Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, December 1, 2015

Kufanikisha falsafa ya Sasa Kazi tu! ni kazi kweli kweli!

Tunajifunza mengi kwa kusikiliza. Leo nimemsikiliza mama wa kijijini Butiama akilalamika kwangu tena kuhusu binti yake kuondoka nyumbani na kuhamia kwa mtu aliyezaa naye.

Tatizo ni kuwa binti mwenyewe ana umri wa miaka 15 tu, na aliyempa ujauzito ni mtu mzima. Alimpa hiyo mimba binti akiwa shuleni, na kwa mujibu wa sheria zilizopo angestahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Hayo hayakutokea.

Nahisi hayakutokea kwa sababu mama wa binti, badala ya kupeleka hilo suala mbele ya sheria, alifikia makubaliano na huyo jamaa na inawezekana kuwa alikuwa anapewa pesa ili kutulia.

Sasa leo kalalamika tena kuwa binti karudi kule kule na akaniambia kuwa sasa anakusudia kufikisha suala hilo polisi. Lakini njia anayotumia haijanyooka vizuri. Kaniambia kuwa ana jirani yake polisi ambaye amemuomba aende kumkamatia yule mhalifu.

Jirani yake kakubali lakini amemwambia ampe shilingi elfu kumi ili amfanyie hiyo kazi. Yeye alisema hana hizo pesa, na akamwambia yule jirani kuwa amfanyie tu hiyo kazi kwa kuwa wanahusiana pia kiukoo. Jirani polisi hakusumbuliwa sana na hoja ya uhusiano wa kiukoo, na amemwambia mlalamikaji atafute angalau shilingi elfu tano ili afanye hiyo kazi.
 
Rais John Magufuli (wa pili kutoka kushoto), akiwa na marais wastaafu (kutoka kushoto kwenda kulia) Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Mrisho Kikwete, na Benjamini William Mkapa. (Picha kwa hisani ya CCM Blog)

Miongoni mwa vielelezo kuwa uongozi ni kazi kubwa ni pamoja na tukio hili. Kwenye ngazi hii ya chini, kujenga imani kuwa falsafa ya Sasa Kazi tu! itafanikiwa ili mradi yupo rais na waziri mkuu wachapa kazi ni ndoto tu. Mabadiliko chanya yatapatikana iwapo wote tutashiriki kwa namna tunavyoweza kuleta mafanikio tunayotarajia.

Wednesday, November 11, 2015

Adha za Mwenge wa Uhuru

Sina tatizo na madhumuni ya mbio za Mwenge wa Uhuru, lakini ninaona kasoro kubwa katika baadhi ya vipengele vya mchakato wa mbio hizo unavyoendeshwa.

Mwenge unapohamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, barabara zote huwa au hazipitiki au zinapitika kwa shida. Barabara zinafungwa mpaka Mwenge upite. Wale wenye shida za dharura wanakuwa hawawezi kutumia usafiri wa barabara kufuatilia shida zao.

Hata mgonjwa mahututi ambaye anapelekwa hospitali au kwenye kituo cha afya anaweza kujikuta ndani ya gari akisubiri Mwenge upite kwanza, ndipo gari alilopanda (kama siyo la kubeba wagonjwa) liweze kuruhusiwa na kuendelea na safari yake.

Gari zikiwa zimesimamishwa eneo la Kisesa, Mwanza, zikisubiri msafara wa Mwenge wa Uhuru upite.
Na isingekuwa vibaya sana iwapo watu wangelazimika kusubiri kwa muda kidogo tu kupisha Mwenge upite. Tatizo ni kuwa wakati mwingine watu husubirishwa kwa muda mrefu sana ili msafara wa Mwenge upite, hata pale ambapo msafara huo unaelekea njia tofauti. Ili mradi tu unapishana nao, basi utalazimika kusimama.

Mwenge wa Taifa ni nembo ya Taifa na nadhani maana ya kusimamishwa watu njiani ni kutoa heshima kwa hiyo nembo ya Taifa. Sijui kama hii ndiyo mantiki ya hatua hizi, lakini inawezekana pia kuwa watu husimamishwa kwa sababu ya kipengele kimoja ambacho nadhani kipo kwenye Sheria ya Usalama Barabarani ambacho kinatamka kuwa msafara rasmi ni lazima upishwe.

Nadhani msafara wa Mwenge unapewa hadhi ya msafara rasmi, kama msafara wa rais au viongozi wengine wa ngazi ya juu. Hatari iliyopo ni kuwa msafara wa Mwenge unaweza kumsubirisha mgonjwa mahututi na asiwahi kupata huduma ya matibabu ambayo inaweza kuokoa maisha yake.

Tuesday, November 10, 2015

Mwalimu Nyerere na nguzo ya uwajibikaji kwa wote katika uongozi

Kwenye kijitabu chake, Ujamaa ni Imani 1: Moyo kabla ya silaha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anasema:

Alinijia Mzanaki mmoja mwaka 1961, mara tu baada ya kupata uhuru. Anataka kazi; anasema, "Mzanaki ndiye Rais, basi sisi Wazanaki tutainuka." Nikamwambia, "Nenda, uko utaratibu wa kupata kazi." Akaniambia, "Na mimi vilevile niende huko?" Nikamwambia, "Kwa nini usiende huko?" Akasema, lazima nije kwako; sasa Mwalimu wewe umekwisha pata, ndugu zako wengine vile vile wapate. Sasa tusipoanza sisi Wazanaki waanze nani? Na wakubwa ndio wa kula, na wakati wa kula umefika; basi tule!"
            (Uk. wa 40)

Yameharibika mengi kwenye nchi hii kwa sababu viongozi wengi wanaamini kuwa uongozi ni sehemu ya kujineemisha wao na familia zao. Na kwa wale ambao hawana ndugu au marafiki kwenye sehemu muhimu za uongozi, uwezekano wa kupata ajira au haupo kabisa au ni finyu sana.
Mwalimu Nyerere

Kurudisha mfumo ambao unatoa fursa sawa kwa wote inawezekana kabisa.

Sunday, November 8, 2015

Yanayotokea niliyatabiri

Kwenye makala yangu ya tarehe 14 April 2015 kwenye gazeti la Jamhuri nilitoa maoni yangu juu ya Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 na kutahadharisha kuwa ni sheria ambayo itawafikisha wengi mahakamani, na hata gerezani.

Na tayari kuna kesi zimeshafikishwa mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kukiuka sheria hii.

Nilitoa hoja kuwa, pamoja na kuwa sheria hii inakusudia kudhibiti uhalifu unaotokea kwa matumizi ya mifumo ya mtandao wa habari na mawasiliano, ni sheria ambayo ina hitilafu kubwa zenye kuhatarisha uhuru wa kusambaza na kutoa maoni mbalimbali ndani ya jamii.

Hakuna raia ambaye analazimishwa kupenda sheria mbalimbali ambazo anaona zina kasoro au hitilafu. Lakini zinabaki kuwa ni sheria na yoyote ambaye hataki, kwa makusudi, kusimama kizimbani kujibu mashtaka ya kukiuka hizo sheria anapaswa kuwa mwangalifu asifike huko.

Njia muafaka ya kuepuka kuishia kubaya ni kuweka mikakati ya pamoja ya kupinga hizi sheria zenye kasoro kwa taratibu zilizopo, za kisheria.

Hoja ya kuwa unawezaje kupinga sheria zenye hitilafu kwa kutegemea serikali ambayo ilipitisha sheria hizi ni hoja yenye nguvu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania chama tawala kimeshinda uchaguzi kwa asilimia ndogo kuliko kwenye chaguzi zote zilizopita. Mimi naamini kuwa ushindi huo mwembamba unaweza kuleta mabadiliko hata kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa tofauti na serikali zake zilizopita, ikawa ni serikali ambayo inasikiliza maoni ya Watanzania na kuanza kupitia upya zile sheria ambazo zinalalamikiwa na watu.

Wasiposikiliza wajiandae kuongeza mahakimu, na kujenga magereza kwa wingi.

Monday, September 21, 2015

Ushauri kwa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza

Nimepiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 1985. Ningeweza kupiga kura mwaka 1980 lakini sikuwa nchini wakati huo, nilikuwa masomoni. Naamini kuna vijana wengi ambao watakuwa wanapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka huu na naomba nitoe ushauri mdogo kwao.
Nikiwa na Mwalimu wangu, Godian Muikza (kushoto) ambaye ni diwani anayemaliza muda wake wa Kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini.

Kwanza lipo suala muhimu la kuchambua ahadi. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1985 nilimpa kura ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi na ya ubunge nilimpa Kapteni Ukiwaona Ditopile Ramadhani Mwinshehe Mzuzuri. Siku zile sikuwahi kuhudhuria mkutano wowote wa kampeni za uchaguzi kwa hiyo kura yangu ya ubunge sikupiga kutumia kigezo kikubwa zaidi ya kufurahishwa na jina la mgombea. Sikumbuki hata alikuwa anagombea nafasi ile dhidi ya nani, lakini nakumbuka ilikuwa wanawania nafasi ya ubunge wa jimbo la Ilala. Mgombea urais, Mzee Mwinyi, alikuwa ana fursa ya kusikika zaidi ya wagombea ubunge kwenye vyombo vya habari kwa hiyo yeye tulimsikia zaidi ya wagombea ubunge.

Hata mwaka huu naamini kuna wapiga kura wengi watajitokeza wa aina yangu, kama nilivyokuwa mimi mwaka 1985 na kupiga kura kwa kufurahishwa na jina la mtu tu bila hata kuchambua kwa makini sera anazowakilisha mgombea huyo. Mwaka 1985 hatukuwa na vyama vingi, lakini sasa vipo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya msingi ya mpiga kura yoyote kuacha kuweka sera za vyama kwenye mizania na kuamua chama kipi kitapata kura yake. Hatuna uhakika kuwa yanayoahidiwa yatatekelezwa, lakini bado ni muhimu kuchambua sera tofauti. Akishinda mtu wako na asipotekeleza ilani yake angalau unayo sehemu ya kuanzia kumhoji. Kama ulimchagua kwa mkumbo tu hutakuwa na kigezo cha kuamua kuwa hajatimiza ahadi zake.
Wapiga kura wa Butiama wakipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010


Pili, nazungumzia wale ambao wana uhakika mkubwa wa matokeo ya ushindi kwa wanaowaunga mkono, ikiwa ni vyama vya siasa au mgombea mmoja mmoja. Kusikiliza na kuamini na kauli kama “ushindi ni lazima” ni mwanzo wa kukaribisha vurugu. Kama kiongozi anatumia kauli hiyo kuhamasisha tu wafuasi wake ili waweke juhudi kubwa kwenye kampeni inaweza kuwa haina madhara. Lakini kauli hiyo inaweza kufasiriwa kuwa “tumeshashinda hata kabla ya kupiga kura na mtu yoyote atakayesema kuwa hatujashinda ni muongo na ametuibia kura.” Hapo tunakaribisha vurugu.

Mwaka 2010 niliteuliwa wakala wa mgombea ubunge na nilijifunza kitu kimoja cha msingi. Kama wakala wa mgombea yuko makini, siyo rahisi kuibiwa kura. Sikulala siku hiyo mpaka matokeo yalipothibitishwa na msimamizi wa uchaguzi alfajiri ya siku iliyofuata. Wanaoibiwa kura ni wale ambao wameweka mawakala ambao siyo waaminifu au ambao hawakuwa makini. Mtu akitaka kuibiwa, ataibiwa.
Kulia ni Mhe. Vincent Nyeerere, Mbunge wa Musoma Vijijini kupita Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) anayemaliza kipindi chake cha ubunge aliyeniteua kusimamia kura zake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kushoto ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kapteni Godfrey Ngatuni.
Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi tumesikia shutuma kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo wataalamu wa kuiba kura. Kama hizo shutuma ni za kweli, sioni sababu yoyote ya kutoana roho kwa sababu sasa hivi Mhe. Edward Lowassa amehamia upande wa pili. Yeye amekulia na kujifunza siasa ndani ya CCM na, kwa vyovyote vile, atakuwa amehama na uelewa uliobobea wa mbinu zinazotumika kuiba kura na atakuwa anafahamu mbinu za kutumika kuzuwia wizi huo. Mwizi hawezi kumuibia mwizi.
Mwanachama wa Chama cha wananchi (CUF) akielekea kwenye mkutano wa kampeni jijini Mwanza mwaka 2010.

Kwa sababu hii sioni kabisa busara ya mtu yoyote kutamka kuwa kaibiwa kura kama yeye mwenyewe hataki kuibiwa kura. Labda atumie kauli hiyo kama kisingizio cha kupinga matokeo. Tunao wajibu wa kujenga mazingira yenye kulinda amani, lakini tunao pia uwezo wa kuweka mazingira yanayobomoa amani.

Uchaguzi huu umeibua ushindani mkubwa kati ya CCM na vyama vinavyowakilishwa na UKAWA. Kwa bahati mbaya, ushindani unaonyesha dalili za uhasama na muelekeo kuwa kipindi hiki cha kampeni kitaibua matukio ya kuvunjika kwa amani. Lakini amani itavunjika tu iwapo wapiga kura tutakubali ivunjike. Na amani inapovunjika hutasikia hata siku moja kuwa Mhe. John Magufuli au Mhe. Edward Lowassa kavunjika mguu kwa sababu ya vurugu za kisiasa.


Bado sijaona sababu ya msingi ya kuvunjika kwa amani kutokana na uchaguzi. Usikubali kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani.