Imefika wakati Jeshi la Polisi libadilike kidogo.
Kuna umuhimu wa polisi kuboresha huduma kwa tunaofika kwenye vituo vya polisi ili tupate huduma inayoridhisha. Nazungumzia wahalifu na wasiyo wahalifu. Wote tunastahili kupewa huduma ya kuridhisha.
Hivi karibuni, nikiwa naendesha gari, nilisimamishwa Singida mjini na afisa usalama barabarani kwa kosa la kutosimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu.
Nilikiri kosa haraka na kukubali kulipa faini ili niendelee na safari. Suala ambalo lingechukua dakika tano lilichukua saa nzima.
Nilielekezwa kwenda kituoni na afisa aliyenikamata akafika baada ya dakika kumi kunijazia hati ya malipo. Nilipodai risiti nikaambiwa mhasibu ameshaondoka, nirudi asubuhi kuchukua risiti. Ilikuwa saa kumi jioni.
Nilimfahamisha kuwa niko safarini na isingewezekana kurudi asubuhi. Ilikuwa naambiwa nirudi asubuhi kama vile naishi Singida.
Ni mpaka mhasibu alipopigiwa simu na afande ndipo aliporudi na kuniandikia risiti. Alikuwa kanuna sana kwa kurudishwa ofisini. Mdomoni alikuwa na kijiti cha kuondoa nyama zinazobaki kati ya meno baada ya kula nyama ya kuchoma.
Maoni yangu ni kuwa wakati wowote mhalifu anapotozwa faini anapaswa kupewa risiti wakati huo huo anapotozwa faini. Siyo sawa polisi wakatumia sheria kutoza faini halafu wakapuuzia kutoa risiti wakati huo huo.
Ama sivyo mhasibu anapofunga ofisi na faini zisitozwe.
Halafu, si tumeshapewa somo kuwa tusilipie kitu chochote bila kudai risiti? Au hilo somo haliwahusu polisi?
Mimi naamini linawahusu. Kupewa risiti baada ya kulipa faini si hisani. Ni haki.
No comments:
Post a Comment