Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, April 14, 2013

Jifunze Kiswahili kwa njia ya mtandao

Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Georgia inatoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa njia ya mtandao.

Maelezo yaliyopo kwenye tovuti inayoitwa Kiswahili kwa Komputa yanaonyesha kuwa kozi hiyo ya Kiswahili inaendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu na inaelekea kuwa hufundishwa darasani pamoja na nyongeza ya masomo yaliyopo kwenye tovuti hiyo.

Mbali na kuwa Kiswahili sahihi ni "kompyuta" na siyo "komputa" na kuwa baadhi ya matamshi yaliyorekodiwa kwa njia ya sauti yanatofautiana na matamshi niliyozowea kusikia (mfano "redio" inatamkwa "radio"), tovuti hiyo bado inaweza kuwa ya manufaa makubwa na inaweza kumsaidia mwanafunzi yoyote wa lugha ya Kiswahili ambaye anafahamu vyema Kiingereza na anaweza kujifunza mwenyewe kutokana na maelezo yaliyopo.

Anwani ya tovuti hii hapa: http://www.africa.uga.edu/Kiswahili/doe/index.html

Kila mwaka wa masomo una sura sita, na kozi inakamilika kwa sura 18. Mwisho wa kila sura mwanafunzi anapaswa kufanya mtihani ambao unaweza kutumwa kwa njia ya mtandao kwa mwalimu kwa masahihisho.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/02/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2013/01/lugha-yetu-kiswahili.html

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya nne kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya nne kati ya sehemu nne)

Ikiwa kulikuwa na mchango wa serikali katika muziki, basi ulikuwa mdogo au ulikuwa ni kwa shughuli maalumu lakini si kwa kutengeneza mazingira ya kuwezesha unafuu kwa wanamuziki kwa ujumla. Idara ya Utamaduni imeendelea kupata bajeti ndogo ambayo imefanya Baraza La Sanaa La Taifa kuendelea kubaki Dar es Salaam tu, likibangaiza kuweko kwa kutegemea kutoa vibali mbalimbali kwa wasanii, na nguvu zake kuonekana Dar es Salaam tu. Na kwa kuwa hakuna Maafisa Utamaduni Mkoa, na Maafisa Utamaduni Wilaya na Manispaa wako chini ya serikali za mitaa hivyo kuwa wizara tofauti na Waziri wa Utamaduni, nguvu za serikali katika utamaduni ni 0.

COSOTA, chombo ambacho shughuli yake ilikuwa ni kulinda hakimiliki za wasanii na ambacho kilikuwa chini ya wasanii, kwa kinyemela kabisa kimerudishwa katika mikono ya serikali, lakini bado kinakusanya mirabaha 'kwa niaba ya wasanii' huku kukiwa na bodi isiyo na uwakilishi wa wasanii kuanzia 2007. Swali: utakusanyaje pesa kwa niaba yangu lakini huniruhusu kujua ni kiasi gani umekusanya, unazitumiaje na ukiulizwa unakuwa mkali!!!!!!? Kuna wasanii wamekuwa wakidai kurudishiwa COSOTA, ushauri wangu wasanii wakae wajipange  na kuelewa vizuri sheria ya Hakimiliki kabla ya kujitwishwa zigo hilo la miba.

Katika miezi sita ya mwisho ya 2012 kumejitokeza spidi kali ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato kutengeneza mazingira ya kukusanya mapato kutokana na mauzo ya kazi za muziki na filamu. Kimsingi kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi na wasanii ni wananchi pia, lakini taratibu zake ndiyo zinanipa utata, hasa pale ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa njia hii itasaidia wasanii kwa kupunguza kuibiwa. 

Sentensi hii inaonyesha wazi anayeiongelea au hajui mfumo wa biashara ya kazi muziki, au kwa makusudi anapotosha ili kuficha kitu. Wasanii wengi huwa wamekwishalipwa kwa kazi ambazo zimesambaa na ziko barabarani zinaibiwa, wanaoibiwa ni wasambazaji. Hivyo kulinda kazi hizo unamlinda msambazaji si msanii. Pia kuanza kukusanya kodi kwa kazi hizi kumepewa jina ‘kurasimishwa  kwa kazi ya usanii’. 

Kuna mabilioni wasanii wanatakiwa walipwe na watumiaji wa kazi za sanaa, kama redio na TV, mapromota, waajiri na kadhalika lakini hakuna anaeliongelea hilo wala hakuna anaetamka takwimu hizo. Kuna kazi ya kurudisha mitaala ya masomo ya sanaa mashuleni, kurudisha vyuo vya walimu wa sanaa, kurudisha maafisa utamaduni kuwa chini ya Wizara ya Utamaduni kuwawezesha kufanya kazi zao kadiri ya Sera ya Utamaduni, na mengine mengi ya aina hiyo ndiyo ningeona kurasimisha kazi za sanaa. Lakini kukusanya kodi tu kwa kazi ambazo hata hivyo mikataba yake mingi inautata na kuita urasimishaji si sahihi.

Katika nchi nyingi critics au watu ninaoweza kuwaita Kiswahili wakosoaji, huwa ni muhimu katika maendeleo ya sanaa. Watu hawa hupata heshima kutokana na kuweza kuangalia mapungufu katika kazi za sanaa na kuyasema, jambo ambalo hupelekea wasanii kujirekibisha na kutengeneza kazi bora zaidi. Hapa kwetu kutoa ushauri ni kutafuta matusi, toka kwa wasanii wenye kazi husika, vyombo vya habari na hata sehemu ya jamii. Umefika muda wahusika kuchukua uchambuzi kama changamoto za kuboresha kazi.

Niliyoyataja hapa yote yako wazi. Ninachotegemea ni kuona 2013 hatua zinaanza kupigwa kurekebisha ili wanamuziki wa nchi hii nao wapate nafasi sawa na wengine wa nchi nyingine.

John Kitime
31.12.2012
Sinza, Dar es Salaam 

Taarifa zinazohusiana na hii:

Friday, March 22, 2013

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya tatu kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya tatu kati ya sehemu nne)


Tasnia ya muziki wa Tanzania katika tafiti mojawapo umeitwa ‘the radio-driven contemporary music industry’. Kwa maneno rahisi, tasnia ambayo imekuwa inaendeshwa na redio. Redio zimekuwa na uwezo wa kumpandisha na kumshusha mwanamuziki, kumtafutia soko, kumzibia soko na kadhalika. Hali hii ikisindikizwa na rushwa ambayo imetapakaa katika jamii yetu, unapata picha kuwa kungeweza kukawa na sura bora au tofauti ya muziki hali isingekuwa ilivyo.

Kuna ripoti za watu kutoa hongo nyimbo za wenzao zisipigwe, hongo ili nyimbo zipigwe, visasi vya kuzuia nyimbo zisipigwe na kadhalika. Na katika jamii ambayo imekuwa na kawaida ya kutegemea vyombo vya habari kujua muziki gani mpya na mzuri, uwanja huu si uwanja ulio tambarare hata kidogo. Bahati mbaya inaonekana wenye vyombo hivi wako mbali na ukweli unaoendelea katika vyombo vyao au kwa kutokujua au kupuuza.

Janga hili limevikumba hata vyombo ambavyo vinaendeshwa na taasisi za dini. Wanamuziki wa muziki wa injili nao pia wanalia kudaiwa rushwa na watangazaji wa radio za injili!.  Nakumbuka siku niliyopata nafasi kuongea na kiongozi mmoja wa dini ambaye kanisa lake linaendesha kituo cha redio, nilipata mshangao baada ya mkuu huyo, kuanza kutetea watangazaji wake badala ya kuamua kufanya uchunguzi wa tuhuma.

Umefika muda wa redio kuanza kujigawa kimuziki. Ni kichekesho mji kuwa na vituo vya redio 30 halafu vyote vinapiga aina hiyohiyo ya muziki, wakati kuna aina mbalimbali za watu. Ajabu ni kuwa wenye redio wanajua kuwa katika nchi nyingine unaweza kukuta redio iliyoamua kupiga aina fulani tu ya muziki, Jazz Radio, Country music Radio, Classic Music Radio, lakini hilo limekuwa gumu kwao kutekeleza hapa. Kuwe na utofauti, wasikilizaji tuko wa aina tofauti.

Vyombo vya habari vijitahidi kupata wataalamu husika wa aina tofauti za muziki, muziki unaviingizia vyombo hivyo mabilioni ya fedha, vyombo vya habari viupe heshima yake. Bila muziki hakuna redio.

Magazeti yamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza aina mbalimbali za wasanii na sanaa. Pamoja na hongera kwa kazi nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ipo tupu, hakuna wataalamu wa uandishi wa habari za muziki. Hivyo habari nyingi za muziki zinaandikwa na waandishi kama wapenzi wa muziki na si wataalam wa uandishi wa muziki, jambo ambalo liko tofauti na uandishi wa michezo, kwa mfano soka. Unaweza ukasoma habari ya soka ambapo mwandish atakueleza nafasi za wachezaji, kama ni faulo, ni nini kilisababisha, na kama ni goli lilikuwa ni la kichwa au kona au penalty. Hili haliko katika muziki. Utaambiwa tu bendi ilipagawisha, au msanii fulani ateka nyoyo za wapenzi, na maelezo ya juu juu kama yale.

Kunahitajika kuanzishwa mafunzo ya elimu ya uandishi wa kazi za sanaa. Hili litapunguza hata vurugu kama zilizotawala mwaka huu za wapiga picha kufikia hata kulala chini ili tu wapate picha ya nguo za ndani za msanii na hayo ndio kuwa maelezo makuu ya onyesho zima la muziki.

(itaendelea)

Taarifa zinazohusiana na hii:

Thursday, March 21, 2013

Mada yangu ya leo: Viongozi wakae maofisini na kupunguza uzinduzi

Kwa maoni yangu, viongozi wetu hawana muda wa kutosha kukaa kwenye ofisi zao na kufanya kazi ambayo walipa kodi wanatarajia zisimamiwe na viongozi wao. Sababu kubwa inayosababisha tatizo hili ni viongozi wetu kukubali mialiko ya uzinduzi wa kila jambo ambalo Watanzania wanaweza kubuni.

Na hapa sizungumzii viongozi wakuu tu wa nchi, nazungumzia viongozi wa ngazi zote kwa sababu nchini Tanzania imekuwa desturi sasa kwa kila jambo kuwa na uzinduzi rasmi, kuanzia kanda mpya ya kwaya mpaka kinywaji kipya.

Lakini ni dhahiri kuwa mifano inayopatikana kwa urahisi inawahusu viongozi wakuu wa nchi kwa kuwa habari zao zinaandikwa zaidi kuliko zile za viongozi wa ngazi za chini.

Angalia mifano ifuatayo ya Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu, na utapata picha ya ukubwa wa tatizo hili:

Rais Jakaya Kikwete
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Bilal
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Ni dhahiri kuwa kwa kila kiongozi kuna sehemu au shughuli fulani ambayo anapaswa kuhudhuria kwa sababu ya umuhimu wa shughuli yenyewe na nafasi yake katika uongozi, lakini ni dhahiri kuwa kuna shughuli nyingine nyingi ambazo hazina umuhimu kwa viongozi wetu kuhudhuria.

Kuna umuhimu kwa sheria kutumika kutamka shughuli rasmi ambazo viongozi wa ngazi ya Taifa wanapaswa kuhudhuria ili kupunguza mlolongo wa shughuli ambazo tunaoona zinazinduliwa na viongozi hawa. Hili likifanyika, litapunguza gharama kwa serikali na pia kuwapa muda mkubwa zaidi viongozi wetu kubaki kwenye sehemu zao za kazi na kusimamia vyema shughuli za serikali.

Kama nilivyosema awali, hapa nimetoa mifano ya viongozi wa kitaifa kwa sababu ndiyo mifano iliyo rahisi kuitoa. Lakini hili ni tatizo lililopo katika ngazi zote, kuanzia mawaziri mpaka watendaji wa vijiji.

Watanzania nao wabadilishe fikra kuwa haiwezekani kuchapa kazi bila kufanya uzinduzi.

Sunday, March 17, 2013

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya pili kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya pili kati ya sehemu nne)

Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio ambao muziki huu unastahili kurekodiwa. Studio nyingi zimejengwa kwa ajili ya muziki wa aina ya Bongoflava tu. Zile studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi gharama yake huwa ni kubwa sana.

Kundi la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa kiasili, kuwa na muziki huo ukifuata taratibu nzuri ya kurekodiwa unauza vizuri sana. Bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha muziki na ngoma zao, vinaiga uchezaji wa Makirikiri.

Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya; sijausahau. Kwa kweli muziki huu umebaki  hasa kwenye muziki wa injili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.

Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini  kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii.

Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndiyo alama ya muziki wa Tanzania. Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, Afrika Kusini; pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao.

Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndiyo unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndiyo wamekuwa waalimu wetu wakuu.

Ushauri kwa ma-producer wa Bongoflava: kuangalia pia muziki wetu wa asili humu ndani ya nchi ili tuje tumalize 2013 na kitu chetu ambacho Wanaigeria, Wakongo nao pia waige toka kwetu. Inawezekana sana maana wimbo wa Weekend wa Afro70 uliwahi kuweko katika  kumi bora 1972, Nigeria.

Muziki wa injili pamoja na kuwa ndiyo unaotegemewa kutufundisha maadili, ulikuwa na kasoro moja kubwa nayo ni kukosa maadili kwa ku-copy na ku-paste. Nyimbo nyingi zilizokuwa maarufu na kuteka hisia za maelfu ya watu zilikuwa ni kuiga moja kwa moja kutoka Afrika ya kusini. Najiuliza je ndiyo kilichopunguza moto wa muziki huu 2012? Kulikuwa hakuna za kukopi? Wanamuziki wa injili kama ilivyo kwa ushauri kuhusu Bongoflava, ni muda wa kurudi nyuma na kutumia rasilimali ya utamaduni iliyoko kuleta mabadiliko na kukuza soko la muziki huo.

(itaendelea)

Taarifa zinazohusiana na hii: