Promota wa ndondi za kulipwa, Ibrahim Kamwe, anaeleza kwa nini baadhi ya mabondia wanajiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Ibrahim Kamwe |
Asili ya mabondia wengi duniani wanatoka katika familia
duni. Kwa mfano hapa kwetu ni nadra kumkuta bondia ametoka Upanga, Oysterbay,
au Masaki ushuwani, nikiwa na maana mabondia wengi wanatoka uswahilini. Ni
watu wa hali duni. Wengi wetu hatujakalia madawati ya shule na wengine
tuliojitahidi tumefika darasa la tano au sita. Kama wazazi walikomaa ndiyo
tunamaliza la saba.
Baadhi yetu tukiwa na umri wa kuanzia miaka sita nyumbani huwa tunaanza
kupewa uzowefu wa kuuza visheti, maandazi, vitumbua, karanga n.k. na vikibaki
nyumbani hauli chakula mpaka viishe. Shuleni mwalimu mkali, darasani hafundishi
mpaka usome tuisheni ndiyo unapata kufundishwa kidogo, na ukishindwa maswali
yake unapata viboko vya ghadhabu. Hapo ndipo tunapoamua kuachana na shule na
kutinga mitaani. Michezo yetu ni katika madampo na vichochoroni na tukifikia
umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea tunajua jinsi ya kutafuta pesa kwa kuuza
njiwa, kucheza kamari, malani, kuiba kuku na bata, na kwa wale walio watukutu
zaidi kuuza na kuvuta bangi ni sehemu ya maisha ya kawaida tu huku mitaani
kwetu.
Mara nyingi mlo kwetu ni mmoja tu kiubishoo au kuwa wageni ndiyo
tunakula milo miwili. Katika maisha yetu muda mwingi tupo huru na michezo
kuliko kusoma, hasa kolokolo, ngoma, mpira, na ngumi. Mpira tunacheza mabarabarani,
vichochoroni, na kwenye madampo, wakati ngumi tunajifundisha katika makamali,
vichochoroni, au uwani kwa kina masta. Begi au tairi linafungwa juu ya mti,
tizi linaendelea bila vifanyio vya mazoezi vilivyo rasmi. Mwendo mdundo
tunasonga na tunashinda au kufanya vizuri katika mashindano yetu tunayoshiriki
na hali yetu duni hii hii ya kimaisha, na majina yetu kutangazwa sana katika
vyombo vya habari na kupata umaarufu mkubwa nchini, nchi jirani na hata
nchi za Ulaya.
Lakini ukibahatika kututembelea na kuangalia tunapoishi na familia
zetu na umaarufu tuliyonao, utakuta maisha yetu mabovu na yanasikitisha.
No comments:
Post a Comment