Promota wa ndondi za kulipwa, Ibrahim Kamwe, anaeleza kwa nini baadhi ya mabondia wanajiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Siku za hivi karibuni kuna vimaendeleo kidogo kwa baadhi ya
mabondia; tunafanya mazoezi katika
vilabu vya pombe kwa kuwalipa kodi ya mazoezi wenye baa. Naweza kusema Tanzania
hakuna sehemu rasmi za kufanyia mazoezi ya ndani zilizotengwa na serikali
kwa ajili ya raia wake wapenda michezo na kama zipo ni chache na ziko katika
makambi ya jeshi kwa masharti magumu kwa raia wa kawaida.
Siku za nyuma wakazi
wa mjini kama vile Kisutu, Gerezani na Kariakoo walikuwa wanafanya mazoezi pale
Arnatoglou. Siku hizi huwezi kusikia kuna mwanamichezo katokea Gerezani au
Kariakoo. Iliyobaki kwao ni kuuza na kutumia madawa ya kulevya na kukimbizana
na wafanyabiashara wa maeneo hayo. Naweza kuilaumu serikali kwa kutoendeleza
michezo bali ilishiriki kuuwa kabisa michezo maeneo hayo na mengineyo zaidi.
Kwa sisi tulioanza kukua kimichezo pambano la ngumi likiandaliwa
huwa tunalipwa kuanzia shilingi 5,000/- mpaka 20,000/- kwa mapambano haya
madogomadogo na iwapo kutakuwa na pambano kubwa na kupata bahati ya kucheza
unaweza kulipwa shilingi 40,000/- mpaka 100,000/-. Mapambano makubwa yanaweza
kuwa moja, mawili, au matatu kwa mwaka; hayazidi hapo. Haya mapambano madogo
tunaweza pata mawili mpaka sita kwa mwaka.
Msiwaone mabondia wakicheza mkadhani wana kipato kikubwa. La
hasha! Ni wale tu wachache waliobahatika kupata wadhamini au waratibu wenye
uwezo wa kipesa ndiyo kidogo hutoka.
Kwa sisi wengine ukiangalia elimu ya kusoma hatuna, kazi hakuna,
na mchezo wa ngumi tunaupenda na pengine tuna vipaji na kufanya vizuri
katika mapambano yetu. Hivyo mchezo ndiyo huwa kama ajira yetu kwa sababu
tunapata chochote kidogo kupitia mchezo huo kuliko kuiba au kukimbizana na
mapolisi katika kamari na kuishia jela.
Kwetu sisi mabondia huona ni jambo la kifahari na hufurahi mno
pale tu tunapopata pambano la nje ya nchi na hufurahia kupanda ndege na vile
vimisosimisosi tunavyopata tukiwa mahotelini ugenini. Tukihadithiana mambo ya
safari uswahilini kwetu tunahisi tunakosa mambo mengi ya raha.
Hapo ndipo mawakala wa ngumi hutupata na mabondia huwa wanadiriki
kukubali kwenda kucheza popote tukijua tutapanda ndege, tunakula raha bila
kujali na wala kuhoji tuendako tutalipwa kiasi gani cha pambano
nitakalocheza wala kujua usalama wangu.
(itaendelea
na sehemu ya tatu)
No comments:
Post a Comment