Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, May 18, 2014

Mwanza, juzi

Juzi nikiwa jijini Mwanza, mtu mmoja nisiyemfamu aliniomba pesa. Nilimjibu kuwa sikuwa na pesa za kumpa. Aliendelea kuniomba. Nilisisitiza sikuwa na pesa.

Akasema: "Du! Sasa mheshimiwa unaniacha na hali mbaya sana."

Mimi: "Vumilia. Leo huna, kesho utapata."

Yeye: "Tutafika kweli? Eti wanasema tusubiri mpaka mwaka 2025 ndiyo mambo yatakuwa mazuri kwetu sisi maskini? Tutakuwa bado tunaishi kweli?

Mimi: "Vumilia. Tutafika."

Niliondoka nikiwaza kuhusu matarajio ya raia mwenzangu kuhusiana  na Visheni ya Maendeleo ya 2025 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Ikifika tarehe 1 Januari 2026 na hali yake iko vile vile patachimbika.

Tuesday, May 13, 2014

Uandishi ni kazi kweli kweli!

Ni muda mrefu sasa sijachapisha habari zozote hapa kwenye blogu yangu. Uandishi wa mara kwa mara siyo kazi ndogo, hasa pale mwandishi anapotarajiwa kuongea jambo la maana kila wakati, na kufanya hivyo mara kwa mara.

Tatizo mojawapo linalonizuwia kuandika mara kwa mara ni kusafiri huku na kule kwa shughuli mbali mbali. Nimejenga mazowea ya kuandika nikiwa sehemu moja tu: nyumbani. Ninaposafiri sipati utulivu wa kutosha kuniwezesha kuandika vyema.

Hata hivyo naweka kando hivyo visingizio na natarajia kuanza tena kuhuisha blogu hii kwa kuweka habari hapa na maoni yangu ya masuala kadha wa kadha.

Friday, December 27, 2013

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Tatu na ya Mwisho)

Kwenye makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na alizikwa  tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunu nchini Afrika ya Kusini.

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Tatu na ya Mwisho)
Na Notburga Maskini*

Heshima katika historia ya nchi na dunia
Kilio kinachoendelea hivi sasa na heshima kubwa waliyopewa mashujaa wetu waliolala ni changamoto kubwa kwa kizazi kinachofuata. Walijitoa thamani kupigania heshima ya binadamu. Kinachoendelea sasa ni heshima kubwa kwao hata wakiwa wamelala na kama alivyowahi kusema Mzee Mandela katika nukuu zake: “Ukijiheshimu hata simba atakuogopa na kukuheshimu”. Taarifa zilizotangazwa na gazeti moja nchini kuwa Alqaida na al Shaabab hawatafanya mashambulizi katika kipindi hiki cha maombolezo ni kielelezo cha ukweli wa nukuu hiyo ya shujaa wetu, Baba wa Taifa la Afrika ya Kusini.
 
Waombolezaji wakitoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Nelson Mandela tarehe 11 Desemba 2013, wakati mwili wake ulipohamishiwa kwenye majengo ya Union jijini Johannesburg. (Picha ya GCIS).
Hii ni heshima japo yeye hafungamani na itikadi wala vitendo vya makundi hayo bali anafungamana na upendo, msamaha na kutokulipa visasi. Naamini iwapo dunia itajifunza haraka kutoka kwa shujaa huyu pengine vitendo hivi vinaweza kuisha na wahusika kuendelea kuwa watu wa amani.

Je tuko tayari kujifunza?
Sisi tuliobaki nyuma pamoja na kuomboleza tuna maswali ya kujiuliza na kutoa majibu sasa, iwapo:
1)      Tuko tayari kurejesha na kuendeleza mfumo wa kidhalimu unaodhalilisha na kunyonya binadamu wengine hasa wafanyakazi na wakulima;
2)      kuwafanyisha kazi ngumu wafanyakazi na wakulima bila kuwalipa ujira stahiki au kuratibu bei za mazao yao kwa kisingizio cha utandawazi huku kukiwa na lengo la kushirikiana na wanyonyaji kujilimbikizia mali binafsi kupitia jasho lao;
3)      kuendeleza wizi wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya wanyonge na kupuuza ustawi na maendeleo yao.

Ama:
1)      Tunadhamiria kujifunza kwa mashujaa wetu Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere, kuenzi maisha yao, na kuendeleza mema yao, kwa kuwa wafanyakazi bora, watumishi waadilifu, wabunifu, na waaminifu wa wananchi wetu;
2)      Haki na nafasi za raia kumiliki rasilimali za mataifa yetu kwa usawa zinalindwa na kuwezeshwa hata kama maisha na maslahi binafsi yatatishiwa;
3)      Tutawalinda na kutetea haki za kiraia, na kuishi bila kuwatisha, kuwauwa katika kulipiza visasi au mapigano ya wenyewe kwa wenyewe,  kwa lengo la kustawisha jamii, kuondoa umaskini, na kudumisha heshima ya binadamu iliyoasisiwa na mashujaa hawa.

Kupokea mauti kwa ujasiri na fedheha za kiuongozi
Inaleta maana kuchagua kulinda na kutanguliza maslahi ya umma na Taifa, ili historia isije tuhukumu kwa kutotimiza wajibu tunaopaswa kufanya kwa jamii na nchi zetu wakati wa uhai wetu. Hali hii itatuwezesha kupokea mauti kwa ujasiri na imani kubwa. Kitendo cha fedheha kilichomkuta kiongozi mkuu wa sasa wa Afrika Kusini kuzomewa mbele ya uso wa dunia  na wananchi wake waliomchagua kidemokrasia si cha kupuuzwa hata kidogo. 

Ni muhimu kujifunza na kujitahidi kubadilika ili kuepusha shari na matokeo mengine mabaya ambayo huletwa na tabia za viongozi kuonekana wanajijali binafsi. Kuwaumbua viongozi hasa wale wasiojitambua husababisha hasira na kulipiza kisasi kwa wanaothubutu kufanya hivyo. Hali hii husababisha mitafaruku; huweza kugawa taifa na kuondoa amani. Naamini yote mazuri yaliyopiganiwa wakati wa uhai wa Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere yamewekwa katika msingi imara ya kuwezesha kuyaendeleza. Kazi kubwa ni kwa tuliobaki nyuma kuamua na kuanzia walipoachia.

Kwaheri Mzee Nelson Rolihlalha Mandela. Mungu akupumzishe kwa amani na raha ya milele akujalie kama ulivyonuwia katika matendo na maisha yako.


*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Friday, December 20, 2013

Leo kumbukumbu ya kufariki Hayati Alex Nyirenda

Leo ni miaka mitano tangu kufariki Hayati Brigedia Alex Gwebe Nyirenda aliyefariki Dar es Salaam mwaka 2008 kwa ugonjwa wa saratani ya koo.

Usiku wa tarehe 8 Desemba mwaka 1961, muda mchache kabla ya kutimia saa 6:00 kamili usiku, siku ambapo Tanganyika ilipata uhuru wake, Brigedia Nyirenda alikuwa kileleni mwa Mlima Kilimanjaro kupandisha bendera ya taifa jipya la Tanganyika wakati bendera ya Uingereza ilipokuwa inateremshwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Luteni Alex Nyirenda, akiwa na bendera ya Tanganyika na Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro siku Tanganyika ilipopata uhuru wake, tarehe 9 Desemba 1961. (Picha ya Idara ya Habari, Maelezo
Miaka mwili kabla, tarehe 22 Oktoba 1959, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akihutubia Baraza la Kutunga Sheria, alisema yafuatayo:

Sisi watu wa Tanganyika tunataka kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilmanjaro umulike nje ya mipaka yetu na kuleta tumaini pale ambapo kulikuwa hakuna matumaini, upendo pale ambapo palikuwa na chuki, na heshima pale 

palipojaa dharau.

Miaka miwili kabla, tarehe 22 Oktoba 1959, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akitoa hotuba kwenye Baraza la Kutunga Sheria, alisema yafuatayo: 
Huu mwenge ambao baadaye ulikuja kujulikana kama Mwenge wa Uhuru ulisimikwa juu ya Mlima Kilimanjaro na Nyirenda, ukiashiria msimamo wa muda mrefu na usiotetereka wa Tanzania kuunga mkono juhudi za ukombozi wa nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya mwanzo ya sitini zilibaki chini ya ukoloni na tawala za kibaguzi.

Mwaka 1958 Nyirenda alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuhitimu kutoka Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst cha nchini Uingereza. Aidha, kabla ya uhuru, alikuwa Mwafrika wa kwanza kuwa afisa ndani ya Kings African Rifles, jeshi la kikoloni la Uingereza ambalo baada ya uhuru ndiyo likabadilishwa na kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Alikuwa na uhusiano wa kiukoo na rais wa zamani wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, jambo ambalo linakumbusha Waafrika kwamba wako karibu sana kuliko mipaka ya nchi zao inavyoashiria.

Wednesday, December 18, 2013

Lugha Yetu Kiswahili

Hivi karibuni, wakati nikisikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili la Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mtangazaji alisoma taarifa za majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuanza kutumia ndege zinazosemekana kuruka bila rubani, kwa Kiingereza zikijulikana kama drones.

Ukweli ni kuwa ndege hizo zinaongozwa na marubani ambao wako ardhini kwenye vituo maalum.

Mtangazaji alitumia neno "drone" lakini akauliza iwapo lipo neno la Kiswahili lenye kutoa maana hiyo hiyo. Mimi haraka haraka niliangalia kwenye kamusi ya Kiingereza kwa Kiswahili ya Taasisi ya Uchungizi wa Kiswahili (TUKI), toleo la mwaka 2006, na nikatuma ujumbe mfupi wa maandishi BBC: "drone ni nyuki dume."

Wasikilizaji wengine nao wakatuma majibu yao, mmoja akipendekeza kuwa tafsiri sahihi iwe "ndege tiara." Hayakuwa mashindano na hakuna aliyepewa zawadi yoyote, lakini nakiri kuwa "ndege tiara" inasikika vizuri zaidi kuliko "nyuki dume."

Habari inayozungumzia shambulizi la nyuki dume dhidi ya wapiganaji itachukuliwa na maana kuwa ni nyuki ndiyo waliofanya shambulio hilo na siyo ndege inayoruka angani.

Wataalamu wa lugha ya Kiswahili mnasemaje?