Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, December 18, 2013

Hatua kumi za mauaji ya kimbari: 7 na 8

Nimetembelea Rwanda hivi karibuni na nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea mojawapo ya vituo vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Jambo moja la msingi ambalo Watanzania tunaweza kijufunza ni kuwa maafa yaliyotokea Rwanda yanaweza kutokea pia Tanzania. Kwa mujibu wa wachunguzi wa sababu zinozogeuza binadamu mmoja kuwa adui wa binadamu mwenzake na hata kufikia hatua ya kumaliza uhai wa mwenzake ziko duniani kote.

Sababu hizi zinaanza na mchakato wenye hatua nyingi ambao hufikia mauaji kama yale yaliyotokea Rwanda. Kinachozuwia maafa kama hayo kutokea ni hatua mahususi zinazopaswa kuchukulia na jamii za kukatisha uendelezwaji wa huo mchakato.

Kwa mujibu wa Dr. Gregory Stanton wa Genocide Watch, hatua za viashiria vya kuwepo kwa mchakato na za kuzuwia maafa kama ya Rwanda ziko kumi.

Hatua ya Saba: Mipango

Hatua hii inahusisha kuunda mfumo wa kijeshi, kutoa mafunzo kwa wanamgambo, kukusanya silaha za maangamizi, na kuzitawanya kwa wauaji.

Hatua za kuepusha Mipango

Pale inapothibitishwa dalili za mipango kufanyika, basi tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea mauaji ya kimabri utolewe. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litowe onyo kuwa litakuwa tayari kuchukua hatua pale tu ambapo lina uhakika kuwa litachukua hatua madhubuti za nguvu dhidi ya wahusika. Viongozi wa dunia wawaonye wale wanaokusudia kutenda maangamizi kuwa watachukuliwa hatua dhidi ya uhalifu watakaoufanya. Msaada wa kibinadamu unadaliwe. Majeshi ya kikanda yaandaliwe na kupewa uwezo wa kujiandaa na wa kifedha.
"Amri Kumi za Gitera" ni waraka uliotolewa na kiongozi wa kabila wa Wahutu kuchochea mauaji ya kabila la Watusi kabla ya mauaji ya kimbari ya Rwanda.  

Hatua ya Nane: Mateso

Katika hatua hii watu wanagawanywa kwa misingi ya ukabila na dini. wahanga wananyang'anywa mali zao. Wahanga hufukuzwa kutoka kwenye nyumba zao. Katika baadhi ya nchi wahanga walihamishwa na kuwekwa kwenye maeneo mahususi ya miji.  Katika baadhi ya nchi wahanga walikusanywa kwenye kambi za wakimbizi wa ndani.

Itaendelea na: 
  • Hatua ya Tisa: Mauaji
  • Hatua ya Kumi: Ukanushaji
Taarifa nyingine zinazohusian na hii:

Tuesday, December 17, 2013

Mandela! Mandela! Mandela! (sehemu ya pili ya awamu tatu)

Kwenye makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na kuzikwa leo, tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunnu nchini Afrika ya Kusini.

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Pili)
Na Notburga Maskini*

Migongano ya Kitabaka
Matabaka ya mabwana na watwana yalijitokeza kutokana na unyonyaji, udhalilishaji, na ubaguzi uliofanywa na makundi dhalimu ambayo yalijitokeza na kuonekana katika mifumo ya kijamii kwa maana ya Ukomunisti na Ubepari ambapo mabwana au wenye nguvu, waliwadhalilisha wanyonge; ilitengeneza tabaka la watu wachache matajiri wa kupindukia ambao wameshikilia na kuwekeza asilimia 80 ya utajiri wa dunia katika mtaa wa tano (the 5th Avenue New York).  

Tabaka la pili ni la umma wa wakulima na wafanyakazi maskini na wanyonge katika nchi zetu na duniani ambao bidii na jasho lao haviwawezeshi kujikwamua kutokana na mirija ya dhuluma iliyopangwa na tabaka hili  la watu wachache lakini lenye nguvu kubwa kiuchumi na kiutawala. Tabaka la tatu ni tabaka la maskini wa kutupwa miongoni mwao wakiwemo wazee, wastaafu, vijana wasio na ardhi wala ajira, wanawake na watoto.

Hali hii  ya kuhuzunisha na tishio kwa amani ya nchi zetu na dunia ilionekana mapema machoni na kwenye mioyo ya viongozi hawa mashujaa Nelson Rolihlahla Mandela na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Waliichukia na kufanya bidii kubwa kuchukua hatua sawia kupambana ili kuona mfumo wa haki usawa na heshima kwa binadamu unasimikwa dhidi ya mifumo ya unyonyaji, ubaguzi na udhalilishaji.

Kazi iliyobaki ya kugawa rasilimali hizi za dunia ziweze kuwafikia watu wengi na kuondoa umaskini duniani ndio njia pekee ya kumuenzi Mzee Mandela bila unafiki. Tunahitaji mashujaa kama Mzee Nelson Mandela na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao wataweka ushawishi na kupambana hasa wakati huu zinapoonekana dalili kuwa jambo hili linawezekana. Kifo cha shujaa huyu  tumeshuhudia viapo na dhamira zikiwekwa kanisani na hadharani kuashiria kuwa tayari hata kufa ili kutetea ustawi wa binadamu na amani duniani. 


State Funeral of former President Nelson Mandela, 15 Dec 2013
Picha: Maafisa wa jeshi la Afrika ya Kusini wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Marehemu Nelson Mandela kwenye mazishi ya taifa yaliyofanyika tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunu, jimbo la Eastern Cape.

Kusaliti na kuvunja tabaka
Mzee Nelson Mandela na Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni mwa watu waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuumwa na kuchukizwa na hali mbaya ya binadamu wote. Waliona ubaya na adha inayotokana na binadamu kumdhalilisha binadamu mwingine na hatari yake kwa amani ya dunia hivyo hawakuivumilia hata kwa sekunde chache. Walipinga hali hii pamoja na uwezo waliokuwa nao kutokana elimu na nafasi zao za kuzaliwa wakiwa watoto wa machifu, ambapo wangaliweza kuungana na wadhalilishaji na kuwa wanufaikaji wa mifumo dhalimu iliyojaa uroho, uchoyo, dharau, na tamaa.

Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere walizungumza kwa sauti kubwa na hivyo kuweka ushawishi mkubwa ndani ya jamii na nchi zao na kuanzisha vuguvugu la mapambano yaliyokusudia kuleta heshima kwa binadamu. Ni dhahiri kuwa walitumia maisha yao hapa duniani kujitoa mhanga kwa ujasiri wa kupindukia hata kuuwa matabaka yao (class suicide) kupigania usawa haki na heshima kwa binadamu. Ndiyo maana kuondoka kwao duniani Mzee Nelson Mandela aliyetanguliwa na rafiki yake mkubwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere muongo mmoja na nusu uliopita kunaleta mshtuko na wasiwasi mkubwa kwa amani ya dunia, usawa, ubinadamu, demokrasia, na utawala bora.  Hii inatokana na ukweli kwamba binadamu wa aina hii hutokea kwa nadra sana.

Itaendelea na: Heshima katika historia ya nchi na dunia


*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Sunday, December 15, 2013

Mandela! Mandela! Mandela! (sehemu ya kwanza ya awamu tatu)

Kwenye makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na kuzikwa leo, tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunnu nchini Afrika ya Kusini.

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Kwanza)

Na Notburga Maskini*

Hiki kimekuwa ni kilio cha dunia nzima kumwomboleza shujaa mpigania uhuru, amani, haki, utu na utawala bora duniani, mwana wa bara la Afrika mwenye asili ya Afrika ya Kusini Nelson Rolihlahla Mandela mwanaharakati, kiongozi wa chama cha ANC na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini; aliyeaga dunia tarehe 5 Desemba 2013.  Mimi binafsi na kwa niaba ya wafanyakazi wa Tanzania naungana na Watanzania wenzangu, wafanyakazi wa Afrika ya Kusini na Dunia kuomboleza msiba huu mkubwa ambao ni pigo kubwa kwa tabaka la wafanyakazi duniani na vilevile ni pigo dhidi ya utawala bora, haki, amani na utu. 

South Africans mourn the
death of the late former President Nelson Mandela, 8 Dec 2013
Picha: Wanachama wa Umkhonto We Sizwe, lililokuwa jeshi la chama cha African National Congress lilioendesha mapambano ya kivita dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika ya Kusini, wakiwasili kwenye makazi ya jijini Johannesburg ya marehemu Nelson Mandela tarehe 8 Desemba 2013. (Picha ya GCIS).

Niandikapo makala hii nakumbuka mwaka 2003 nilipokuwa jijini Johannesburg kuhudhuria mkutano wa dunia kuhusu uwekezaji wa mitaji Afrika, Kusini mwa Sahara kwenye ukumbi mmojawapo katika jengo maarufu la Sandton. Wakati wa kutoka ukumbini tulikutana nae ana kwa ana mlangoni akiwa na watu wengine, nafikiri kiongozi huyu alitokea kwenye ukumbi mwingine wa mkutano katika jengo hilo. Binafsi nilifurahi sana kumuona Mzee Mandela aliyekuwa katika hali ya kawaida kabisa. Hata hivyo mimi na hata wenzangu hatukuweza kufanya chochote angalau kuweza kumsalimia kutokana na kutofahamu taratibu na mipaka ya kiitifaki.  Alikuwa ni kivutio kikubwa kwetu sote tuliokuwepo siku hiyo.

Afrika Kusini na Tanzania
Ndugu zetu wa Afrika ya Kusini kama ilivyokuwa kwetu Watanzania tarehe 14 Oktoba 1999 alipotuaga Mwasisi wa Taifa hili, mwanamapinduzi aliyeheshimika duniani, na kipenzi cha Watanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nao wanapitia hali ngumu iliyojaa majonzi, vilio, na mashaka lakini pia wakimshukuru Mungu kwa zawadi kubwa aliyoupatia umma wa Afrika Kusini, Bara la Afrika na Dunia.

Katika kitabu chake cha dondoo Nelson Mandela By Himself, 2013 Mzee Mandela anatufariji kwa maneno yake mwenyewe kuwa: 

“kifo hakikwepeki. Wakati binadamu ameshatimiza yale aliyofikiri kuwa ni wajibu wake kwa watu wake na nchi yake, anaweza kupumzika kwa amani.  Naamini kuwa nimefanya bidii kutimiza wajibu huo na ndio maana nitalala katika umilele”  

Ni dhahiri kuwa Mzee Mandela ameondoka akiwa anaridhishwa na bidii kubwa aliyoweka katika kazi kubwa aliyoifanya ya kuondoa ubaguzi wa rangi na udhalilishwaji wa mtu mweusi katika nchi yake ya Afrika ya Kusini. Pengine Watanzania na waombolezaji tuliobaki yafaa kutafakari sasa kuhusu wajibu wetu kwa watu wetu na nchi zetu na iwapo tutaweza kuwa jasiri na kusema maneno hayo siku yetu itakapofika. 

Imani na mapenzi ya Umma dhidi ya chuki za maadui
Mzee Nelson Mandela kama alivyokuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wameteka mioyo ya walimwengu na wananchi wao kwa imani yao katika utu badala ya vitu, na kusimamia kwa vitendo bila ya kutetereka. Wanamapinduzi hawa wa Afrika waliweka mbele maslahi ya taifa na utu wa watu wao.  Walijitoa muhanga maisha yao yote kwa ajili ya nchi zao na watu wao jambo ambalo ni nadra kwa viongozi wengi tuliowashuhudia katika karne ya ishirini.

Wakati Mwalimu Julius Nyerere akiongoza mapambano ya ukombozi wa Bara la Afrika na dhidi ya udhalimu dhidi ya ubinadamu ikiwemo Afrika Kusini yenyewe, alitengeneza maadui waliotokana na kundi la wakandamizaji waliojijengea uhalali na kuamini kuwa wao ni bora kuliko binadamu wengine. Hata hivyo maadui hao kama tunavyoshuhudia leo wamejirudi na kujifunza thamani ya utu na utaifa katika kutumikia umma. 

Isingewezekana wakati ule wa mapambano ya ukombozi kuwa Afrika ya Kusini ingebadilika na kuwa kama ilivyo sasa. Kinachodhihirika hapa ni nguvu ya upendo, msamaha, na uzalendo kwa nchi na watu wake vinavyoweza kuleta mabadiliko chanya.  Hili ni somo kubwa kwa Afrika na Dunia.

Itaendelea na: Migongano ya Kitabaka

*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).


Friday, December 13, 2013

Afrika Kusini waomboleza kifo cha Nelson Mandela

Katika maeneo mbali mbali nchini Afrika Kusini wananchi wamejitokeza kuweka sahihi na kuweka kumbukumbu baada ya kifo cha Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwenye picha (juu) wananchi wa Afrika Kusini waliopo Johannesburg wakiandika kwenye bango la kumbukumbu.

Mzee Mandela atazikwa tarehe 15 Desemba 2013.

Sunday, December 1, 2013

Hatua kumi za mauaji ya kimbari: 5 na 6

Nimetembelea Rwanda hivi karibuni na nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea mojawapo ya vituo vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Jambo moja la msingi ambalo Watanzania tunaweza kijufunza ni kuwa maafa yaliyotokea Rwanda yanaweza kutokea pia Tanzania. Kwa mujibu wa wachunguzi wa sababu zinozogeuza binadamu mmoja kuwa adui wa binadamu mwenzake na hata kufikia hatua ya kumaliza uhai wa mwenzake ziko duniani kote.

Sababu hizi zinaanza na mchakato wenye hatua nyingi ambao hufikia mauaji kama yale yaliyotokea Rwanda. Kinachozuwia maafa kama hayo kutokea ni hatua mahususi zinazopaswa kuchukulia na jamii za kukatisha uendelezwaji wa huo mchakato.

Kwa mujibu wa Dr. Gregory Stanton wa Genocide Watch, hatua za viashiria vya kuwepo kwa mchakato na za kuzuwia maafa kama ya Rwanda ziko kumi.

Hatua ya Tano: Uratibu

Kwa kuwa mauaji ya kimbari yanaendeshwa na makundi dhidi ya makundi mengine, yanahitaji kuratibiwa. Kwa kawaida, ni dola inayoratibu maafa haya kwa kutoa fedha na silaha kwa makundi yanayoendesha mauaji.

Mfano wa Uratibu: Rwanda

Tabaka la watu wenye uwezo ndani ya Rwanda walitoa silaha kwa kundi la Interahamwe ambalo liliendesha mauaji. Serikali na wafanyabiashara wa Kihutu walitoa mapanga 500,000 na kuandaa kambi za mafunzo za "kulinda vijiji vyao" kwa kuua Watutsi.

Hatua za kuepusha Uratibu

Kuchukulia makundi yenye muelekeo wa kuchochea mauaji kama makundi ya jinai. Chukua hatua za kufanya uanachama ndani ya makundi hayo kuwa kosa la jinai na kushinikiza viongozi wao kukamatwa.

Kunyima visa kwa viongozi wa makundi haya na kukamata mali zao zilizopo nchi za nje.

Kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya makundi yanayoeneza chuki na dhidi ya serikali zinazounga mkono chuki kwa misingi ya dini na ukabila.
Wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 kwenye shimo hili zilikutwa maiti za maelfu ya wahanga wa mauaji hayo.

Hatua ya Tano: Kingamizi

Katika hatua hii mambo kadhaa yanajitokea, ikiwa ni pamoja na :

  • wenye siasa kali wanakuwa na nia ya kutenganisha makundi
  • makundi yenye kuchochea chuki na kuchapisha propaganda yenye nia ya kugawa watu
  • sheria zinapitishwa kuharamisha ndoa kati ya watu na makundi yanayokusudiwa kuwa tofauti
  • wenye msimamo wa kati wananyamazishwa, kutishwa, na kuuwawa

Mifano ya Kingamizi: Ujerumani

Maandamano yaliandaliwa dhidi ya wafanyabiashara wenye asili ya Kiyahudi, na Wajerumani wenye msimamo wa kati waliopinga kitendo hiki ndiyo walikamatwa kwanza na kupeleka kwenye kambi za mauaji.

Hatua za kuepusha Kingamizi

Pinga kwa kila hali sheria na sera zinazobagua makundi au zinazonyima haki za kiraia kwa makundi. Weka walinzi wa silaha kulinda viongozi wenye msimamo wa kati, kama ambavyo imefanyika Burundi. Shinikiza kuachiliwa kwa viongozi wenye msimamo wa kati ambao wanakamatwa, na kudai na kuendesha uchunguzi kwa wale viongozi wa aina hiyo ambao wameuwawa.

Pinga kupinduliwa kwa serikali na makundi yenye siasa kali.

Itaendelea na:
  • Hatua ya Saba: Mipango
  • Hatua ya Nane: Mateso