Jumatatu 25 Agosti 2008
Le na Yahoo walianza safari ya kuelekea Kilele cha Uhuru saa 10:00 alfajiri kuwahi mawio. Baada ya kupambazuka nilitembea juu ya eneo la tambarare la kasoko (shimo la katikati ya volkano) nikiwa pamoja na muongozaji msaidizi hadi Stella Point ambako nilituma ujumbe wa maandishi wa simu niliyokusudia kuutuma jana tokea kileleni: "Salamu toka Kilele cha Uhuru, kilele cha Mlima Kilimanjaro (mita 5,896)..."
Baadhi ya majibu niliyoyapata yalikuwa yanapendeza. Joseph Ibanda, rubani, aliandika: "..kwa hakika mandhari itakuwa ya kustaajabisha hapo ulipo..." Asingeweza kutumia msemo uliyo bora zaidi kuelezea hisia zangu na hapakuwa na sehemu bora zaidi kupata hizo hisia kuliko pale niliposimama wakati nasoma ujumbe wake.
Hema langu mbele ya barafu katika Kambi ya Crater |
Kushoto kwangu kulikuwa na eneo pana la wazi kati ya Kibo na Mawenzi, mbali lakini kukionekana vizuri kabisa. Chini zaidi kulikuwa na mandhari nzuri kwa kiasi cha mita 1,500 halafu utando mzito wa mawingu. Siwezi kuelezea msisimko wa kusimama juu ya ardhi na wakati huo huo kuwa uko juu ya mwaingu, zaidi ya mita 1,500 juu ya mawingu. Ni rubani tu anaweza kutamka alivyotamka Joseph.
Baada ya kuutangazia ulimwengu kuwa nimefanikiwa kufika kileleni, tulianza kuteremka kuelekea Kambi ya Barafu. Wabeba mizigo wanaotupita kwa kasi wanaleta mkanganyiko katika ugumu unaowakabili watu wanaopanda mlima kwa mara ya kwanza. Na hakuna sehemu ambapo ugumu huu unajitokeza kwa kiasi kikubwa kama kipande kati ya Kambi ya Barafu na Stella Point. Ni hapa ambapo wengi ambao wanashindwa kuendelea kutokana na athari za kuwepo katika hali ya uwanda wa juu pamoja na matumizi ya nguvu wanajitenga na wale wazoefu wa kupanda milima. Katika mazingira haya, mzee wa takribani miaka 70 alitupita kama vile anakimbia akiwa na muongozaji wake akijitahidi kwenda kwa kasi ya yule mzee. Michezo ya Olimpiki ya Beijing ikiwa iko mbioni nahisi kuwa huyu mzee anaweza kuwa anatumia madawa ya kuongeza nguvu. Anaweza kuwaadhiri hata wale wenye umri wa kuwa wajukuu zake.
Tunavyozidi kuteremka baada ya kupita Kambi ya Barafu tunakutana na wanaoelekea kileleni. Wanauliza, "Hali ilikuwaje? Jibu langu la mwanzo nasema "kasheshe". Le anatoa jibu ambalo la kutia moyo zaidi. Anasifia mandhari na kusema, "Nzuri sana, ya kustaajabisha." Halafu nakumbuka kuwa hata mimi nilipanda Kilimanjaro kwa madhumuni ya kuona mandhari: mandhari ya kuvutia ya Mawenzi jua lilipochomoza; taswira za umbali mrefu na muonekano wa njia zenye mizungukuko zilizopo kwenye kipande kati ya Mawenzi na Kibo; na hali ya kujisikia kama niko kwenye Ncha ya Kaskazini nilipokuwa kwenye Kambi ya Crater. Lakini, baba lao, kusimama juu ya ardhi na kutazama mawingu yakiwa chini yako. Nilisimama pale nikivuta hewa ya ubaridi ya mlimani na nilichoweza kusema tu ni "kasheshe."
Leo tulitembea kutoka Kambi ya Crater (iliyopo mita 5,790 juu ya usawa wa bahari), kupita Kambi ya Barafu (iliyopo mita 4,600 juu ya usawa wa bahari), kupita Kambi ya Millenium ya Juu (iliyopo mita 3,797 juu ya usawa wa bahari), mpaka Kambi ya Mweka (iliyopo mita 3,100 juu ya usawa wa bahari) ambako tulilala kwa siku ya mwisho. Hii ilikuwa ni safari moja ngumu sana, na nilihisi misuli yangu ya miguu ikianza kufikia kikomo kutokana na kutembea mara kwa mara kwa siku sita.
Makala ijayo: akili zilizoganda na sababu ya kuacha kuvuta sigara
Makala zinazohusiana na hii:
1 comment:
Mheshimiwa Madaraka,
Habari za Mwitongo?
Naamini hujambo na kazi unachapa kweli kweli.
Nimesubiri kwa hamu, kisa chako kumalizia
hakika nataka kujua, gea ulotumia kuacha kuvuta sigara
makala ya kumi nimesubiri weeee...mbona kimya?
Kiu ni kubwa ya kujua mwisho wa mwanzo.
Ubarikiwe ndugu maana simulizi zako tamu.
Post a Comment