******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012
makala ya John Kitime
(Sehemu ya tatu kati ya sehemu nne)
Tasnia
ya muziki wa Tanzania katika tafiti mojawapo umeitwa ‘the radio-driven contemporary music industry’. Kwa maneno rahisi,
tasnia ambayo imekuwa inaendeshwa na redio. Redio zimekuwa na uwezo wa
kumpandisha na kumshusha mwanamuziki, kumtafutia soko, kumzibia soko na
kadhalika. Hali hii ikisindikizwa na rushwa ambayo imetapakaa katika jamii
yetu, unapata picha kuwa kungeweza kukawa na sura bora au tofauti ya muziki
hali isingekuwa ilivyo.
Kuna
ripoti za watu kutoa hongo nyimbo za wenzao zisipigwe, hongo ili nyimbo
zipigwe, visasi vya kuzuia nyimbo zisipigwe na kadhalika. Na katika jamii
ambayo imekuwa na kawaida ya kutegemea vyombo vya habari kujua muziki gani mpya
na mzuri, uwanja huu si uwanja ulio tambarare hata kidogo. Bahati mbaya
inaonekana wenye vyombo hivi wako mbali na ukweli unaoendelea katika vyombo
vyao au kwa kutokujua au kupuuza.
Janga
hili limevikumba hata vyombo ambavyo vinaendeshwa na taasisi za dini.
Wanamuziki wa muziki wa injili nao pia wanalia kudaiwa rushwa na watangazaji wa
radio za injili!. Nakumbuka siku
niliyopata nafasi kuongea na kiongozi mmoja wa dini ambaye kanisa lake
linaendesha kituo cha redio, nilipata mshangao baada ya mkuu huyo, kuanza
kutetea watangazaji wake badala ya kuamua kufanya uchunguzi wa tuhuma.
Umefika
muda wa redio kuanza kujigawa kimuziki. Ni kichekesho mji kuwa na vituo vya redio
30 halafu vyote vinapiga aina hiyohiyo ya muziki, wakati kuna aina mbalimbali
za watu. Ajabu ni kuwa wenye redio wanajua kuwa katika nchi nyingine unaweza
kukuta redio iliyoamua kupiga aina fulani tu ya muziki, Jazz Radio, Country
music Radio, Classic Music Radio, lakini hilo limekuwa gumu kwao kutekeleza
hapa. Kuwe na utofauti, wasikilizaji tuko wa aina tofauti.
Vyombo
vya habari vijitahidi kupata wataalamu husika wa aina tofauti za muziki, muziki
unaviingizia vyombo hivyo mabilioni ya fedha, vyombo vya habari viupe heshima
yake. Bila muziki hakuna redio.
Magazeti
yamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza aina mbalimbali za wasanii na sanaa.
Pamoja na hongera kwa kazi nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ipo tupu, hakuna
wataalamu wa uandishi wa habari za muziki. Hivyo habari nyingi za muziki
zinaandikwa na waandishi kama wapenzi wa muziki na si wataalam wa uandishi wa
muziki, jambo ambalo liko tofauti na uandishi wa michezo, kwa mfano soka.
Unaweza ukasoma habari ya soka ambapo mwandish atakueleza nafasi za wachezaji,
kama ni faulo, ni nini kilisababisha, na kama ni goli lilikuwa ni la kichwa au
kona au penalty. Hili haliko katika muziki. Utaambiwa tu bendi ilipagawisha, au
msanii fulani ateka nyoyo za wapenzi, na maelezo ya juu juu kama yale.
Kunahitajika
kuanzishwa mafunzo ya elimu ya uandishi wa kazi za sanaa. Hili litapunguza hata
vurugu kama zilizotawala mwaka huu za wapiga picha kufikia hata kulala
chini ili tu wapate picha ya nguo za ndani za msanii na hayo ndio kuwa maelezo
makuu ya onyesho zima la muziki.
(itaendelea)
Taarifa zinazohusiana na hii:
No comments:
Post a Comment