Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, November 1, 2013

Mtwara sawa lakini Loliondo hapana?

Nimekuwa na msimamo unaofanana kidogo na sera ya serikali juu ya rasilimali za Tanzania; kwamba ni mali ya Watanzania wote, na siyo ya wale walio karibu na hiyo rasilimali. Sikubaliani na hoja kuwa wale wananchi walio karibu na rasilimali ndiyo wapewe upendeleo zaidi juu ya kufaidika na rasilimali hiyo.

Sababu yangu ya msingi ni kuwa kufanya upendeleo wa aina hiyo kutajenga ubaguzi dhidi ya Watanzania wengine. Watanzania wengine wataonekana kuwa "wanaingilia" rasilimali inayopaswa kutumika na wale wazawa wa eneo husika tu. Na ndiyo maana napata shida kuunga mkono hoja ya baadhi ya Watanzania, kama wale wananchi wa Mtwara, wanaodai rasilimali ya gesi ni yao kwanza.

Lakini hatuwezi kusema hatuelewi kwanini kuna madai kama yao. Unaweza kujenga hoja nzuri kuzungumzia kwanini wananchi wa Mtwara wanaamua kuwa gesi ya Mtwara ni yao. Ni ubovu wa sera za muda mrefu za serikali zilizopuuza umuhimu wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanafaidika na rasilimali yao. Haya ni matokeo ya muendelezo ule wa sera zinaotoa vipengele vya upendeleo kwa wawekezaji na ulipaji wa mrahaba pekee. Mwekezaji aliweza kumiliki asilimia 100 ya mradi wa rasilimali muhimu na kuilipa serikali au kodi kidogo au kusamehewa kabisa na kiwango cha mrahaba ambacho, kimsingi, kilikuwa kidogo sana.

Wananchi waliofundishwa miaka nenda rudi kuwa yatosha kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji na malipo ya mrahaba wa chini ya asilimia tano hawakuelewa hilo somo na hawataweza kulielewa hata kwa karne nzima. Matokeo yake ni kupoteza imani kabisa kwa serikali na maamuzi yoyote inayoyafanya kwenye eneo la uwekezaji. Tunachoshuhudia sasa ni wananchi "kuchukua chao mapema"; kwamba rasilimali ambazo ziko jirani nao ni lazima ziwape faida wao. Watanzania wengine wahangaike na mali zilizopo maeneo yao. 

Huu ni mwanzao wa kuparaganyika kwa nchi. Wale wasio na rasilimali watakula wapi? Watapata ajira wapi? CHADEMA wamejaribu kuelezea namna utaratibu wa kila mtu na chake (majimbo) na kidogo kilichopo kipelekwe kwenye serikali kuu lakini kwangu mimi sera hii ina walakini kuwa itaanza kupandikiza hisia kuwa Mlima Kilimanjaro una wenyewe. Hali kadhalika Serengeti, Selous, na mbuga nyingine ambazo zinaliingizia Taifa mabilioni ya shilingi kila mwaka. Vivyo hivyo kwa gesi na mafuta yanayosubiriwa kwa hamu.

Badala ya kuitaka serikali iwajibike zaidi katika kuwanufaisha wananchi wake, tunaanza kugawana kile kidogo kilicho jirani yetu. Ni sawasawa na wenyeji kugombania makombo baada ya chakula kutengewa wageni.

Kutegemea kuwa jambo litatokea (ubaguzi wa watu kutokana na maeneo yao ya asili) hakuthibitishi kuwa jambo hilo kweli litatokea. Lakini binadamu wote tunaishi kwa kufanya maamuzi kuhusu yaliyokwisha tokea zamani, ya sasa, na matarajio yetu ya yale yanayoweza kutokea. Ndiyo msingi wa mipango yote thabiti, kwa hiyo siyo rahisi kujenga hoja kupuuza hoja za aina hii.

Sasa basi tugeukie Loliondo. Wakati siungi mkono madai ya wananchi wa Mtwara naunga mkono madai ya wale wa Loliondo ambao wanapinga kusudio la serikali la kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa wawekezaji kwa shughuli za utalii, pamoja na serikali kutaka watu hao wahame kupisha shughuli za uwekezaji. Wamasai wapatao 30,000 na ng'ombe zao wahamishwe ili kupisha shughuli za utalii.

Bado nina msimamo kuwa Tanzania ni ya wote lakini kwa wakazi wa tarafa ya Loliondo, ambao wengi wao ni wafugaji na wanaoishi maisha yanayotegemea sana ardhi wanayokalia kwa ustawi wao na wa mifugo yao, kugawa hayo maeneo kwa matumizi ya wawekezaji ni kuwanyima Watanzania hawa chanzo cha msingi kinachobeba mfumo wao wa maisha.

Hii ni sawa na kuhatarisha uhai wao. Hasara atayopata mkazi wa Loliondo atakayehamishwa haiwezi kamwe kufidiwa na kiasi chcochote cha pesa, hata kama pesa hizo zisingieishia serikalini na zikagawiwa kwa wakazi hao.

Mkazi wa Mtwara ana haki kuhoji serikali ionyeshe faida kwake (na kwa Watanzania wengine) ya sera ya muda mrefu ya uwekezaji, lakini hata kama madai ya kuweka Mtwara viwanda muhimu vya sekta ya gesi haitatimizwa, maisha ya mwana-Mtwara hayatabadilika kwa kiasi kikubwa kulinganishwa na athari na matatizo makubwa ambayo atayapata mkazi wa Loliondo ambaye maisha yake yataathrikia kutokana na kuhamishwa kwenye ardhi ambayo anaitegemea kila siku kwa maisha yake na kwa mifugo yake.

Katika mazingira haya, madai ya wananchi hawa wa Loliondo ni sahihi kabisa, kwa maoni yangu. Ya Mtwara bado yanahitaji kujengewa hoja zaidi.

Taarifa nyingine zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/09/john-mnyika-wa-chadema-anajibu-hoja.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/amani-millanga-bado-anahoji-sera-ya.html

Sunday, October 27, 2013

Wageni toka Kagera wamtembelea Mama Maria Nyerere

Viongozi wa kikundi cha wajane na yatima kutoka mkoa wa Kagera walimtembelea Mama Maria Nyerere, kijijini Butiama hivi karibuni.
Grace Mahambuka, mwenyekiti wa kikundi cha Wajane na Yatima Kagera akitoa zawadi ya "akamwani" (kahawa ya kutafuna) kwa Mama Maria Nyerere (kushoto) Mwitongo, Butiama.
Msafara uliongozwa na mwenyekiti wao, Mama Grace Mahambuka, ambaye aliongozana na Mama Agnes Paulo Mukuta ambaye ni mdau wa maendeleo anayeunga mkono kikundi hicho. Mwingine katika msafara huo alikuwa Sittiwarth Mugasha ambaye ni yatima na msanii muimbaji wa kikundi cha Umoja wa Wanawake Wajane na Yatima Band.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/kumbukumbu-ya-siku-ya-kufariki-mwalimu.html

Saturday, October 26, 2013

Madaraka Nyerere: Niliwahi kumsaidia baba pesa

Madaraka Nyerere: Niliwahi kumsaidia baba pesa

Mahojiano haya nilifanya na Stella Nyemenohi wa gazeti la Habari Leo. Yamechapishwa tena hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya miaka 14 tangu kufariki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Bofya hapo juu kusoma mahojiano yote.

Friday, October 25, 2013

Msiofahamu vyema Kiingereza zungumzeni na andikeni kwa Kiswahili, mtafanya makosa machache zaidi

Hili nimeshalisema sana lakini naona kuna umuhimu kulirudia: tofauti na Watanzania wengi tunavyoamini, kufahamu vyema lugha ya Kiingereza siyo ishara kuwa anayeifahamu vyema lugha hiyo ni mtu aliyesoma kwa kiwango cha juu. Inasemekana kuwa John Major, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, alikuwa na elimu ndogo sana lakini hatuna shaka kuwa alifahamu Kiingereza vizuri sana.

Tunang’ang'ania lugha ya Kiingereza tunapoongea au kuandika kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo tutaonekana ni wasomi sana. Kiingereza ni lugha kama lugha nyingine: Kichina, Kijapani, Kifaransa, na hata Kizanaki.
Ni kweli mtu anapoongea au kuandika lugha vyema inaashiria kuwa yeye ni msomi kwa maana ya kwamba yawezekana amekaa kwenye mfumo wa elimu kwa miaka mingi na bila shaka amejifunza misingi ya hiyo lugha anayoongea. Lakini ukweli unabaki kuwa hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja kati ya kuongea na kuandika lugha yoyote kwa ufahasaha na kiwango cha elimu cha mhusika.

Naona mara kadhaa mwenye mitandao ya jamii watu wakijaribu kujipambanua kuwa waandikaji wazuri wa lugha ya Kiingereza lakini kinachojitokeza ni kuwa hawana uwezo huo.

Unaweza kujiuliza: kwanini baadhi ya hawa wanaoamini kuwa kufahamu vyema matumizi ya lugha ya Kiingereza ni ishara ya usomi wasitumie lugha yao mama, Kiswahili, kwa sababu wengi wanaowaandikia wanafahamu lugha hiyo? Kama jamii nzima inaamini kuwa kufahamu Kiingereza ndiyo hali ya kujivunia basi ni vigumu kuona mabadiliko.

Jambo la msingi ingekuwa kwa wale wasiofahamu lugha vyema – siyo Kiingereza tu – wajifunze hizo lugha vyema ili pale wanapoongea au kuandika basi wafanye hivyo kwa ufasaha na kuweza kuwa walimu wa wengine. Ukweli ni kuwa kama hufahamu lugha ya Kiswahili vyema ni vigumu kujifunza lugha nyingine kwa ufasaha.

Lakini kuna suala moja la msingi linajitokeza: iwapo hufahamu kuwa hufahamu basi tatizo ni kubwa zaidi. Kuna mwanahabari mmoja mwandamizi aliwahi kuandika makala akisema kuwa ili mtu apate uwezo wa kufahamu kuwa hafahamu anahitaji kiwango fulani cha elimu. Kwa maana nyingine, inahitaji kuwa msomi kidogo kubaini kuwa huna uwezo na jambo fulani.

Inawezekana kuwa mfumo wetu wa elimu umekuwa duni kwa muda mrefu sana kiasi ambapo limejengeka tabaka kubwa la Watanzania ambao wako kwenye kundi hilo la kuwa watu wasiofahamu kuwa hawafahamu na basi hujikuta wakiandika na kusema vitu ambavyo siyo sahihi kwa Kiingereza wala Kiswahili.

Jambo lingine ambalo linatuangamiza kabisa ni kuwa Watanzania ni wagumu sana kusahihisha wenzao pale wanapokosea kwenye matamshi na maandishi. Mkosoaji anaonekana siyo mstaarabu au huonekana anataka kujipambanua kuwa yeye anafahamu zaidi ya wenzake. Matokeo yake ni kuwa matumizi yasiyo sahihi ya lugha yanaendelea kushamiri kwenye jamii.

Nimesikiliza mara nyingi tangazo linalosikika hivi karibuni kwenye vyombo vya habari ambapo binti anatamka namba za simu na anataja “zilo zilo” akimaanisha “ziro ziro” au “sifuri sifuri.” Hilo tangazo limepitiwa na wahusika na hawakuona kasoro yake. Matokeo yake mamilioni ya watoto wanalisikiliza na kuamini kuwa kutamka “zilo” ni sahihi. Najiuliza: hawa wahusika ndiyo wale wale waliopoteza uwezo wa kutofahamu kuwa hawafahamu, au ndiyo ule ustaarabu wetu wa kutosahihisha makosa?


Maoni yangu ni kuwa tujifunze Kiswahili vyema kwanza kabla ya kujaribu kujifunza lugha nyingine. Ni kazi ndogo zaidi kumfundisha Kiswahili mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama kuliko kumfundisha Kiingereza (au lugha nyingine) mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama. Na hili ni kweli hata kwa yule ambaye Kiswahili ni lugha yake mama na anayetamka “zilo zilo.”

Taarifa zinazofanana na hii:

Monday, October 7, 2013

Msafara mwingine wa Mlima Kilimanjaro wamalizika, safari hii kuchangia pesa kwa shule ya Kichalikani

Ndiyo kwanza nimemaliza kukwea Mlima Kilimanjaro katika mwaka wa 6 wa The Mwalimu Nyerere/Mt. Kilimanjaro Charity Climb kuchangisha pesa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule iliyopo kwenye kijiji cha Kichalikani, wilayani Mkinga, mkoa wa Tanga.

Pamoja nami katika msafara wa Mlima Kilimanjaro alikuwa E. Gassana. Tulifika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro asubuhi ya tarehe 5 Oktoba, saa 2:30 asubuhi.
Kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, mita 5,895 juu ya usawa wa bahari na sehemu iliyo juu kuliko zote katika bara la Afrika, kutoka kushoto: Pius Yahoo, muongozaji wetu; E. Gassana; mwandishi wa blogu hii; na Musa Juma, muongozaji msaidizi.
Wakazi wa kijiji cha Kichalikani walianza ujenzi wa shule mwaka 2009 kwa kutumia sehemu ya ushuru uliokusanywa kwenye soko la samaki. Baada ya kuona jitihada hizi, Saidi Masimango, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia na Habari ya Shirika la Hifadhi ya Jamii alichangia shilingi milioni moja. Masimango alifariki mwezi Julai 2013.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, naye alichanga mabati 33, wakati Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alitoa mabati 100.

Kiasi cha shilingi milioni 7 zinahitajika kumalizia kazi za ujenzi ambazo hazijakamilika pamoja na kununua madawati.
Tafadhali changa kwa njia zifuatazo:

Jina la Akaunti: Kijiji cha Kichalikani
Benki: National Microfinance Bank
Namba ya Akaunti: 4193300163
Tawi: Mkwakwani, Tanga.

Wanaochangia wanaombwa kutuma majina kamili na viwango vilivyotolewa (kwa madhumuni ya kuchapisha orodha kamili kwenye gazeti la Jamhuri) kwa:


Hata wasiopenda majina yao yachapishwe nao wanaombwa kuwasilisha hizo taarifa kwa njia hiyo ya barua pepe (majina hayatachapishwa).

Kuchangia kwa njia ya simu tumia namba ifuatayo (pesa zitakusanywa na kuwekwa kwenye akaunti ya benki iliyotajwa juu):
+255 755 570 795