Nilimudu kwa jitihada kubwa kuishi hizo siku kumi bila kula nyama na niliporudi Tanzania watu walioniona walisema kuwa nilionekana kijana kuliko ninavyostahili. Nilihisi kuwa yawezekana kuwa kulishwa mboga za majani kwa siku kumi bila hiari yangu nikiwa London ndiyo kulisababisha mimi kuonekana kijana.
Imani yangu kuwa ulaji wa mboga za majani kwa siku kumi ndiko kulisababisha kupunguza kuzeeka kwangu ilinisukuma kuacha kula nyama na nikaanza jitihada ya kuwa mlaji mboga za majani tu na kuacha kula aina zote za nyama.
Mwaka mmoja baada ya hapo, nikiwa kwenye mkutano jijini Maputo, Msumbiji, nilipata fursa ya kuonana na Dk. Kenneth Kaunda, rais mstaafu wa Zambia ambaye ni maarufu pia kuwa mtu ambaye hali nyama.
Rais mstaafu wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, kulia. |
Aliniambia aliacha kula nyama mwaka 1952 kupinga sera za kibaguzi za serikali ya kikoloni ya Waingereza iloyoelekeza wamiliki wa bucha kuweka madirisha mawili tofauti ya kuwauzia nyama Waafrika na wazungu. Yeye hanywi pombe, kahawa, wala chai lakini anakunywa maji ya matunda kila siku.
Kitendo hicho cha upinzani wa kisiasa kinaelekea kufanikisha kupunguza idadi kubwa ya miaka ya huyu rais mstaafu mwenye umri wa miaka 88. Ni mwingi wa nguvu na mchangamfu sana. Kwenye mkutano Maputo kila alipoitwa kwenye jukwaa alienda kwa mchakamchaka.
Mtanziko mkubwa unaonikabili, mkubwa zaidi kuliko uamuzi wa kuacha kula nyama, ni kipi kitakachofuata kuacha kula kati ya samaki na kuku.
No comments:
Post a Comment