Katika moja ya hafla zilizoandaliwa na Rais wa Msumbiji wa wakati huo Armando Guebuza, nilipata fursa ya kukaa na mzee mmoja mpiganaji wa zamani wa jeshi la ukombozi la FRELIMO ambaye alishiriki kwenye vita ya ukombozi ya Msumbiji.
Alinisimulia mengi juu ya maisha yao walivyokuwa kwenye kambi za FRELIMO zilizokuwa Tanzania, na baadhi ya matukio katika vita iliyoshiriki.
Alisema kuna wakati Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ilitembelea baadhi ya maeneo yaliyokombolewa ndani ya Msumbiji na kupokelewa na Samora Machel, wakati huo akiwa rais wa FRELIMO aliyeshiriki mwenyewe katika mapambano.
Waliandaa chakula kwa ujumbe ulioyoongozwa na Katibu Mtendaji wa kamati, Hashim Mbita. Lakini walipokuwa tayari kuanza kula tu, hapo hapo ndege za jeshi la Ureno zilianza kushambulia kambi ile na chakula kikaachwa ili kunusuru maisha yao.
Inaelekea jeshi la Ureno lilipata taarifa ya ziara ile.
Mwalimu Nyerere na Samora Machel kwenye moja ya mikutano ya hadhara. |
Niliambiwa kuwa Samora mwenyewe aliongoza mikakati ya kulinda usalama wa ule ujumbe, akiwatanguliza wageni wakikimbia mbele na wakiwa wamezungukwa na ulinzi mkali wa wapiganaji wa FRELIMO. Nikaambiwa Samora mwenyewe alikuwa wa mwisho, nyuma ya kila mtu, akiwa ameshika bastola yake mkononi.
Ni kielelezo cha ushujaa wa baadhi ya viongozi wetu wa zamani. Yule mzee alinitolea simulizi hii huku akicheka kuwa wageni hawakuweza kula siku ile.
Taarifa nyingine ambazo unaweza kupendelea kusoma:
https://muhunda.blogspot.com/2016/12/redio-ya-Mwalimu-Nyerere.html
https://muhunda.blogspot.com/2012/09/wageni-wa-butiama.html
No comments:
Post a Comment