Hii ni makala yangu ya tarehe 18 Julai 2017 kwenye safu yangu inayoitwa Ujumbe toka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri linalochapishwa kila Jumanne.
******************************
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika lisilo la
kiserikali Global Justice Now inaeleza jinsi gani bara la Afrika linavyoibiwa
rasilimali yake.
Ripoti hiyo, inayoitwa Honest Accounts 2017, inaeleza kuwa
kwa mwaka 2015 mali na pesa za thamani ya Dola za Marekani bilioni 203 zimetoka
Afrika kwa njia ya faida ambazo mashirika ya kimataifa yamepata kutokana na
shughuli za biashara na uzalishaji barani Afrika, na kwa mianya haramu ya pesa
zinazotumwa nje. Wakati huo huo ni kiasi cha Dola bilioni 161.6 tu ambazo kwa
mwaka huo ziliingia barani Afrika kwa njia ya mikopo, kutuma pesa kwa watu
binafsi kutoka nje ya bara la Afrika, na misaada.
Huu utafiti unatukumbusha tu kuwa bara la Afrika ni tajiri,
lakini kwa bahati mbaya Waafrika tunakubali, au kwa kutokujua au kwa
kudanganywa, kuwa sisi ni maskini. Hali hii inatufanya sisi na serikali zetu
kuwa na mawazo ya ombaomba ambaye badala ya kutumia uwezo aliojaliwa kutafuta
riziki, anazunguka mitaani kuomba watu pesa za kuendesha maisha yake.
Taarifa inaendelea kufafanua jinsi bara la Afrika
linavyoibiwa na mashirika ya biashara ya kimataifa. Wakati bara la Afrika
linapokea kiasi cha Dola bilioni 19 kwa njia ya misaada kutoka nje, kiasi cha
Dola bilioni 68 zinahamishwa kwenda nje na mashirika haya ambayo, kwa kawaida
na kwa makusudi, hayataji thamani halisi za bidhaa wanazoingiza barani Afrika
na mali inayoondoshwa kwenda nje. Ni hitimisho ambalo linafanana na hitimisho
lililofikiwa na taarifa ya kwanza ya makinikia. Tofauti ni kuwa taarifa hii
haitolewi na wataalamu waliyotumwa na Rais John Magufuli ila na shirika
lililopo Ulaya ambalo linamulika kiwango cha wizi dhidi ya Afrika.
Pamoja na shutuma hizi dhidi ya wizi unaoendelea kudhoofisha
maisha ya Waafrika, ni muhimu kutofautisha aina ya wizi huu. Kwanza, upo wizi
ambao lazima tukubali kuwa ni wizi halali ambao unalindwa na sera na sheria
mbovu zilizopitishwa na mabunge ya nchi za Afrika kulinda mifumo inayonyima
Waafrika fursa ya kufaidika na utajiri wao.
Tutakuwa tunajidanganya kama hatutakubali kuwa rushwa ni
mojawapo ya vichocheo vikubwa ambavyo vilisababisha baadhi ya nchi hizi kuweka
sera na sheria ambazo, kwa ujumla wake, hazilindi maslahi ya Waafrika bali
zinalinda maslahi ya mashirika ya nje kufuja rasilimali za bara letu na
kuwaacha wananchi wake kuwa watumwa wa mali yao wenyewe.
Hata hivyo yapo mazingira ambayo hayasukumwi na rushwa
ambapo inaziweka nchi za Afrika wakati kwenye shida kubwa za kiuchumi
zinazowalazimisha kuweka mazingira yasiyo na manufaa kwa wananchi wake.
Madai ya kutaka kubadilisha mifumo hii ambayo yamejitokeza
sasa nchini Tanzania yamewahi kujitokeza kwenye sekta ya madini nchini Zambia. Ilipobinafsisha
migodi yake ya kuchimba shaba, Serikali ya Zambia ilikuwa inakabiliwa na
uzalishaji mdogo na gharama kubwa ya kugharimia uzalishaji iliyokadiriwa kufikia
Dola milioni moja kwa siku.
Ilipotafuta msaada kutoka mashirika ya fedha ya nje
ikaambiwa dawa ni moja tu: ubinafsishaji. Kwa usiri ule ule ambao tuna uzoefu
nao hata sisi, serikali ya Zambia ilifanya majadiliano ya ubinafsishaji na
wawekezaji ambao, ingawa sheria ya madini ilitaka walipe mrahaba wa asilimia 3 kwa
serikali kwa mauzo ya shaba nje ya nchi, mkataba wa siri uliwaruhusu kulipa
asilimia 0.6. Aidha, makampuni ya kuchimba madini yakapunguziwa kodi ya mapato
kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba wafanyakazi waliowaajiri wakawa wanalipa kodi
kubwa zaidi kuliko makampuni hayo.
Huu nauita wizi halali, kwa sababu kimantiki ni wizi tu hata
kama unalindwa na sheria za nchi. Pili, upo wizi ambao unakatazwa kwa mujibu wa
sheria. Inakadiriwa kuwa kiasi cha Dola bilioni 29 zinafujwa barani Afrika
kutokana na biashara haramu ya magogo, uvuvi, na biashara za wanyamapori na
mimea. Biashara haramu ya pembe za ndovu inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola
bilioni 10.
Njia nyingine ambayo inainyima Afrika manufaa inayotokana na
mali yake ni kukosekana kwa viwanda vinavyochakata malighafi zake. Tunauza
pamba nje ya nchi halafu tunanunua nguo zinazotokana na pamba hiyo. Tofauti ya
thamani ya malighafi na bidhaa iliyotengenezwa inabaki nje.
Tunaruhusu utaratibu wa kupeleka nje makinikia badala ya
kuweka mitambo barani Afrika ya kuchakata madini, na kwa hali hiyo kukosa
ongezeko la thamani ya mali inayopelekwa nje na mapato kwa serikali zetu.
Kwa kifupi ripoti iliyotolewa inatukumbusha tu kuwa sehemu
kubwa ya nchi zinaozoendelea zinanufaika na utajiri wa Afrika kuliko sehemu
kubwa ya Waafrika wenyewe. Zile porojo kuwa nchi tajiri zinasaidia bara la
Afrika hazina ukweli wowote. Ni bara la Afrika ambalo linasaidia nchi tajiri.
Kuna hotuba nzuri sana ya Mwalimu Nyerere inayotuasa tusikubali
kusikia kelele tunazopigiwa tunapoazimia kufanya jambo lenye manufaa. Kwenye
hotuba anasema kuwa tunapozidi kukaribia lengo, na kelele zitazidi kuwa kubwa.
Vita vya kurudisha mikononi mwa Waafrika utajiri wao
inahitaji kutumia uzoefu mkubwa na maarifa. Lakini ni vita ambayo inahitaji
kuiendesha huku tukiwa tumeziba masikio kuepuka kuyumbishwa na kelele ambazo
zinazidi kuongezeka ili kutuondoa kwenye safari ya kurejesha na kuimarisha
hadhi na heshima ya bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment