Nachapisha tena makala iliyochapishwa tarehe 26 Aprili 2016 kwenye safu yangu "Ujumbe toka Muhunda" ndani ya gazeti la Jamhuri. Katika makala hiyo narudia ukweli ambao unasahauliwa, ya kuwa wazo la muungano ni wazo la Sheikh Abedi Amani Karume. Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuuwawa kwake.
********************************
Muungano ni pendekezo la Sheikh Karume
Na G. Madaraka Nyerere
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo unatimiza miaka 52. Kwa
binadamu miaka 52 siyo haba, na aliyoitimiza tunamuita mzee. Kudumu kwa muda
mrefu kiasi hiki kunapaswa kupongezwa, ingawa si wakati wote wanaostahili
pongezi wanaipata.
Tarehe ya leo, miaka 52 iliyopita, Mwalimu Julius Nyerere na
Sheikh Abeid Amani Karume, waliweka sahihi hati ya kuunganisha Tanganyika na
Zanzibar. Lakini wengi wanapoandika au kuzungumzia Muungano huweka msisitizo wa
mchango wa Mwalimu Nyerere na imani yake kubwa juu ya umuhimu wa kuungana. Kwa
maoni yangu, Sheikh Karume hapati sifa anayostahili kama muasisi wa Tanzania.
Kwenye mahojiano ndani ya filamu iliyoandaliwa na M-Net,
Mzee Rashidi Kawawa alifafanua kuwa wazo la kuunganisha Tanganyika na Zanzibar
lilitolewa na Mzee Karume, halikuwa wazo la Mwalimu Nyerere. Ni kweli kuwa Mzee
Karume alitoa wazo kwa mtu ambaye tayari alikuwa anaamini juu ya umuhimu wa
umoja, na bila shaka ndiyo sababu ya kukubaliwa.
Naye Mama Maria Nyerere amesimulia kuwepo Ikulu Dar es
salaam siku Karume alipotoa wazo hilo. Mzee Karume alikuwa Dar kwa shughuli za
kikazi, na ni katika mazungumzo na Mwalimu baada ya mazungumzo yake rasmi ya
kikazi ndipo mazungumzo ya muungano yalianza. Mwalimu alianza kulalamika juu ya
kasi ndogo ya mchakato wa kuunganisha nchi tatu za Afrika Mashariki ili kuunda
shirikisho. Hapo hapo Karume alimwambia Mwalimu kuwa kama mchakato huo
unachelewa, basi yeye yuko tayari Zanzibar iungane na Tanganyika. Na kuongeza:
“Wewe utakuwa rais, mimi nitakuwa makamu wako.”
Wazo la kujenga umoja halikuwa geni kwa Mwalimu Nyerere, kwa
hiyo haihitaji utafiti wa kina kubaini sababu ya kulikubali mara moja na kulivalia
njuga wazo la Mzee Karume. Agenda ya kuleta umoja wa nchi za bara la Afrika
ilikuwa ni mojawapo ya mikakati ya chama cha TANU wakati wa harakati za
kutafuta uhuru wa Tanganyika.
Wataalamu wengi wa kikatiba wamekosoa taratibu zilizofuata
kukamilisha wazo la Mzee Karume mpaka kufikia kuwekwa sahihi hati ya Muungano kati
yake na Mwalimu Nyerere tarehe 26 Aprili 1964. Na hapa lawama kubwa
inamuangukia mpokea wazo, Mwalimu Nyerere.
Pamoja na kwamba ziko hoja nzuri za kukosoa mchakato
wenyewe, zipo pia hoja kinzani ambazo hazikubali kuwa Muungano ni batili.
Malumbano haya, miaka 52 baadaye, bado yanaendelea. Lakini yasituyumbishe
tukasahau kuwa ni Mzee Karume ndiyo alianzisha hoja ya muungano.
Zipo taratibu za kugeuza simulizi za wazee kuwa historia
rasmi, na pengine wakati umefika sasa wa wanahistoria kufanyia utafiti kipengele
hiki cha historia ambacho hakipewi uzito unaostahili.
Kuna wakati baadhi ya wasomi wetu, katika kutafuta sababu zinazowaridhisha
wao juu ya historia ya Muungano, walisisitiza kuwa wazo la Muungano liliibuliwa
na afisa mmoja wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA. Kwa mawazo yao sisi
hatuna uwezo wa kufikiri kuwa Muungano ni muhimu kwetu, tunahitaji Wamarekani
kutufundisha. Miaka hiyo ya sitini, kila tukio liliwekwa kwenye mizani ya vita
kati ya itikadi za nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani, na itikadi za
nchi za mashariki zikiongozwa na Urusi.
Kama siyo imani ya kuona kuwa kila jema na lenye manufaa
hutoka nje tu, basi inakuwa ni jitihada pia ya kupuuza mchango wa viongozi wetu
katika kujenga na kuimarisha Muungano kwa kushawishi kuwa mawazo yao
yalipandikizwa na wale ambao tunaamini hawana nia njema bali wanalinda masilahi
yao.
Bahati nzuri, kama vile alifahamu mapema kuwa haya maneno
yatasemwa Mwalimu Nyerere aliwajibu mapema watu hawa. Katika chapisho la chama
cha TANU la Juni 1960 lililosisitiza haja ya kuwepo kwa shirikisho la Afrika
Mashariki, Mwalimu aliweka msimamo wake na wa TANU juu ya shirikisho kwa kusema
(siyo tafsiri rasmi):
“Katika watu wanaounga shirikisho watapatikana watu ambao
wanasukumwa na sababu tofauti….watakuwepo wafanyabiashara…kutakuwa na kila aina
ya watu upande wa shirikisho na watakuwa na kila sababu. Lakini hoja ya
shirikisho inajitosheleza kwa uhalali wake yenyewe. Thamani ya almasi
haitegemei tabia ya wale wanaoichimba. Madini ni almasi, au siyo almasi. Iwapo shetani
mwenyewe atajitokeza na kuunga mkono huu mpango wa shirikisho, ujio wake
hautabadilisha mawazo yangu juu ya shirikisho au juu ya shetani mwenyewe.”
Mawazo ya Sheikh Abeid Amani Karume ya kuunganisha Zanzibar
na Tanganyika yalitua kwa muumini mkubwa wa umoja wa watu, na hasa umoja wa
nchi za Afrika, Mwalimu Nyerere. Lakini tukubali kuwa bila Mzee Karume upo
uwezekano kuwa hadi sasa tungekuwa hatuna Tanzania.
Miaka 52 baadaye, kwenye mazingira ya vijana wetu kutumia
muda wao mwingi kutumiana ujumbe kwenye Twitter, Facebook, na Instagram kuliko
kufukua yaliyojichimbia kwenye vitabu pamoja na kutafiti yale ambayo hayapendi
kusemwa, ipo hatari kuwa yale ya CIA yataendelea kuwekewa uzito zaidi kuliko
yale ambayo hayakidhi malengo ya mada za wasomi.
Taarifa nyingine inayohusiana na hii:
No comments:
Post a Comment