.

Wapiga kura wakarudia tena kufanya hivyo hivyo mwaka 2010. Ni dhahiri kuwa kwa sehemu nyingi za Tanzania wapiga kura wanachagua mtu na siyo chama. Swali: Ina maana wagombea wanapoteza muda kunadi sera wakati wa kampeni?

Saturday, July 9, 2011

Wageni wa Butiama: Kwaya ya Uamsho ya Musoma yafika Mwitongo kutengeneza video


Kwaya ya Uamsho ya Dayosisi ya Musoma ya Kanisa la Anglikana ilizuru Mwitongo juzi kuandaa video ya nyimbo ambazo inakusudia kutoa katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa. 
 Katika ya miaka ya hivi karibuni kwaya kadhaa zimetembelea Butiama kwa madhumuni ya kutengeneza video kutokana na mandhari murua iliyopo kwenye eneo la Mwitongo.

Wednesday, July 6, 2011

Kituo cha redio kwenye Mtandao chaanzishwa

Taarifa hizi nimepata hivi punde toka kwa  Sillah Mbuya:
JINA LA WEBSITE: TONE INTERNET RADIO

LINK: 
http://www.toneinternetradio.blogspot.com

Tunapenda kuwatambulisha Watanzania wote waishio popote Duniani kwamba kuanzia sasa wanaweza sikiliza redio kupitia mtandao yani "Internet" Buree. Tumeona tufanye hivi kwa kutambua kwamba pamoja na kuwa Watanzania wengi wapo hapa nchini na wengi wao kwa sasa wanatumia Mtandao na wanapenda sikiliza redio kupitia Mtandao, lakini pia tumezingatia na Watanzania wenzetu wanaoishi nje ya nchi wapate burudani, habari na mambo mengine mengi kutoka Tanzania. Kupitia Tone  Internet Radio watakuwa hawajisikii upweke na kuona kama wapo Tanzania. Pia Tone Radio inawapa nafasi wasanii wa muziki wa aina yoyote Tanzania kuleta nyimbo zao hapa studio na sisi kutangaza kazi zao bure kwa kututumia nyimbo zao kupitia toneinternentradio@yahoo.com .
Karibuni sana
Tunatanguliza shukurani zetu za dhati na karibuni sana...
Tone Internet Radio Pamoja Tutafika

Sillah Mbuya