Tunajifunza mengi kwa kusikiliza. Leo nimemsikiliza mama wa
kijijini Butiama akilalamika kwangu tena kuhusu binti yake kuondoka nyumbani na kuhamia
kwa mtu aliyezaa naye.
Tatizo ni kuwa binti mwenyewe ana umri wa miaka 15 tu, na
aliyempa ujauzito ni mtu mzima. Alimpa hiyo mimba binti akiwa shuleni, na kwa
mujibu wa sheria zilizopo angestahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Hayo
hayakutokea.
Nahisi hayakutokea kwa sababu mama wa binti, badala ya
kupeleka hilo suala mbele ya sheria, alifikia makubaliano na huyo jamaa na
inawezekana kuwa alikuwa anapewa pesa ili kutulia.
Sasa leo kalalamika tena kuwa binti karudi kule kule na
akaniambia kuwa sasa anakusudia kufikisha suala hilo polisi. Lakini njia anayotumia
haijanyooka vizuri. Kaniambia kuwa ana jirani yake polisi ambaye amemuomba
aende kumkamatia yule mhalifu.
Jirani yake kakubali lakini amemwambia ampe shilingi elfu
kumi ili amfanyie hiyo kazi. Yeye alisema hana hizo pesa, na akamwambia yule
jirani kuwa amfanyie tu hiyo kazi kwa kuwa wanahusiana pia kiukoo. Jirani polisi
hakusumbuliwa sana na hoja ya uhusiano wa kiukoo, na amemwambia mlalamikaji atafute
angalau shilingi elfu tano ili afanye hiyo kazi.
Miongoni mwa vielelezo kuwa uongozi ni kazi kubwa ni pamoja
na tukio hili. Kwenye ngazi hii ya chini, kujenga imani kuwa falsafa ya Sasa
Kazi tu! itafanikiwa ili mradi yupo rais na waziri mkuu wachapa kazi ni
ndoto tu. Mabadiliko chanya yatapatikana iwapo wote tutashiriki kwa namna
tunavyoweza kuleta mafanikio tunayotarajia.
2 comments:
good post
Kusema kweli miongoni mwa vitu vitakavyokwamisha falsafa hii ni pamoja na jamii kudhania kuwa hii inawahusu watumishi WA serikali peke yao. Lakini pia wakuu WA idara kutumia mwanya huo kupenyeza chuki zao binafsi na watumishi walioko chini yao na kuwanyanyasa.
Post a Comment