Mwaka 2012, nikiwa kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro nikiongozana na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto ya Mwanza, nilipokea simu wakati tukitembea kati ya kambi ya Horombo na kambi ya Kibo.
Aliyenipigia simu alijitambulisha akisema mimi hununua vocha za simu kwenye kibanda chake mjini Musoma.
Alinisimulia kuwa alikuwa anabishana na wenzake, baadhi yao wakisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, wengine wakipinga na kusema siyo kweli. Akaniomba mimi nimalize ubishi wao.
Kwanza, ingawa nilikuwa kwenye njia ya Marangu kuelekea kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, njia ambayo inasemekana kuwa ni moja ya njia rahisi za kufika kileleni, ukweaji Mlima Kilimanjaro wakati wote unampa mtu changamoto za kila aina.
Mawasiliano ya simu za kiganja huwa ni ya kubahatisha kutegemea na sehemu ulipo na kutegemea na hali ya hewa. Mlimani kwenyewe pumzi inavutika kwa kutumia nguvu na jitihada ya ziada. Aidha, kwa sababu ya baridi chaji ya betri ya simu haikai kwa muda mrefu.
Kwa sababu hizo, unapopigiwa simu, unategemea itahusiana na suala la dharura au linalohusiana na kazi au suala lingine la aina hiyo.
Lakini nilielewa kuwa, kwa aliyenipigia simu, kufahamu kama Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga au la ilikuwa muhimu kwake kwa wakati ule.
Nilimwambia kuwa hata mimi husikia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, na wakati fulani wazee wa Yanga walitembelea Butiama nikawauliza swali hilo lakini kwa wakati ule aliponiuliza sikukumbuka walinijibu nini.
Ninachokumbuka ni kusikia mtu akisema kuwa kadi namba 1 ya Dar es Salaam Young Africans huwa haijulikani kapewa nani, na ndiyo hiyo watu wanasema ilikuwa kadi ya Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere mwenyewe aliposimulia kuhusu kuhudhuria mechi za soka alisema ilikuwa muhimu kuwa asikae mtu mbele yake, kwa sababu kila wakati mchezaji alipokaribia kufunga goli naye alikuwa akirusha mguu mbele kupiga mpira hewa.
Bofya kwenye picha hapo chini kusoma taarifa juu ya mechi chache za mpira ambazo Mwalimu Nyerere alihudhuria:
Mwaka 1972, Rais Jaffar El Nimeiry wa Sudan akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye mechi ya soka dhidi ya timu ya taifa ya Sudan. |
http://muhunda.blogspot.com/2013/07/simba-sports-club-wakaribishwa-butiama.html
No comments:
Post a Comment