Mada yangu ya leo siyo ndefu, lakini naamini ni ya muhimu sana.
Ni kwanini watu wengi huwa wagumu sana kutimiza ahadi za muda? Ni kwanini hawawahi kwenye ahadi wanazopanga na watu wengine? Nakiri kuwa tatizo hili hata mimi hunikuta mara moja moja, nikiwa mmojawapo wa watu wanaochelewa kwenye ahadi. Lakini nikijilinganisha na wengine, naona kuna tofauti mkubwa.
Mimi nimeishi kijijini Butiama kwa muda mrefu sasa, na nimeshuhudia kuwa suala la muda halipewi kipaumbele hata kidogo. Nimewahi kupanga mikutano na wanakijiji wenzangu mara kadhaa na pale tulipokubaliana kuwa mkutano utakuwa saa kumi jioni, watu wachache ambao unaweza kusema waliwahi kufika walianza kuingia kwenye ukumbi saa 10:45. Nilipolalamika kwanini wamechelewa kwenye kikao, waliniambia kuwa saa kumi ilimaanisha ni muda wote kati ya saa 10:01 had saa 10:59. Aidha, waliniambia kuwa ningetaka kikao kianze saa kumi basi ningewaarifu watu kuwa kikao ni saa 9:00.
Mimi sikubaliani na wanaosema kuwa hili ni tatizo la Waafrika. Ni Uafrika gani huo ambao hujitokeza siku moja na kujificha siku nyingine? Mwaafrika huyo huyo ukimwambia kuwa basi la kwenda Arusha litapita Butiama saa 11:30 alfajiri atawahi kituoni nusu saa kabla, lakini kwenye ahadi nyingine anachelewa.
Kuwahi katika vikao ni muhimu sana kwa sababu muda ule unaopotezwa kwa kusubiri wachelewaji ungeweza kutumika kufanya mambo kadhaa ya uzalishaji na maendeleo. Nina hakika kuwa hizo dakika ambazo tunazipoteza Tanzania katika mwaka mmoja zinaleta hasara kubwa sana kwenye uchumi.
Monday, May 10, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment