Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, July 21, 2017

Mamlaka ya Mapato Tanzania yawageukia wauza spea

Nimesikia taarifa ya habari asubuhi hii kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania wameanza kukagua maduka ya wauza spea za magari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mamlaka inachunguza bidhaa hizo zilizopo madukani ili kupata uthibitisho wa wenye maduka kuwa wamepata hizo bidhaa kwa njia za halali.

Kwa muda mrefu inaaminika kuwa baadhi ya wenye maduka yanayouza spea za magari wananunua spea hizo kutoka kwa wezi wa magari, au wezi wanaoiba spea kutoka kwenye magari.

Hizi hatua zikiendelea kwa muda mrefu zinaweza kupunguza wizi wa spea za magari, na hata wizi wa magari.

Miaka mingi iliyopita nilipoishi Dar es Salaam niliwahi kuibiwa kioo cha mbele cha gari. Nilipotoa taarifa kituo cha polisi niliambiwa na polisi kuwa wana hakika kuwa kioo changu kitapatikana Gerezani, eneo la Dar es Salaam ambalo huuza bidhaa mbalimbali zilizotumika, nyingi ya hizo zikiwa bidhaa za wizi.

Wezi watapungua
Askari wa upelelezi wawili nilioambatana nao kuelekea Gerezani walinushauri kubaki mbali kidogo na eneo wakati wao walipoingia Gerezani na wakarudi baada ya muda na kuniambia kuwa kioo changu, ambacho kilikuwa na namba ya gari yangu, wamekiona. Hawakutaka niongozane nao kwa sababu walisema nafanana sana na polisi na tungekuwa pamoja tusingepata ukweli.

Cha ajabu ni kuwa wale polisi walinishauri ninunue kioo changu. Bila hivyo walisema sitakipata. Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa kupata mali ya wizi wakati huo.

Bila shaka hizi jitihada mpya za Mamlaka ya Mapato zitapunguza kasi ya wizi, na zitaleta mabadiliko chanya kwa wamiliki wa magari.

Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2016/07/mada-yangu-ya-leo-mwizi-ni-mwizi-tu.html
https://muhunda.blogspot.com/2011/07/maana-sahihi-ya-neno-fisadi.html

No comments: