Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, October 1, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya nane kati ya kumi)

Jumapili Agosti 2008
Ingawa nilikuwa najiamini kwa kiasi kikubwa leo (kwa sababu ya kunywa Red Bull moja jana usiku, na nyingine asubuhi), wenzangu walikuwa na hofu juu yangu. Njia mbadala ambayo tulijadili katika siku chache zilizopita ilikuwa ni kwamba, badala ya kufanya jaribio moja la kufika kileleni toka Kambi ya Barafu kuanzia saa sita usiku, tuliamua kuanza asubuhi. Aidha, kwa njia hiyo mbadala tuliyoijadili, iwapo tutafika Stella Point (baada ya mpando mmoja mkali sana wa leo), na nitajisikia bado naweza kumalizia kilomita moja kufika kilele cha Uhuru ambayo inahusisha mpando mwepesi kwenye sehemu ya juu ya Mlima Kilimanjaro, basi nitamalizia kipande cha kutoka Stella Point mpaka kielele cha Uhuru.

Lakini kama nguvu ya Red Bull itakuwa imeisha mwilini baada ya kufika Stella Point, iliyopo urefu wa mita 5,756 juu ya usawa wa bahari, basi tutaelekea Kambi ya Crater, iliyopo urefu wa mita 5,790 juu ya usawa wa bahari, na tutajaribu kufika kileleni kesho asubuhi. Tulikubaliana pia iwapo Le ataona kama mwendo wangu ni wa polepole sana, yeye na Saidi, msaidizi wa Yahoo, watatuacha na kutangulia. Kila mmoja alihisi begi langu lilikuwa na uzito wa ziada na nilishauriwa kupunguza nguo kutoka kwenye begi na kubaki na vitu muhimu tu.
Kabla tu ya mawio, Kilele cha Mawenzi kinavyoonekana.
Kulinganisha na siku zilizopita, leo kulikuwa na wakweaji wachache zaidi waliyotupita njiani. Na kwa hakika, hata wapagazi, ambao walikuwa wana kawaida ya kutupita kama tumesimama, leo walitembea polepole zaidi wakati tukielekea Stella Point. Wengine walishindwa hata kutupita na waliendelea kutembea nyuma yetu. Tuliona taswira ya kuvutia kabisa ya Mawenzi, kilele cha pili cha Mlima Kilimanjaro, na sehemu ya katikati ya Kibo na Mawenzi, inayoitwa saddle kwa Kiingereza.

Kadiri saa zilivyozidi kupita, wote waliyokuwa na hofu juu yangu walianza kukubali kuwa tulikuwa tunasonga mbele kwa kasi nzuri kabisa. Tulivyowasili Stella Point nilihisi kuwa nina nguvu za kutosha kuelekea kilele cha Uhuru. Nilishangaa kuona kuwa ile kilomita moja ya mwisho iligeuka kuwa sehemu moja ngumu kuliko zote. Yawezekana kabisa kuwa nilikuwa nimeishiwa Red Bull. Kutokea Stella Point, Le alieleka Kambi ya Crater, akikusudia kupanda kileleni baadaye kwa ajili ya machweo na kwa mara ya pili kesho kwa ajili ya mawio.

Nilifika kilele cha Uhuru na Yahoo muda kidogo baada ya saa 9 alasiri, na muda mfupi baadaye raia wa Ujerumani na msindikizaji wake walifika pale kileleni. Tuliwapiga picha, na wao wakatupiga sisi picha. Nilijaribu kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu lakini sikuweza kupata mawasiliano. Kwa mbali kidogo, niliona waya ambao nilihisi kama ulikuwa kwenye sehemu ya juu kidogo kuliko Kilele cha Uhuru. Yahoo na yule muongozaji mwingine walikubaliana nami kuwa sehemu ile ilionekana iko juu zaidi ya pale tulipokuwa, na wakasema kuwa chombo kinachopima urefu kutoka usawa wa bahari huonyesha kuwa kuna sehemu moja kati ya Stella Point na Kilele cha Uhuru ambayo huashiria kuwa ni juu zaidi ya Kilele cha Uhuru. Nikitafakari yaliyopita na hasa baada ya ile fatiki kati ya Stella Point na kilele cha Uhuru, najiuliza iwapo kilele kinaweza kuwa "kimesogezwa" chini kidogo kupunguza idadi ya watu wanaoshindwa kufika kilele halisi.
Yahoo (kushoto) na mimi (kulia) kileleni.
Tulilala Kambi ya Crater mbele ya mwamba mkubwa wa barafu. Nilijihisi kama niko kwenye duara la Ncha ya Kaskazini. Ulikuwa ni usiku wa mhangaiko mkubwa kwangu. Wakati wa mpando wa kuelekea Stella Point nilivuta vumbi nyingi kwa sababu ya kuwa nyuma ya Pius, Le, na Saidi na hali hiyo ilinisababishia kupata shida kubwa kupumua usiku ule. Ilikuwa ni usiku wa baridi kali. Kwa mara ya kwanza, nililala nikiwa nimevaa koti zito la baridi.

Makala ijayo: Kuna mtu anatumia madawa ya kuongeza nguvu?


Makala zinazohusiana na hii:

No comments: