Hii ni makala yangu ya tarehe 11 Agosti 2015 kwenye safu yangu inayoitwa Ujumbe toka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri linalochapishwa kila Jumanne.
******************************************
Kama unahitajika ushahidi kuwa upo umuhimu wa kuruhusiwa kwa
wagombea huru ndani ya Katiba ya Tanzania, basi huo ushahidi umejitokeza baada
ya matukio ya hii karibuni yaliyomo ndani ya siasa za Tanzania.
Tukio lililohitimisha ukweli huo ni kuhama kwa Waziri Mkuu
mstaafu Edward Lowassa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Kwa maelezo yake, amehama kutoka CCM
kwenda CHADEMA kwa sababu “…mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe,
ukiukwaji wa maadili, uvunjifu wa Katiba, na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM.”
Aliendelea kusema: “Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa
upendeleo zaidi na chuki iliyokithiri dhidi yangu.” Kilichotokea Dodoma, kwa
mujibu wa maelezo yake, ni kubaka Demokrasia.
Amehamia CHADEMA akiamini kuwa yale yaliyomkuta ndani ya CCM
hayawezi kutokea ndani ya CHADEMA. Na dalili ni nzuri kwake mpaka sasa kwa
sababu CHADEMA hawakuchukua muda mrefu na walimpa nafasi ya kugombea urais
kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nafasi ambayo CCM haikumpa. Hatimaye amepitishwa
kuwa ni mgombea urais wa muungano wa vyama vya siasa vinavyojulikana kama
UKAWA.
Mwalimu Nyerere amenukuliwa na Lowassa akitamka kuwa Chama
cha Mapinduzi siyo baba yake [Mzee Nyerere Burito], wala mama yake [Mugaya wa
Nyang’ombe] na kuwa akikosa mabadiliko ndani ya chama hicho, basi atayatafuta
nje ya chama hicho. Mheshimiwa Lowassa amekosa mabadiliko ndani ya CCM na
anaamini atayapata ndani ya CHADEMA na UKAWA. Swali ambalo halijaulizwa ni hili:
asiyeona mabadiliko ndani na nje ya CCM anakuwa mtoto wa nani?
Kwangu mimi haipo sababu ya msingi ya kuwepo yatima wa
kisiasa nchini. Jawabu ni kuwepo kwa mfumo wa kikatiba unaoruhusu wagombea huru
kama nguzo ya tatu kwenye siasa. Wagombea huru watatoa fursa kwa wanachama
waliokosa macho ya kuona na masikio ya kusikia fursa za mabadiliko zilizomo
ndani ya chama tawala na ndani ya vyama vya upinzani kutafuta mabadiliko hayo kwingineko
kama wagombea huru, au kama watetezi wa wagombea huru.
Kuna mengi ambayo mtu anaweza kuunga mkono ndani ya sera za
vyama tofauti vya siasa, lakini akawa pia hakubaliani na kipengele cha sera
kwenye vyama hivyo hivyo. Aidha, kuna maamuzi ambayo yanaweza kupitishwa na
chama anachokiunga mkono ambayo hayaafiki. Mtu wa aina hii anapaswa kupewa
fursa ya kikatiba ya kupenyeza mawazo yake bila kulazimika kuchukua uamuzi
ambao tunaousikia kwa baadhi ya watu wa kustaafu siasa au kuachia wadhifa wake
ndani ya chama cha siasa, kwa sababu tu haoni chama ambacho kinawakilisha
matakwa yake kwa wakati huo.
Kinadharia, chama kinachotawala au chama cha upinzani
kinachobaini hali hiyo kitatambua ukomo wa kile ambacho mimi naita jeuri ya
chama, au uhakika wa chama cha siasa kuwa kile kinachoidhinishwa na maamuzi
rasmi au yasiyo rasmi ya chama ndiyo mwisho wa mjadala na kufungwa kwa kikao. Mfumo
wa wagombea huru unaweza kuwa kama sehemu ya mwisho ya kukata rufaa kwa wananchi
kwa sababu hiyo ya uwepo wa kukinzana kwa mitazamo baina ya mtu na mienendo ya
chama alichokiunga mkono.
Woga mkubwa wa washiriki wa siasa za siku hizi ni kushindwa
uchaguzi, siyo kung’ang'ania misimamo ambayo nyakati hizi inaitwa imepitwa na
wakati.
Kwenye nadharia ya siasa chama cha siasa kinapaswa kuwa
tayari kushindwa kwenye uchaguzi kwa sababu ya kushikilia misimamo mbalimbali
ambayo kimekuwa kikiunga mkono kwa mujibu wa sera zake. Kwenye miaka ya mwanzo
baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mwalimu Nyerere, akiwa Waziri mkuu wa wakati
ule, alipingana na baadhi ya wawakilishi wa chama cha TANU bungeni na wa
serikali yake, ambao wakati wa kujadili muswada wa uraia wa Tanganyika walidai
kuwa uraia wa Tanganyika uwe haki ya Watanganyika wenye ngozi nyeusi tu. Katika
kupinga msimamo wa wenzake na akiwa anatetea hoja kuwa kila Mtanganyika anayo
haki ya kuwa raia bila kubaguliwa kwa rangi ya ngozi yake, Mwalimu Nyerere
alisema kuwa serikali yake itakuwa tayari kushindwa kwenye kura bungeni na
kuondoshwa madarakani lakini haiwezi kukiuka misingi ya haki na usawa ambayo
yenyewe iliipigania na kuitetea.
Leo hii ndani ya siasa tunashuhudia kuwa misimamo ni kama
mashati ambayo hubadilishwa kwa mujibu wa mahitaji yanayojitokeza.
Kwa mtazamo wangu, vyama vyote siasa vinaweka mikakati ya
kufika Ikulu tu, kwa kushinda uchaguzi mkuu ujao. Kwa CCM ni kupigana kufa na
kupona kuhakikisha kuwa Edward Lowassa hawi rais wa tano wa Tanzania.
Kwa UKAWA hali hii ni dhahiri kuliko kwa CCM. Hatutarajii
kuwa jambo rahisi kwa vyama vinne vya siasa kukubaliana kwa yote yaliyomo
kwenye sera zao. Kwao jambo la msingi itakuwa “Rais wetu akishaapishwa tutajua
la kufanya.”
Ukweli haupingiki kuwa lipo pengo ndani ya siasa ambalo
linalazimisha sehemu fulani ya wapiga kura ya Watanzania kuwepo kwenye siasa za
vyama ambazo haziwakilishi kikamilifu matakwa yao. Suluhisho ni wagombea huru. Wagombea
huru hawatamaliza hitilafu zilizopo lakini watazipunguza kwa kiasi kikubwa.
Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2017/07/afrika-tunaibiwa-sana-tena-sana.html
Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2017/07/afrika-tunaibiwa-sana-tena-sana.html
No comments:
Post a Comment