Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, August 28, 2012

Hatimaye, watu wa sensa hawa hapa

Jumapili, tarehe 26 Agosti, nilikaa nyumbani siku nzima nikisubiri kuhesabiwa kwenye Sensa ya Taifa lakini sikuona mtu hata mmoja kuja kuniuliza swali. Hatimaye leo maafisa wa sensa ya Taifa wamefika kunihoji maswali yao 62, ambayo kila mshiriki anapaswa kuyajibu.

Wengi wetu hatukukumbuka kuwa ni zoezi la juma zima.
Mimi, kushoto, nikijibu maswali ya Sensa ya Taifa leo asubuhi. 
Ndani ya muda wa dakika kumi zoezi lilimalizika na wakaondoka.

Pamoja na kwamba wengine tulikuwa na shauku kubwa ya kukamilisha kazi hii kuna Watanznia wenzetu ambao kabla ya zoezi hili kuanza wamekuwa wakiendesha kampeni ya wazi kuhimiza Waislamu wasishiriki kwenye sensa kwa sababu maswali yale 62 hayaulizi dini ya anayehesabiwa.

Nimejaribu kuuliza hili swali lakini mpaka leo sijasikia jibu lake: tunataka kujua kuna Watanzania wangapi wa dini mbalimbali ili tutumie hizo takwimu kufanya nini? Mwenye jibu naomba anifahamishe.

Sunday, August 26, 2012

Wageni wa Butiama: Agustino Lyatonga Mrema

Butiama inatembelewa na wageni wengi, baadhi yao mashuhuri, lakini wengi ambao siyo mashuhuri. Wengi wa wageni mashuhuri waliowahi kutembelea Butiama walifika hapo kwa sababu ya kumtembelea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mmojawapo wa hao wageni ni Mhe. Agustino Mrema ambaye amewahi kufika Butiama mara kadhaa. Katika picha hii anaonekana akisalimiana na Mwalimu Nyerere mwaka 1997 wakati wa msiba wa Bibi Mugaya wa Nyang'ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere.

Friday, August 24, 2012

Mada yangu ya leo: Muungano una manufaa

Pamoja na kuwepo malalamiko mengi juu ya muungano uliounganisha Unguja na Tanganyika na kutoa Tanzania, tushukuru kuwepo kwa muungano huu kwa kutuepusha na majanga mengi.

Na wanaopaswa kushukuru zaidi ni Watanzania wa upande ulioitwa Tanganyika kabla ya tarehe 26 Aprili 1964, siku ulipozaliwa Muungano.

Bila Muungano kusingekuwepo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Bila shaka ingekuwepo JWTZ lakini labda ingekuwa ni Jeshi la Wananchi wa Tanganyika.

Leo hii, makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanganyika wangekuwa wakikuna vichwa kutafakari namna ya kupambana na nchi mbili: Malawi na Zanzibar. Yote hii kutokana na kutokuafikiana kwa pande mbili za Muungano kuhusu mgawanyo wa mapato yatakayotokana na mafuta yanayokisiwa kuwepo ndani ya mipaka ya Tanzania kwenye eneo la Bahari ya Hindi, na pia kutokana na madai ya Malawi kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa ni mali ya Malawi, ikiwa ni suala linaloibuliwa na kuwepo kwa uwezekano kuwa kuna shehena kubwa ya mafuta chini ya Ziwa Nyasa. Tanzania haitambui madai hayo ya Malawi na kubainisha kuwa mpaka kati yao upo katikati ya Ziwa Nyasa.

Kwa bahati nzuri Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, ametamka hivi karibuni kuwa mgogoro kati ya Malawi na Tanzania juu ya mpaka wa Ziwa Nyasa hautahusisha vita na kuwa utamalizwa kwa njia za kidiplomasia.

Lakini hapa tusisahau kuwa hata majeshi ya Idi Amin yalipovamia maeneo ya Tanzania mwaka 1978 Serikali ya Tanzania ilifanya jitihada kubwa za kutatua ule mgogoro kwa njia za kidiplomasia. Zile jitihada hazikufaulu kumaliza mgogoro na matokeo yake Tanzania na Uganda zikaingia kwenye vita ambayo ilileta madhara makubwa kwa pande zote mbili.

Hasara ya Uganda: gari la kijeshi lililoteketezwa na majeshi ya Tanzania ndani ya eneo la Tanzania kwenye mji mdogo wa Mutukula.
Na kwa uhakika kwa sababu ya Muungano, mgogoro kati ya Tanzania Visiwani na Tanzania Bara hautahusisha vita. Bila hivyo zingepigwa mpaka mmoja aelewe hoja ya mwenzake. Anaesema Muungano hauna faida yoyote atafakari tena.

Friday, July 20, 2012

Mtanzania Ramadhani Shauri kupambana na Mganda Sande Kizito kuwania ubingwa wa mabara wa IBF Afrika

Mtanzania Ramadhani Shauri atapanda ulingoni siku ya Idd pili kupambana na bondia Sande Kizito kutoka Uganda kugombea mkanda wa IBF katika bara la Africa katika uzito wa unyoja (Featherweight).

Shauri anayefanya mazoezi yake Ubungo, Dar es Salaam, maeneo ya Mabibo na anafundishwa na kocha Mzazi anayetamba kuwa na mabondia wenye nidhamu na vipaji vya hali ya juu.

Ramadhani Shauri ni bondia chipukizi mwenye umri wa miaka 19 na historia yake ya ngumi inafurahisha kila anayeisoma na kuisikia. Ana haiba nzuri inayovutia na anafananishwa na bondia Sugar Ray Leonard wa Marekani kutokana na haiba yake na upiganaji wake.
Ramadhani Shauri, katikati, akiwa ameshika mkanda atakaoupigania dhidi ya bondia Sande Kizito. Kulia ni promota wa pambano, Lucas Rutainurwa na kushoto ni mwandishi wa blogu hii na ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Madaraka Nyerere.
Sugar Ray Leonard alitamba katika miaka ya 70 na 80. Shauri ni Mfalme anayekuja na hivi sasa anatishia maisha ya mabondia wengi katika bara la Afrika.

Ramadhani Shauri ana nidhamu ya hali ya juu na maisha yake katika ngumi yanafurahisha kwa jinsi anavyoishi kwa nidhamu na kufanya mazoezi ya kujijenga katika ngumi. Katika maisha yake anajiepusha sana na matatizo ambayo vijana wengi wametumbukia kama vile uvutaji wa bangi, ngono zembe na mambo mengine yasiyo na malengo katika maisha.

Huyu ndiye kweli Mfalme anayekuja katika ngumi za kulipwa na nchi yetu imepata bahati kubwa sana kuwa na kipaji cha bondia kama huyu.

Mpambano wa Shauri umepewa jina la “The Rumble in the City of Heaven’s Peace” (Vurumai katika Jiji la Amani).

Monday, June 18, 2012

Ukoo mkubwa kuliko maelezo

Mapema kwaka 2000 nilipewa jukumu la kumtambulisha mgeni kwa kundi la wenyeji waliofika kumpokea huyo mgeni nyumbani Butiama. Kabla ya mgeni kufika nilichukuwa kalamu na karatasi na kumuuliza aliye karibu nami jina lake na akanitajia jina na ubini wake. Cha ajabu, alikuwa na ubini kama wangu. Baadaye niligundua kuwa ni mmoja wa baba zangu wadogo.

Niliona aibu sana, lakini naamini kuwa ninayo sababu nzuri ya kutomfahamu. Marehemu babu yangu, Mtemi Nyerere Burito, alikuwa na wake 22. Aidha alikuwa na kina mama wa nyumba ndogo wanne ambao kwa kabila la Wazanaki wanajulikana kama vitungo. Kutokana na uzao wa babu na wake zake, mimi nina ndugu na jamaa wanaokaribia 6,000 kwa hiyo kumfahamu kila mmoja wao siyo jambo rahisi.

Kwa kawaida, uzao uliyonitangulia ulikuwa na watoto wengi, lakini iwapo nitachukuwa wastani wa watoto sita tu kwa kila mme na mke kwa ajili ya kukadiria idadi ya uzao wa Mtemi Nyerere, nikianza na bibi zangu ishirini na wawili, napata idadi ya baba wadogo/shangazi 132, watoto wa baba wadogo/shangazi 792, na wajukuu wa baba wadogo/shangazi 4,752, ikiwa ni jumla ya ndugu 5,676. Na hii ni kutoka upande wa baba mzazi tu.
Kaburi la Mtemi Nyerere Burito, kulia, pamoja na kaburi la mke wake wa tano, Christina Mgaya wa Nyang'ombe, kushoto, katika eneo la Mwitongo kwenye kijiji cha Butiama.

Hata iwapo watapunguzwa wale waliofariki, bado inaacha idadi kubwa ya majina na sura ambazo si rahisi kuzikumbuka, pamoja na kuzingatia kuwa kukumbuka ndugu ni suala linaloweza kujenga mahusiano mazuri kwenye familia kubwa. Swali moja ambalo naulizwa mara kwa mara ninapokutana na ndugu ambao siwafahamu vizuri ni: "Unanifahamu mimi?" Ninapokuwa namfahamu mambo huenda vizuri lakini pale ninaposhindwa kumtambua nakuwa mtu nisiefaa kabisa, nachukuliwa kama mtu ambaye hafanyi jitihada ya kutosha kuwafahamu ndugu zake.
Sehemu ya wanaukoo wa Burito Nyerere wakiwa 
Hivi karibuni nilikutana na binamu zangu wawili ambao mama yao, marehemu shangazi yangu, ni binti wa tatu wa mke wa saba wa Mtemi Nyerere Burito. Pamoja na kuwa anakaribia miaka 50, mmoja wa wale binamu zangu hakuwa ananifahamu, na alikuwa hajawahi kusikia jina langu. Ilikuwa ni faraja kubwa sana kwangu kwa sababu ilikuwa ni ushahidi tosha kwangu kuwa tatizo la kutoweza kuwatambua ndugu zaidi ya 5,000 halikuwa linawakumba tu wale waliokaa sana jijini Dar es Salaam.