Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, October 18, 2010

Lugha yetu Kiswahili

Nilitembelewa Butiama hivi karibuni na Andrea Wobmann, raia wa Uswisi, ambaye alikuwa Tanzania kwa miezi kadhaa akifanya kazi ya kujitolea katika kuendeleza shughuli za utalii jijini Mwanza.

Alisindikizwa na mwenyeji wake toka Mwanza (ambaye jina lake nitaliweka hapa baada ya muda kwa sababu silikumbuki kwa sasa) aliyevaa fulana iliyoandikwa "mzungu."

Awali nilihisi kuwa ile fulana angeivaa Andrea, lakini nilivyopekuwa kwenye kamusi nikagundua kuwa yawezekana sifahamu vizuri tu Kiswahili. Neno hilo, kama lilivyoandikwa kwenye fulana lina maana nyingine zifuatazo, zaidi ya ile maana ambayo wazungumzaji wengi wa Kiswahili tunaifahamu:

1. jambo lisilo la kawaida
2. mafunzo yanayotolewa kwa wanafunzi wa ngazi ya awali
3. ujanja; uerevu

Ingekuwa maandishi ya kwenye fulana yalikuwa "Mzungu", yaani na herufi kubwa ya mwanzo, basi ile maana niliyoidhania mimi ndiyo ingekuwa sahihi, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya mwaka 2001.

Sunday, October 17, 2010

Kumbukumbu ya siku ya kufariki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Alhamisi iliyopita tuliadhimisha kumbukumbu 11 ya kufariki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hapa kijijini Butiama. Maadhimisho yalianza na misa iliyoongozwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki, Musoma.
Mama Maria Nyerere (kulia), akisalimiana na Mkurugenzi wa Mkoa wa Mwanza wa Chuo Kikuu Huria, Ben Kapaya (aliyembeba mwanaye, James), akiwa na mkewe (wa pili toka kulia). Siku hiyo ya maadhimisho James alitimiza umri wa mwaka mmoja.

Baada ya misa ilifanyika sala fupi kwenye kaburi la Mwalimu Nyerere katika eneo la Mwitongo, Butiama.
Makongoro Nyerere (kushoto), mwenyekiti wa mkoa wa Mara wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa na Askofu Michael Msonganzila wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Musoma (kushoto), pamoja na mgeni toka Uganda, Ssalongo Katumba (katikati).  
Na baada ya sala ya kwenye kaburi wageni walipata chakula cha mchana kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Mwitongo.
Makongoro Nyerere (katikati), akiwa na Kisheri Kyanzi Mchere, kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM), tawi la IFM
Baadhi ya wageni waliyofika kwenye maadhimisho hayo ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Godfrey Ngatuni na mkewe. 
Mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Vincent Nyerere (kulia), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Godfrey Ngatuni wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere yaliyofanyika Butiama, tarehe 14 Oktoba 2010.

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya kumi kati ya kumi)

Kumradhi kwa kuchelewa kuleta makala hii ya mwisho katika mtiririko wa makala hizi za safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kutokana na kutingwa na shughuli mbalimbali.

Jumanne 26 Agosti 2008
Baada ya kupata kifungua kinywa tulipiga picha ya pamoja na kuanza safari ambayo kwangu ilikuwa ni ngumu kushuka kueleka lango la Mweka. Njiani kundi la wasichana lilitupita na mmoja akasema, "sirudii tena." Nilimuelewa vyema kwa nini alitamka maneno yale.

Kiasi cha mita 200 kabla ya kufika kwenye lango la Mweka tulikutana na madereva toka Zara Tanzania Adventures ambao walitufuata kwa mguu ili kufahamu iwapo tulikuwa tumechoka sana kiasi cha kushindwa kutembea hatua zile za mwisho. Tulikataa wazo lao la kupanda gari. Ingetia doa tukio ambalo halikuwa la kawaida.

Kuruhusu mwili kuanza kuzowea hali ya kuwa katika nyanda za chini ni suala la umuhimu ule ule kama la kuuzowesha mwili hali ya kuwa nyanda za juu wakati wa kupanda mlima. Yasemekana athari za kuwa katika nyanda za juu zinachukuwa muda kuisha. Kwenye duka la vitu vya ukumbusho lililopo lango la Mweka Le aliinua kofia iliyoandikwa "Hifadhi za Taifa" na akaniomba nifasiri. Sikuweza kukumbuka tafsiri ya Kiingereza na niligeukia maafisa wa Hifadhi ya Kilimanjaro kuomba wanisaidie.

Mmojawapo alisema, "National Parks", na mimi nikasema, "ni kweli! Nimewezaje kusahau hilo!" Mmoja akanijibu, "Usijali, ni kawaida. Akili zako bado zimeganda. Alinipa hoja ya nguvu ya kutolala tena kwenye Kambi ya Crater safari ijayo.

Sasa kuhusu kichwa cha habari cha hii makala: Niliacha kuvuta sigara mwaka wa kwanza nilipoamua kupanda Mlima Kilimanjaro kwa sababu nilikuwa na hofu uvutaji sigara ungenipunguzia nafasi ya kuweza kufika kwenye kilele.

Pesa zilizokusanywa mpaka sasa:

Paundi za Uingereza 440
Dola za Marekani 16,180
Shilingi za Tanzania 2,570,000

Bonyeza hapa kuisoma makala hii kwa Kiingereza

Makala zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/kisa-cha-kuacha-kuvuta-sigara-safari_05.html

Tuesday, October 5, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya tisa kati ya kumi)

Jumatatu 25 Agosti 2008
Le na Yahoo walianza safari ya kuelekea Kilele cha Uhuru saa 10:00 alfajiri kuwahi mawio. Baada ya kupambazuka nilitembea juu ya eneo la tambarare la kasoko (shimo la katikati ya volkano) nikiwa pamoja na muongozaji msaidizi hadi Stella Point ambako nilituma ujumbe wa maandishi wa simu niliyokusudia kuutuma jana tokea kileleni: "Salamu toka Kilele cha Uhuru, kilele cha Mlima Kilimanjaro (mita 5,896)..."

Baadhi ya majibu niliyoyapata yalikuwa yanapendeza. Joseph Ibanda, rubani, aliandika: "..kwa hakika mandhari itakuwa ya kustaajabisha hapo ulipo..." Asingeweza kutumia msemo uliyo bora zaidi kuelezea hisia zangu na hapakuwa na sehemu bora zaidi kupata hizo hisia kuliko pale niliposimama wakati nasoma ujumbe wake. 
Hema langu mbele ya barafu katika Kambi ya Crater
Kushoto kwangu kulikuwa na eneo pana la wazi kati ya Kibo na Mawenzi, mbali lakini kukionekana vizuri kabisa. Chini zaidi kulikuwa na mandhari nzuri kwa kiasi cha mita 1,500 halafu utando mzito wa mawingu. Siwezi kuelezea msisimko wa kusimama juu ya ardhi na wakati huo huo kuwa uko juu ya mwaingu, zaidi ya mita 1,500 juu ya mawingu. Ni rubani tu anaweza kutamka alivyotamka Joseph.

Baada ya kuutangazia ulimwengu kuwa nimefanikiwa kufika kileleni, tulianza kuteremka kuelekea Kambi ya Barafu. Wabeba mizigo wanaotupita kwa kasi wanaleta mkanganyiko katika ugumu unaowakabili watu wanaopanda mlima kwa mara ya kwanza. Na hakuna sehemu ambapo ugumu huu unajitokeza kwa kiasi kikubwa kama kipande kati ya Kambi ya Barafu na Stella Point. Ni hapa ambapo wengi ambao wanashindwa kuendelea kutokana na athari za kuwepo katika hali ya uwanda wa juu pamoja na matumizi ya nguvu wanajitenga na wale wazoefu wa kupanda milima. Katika mazingira haya, mzee wa takribani miaka 70 alitupita kama vile anakimbia akiwa na muongozaji wake akijitahidi kwenda kwa kasi ya yule mzee. Michezo ya Olimpiki ya Beijing ikiwa iko mbioni nahisi kuwa huyu mzee anaweza kuwa anatumia madawa ya kuongeza nguvu. Anaweza kuwaadhiri hata wale wenye umri wa kuwa wajukuu zake.

Tunavyozidi kuteremka baada ya kupita Kambi ya Barafu tunakutana na wanaoelekea kileleni. Wanauliza, "Hali ilikuwaje? Jibu langu la mwanzo nasema "kasheshe". Le anatoa jibu ambalo la kutia moyo zaidi. Anasifia mandhari na kusema, "Nzuri sana, ya kustaajabisha." Halafu nakumbuka kuwa hata mimi nilipanda Kilimanjaro kwa madhumuni ya kuona mandhari: mandhari ya kuvutia ya Mawenzi jua lilipochomoza; taswira  za umbali mrefu na muonekano wa njia zenye mizungukuko zilizopo kwenye kipande kati ya Mawenzi na Kibo; na hali ya kujisikia kama niko kwenye Ncha ya Kaskazini nilipokuwa kwenye Kambi ya Crater. Lakini, baba lao, kusimama juu ya ardhi na kutazama mawingu yakiwa chini yako. Nilisimama pale nikivuta hewa ya ubaridi ya mlimani na nilichoweza kusema tu ni "kasheshe."

Leo tulitembea kutoka Kambi ya Crater (iliyopo mita 5,790 juu ya usawa wa bahari), kupita Kambi ya Barafu (iliyopo mita 4,600 juu ya usawa wa bahari), kupita Kambi ya Millenium ya Juu (iliyopo mita 3,797 juu ya usawa wa bahari), mpaka Kambi ya Mweka (iliyopo mita 3,100 juu ya usawa wa bahari) ambako tulilala kwa siku ya mwisho. Hii ilikuwa ni safari moja ngumu sana, na nilihisi misuli yangu ya miguu ikianza kufikia kikomo kutokana na kutembea mara kwa mara kwa siku sita.

Makala ijayo: akili zilizoganda na sababu ya kuacha kuvuta sigara


Makala zinazohusiana na hii:

Friday, October 1, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya nane kati ya kumi)

Jumapili Agosti 2008
Ingawa nilikuwa najiamini kwa kiasi kikubwa leo (kwa sababu ya kunywa Red Bull moja jana usiku, na nyingine asubuhi), wenzangu walikuwa na hofu juu yangu. Njia mbadala ambayo tulijadili katika siku chache zilizopita ilikuwa ni kwamba, badala ya kufanya jaribio moja la kufika kileleni toka Kambi ya Barafu kuanzia saa sita usiku, tuliamua kuanza asubuhi. Aidha, kwa njia hiyo mbadala tuliyoijadili, iwapo tutafika Stella Point (baada ya mpando mmoja mkali sana wa leo), na nitajisikia bado naweza kumalizia kilomita moja kufika kilele cha Uhuru ambayo inahusisha mpando mwepesi kwenye sehemu ya juu ya Mlima Kilimanjaro, basi nitamalizia kipande cha kutoka Stella Point mpaka kielele cha Uhuru.

Lakini kama nguvu ya Red Bull itakuwa imeisha mwilini baada ya kufika Stella Point, iliyopo urefu wa mita 5,756 juu ya usawa wa bahari, basi tutaelekea Kambi ya Crater, iliyopo urefu wa mita 5,790 juu ya usawa wa bahari, na tutajaribu kufika kileleni kesho asubuhi. Tulikubaliana pia iwapo Le ataona kama mwendo wangu ni wa polepole sana, yeye na Saidi, msaidizi wa Yahoo, watatuacha na kutangulia. Kila mmoja alihisi begi langu lilikuwa na uzito wa ziada na nilishauriwa kupunguza nguo kutoka kwenye begi na kubaki na vitu muhimu tu.
Kabla tu ya mawio, Kilele cha Mawenzi kinavyoonekana.
Kulinganisha na siku zilizopita, leo kulikuwa na wakweaji wachache zaidi waliyotupita njiani. Na kwa hakika, hata wapagazi, ambao walikuwa wana kawaida ya kutupita kama tumesimama, leo walitembea polepole zaidi wakati tukielekea Stella Point. Wengine walishindwa hata kutupita na waliendelea kutembea nyuma yetu. Tuliona taswira ya kuvutia kabisa ya Mawenzi, kilele cha pili cha Mlima Kilimanjaro, na sehemu ya katikati ya Kibo na Mawenzi, inayoitwa saddle kwa Kiingereza.

Kadiri saa zilivyozidi kupita, wote waliyokuwa na hofu juu yangu walianza kukubali kuwa tulikuwa tunasonga mbele kwa kasi nzuri kabisa. Tulivyowasili Stella Point nilihisi kuwa nina nguvu za kutosha kuelekea kilele cha Uhuru. Nilishangaa kuona kuwa ile kilomita moja ya mwisho iligeuka kuwa sehemu moja ngumu kuliko zote. Yawezekana kabisa kuwa nilikuwa nimeishiwa Red Bull. Kutokea Stella Point, Le alieleka Kambi ya Crater, akikusudia kupanda kileleni baadaye kwa ajili ya machweo na kwa mara ya pili kesho kwa ajili ya mawio.

Nilifika kilele cha Uhuru na Yahoo muda kidogo baada ya saa 9 alasiri, na muda mfupi baadaye raia wa Ujerumani na msindikizaji wake walifika pale kileleni. Tuliwapiga picha, na wao wakatupiga sisi picha. Nilijaribu kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu lakini sikuweza kupata mawasiliano. Kwa mbali kidogo, niliona waya ambao nilihisi kama ulikuwa kwenye sehemu ya juu kidogo kuliko Kilele cha Uhuru. Yahoo na yule muongozaji mwingine walikubaliana nami kuwa sehemu ile ilionekana iko juu zaidi ya pale tulipokuwa, na wakasema kuwa chombo kinachopima urefu kutoka usawa wa bahari huonyesha kuwa kuna sehemu moja kati ya Stella Point na Kilele cha Uhuru ambayo huashiria kuwa ni juu zaidi ya Kilele cha Uhuru. Nikitafakari yaliyopita na hasa baada ya ile fatiki kati ya Stella Point na kilele cha Uhuru, najiuliza iwapo kilele kinaweza kuwa "kimesogezwa" chini kidogo kupunguza idadi ya watu wanaoshindwa kufika kilele halisi.
Yahoo (kushoto) na mimi (kulia) kileleni.
Tulilala Kambi ya Crater mbele ya mwamba mkubwa wa barafu. Nilijihisi kama niko kwenye duara la Ncha ya Kaskazini. Ulikuwa ni usiku wa mhangaiko mkubwa kwangu. Wakati wa mpando wa kuelekea Stella Point nilivuta vumbi nyingi kwa sababu ya kuwa nyuma ya Pius, Le, na Saidi na hali hiyo ilinisababishia kupata shida kubwa kupumua usiku ule. Ilikuwa ni usiku wa baridi kali. Kwa mara ya kwanza, nililala nikiwa nimevaa koti zito la baridi.

Makala ijayo: Kuna mtu anatumia madawa ya kuongeza nguvu?


Makala zinazohusiana na hii: