******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012
makala ya John Kitime
(Sehemu
ya kwanza kati ya sehemu nne)
Mwaka
2012 ndiyo huo umetokomea Ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na
yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki
wa bendi, matarumbeta, muziki wa injili, na muziki wa kiasili.
Si
siri kuwa muziki wa Bongoflava ndiyo uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari
na sehemu nyingi za maonyesho ukifuatiliwa na muziki wa Taarabu na muziki wa injili.
Katika
muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndiyo waliokuwa wakipewa
kipaumbele katika tasnia hii. Waimbaji
katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndiyo waliotajwa na kupewa sifa
kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita
katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama
mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali.
Hakuna
ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndiyo muziki uliopewa muda mchache
sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo
zimejikita kufuata mipigo ya Kikongo zilipewa nafasi zaidi ya bendi ambazo
zimejichagulia njia nyingine za muziki wao.
Kuna
sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa Bongoflava kuchukua nafasi zaidi
katika vyombo vya habari. La kwanza ni uwingi wa kazi za Bongoflava
zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya aina moja au nyingine, na katika
studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo
kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea
kutawala anga ya vyombo vya habari, na pia ni kutokana na mfumo wa vyombo vyetu
vyote kujikita katika mfumo wa aina fulani tu za muziki.
Kwa
mtazamo wangu heka heka za muziki wa injili zilipungua 2012. Yale matamasha
makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa
nyingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Muziki
wa Taarabu haujaleta mabadiliko kimuziki. Mengi yaliyofanywa katika 2012 ni
marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show
katika taarabu, upigaji wa gitaa na kuliachia peke yake kama ilivyokuwa kwa
bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini na zile video za kucheza
mbele ya viwanja vya hoteli. Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo
tena ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo pia.
Bendi
ziko katika wakati mgumu. Wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa
muziki wa bendi haupigwi, kumekuweko na jitihada ndogo za bendi kurekodi nyimbo
mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo muziki wa bendi
ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kurushwa hewani.
Bendi chache zilizorekodi hazijaja na
nyimbo zilizoweza kuteka umma wa Watanzania na hivyo kusababisha muziki
huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi
yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla
hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi.
(itaendelea)
Taarifa zinazohisiana na hii:
sehemu ya pili ya makala hii
sehemu ya tatu ya makala hii
Taarifa zinazohisiana na hii:
sehemu ya pili ya makala hii
sehemu ya tatu ya makala hii
No comments:
Post a Comment