Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, August 12, 2015

Lugha yetu Kiswahili: Kiswahili kinasambaa toka Scotland mpaka Butiama

Wanafunzi 12 toka Chuo Kikuu cha Edinburgh wapo kijijini Butiama kujifunza Kiswahili kwa mwezi mmoja.

Mafunzo yao ni sehemu ya mpango wa Chuo Kikuu cha Edinburgh kuvutia wanafunzi kutoka nje ya Scotland kujiunga na masomo mbalimbali katika chuo hicho maarufu, ambacho mmoja wa wanafunzi wake mashuhuri ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wanafundishwa Kiswahili na walimu Watanzania watatu.
Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh wakiwa Butiama, pamoja na walimu wao wa lugha ya Kiswahili.
Kuwepo kwa wanafunzi wa lugha ya Kiswahili kutoka Edinburgh hapa Butiama kwa Mwalimu Nyerere, ambaye pia anatambuliwa kama mmoja wa viongozi wa Tanzania ambao walitoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ni suala la fahari kubwa kwa mmoja wa waratibu wa mafunzo haya ya Kiswahili, Dk. Thomas Molony, ambaye mwaka jana alichapisha kitabu juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere kinachoitwa Nyerere: The Early Years.

Akiwa Butiama wakati akifanya utafiti wa kitabu chake, nilipata fursa ya kuchangia kwa kiwango kidogo taarifa ambazo hatimaye alizitumia kwenye kitabu hicho.

Na mimi nakubaliana naye. Naamini kuwa Mwalimu Nyerere angekuwa hai angefurahi sana kushuhudia wanafunzi kutoka chuo chake cha zamani wakiwa Butiama kujifunza lugha ambayo yeye mwenyewe aliipenda na aliyoshiriki kuiimarisha.

Tuesday, July 14, 2015

Kwenye mchakato huu, dozi ya politiki ilizidi kiwango

Nafikiri ni General Defao aliyeimba: "umekalia politiki tu, kazi hufanyi". Katika kipindi ambacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiendelea na mchakato wa kupata mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, hali hiyo ya kukalia politiki tu imekuwa kweli kwa watu wengi.

Wengi tunatambua umuhimu wa mchakato wowote wa kisiasa kama jambo muhimu katika jamii na jambo la msingi ni kupata viongozi wanaosimama kuwakilisha matakwa ya wengi. Na bila shaka ni suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulifuatilia kwa karibu sana.

Lakini mchakato huo unapotufanya tuache kila kitu, hata zile kazi ambazo zinatulipa ajira, basi suala la siasa linakuwa limezidi dozi ya kawaida. Kuna watu wengi tu ambao hawakuwa na nafasi yoyote katika vikao vya maamuzi vya CCM vilivyokaa Dodoma kumpitisha John Magufuli ambao walienda Dodoma kufuatilia mchakato huo.

Baadhi ya ambao hatukuwa Dodoma tulikaa muda wote tukisikiliza taarifa kwenye vyombo vya habari kufuatilia mchakato. Wengine wengi walitumia muda wao kujibishana na wenzao kwenye mitandao ya jamii. Dozi haikuwa ndogo hata kidogo.
"I've always been and will continue to be a proud member of the ruling party CCM...I'm happy with all the five candidates and know that we'll get a great President to lead our beautiful nation...All the best....God Bless Tanzania󾍛....#ccm #chamachamapinduzi #januarymakamba #membe #magufuli #migiro #amina #umojaniushindi #tanzania"
Baadhi ya watia nia waliofikia hatua za mwisho za mchakato wa kupata mgombea urais wa CCM
Naamini watafiti wanaweza kubaini kushukua kwa uzalishaji katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita.

Tushukuru kuwa mchakato huu wa CCM umeisha na labda watu watarejea kwenye maisha yao na majukumu yao ya kila siku.

Monday, June 22, 2015

Utamaduni wa utoaji majina miongoni mwa kabila la walango wa Uganda

Nimepata fursa hivi karibuni ya kuonana tena na mmoja wa watoto wa kiume wa rais wa zamani wa Uganda, Apollo Milton Obote na tuliongelea utamaduni wa kutoa majina kwa kabila lao la walango.

Nilipenda kufahamu kwa nini jina lake halina ubini wa baba yake, Obote. Yeye anaitwa Eddy Engena-Maitum, na ni askofu wa kanisa la Bright Morningstar Ministry. Alinijibu kuwa kwa mila na desturi za kabila lao, kila mtoto anayezaliwa anapewa majina yake bila kuweka jina la baba mzazi. Alifafanua kuwa majina yote ya baba yake ni yake, hakutumia ya baba yake (babu yake Eddy).

Mdogo wake naye anafuata utaratibu huo huo: ni Jimmy Akena, ambaye ni mwanasiasa na rais wa chama cha Uganda Peoples' Congress. Aidha, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika 2017. Alipomuoa mbunge mwenzake Betty Amongi mwaka 2013 Rais Yoweri Museveni alihudhuria harusi hiyo.

Mimi (kulia), nikiwa pamoja na Askofu Eddy Engena-Maitum jijini Kampala hivi karibuni.
Eddy anafafanua kuwa zipo faida na hasara za kutotumia ubini wa baba yao. Wakati mwingine akijitambulisha kama mtoto wa Milton Obote wale wasiomfahamu humtilia shaka wanapoona kuwa jina lake kamili halina jina la baba yake. Faida ni kuwa pale inapokuwa siyo lazima kujitambulisha hivyo inampa fursa ya kubaki bila utambulisho huo ambao, kwa watoto ambao wazazi ni wanasiasa inaweza kuwa ni jambo linalozua hisia tofauti kwa wanaobaini hali hiyo. Inaweza kutokea kubebeshwa kesi ambayo siyo yako.

Monday, April 13, 2015

Hapa ndipo alipozaliwa Mwalimu Nyerere

Hapa ndipo miaka 93 iliyopita alizaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kijijini Butiama.
Ni eneo la Mwitongo alipoishi baba yake Mtemi Nyerere Burito wa kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, na mama yake, Mgaya wa Nyang'ombe, aliyekuwa mke wa tano kati ya wake 22 wa Mtemi Nyerere.

Leo eneo hili ni sehemu inayotembelewa na mamia ya wageni kila mwezi kutoka sehemu mbalimbali.

Saturday, March 14, 2015

Mahojiano yangu kuhusu wagombea urais

Majuma kadhaa yaliyopita nilihojiwa na mwandishi wa habari wa Mwanza kuhusu maoni yangu juu ya wagombea urais waliojitokeza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

Sehemu ya mahojiano hayo imechapishwa hapa.