Juu ya vilima vya Matopo, jirani ya mji wa Bulawayo nchini Zimbabwe, lipo kaburi la Cecil Rhodes. Anajulikana kwa sifa nyingi kwa wanaompenda, lakini anajulikana pia kama mbaguzi wa rangi wa kiwango cha juu kabisa.
Alienda kwanza Afrika ya Kusini kulima pamba lakini baadaye akavutiwa na almasi na mwaka 1871 akaachana na kilimo na kuanza kusaka almasi na ardhi. Alianza kukamata vitalu na kufanya manunuzi ya ardhi, na baadaye akaanzisha De Beers Mining Company.
Alijiingiza kwenye siasa kupitia koloni la Waingereza la Cape na alikuwa kinara wa kununua ardhi zilizosababisha kupatikana kwa maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa Waafrika kwa ajili ya shughuli zake za uchimbaji madini. Mwaka 1888, Rhodes alipeleka mawakala wake kwa Mfalme Lobengula wa Matebele (sasa sehemu ya Zimbabwe) ambao walimrubuni akaamini alikuwa akiweka sahihi mkataba wa uchimbaji wa madini wakati ukweli ukiwa alikuwa ameuza himaya yake yote kwa Rhodes.
Kwa nguvu ya Serikali ya Uingereza Rhodes aliruhusiwa kuendeleza maeneo aliyoyamiliki kwa kutumia British South African Company. Akitumia eneo alilopora kwa Mfalme Lobengula, Rhodes aliongeza udhibiti kuelekea kaskazini mpaka Rhodesia ya Kaskazini (Sasa Zambia), Nyasalaand (sasa Malawi), na Bechuanaland Protectorate (sasa Botswana). Maeneo yote haya baadaye yakawa makoloni ya Uingereza.
Uporaji wake wa ardhi ulileta shida kwa mamilioni ya Waafrika na athari zake zinaendelea mpaka leo hii kwenye baadhi ya maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na Zimbabwe.
Inasemekana kuwa mavetarani wa vita vya ukombozi vya Zimbabwe wanapinga kuwepo kwa kaburi la Rhodes na wamewahi kujaribu kulilipua kwa mabomu.
1 comment:
pia hadithi nyingine zinasema alikwenda afrika kusini kutafuta hali ya hewa iliyokuwa inapatana na maradhi aliyokuwa nayo. alipofika huko akaona inafaa na kuamua kuweka makazi huko.
Post a Comment