Ukisikiliza
sehemu kubwa ya maoni ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi juu ya kiongozi
wa Cuba Fidel Castro, utaafiki kuwa hana mchango wowote wa maana kwa binadamu wenzake.
Inahijati kujikumbusha kidogo sehemu ya historia ya ukombozi wa bara la Afrika ili
kupata picha tofauti.
Castro,
kiongozi wa Cuba kwa karibia miaka 50, amefariki hivi karibuni na kuzikwa
jijini Havana. Ni aina ya kiongozi ambaye anapewa sifa nyingi na kushutumiwa
vikali wakati huo huo.
Hatushangai sana kusikia ukosoaji
mkubwa dhidi ya Fidel Castro na uongozi wake. Yeye, pamoja na wapiganaji
wenzake waliongoza mapambano mwaka 1956, na hatimaye kufanikiwa kufanya mapinduzi
mwaka 1958, yaliyong’oa madarakani utawala wa Fulgencio Battista uliokuwa unaungwa
mkono na Marekani. Ni kuangushwa kwa Batista ndiyo kuliibua uhasama wa Marekani
dhidi ya Cuba.
Kufanikiwa kwa mapinduzi
dhidi ya Batista ilikuwa tishio kubwa dhidi ya Marekani katika nyanda nyingi.
Lakini hatari kubwa zaidi kwa Marekani ilikuwa kufanikiwa kwa kundi dogo la
wapiganaji walioanzisha mapambano wakiwa na bunduki mbili tu, na hatimaye kufanikiwa
kuangusha utawala ulioungwa mkono na taifa kubwa. Kwa sera za nchi za nje za
Marekani, eneo la Amerika ya Kusini lilikuwa himaya yake na Cuba ya Castro
ilikuwa mfano wa kupata jirani mpya mkorofi.
Huu ulikuwa mfano
hatarishi kwa maslahi ya Marekani, mfano ambao ungeweza kuigwa na watu kwenye
mataifa mengi ya Amerika ya Kusini ambapo Marekani ilikuwa imesimika nguvu zake
za kiuchumi na kijeshi.
Wakati huo Ukomunisti
ulionekana kama kirusi ambacho kisipodhibitiwa kingeweza kusambaa na kuathiri
mawazo ya mamilioni ya watu ulimwenguni. Cuba ya Fidel Castro haikupaswa
kufanikiwa kwa hali yoyote. Mwaka 1960 serikali ya Cuba ilipotaifisha mitambo
ya kusafisha mafuta ghafi iliyomilikiwa na kampuni za Marekani serikali ya
Marekani ilianzisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba, vikwazo ambavyo bado
vimekuwepo kwa zaidi ya miaka 55.
Licha ya kuwepo vikwazo
hivi vya kiuchumi Cuba imefanikiwa kufikia maendeleo makubwa katika huduma za
afya, kuongezeka kwa umri wa kuishi, kufanikiwa kwa mpango wa chanjo kwa
watoto, na kuboreshwa kwa mifumo ya elimu ambayo inalingana hata na nchi
zinazotajwa kuwa zimeendelea. Tanzania tunatambua mchango wa Cuba katika kuleta
madaktari ambao wamefanya kazi maeneo mengi ya nchi. Lakini Cuba haijatoa
msaada wa madaktari tu, bali imesomesha maelfu ya madaktari siyo tu kutoka nchi
zinazoendelea bali hata kutoka mataifa makubwa ikiwemo Marekani yenyewe.
Kwenye bara la Afrika,
pamoja na kuandamwa na Marekani na nchi za Magharibi, Cuba imetoa mchango
mkubwa sana katika jitihada za Waafrika za kusaka na kulinda uhuru wa nchi zao.
Miaka ya sitini Cuba ilituma wapiganaji wake nchini Algeria, Congo, na Guinea
Bissau.
Katika miaka ya themanini
tulishuhudia tena utayari wa Cuba kusaidia Waafrika kutetea maslahi ya nchi zao
dhidi ya nguvu ya ubepari na ubeberu. Wanajeshi wa Cuba walipigana na wenzao wa
Angola kudhibiti mashambulizi ya jeshi la serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini
yaliyokuwa yamevamia Angola tangu 1983. Mwaka 1988 kwenye mapambano
yaliyofanyika kwenye mji wa Cuito Cuanavale wanajeshi wa Afrika ya Kusini
walishindwa kuvuka ngome iliyosimikwa na wanajeshi wa Cuba, Angola, na
wapiganaji wa vyama vya ukombozi vya Afrika ya Kusini na hivyo kushindwa
kutimiza kusudio lao la kuteka mji mkuu Luanda.
Kuiokoa Afrika ya Kusini
aibu ya kushindwa kwenye mapambano ya Cuito Cuanavale, Marekani, ambayo nayo
kimaslahi ilikuwa upande wa Afrika Kusini kwa kisingizio cha kupinga kusambaa
kwa Ukomunisti nchini Angola na barani Afrika, ilijitokeza kama msuluhishi kati
ya Cuba, Angola, na Afrika ya Kusini. Ushindi huu kwa Angola na Cuba ndiyo uliharakisha
uhuru wa Namibia chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Aidha, kwa ushindi ule
watawala wa serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini wakang’amua kuwa kipo
kikomo cha kutumia nguvu za kijeshi kulinda utawala wao wa kibaguzi. Kuendelea
kuanguka kwa tawala za kibaguzi kwenye makoloni ya Ureno, pamoja na Zimbabwe
kulionekana tishio kwa utawala wa Afrika ya Kusini, na hivyo kuchochea mikakati
ya hujuma na vita dhidi ya nchi jirani ambazo zilitoa msaada kwa harakati za
ukombozi za Afrika ya Kusini.
Kwa pigo moja la Cuito
Cuanavale Cuba ya Fidel Castro ikaweka chachu ya ukombozi kwa Angola, Namibia,
na Afrika ya Kusini.
Kama wapo Waafrika ambao
watauonea aibu mchango huu mkubwa wa Fidel Castro na Cuba kwa bara la Afrika,
basi tukubali kuwa maneno tunayolishwa kila siku yamefanikiwa kutufundisha
kusikiliza yale tunayoambiwa tu na kutuzuwia kufanya maamuzi yetu wenyewe juu ya
nani ni muhimu katika historia ya bara letu. Cha ajabu ni kuwa baadhi yetu tuko
tayari kuyakubali hayo maneno kutoka kwa wale wale ambao wakati wa mapambano
walishikamana na kusaidiana na maadui wa ukombozi wa bara la Afrika.
Hawapo viongozi wasiyo na
mapungufu, na hata kama Fidel Castro alikuwa na mapungufu katika uongozi wake, haituzuwii
Waafrika kutambua mchango wake muhimu katika ukombozi wa bara letu. Hili suala
linahitaji kuisoma historia tu, halihitaji hata mjadala.
No comments:
Post a Comment