Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, May 2, 2010

Watemi na nyoka


Umbali wa kilomita 20 toka Butiama kwenye barabara inayoelekea Fort Ikoma na kwenye mbuga za Serengeti kipo kijiji cha Nyamuswa, makazi ya aliyekuwa Mtemi wa Ikizu, Chifu Mohamed Makongoro Matutu aliyefariki mwana 1958.

Nimetembela makazi ya Mtemi Makongoro mara kadhaa na kufahamishwa kuwa kuna nyoka mkubwa katika eneo la mawe lililopo karibu na makazi yake. Mwanae mmoja ambaye alinizungusha kwenye eneo hilo kumsaka huyo nyoka anasema ni nyoka wa siku nyingi sana na yeye anakumbukua kuwepo huyo nyoka hapo nyumbani wakati wa utoto wake, yeye mwenyewe kwa sasa nikikadiria ana miaka karibu 60.

Ingawa hatukufanikiwa kumuona huyo nyoka mkubwa na mkongwe niliambiwa ni nyoka ambaye yuko eneo hilo la Mtemi Makongoro kwa ridhaa ya Mtemi mwenyewe na kwa sababu hiyo wanaoendelea kuishi pale hawamdhuru. Mara moja moja hujitokeza kutoka eneo la kilima na mawe na kuota jua nyakati za asubuhi, lakini wakati mwingine hutoka eneo hilo ambalo liko mwendo mfupi kutoka makazi ya watu na kupitapita wanakoishi watu. Inasemekana kuwa ni nyoka wa miaka mingi sana mpaka ameota majani sehemu ya juu ya kichwa chake.

Hapa Butiama, eneo ambalo aliishi Mtemi Nyerere Burito ni eneo lenye nyoka mkubwa ingawa hata huyo bado sijapata fursa ya kumuona. Huyo nyoka huishi ndani ya nyumba mojawapo ambayo alikuwa akiishi Mwalimu Nyerere, nyumba ambayo haitumiki kwa muda mrefu sasa. Nyoka huyo huhama kwenye nyumba hiyo watu wanapoitumia, lakini hurudi ndani wanapoondoka.

Imani za Wazanaki kuhusu wanyama na nyoka zinaweza kuwa zinafanana kidogo na zile za Waikizu wa Nyamuswa. Wazanaki hawadhuru wanyama, hasa wale wanaoishi katika maeneo alipoishi mtemi. Kuna imani wanyama hao wanaweza kuwa ni mizimu.

Katika chumba kimojawapo cha nyumba inayosemekana ina nyoka huyo mkubwa nimekumbana na nyoka wadogo mara kwa mara kwenye meza ninayotumia kufanya kazi zangu, pamoja na kuwashuhudia wakipita kwenye sakafu. Inaelekea ni nyoka ambao huzaliwa ndani ya nyumba lakini wakikua hutoka nje ya nyumba. Hivi karibuni nimewatoa nje nyoka wadogo watatu, na kwa kuwa muda kidogo umepita bila kuwaona nahisi uwepo wangu ndani ya nyumba ile unawafanya waanze kuihama.
Kwa muda mrefu nilikuwa nahisi kuwa aina ya nyoka ambao nimewona na kuwatoa nje ni wenye sumu kali, lakini sikuweza kuthibitisha mpaka hivi karibuni. Kitabu cha aina mbalimbali ya nyoka kinaainisha kuwa nyoka aliye kwenye picha (juu) ambaye nilimtoa nje anajulikana kama Mamba Mweusi (Black Mamba). Anaitwa Mamba Mweusi kwa sababu akifungua mdomo eneo lote la ndani ya mdomo pamoja na ulimi wake una rangi nyeusi. Anapokua anafikia urefu wa zaidi ya mita 2.

No comments: