Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, March 2, 2018

Hii ndiyo mila ya Kizananki ya kurudisha mahari

Miaka ya hivi karibuni baada ya kufariki mmoja wa shangazi zangu, nilipigiwa simu na baba yangu mdogo kunipa taarifa ya msiba na kunitaka nifike kwenye msiba.

Nilichelewa kidogo kufika kwenye msiba na aliendelea kunipigia simu mara kwa mara kunihimiza nifike mapema kwenye msiba. Alisema: "huu ni msiba wenu, njoo haraka!"

Sikuelewa maana ya ule kuwa "msiba wetu" mpaka baadaye.

Katika mila ambayo ilifuatwa miongoni mwa Wazanaki, mume anaweza kurudishiwa mahari na ndugu wa mke ili kuhalalisha wanandoa wawili kuachana na mke kurudi kwa ndugu zake.

Hili hutokea kwa sababu za kutoelewana kwa wanandoa, na hasa kama ndugu wa mke wanaamini kuwa dada yao anateswa au kudhalilishwa na mume wake.

Nilichojifunza kwenye msiba ni kuwa Mwalimu Nyerere alirudisha mahari kwa mume wa shangazi yangu na shangazi akarudi kuishi miongoni mwa ndugu zake.

Kwa desturi ya enzi hizo mke anayerudi nyumbani anatunzwa na ndugu zake. Kwa huyo shangazi, Mwalimu Nyerere alimjengea nyumba na aliendelea kuishi kwenye kijiji cha Butiama mpaka alipofariki.

Kwa mila hii mahitaji yake yote makubwa pamoja na ya watoto wake yatatimizwa  na ndugu zake. Aidha, inapotokea binti zake kuolewa basi mahari yao inachukuliwa na hao waliomrudisha nyumbani. Kwa mantiki hiyo, hata unapotokea msiba gharama za msiba zinabebwa na waliomtoa kwa mume wake.

Na ndiyo hapo nikaelewa kauli ya baba yangu mdogo: "huu ni msiba wenu!" Mwalimu Nyerere ana warithi wake ambao wanapaswa kurithi pia majukumu yake.

Lakini mila na desturi zinabadilika. Wakati wa msiba uliibuka ubishi mkali kati ya wazee juu ya mila hiyo. Baadhi yao waliona kuwa haipaswi kufuatwa kwa sasa.

Tuesday, December 19, 2017

Hili sijalielewa hata kidogo

Imefika wakati Jeshi la Polisi libadilike kidogo.

Kuna umuhimu wa polisi kuboresha huduma kwa tunaofika kwenye vituo vya polisi ili tupate huduma inayoridhisha. Nazungumzia wahalifu na wasiyo wahalifu. Wote tunastahili kupewa huduma ya kuridhisha.

Hivi karibuni, nikiwa naendesha gari, nilisimamishwa Singida mjini na afisa usalama barabarani kwa kosa la kutosimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu.

Nilikiri kosa haraka na kukubali kulipa faini ili niendelee na safari. Suala ambalo lingechukua dakika tano lilichukua saa nzima.

Nilielekezwa kwenda kituoni na afisa aliyenikamata akafika baada ya dakika kumi kunijazia hati ya malipo. Nilipodai risiti nikaambiwa mhasibu ameshaondoka, nirudi asubuhi kuchukua risiti. Ilikuwa saa kumi jioni.

Nilimfahamisha kuwa niko safarini na isingewezekana kurudi asubuhi. Ilikuwa naambiwa nirudi asubuhi kama vile naishi Singida.

Ni mpaka mhasibu alipopigiwa simu na afande ndipo aliporudi na kuniandikia risiti. Alikuwa kanuna sana kwa kurudishwa ofisini. Mdomoni alikuwa na kijiti cha kuondoa nyama zinazobaki kati ya meno baada ya kula nyama ya kuchoma.

Maoni yangu ni kuwa wakati wowote mhalifu anapotozwa faini anapaswa kupewa risiti wakati huo huo anapotozwa faini. Siyo sawa polisi wakatumia sheria kutoza faini halafu wakapuuzia kutoa risiti wakati huo huo.

Ama sivyo mhasibu anapofunga ofisi na faini zisitozwe.

Halafu, si tumeshapewa somo kuwa tusilipie kitu chochote bila kudai risiti? Au hilo somo haliwahusu polisi?

Mimi naamini linawahusu. Kupewa risiti baada ya kulipa faini si hisani. Ni haki.

Saturday, November 18, 2017

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao ni adhabu ya sheria, na kukutana uso kwa uso na unayemtukana.

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ni sheria ambayo inaainisha matusi kama mojawapo ya makosa ambayo yanaweza kumtia mtu hatiani kwa yale anayoyaandika au kwa picha anazoweka mtandaoni. Kuna baadhi ya watu, au kwa kutokujua sheria au kwa makusudi, tayari wametiwa hatiani na maandiko ambayo yanaainishwa kuwa makosa kwenye sheria hii.

Na sina shaka kuna wengi wengine watakumbwa na tatizo hilo kwa sababu inaelekea kuna watu wanaamini kuwa akiwa kajibanza pembezoni mwa nchi akarusha matusi kwenye mtandao basi siyo rahisi kupatikana.

Tatizo la kuonana uso kwa uso limenitokea leo baada ya kutembelewa Butiama na Fabian Zegge, "rafiki" wa mtandao ambaye sikutarajia kuonana naye hata siku moja. Alifika Musoma kwenye shughuli zake na akaamua kunitembelea Butiama.

Mara baada ya kusalimiana naye nilimwambia kuwa angekuwa ni mtu ambaye tulirushiana maneno yasiyo na ustaarabu katika mawasiliano yetu kwenye mtandano, leo hii ningeona aibu kujitokeza kusalimiana naye. Ningemwambia amekosea namba ya simu aliponipigia awali kutaka kufahamu iwapo nipo nyumbani.
Kutoka kushoto kwenda kulia: mimi, Fabian Zegge, na mwenyeji wake.
Nimejifunza mambo mawili ya msingi leo: kwanza, hawa "marafiki" wa ndani ya mtandao ambao wengi wetu tunaamini hatutaonana nao hata siku moja ni watu ambao tunaweza kuonana nao wakati wowote. Sikutarajia kuonana na Fabian Butiama.

Pili, na kwa kutambua ukweli huo, nimeone umuhimu kwamba tunapowasiliana na watu mbalimbali kwenye majukwaa kwenye mtandao tunapaswa kuongozwa na ustaarabu kwenye kauli zetu.

Bila kuzingatia hayo tutaumbuliwa na sheria au aibu ya kukutana na tunaowatukana.

Saturday, November 11, 2017

Mimba zisizoisha za Chausiku Suleiman

Zaidi ya miaka sita iliyopita nilipata fursa ya kumtembelea mama mmoja, Chausiku Suleiman, anayeishi Maji Chai, jirani na Tengeru kwenye barabara kuu ya kutoka Moshi kwenda Arusha. Alinipa simulizi za ajabu. Yeye anapata ujauzito kila anapojifungua, bila hata kukutana na mume wake.

Nilipoonana naye alikuwa na umri wa miaka 47 na alikuwa na watoto 16 aliyewazaa ndani ya kipindi cha miaka 30. Tatizo lake lilianza alipopata ujauzito wa mtoto wa tano. Majuma matatu baada kujifungua alihisi kuwa alikuwa mjamzito tena. Nilipoonana naye mwaka 2011 alisema kuwa mimba yake wakati huo ilikuwa ina zaidi ya miaka mitatu.

Chausiku Suleiman akiwa na baadhi ya watoto wake, Maji Chai, Arusha.
Nilipomuuliza iwapo ametafuta ushauri wa daktari aliniambia kuwa madaktari wameshindwa kubaini tatizo lake na wameshindwa kuona kama ana kichanga tumboni.

Alisema anahisi kuwa madaktari wanaamini kuwa ana imani kuwa na tatizo ambalo halipo.

Saturday, September 2, 2017

Hivi Mwalimu Nyerere alikuwa Yanga au Simba?

Hivi Mwalimu Nyerere alikuwa Yanga au Simba? Hili ni swali ambalo nimewahi kuulizwa sehemu ambayo sikutarajia kabisa kuulizwa.

Mwaka 2012, nikiwa kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro nikiongozana na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto ya Mwanza, nilipokea simu wakati tukitembea kati ya kambi ya Horombo na kambi ya Kibo.

Aliyenipigia simu alijitambulisha akisema mimi hununua vocha za simu kwenye kibanda chake mjini Musoma.

Alinisimulia kuwa alikuwa anabishana na wenzake, baadhi yao wakisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, wengine wakipinga na kusema siyo kweli. Akaniomba mimi nimalize ubishi wao.

Kwanza, ingawa nilikuwa kwenye njia ya Marangu kuelekea kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, njia ambayo inasemekana kuwa ni moja ya njia rahisi za kufika kileleni, ukweaji Mlima Kilimanjaro wakati wote unampa mtu changamoto za kila aina.

Mawasiliano ya simu za kiganja huwa ni ya kubahatisha kutegemea na sehemu ulipo na kutegemea na hali ya hewa. Mlimani kwenyewe pumzi inavutika kwa kutumia nguvu na jitihada ya ziada. Aidha, kwa sababu ya baridi chaji ya betri ya simu haikai kwa muda mrefu.

Kwa sababu hizo, unapopigiwa simu, unategemea itahusiana na suala la dharura au linalohusiana na kazi au suala lingine la aina hiyo.

Lakini nilielewa kuwa, kwa aliyenipigia simu, kufahamu kama Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga au la ilikuwa muhimu kwake kwa wakati ule.

Nilimwambia kuwa hata mimi husikia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, na wakati fulani wazee wa Yanga walitembelea Butiama nikawauliza swali hilo lakini kwa wakati ule aliponiuliza sikukumbuka walinijibu nini.

Ninachokumbuka ni kusikia mtu akisema kuwa kadi namba 1 ya Dar es Salaam Young Africans huwa haijulikani kapewa nani, na ndiyo hiyo watu wanasema ilikuwa kadi ya Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere mwenyewe aliposimulia kuhusu kuhudhuria mechi za soka alisema ilikuwa muhimu kuwa asikae mtu mbele yake, kwa sababu kila wakati mchezaji alipokaribia kufunga goli naye alikuwa akirusha mguu mbele kupiga mpira hewa.

Bofya kwenye picha hapo chini kusoma taarifa juu ya mechi chache za mpira ambazo Mwalimu Nyerere alihudhuria:
Mwaka 1972, Rais Jaffar El Nimeiry wa Sudan akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye mechi ya soka dhidi ya timu ya taifa ya Sudan.
Taarifa nyingine kama hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/07/simba-sports-club-wakaribishwa-butiama.html