Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, December 15, 2010

CCM wafungua tawi Uingereza, CHADEMA juu ya Mlima Kilimanjaro

Taarifa zilizonifikia hivi punde zinaeleza kuwa baadhi ya Watanzania waishiyo katika mji wa Luton Uingereza walijumuika 12 Desemba 2010 kwa ajili ya ufunguzi wa tawi jipya katika mji wa Luton, ufunguzi uliyofanyika katika hoteli ya Chiltern UK.

Taarifa hiyo, kwa hisani ya Tawi la CCM Uingereza inaendelea:
Wengi wao wanasema wana imani kubwa na CCM katika kuiongoza Tanzania kwa kuonyesha muelekeo wa kuwa na imani na vijana wasomi wachapakazi waliyoko ndani na nje ya nchi.



Ufunguzi huo ambao uliongozwa na mwenyekiti wa tawi la CCM - UK, Maina Owino, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa CCM akiwemo Katibu Mwenezi wa Siasa, Moses Katega. Pia viongozi kutoka mashina ya Reading, Birmingham na sehemu zote za London walijumuika.


Katika hotuba yake fupi Ndugu Maina Owino alitoa changamoto nyingi za mafanikio  yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika nyanja mbalimbali kama madini, elimu, ukusanyaji wa mapato ya serikali, waajiriwa wenye sifa za kukidhi nafasi za uongozi serikalini katika nyanja zote, na ujasiriamali kwa Watanzania wanaojitafutia maendeleo bila bugudha.


Changamoto kuhusu ushiriki wa vijana wasomi hapa Uingereza kuingia katika mchakato wa siasa ndani ya Chama ili kuleta mabadiliko yatakayozidi kukiimarisha Chama kisera na kuzidi kuwaletea Watanzania maendeleo katika nyanja mbalimbali kupambana na umasikini yalitolewa na katibu wa shina jipya la Luton aliyechaguliwa siku hiyo, Ndugu Abraham Sangiwa, na kuungwa mkono na wajumbe wote waliyohudhuria ufunguzi huo.


Viongozi waliochaguliwa ni:


Albert Ntmi - Mwenyekiti
Abraham Sangiwa - Katibu Mkuu
John Mbwete - Mjumbe
Sammy Martin - Mjumbe
Norman Wage - Mjumbe

Wakati huo huo, siku mbili zilizopita, nikielekea kilele cha Mlima Kilimanjaro, katika kambi ya Barafu, ambayo ni kituo cha mwisho kabla ya safari ya kufika kilele cha Uhuru niliona bendera ya CHADEMA ikipepea.


Kwa mujibu wa taarifa nilizopata toka kwa wapagazi wanaosindikiza wageni kupanda Mlima Kilimanjaro wanaojulikana miongoni mwao kama "wagumu", kutokana na kazi ngumu wanayofanya kusindikiza wageni juu ya mlima huu maarufu, shughuli za CHADEMA zimeanza juu ya Mlima Kilimanjaro miaka mitatu iliyopita.

CHADEMA hawana tawi juu ya Mlima Kilimanjaro ila nilichoshuhudia mimi na jitihada za wana-CHADEMA kupeperusha bendera ya chama chao kwenye sehemu iliyo juu kuliko zote Tanzania. Kambi ya Barafu ipo urefu wa mita 4,600 juu ya usawa wa bahari.

No comments: