Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, July 14, 2015

Kwenye mchakato huu, dozi ya politiki ilizidi kiwango

Nafikiri ni General Defao aliyeimba: "umekalia politiki tu, kazi hufanyi". Katika kipindi ambacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiendelea na mchakato wa kupata mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, hali hiyo ya kukalia politiki tu imekuwa kweli kwa watu wengi.

Wengi tunatambua umuhimu wa mchakato wowote wa kisiasa kama jambo muhimu katika jamii na jambo la msingi ni kupata viongozi wanaosimama kuwakilisha matakwa ya wengi. Na bila shaka ni suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulifuatilia kwa karibu sana.

Lakini mchakato huo unapotufanya tuache kila kitu, hata zile kazi ambazo zinatulipa ajira, basi suala la siasa linakuwa limezidi dozi ya kawaida. Kuna watu wengi tu ambao hawakuwa na nafasi yoyote katika vikao vya maamuzi vya CCM vilivyokaa Dodoma kumpitisha John Magufuli ambao walienda Dodoma kufuatilia mchakato huo.

Baadhi ya ambao hatukuwa Dodoma tulikaa muda wote tukisikiliza taarifa kwenye vyombo vya habari kufuatilia mchakato. Wengine wengi walitumia muda wao kujibishana na wenzao kwenye mitandao ya jamii. Dozi haikuwa ndogo hata kidogo.
"I've always been and will continue to be a proud member of the ruling party CCM...I'm happy with all the five candidates and know that we'll get a great President to lead our beautiful nation...All the best....God Bless Tanzania󾍛....#ccm #chamachamapinduzi #januarymakamba #membe #magufuli #migiro #amina #umojaniushindi #tanzania"
Baadhi ya watia nia waliofikia hatua za mwisho za mchakato wa kupata mgombea urais wa CCM
Naamini watafiti wanaweza kubaini kushukua kwa uzalishaji katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita.

Tushukuru kuwa mchakato huu wa CCM umeisha na labda watu watarejea kwenye maisha yao na majukumu yao ya kila siku.

Monday, June 22, 2015

Utamaduni wa utoaji majina miongoni mwa kabila la walango wa Uganda

Nimepata fursa hivi karibuni ya kuonana tena na mmoja wa watoto wa kiume wa rais wa zamani wa Uganda, Apollo Milton Obote na tuliongelea utamaduni wa kutoa majina kwa kabila lao la walango.

Nilipenda kufahamu kwa nini jina lake halina ubini wa baba yake, Obote. Yeye anaitwa Eddy Engena-Maitum, na ni askofu wa kanisa la Bright Morningstar Ministry. Alinijibu kuwa kwa mila na desturi za kabila lao, kila mtoto anayezaliwa anapewa majina yake bila kuweka jina la baba mzazi. Alifafanua kuwa majina yote ya baba yake ni yake, hakutumia ya baba yake (babu yake Eddy).

Mdogo wake naye anafuata utaratibu huo huo: ni Jimmy Akena, ambaye ni mwanasiasa na rais wa chama cha Uganda Peoples' Congress. Aidha, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika 2017. Alipomuoa mbunge mwenzake Betty Amongi mwaka 2013 Rais Yoweri Museveni alihudhuria harusi hiyo.

Mimi (kulia), nikiwa pamoja na Askofu Eddy Engena-Maitum jijini Kampala hivi karibuni.
Eddy anafafanua kuwa zipo faida na hasara za kutotumia ubini wa baba yao. Wakati mwingine akijitambulisha kama mtoto wa Milton Obote wale wasiomfahamu humtilia shaka wanapoona kuwa jina lake kamili halina jina la baba yake. Faida ni kuwa pale inapokuwa siyo lazima kujitambulisha hivyo inampa fursa ya kubaki bila utambulisho huo ambao, kwa watoto ambao wazazi ni wanasiasa inaweza kuwa ni jambo linalozua hisia tofauti kwa wanaobaini hali hiyo. Inaweza kutokea kubebeshwa kesi ambayo siyo yako.

Monday, April 13, 2015

Hapa ndipo alipozaliwa Mwalimu Nyerere

Hapa ndipo miaka 93 iliyopita alizaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kijijini Butiama.
Ni eneo la Mwitongo alipoishi baba yake Mtemi Nyerere Burito wa kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, na mama yake, Mgaya wa Nyang'ombe, aliyekuwa mke wa tano kati ya wake 22 wa Mtemi Nyerere.

Leo eneo hili ni sehemu inayotembelewa na mamia ya wageni kila mwezi kutoka sehemu mbalimbali.

Saturday, March 14, 2015

Mahojiano yangu kuhusu wagombea urais

Majuma kadhaa yaliyopita nilihojiwa na mwandishi wa habari wa Mwanza kuhusu maoni yangu juu ya wagombea urais waliojitokeza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

Sehemu ya mahojiano hayo imechapishwa hapa.

Saturday, January 24, 2015

Waheshimiwa wengi sana Tanzania

Neno mheshimiwa limekosa heshima inayokusudiwa kwa maoni yangu.Sababu kubwa ni kuwa Tanzania ina waheshimiwa wengi sana.

Sizungumzii wale watu ambao nafasi zao katika jamii zinatulazimu kuwaita "waheshimiwa", kwa mfano mahakimu, majaji, na wabunge. Nazungumzia tabia iliyojengeka ya matumizi ya "mheshimiwa" kwa kila raia anayezungumza Kiswahili. 

Mimi nilidhani kuwa madhumuni ya kutumia "mheshimiwa" haina tofauti sana na kumuita mtu daktari. Madhumuni ni kumpambanua kama mtu mwenye nafasi muhimu katika jamii ambayo inahitaji kuweka mipaka ya namna watu wengine wanavyowasiliana nae, au kubainisha kuwa ni mtu ambaye anayo taaluma maalum. Kwa upande wa majaji na mahakimu ni viongozi ambao wana majukumu muhimu ndani ya jamii na wanapata upendeleo fulani kwa namna wanavyochukuliwa na jamii. Kwa kuwapa huo upendeleo jamii pia inategemea kuwa waheshimiwa watakuwa watu wanaojiheshimu mbele ya jamii.

Sasa cheo hiki anapopewa kila mtu kuna hatari ya kukigawa kwa watu ambao hawajiheshimu hata chembe na ambao wataharibu maana halisi ya uheshimiwa. Kwa maoni yangu waheshimiwa wanaosimamia kesi mahakamani ndiyo wanastahili zaidi kuitwa waheshimiwa.

Sisi tuliobaki tungerudia kuitana ndugu, ingawa wengi wanaamini undugu unahusiana na siasa ya Ujamaa peke yake. Siyo kweli. Tumsikilize Rais Mstaafu Mkapa, akizungmuza kwenye semina ya Muafaka ya Vyama vya Siasa, Zanzibar, tarehe 7 Machi 2005:

"Ndugu siyo neno la kiitikadi tu, linahusu pia utamaduni wetu. Mtaniwia radhi nikiwaita "Ndugu wanasemina."

Wewe ni ndugu au mheshimiwa?