Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, December 25, 2012

Mkutano wangu na Jaffar Idi Amin

Taarifa ifuatayo ni ya siku nyingi kidogo, na awali niliitoa kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza From Butiama and Beyond tarehe 15 Mei 2009. Nairudia hapa katika mfululizo wa taarifa ambazo niliwahi kuzitoa kwenye From Butiama and Beyond na ambazo naamini wasomanji wangependa kuzirudia kusoma na vilevile kutoa fursa kwa wale ambao bado hawajazisoma kuweza kutafakari niliyoyaandika wakati huo.
***************************************
Mapema mwezi Aprili mimi pamoja na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tulikuwa wenyeji kijijini Butiama wa Jaffar Amin, mmojawapo wa watoto wa kiume wa zaidi ya watoto 50 wa kiongozi wa zamani wa Uganda Idi Amin Dada.

Nakiri kuwa kabla ya ujio wake nilijikuta kwenye mtanziko mkubwa ambao ulinifanya nisite kwa muda kuendelea kuandikia kwenye blogu yangu. Sikuwa na hakika wasomaji wangu wangechukuliaje mkutano wangu na Jaffar. Unapotamka tu 'Idi Amin' basi siku zote utaibua hisia kali, na mimi niligundua hizo hisia zilikinzana na sababu nilizoona zinaafikiana na uamuzi wangu wa kukubali wazo la BBC la kuonana na Jaffar.
Karibu Butiama: Jaffar Amin (kushoto), pamoja na mimi tukiwa Butiama ndani ya nyumba ambayo Mwalimu Nyerere alijengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kumalizika kwa vita kati ya Uganda na Tanzania.
 Nilieleza sababu zangu kwenye makala niliyoandika kwenye safu yangu iitwayo Letter from Butiama. Kwa kifupi niliwjenga hoja kuwa matukio ya kale tuyaache yabakie ya kale na umuhimu wa matukio hayo unajitokeza pale tu ambapo tunahitaji kijufunza jambo kutokana na matukio yaliyopita ili tusirudie makosa ya zamani. Matukio yaliyopita yasitumike kama rungu la kuwapiga wale wa sasa ambao hawahusiki kabisa na matukio ya zamani.

Mkutano wetu na Jaffar ulijikita kwenye wazo la BBC la kuadhimisha, kwa kupitia vipindi kadhaa vya redio vilivyorushwa mwezi Aprili, kumbukumbu ya miaka 30 ya vita vya Kagera, vita kati ya Uganda na Tanzania vya 1979 - 1980. Solomon Mugera, mkuu wa Idara ya Kiswahili ya BBC, alieleza kuwa awali wazo lilikuwa mkutano wetu ufanyike Nairobi. Alibainisha ni Jaffar aliyependekeza kuwa mkutano uhamishiwe Butiama, badala ya Nairobi.

Kwa hiyo katikati ya mwezi Machi nlijiandaa kuonana na Jaffar jijini Nairobi lakini nikafahamu mwishoni kabisa kuwa mkutano ulihamishiwa Butiama pasipo kufahamishwa mapema hayo mabadiliko. Ninahisi kuwa BBC waliendelea na mipango ya kukutana Butiama bila kunifahamisha kwa kuhofu kuwa ningakataa wazo lao.

Nilipata shida kubwa sana kuorodhesha waalikwa. Ilikuwa rahisi kuamua nani kati ya marafiki zangu kuwaalika. Baadhi yao walinirahisishia kazi kwa kuniomba niwaalike. Orodha ngumu ilikuwa ile ya viongozi wa serikali wa mkoa. Sikuwa na hakika iwapo wangehudhuria ingawa hutembelea Butiama mara kwa mara. Niliwatumia mialiko na baadhi yao walihudhuria mkutano ule pamoja na Jaffar.

Mwisho wa yote inaelekea kuwa wale waliofuatilia matangazo ya maadhimisho yaliyorushwa na BBC pamoja na mkutano na Jaffar walibaki na maoni chanya tu kuhusu mkutano wangu na Jaffar. Mtoa maoni mmoja alipendekeza kuwa mtu aliyeibua wazo la kuwakutanisha watoto wa Idi Amin na Julius Nyerere alipaswa kupendekezwa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.
Solomon Mugera wa BBC akihutubia waalikwa.
Ni matumaini yangu kuwa siku Solomon Mugera atakapoinuka akiwa amevalia vazi rasmi kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mjini Oslo (pamoja na kupokea hundi ya dola milioni moja) basi atakumbuka kuniorodhesha mimi pia kwenye orodha yake ya waalikwa.w

No comments: