Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, October 31, 2010

Amani Millanga bado anahoji Sera ya Majimbo ya CHADEMA (sehemu ya kwanza)

Katika taarifa ya Septemba 5 nilitoa maelezo ya Amani Millanga akifafanua hoja zake kupinga Sera ya Majimbo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Nilifanikiwa kupata maelezo katika mfumo wa makala zilizoandikwa na John Mnyika, Kaimu Katibu Mkuu wa CHAEMA na mgombea ubunge wa chama hicho kwa jimbo la Ubungo, akiweka msimamo wa CHADEMA kuhusu sera hiyo ya majimbo.


Baada ya kusoma maelezo ya CHADEMA, Amani Millanga anaendelea kufafanua hoja zake dhidi ya Sera ya Majimbo ya CHADEMA.


Pamoja na kwamba sikufanikiwa kutoa taarifa hizi kabla ya uchaguzi, bado nafikiri kuna umuhimu wa wasomaji kusikia hoja za Amani Millanga.

Sera za Majimbo: Utaifa na Hatima ya Amani Yetu
Na Amani Millanga
Amani Millanga (kulia), akiongea na Afisa Kilimo wa Kijiji cha Butiama, David Sanagara.
Kote duniani tumeshuhudia vita na mauwaji ya kikatili yanavyoendelea kizitafuna nchi changa zenye serikali za majimbo na hata zile zisizokuwa na majimbo. Zipo sababu nyingi za ndani na nje za hali ilivyo katika nchi hizi kukosa amani na umoja lakini miongoni mwa sababu kubwa kabisa ni ukabila na udini ambao unachochewa na umkoa na umajimbo. Mtanzania yoyote mwenye kuchukua kila tahadahari ya kuilinda amani yetu hawezi kukubaliana na sera ya majimbo. Hili si suala la "watu kuwa na hofu, na woga au kubisha," bali ni suala la hatima ya utaifa na umoja wetu. Wahenga wetu walisema, mwenzio akinyolewa wewe tia maji. Kwa nini tujitege bomu ili hali tunajua kuwa likilipuka litatumaliza.


Kuiga, Historia na Maslahi ya Taifa
Yapo mambo mengi ya kujifunza kutoka sehemu mbalimbali duniani lakini si yote yanayotufaa. Miongoni mwa yasiyotufaa ni hili la serikali za majimbo. Sababu za kutokutufaa ziko wazi kabisa: ni kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na hatimaye amani yetu. Umoja, amani na utaifa ndiyo maslahi yetu ya kwanza kabla ya jambo lolote.


Sera yoyote inayolenga kuyaua mambo haya haitufai. Kupoteza amani na umoja ni jambo la siku moja tu. Lakini kuirejesha amani na umoja katika nchi yoyote ni gharama kubwa ni inachukua muda mrefu sana. Mifano iko wazi. Marekani kwa mfano ilikuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 1860 ambapo majimbo ya kaskazini yalizuia majimbo ya kusini mwa nchi hiyo yasijitenge. Athari za vita hiyo ilikuwa ni kubwa mno. Nigeria hali kadhalika ukianzia na Biafra, majimbo ya kasakzini na delta ya mto Niger. Je tuna uhakika gani kwamba Tanzania haiwezi kuingia katika mgogoro wa baadhi ya majimbo kutaka kujitenga? Mmejiandaa vipi kuidhibiti hali hii kwa Tanzania? Je mnataka tuwe kama Nigeria? Hakuna umoja wala amani pale. Tukumbuke kuwa kuwepo kwa serikali za majimbo huko Marekani ya kaskazini, baadhi ya nchi za Ulaya, Afrika Kusini na Australia si kigezo cha sisi Tanzania kuwa na serikali za majimbo kwani wao wana historia yao inayowapa mwanya wa kuwa na majimbo. Tanzania ina historia yake. Historia yetu haituruhusu kuwa na majimbo kwani yataua utaifa wetu. Yataua nchi yetu.


Majimbo ni Ufa
Katika kitabu cha Nyufa, Mwalimu Nyerere anatukumbusha Tanzania bado ni taifa changa sana na kwamba kuna mambo ambayo tunapaswa kuendelea kuyasimamia na kuyalinda kama mboni za macho yetu. Mwalimu anatahadharisha kwa kusema: "Lakini mambo haya ya msingi yanataka yasimamiwe katika nchi changa. Lazima yasimamiwe.


Ukiacha, watu wanarudi kule kule kwenye mawazo ya kijinga jinga. Ukabila, kama ukabila, sisi bado wakabila sana. Kwa hiyo la ukabila lazima liendelee kupigwa vita mpaka life. Halijafa. Ukiwaminya hawa kidogo utakuta ukabila uko pale pale tu!" Mwalimu anaongeza kuwa: "Ukabila bado upo. Kwa hiyo, ukabila lazima uendelee kupigwa vita. Hapana kukaa na kusema 'Tanzania hatuna ukabila'. Hapana. Watu hatujawa Watanzania bado. Kwa hiyo lazima tuendelee kuupiga vita. Na watu wana udini udini" (uk 28).


Serikali za majimbo ni hatari kwani zitatugawa Watanzania kimakabila na hata kidini. Na kwa mgawanyo huu hauwezi kuleta maendeleo ya kweli kwa Tanzania yote kwa pamoja. Kutakuwa na upendeleo fulani kwa majimbo fulani kutoka serikali ya shirikisho na kutakuwa na upendeleo kutoka serikali ya jimbo kwenda wilayani kutegemea ni kabila gani au ni nani kashika uongozi wa taifa au jimbo. Haya mambo yapo hasa kwa nchi changa, tusijifanye hatuyajui.


Hivyo utaifa wetu unapaswa kulindwa kwa kuepuka kila sera au jambo lolote linaloweza kuuweka hatarini. Ukweli ni kwamba umoja na utaifa wetu utayumba iwapo tutakuwa na serikali za majimbo. Huo ni mwanzo wa kuparaganyika kwa Tanzania na hizo ajenda nyingine mlizonazo hazitafanya kazi yoyote kwani taifa halitakuwepo tena. Sera yenu hii itaweka ufa mkubwa na kubomoa taifa letu. Tutakuwa na serikali yenye nchi isiyokuwa na taifa. Nigeria iko hivyo, isomeni historia yake jinsi ambavyo majimbo yamongeza mgawanyiko.


Muungano Kuvunjika
Suala la majimbo ni hatari kwa Muungano wetu. Mnataka kuifanya Zanzibar iwe jimbo? Na kama Zanzibar wakikataa serikali za majimbo, jambo ambalo ni wazi kwamba watakataa kuwa jimbo, je mnatuhakikishia vipi kuwa mtaulinda Muungano wetu?


Sera ya majimbo ni silaha ya kuuvunja Muungano. Na mara tu Tanzania ikigawika huwezi kuondoa umaskini, ujinga na maradhi. Huwezi kuleta maisha bora bali utaleta ubaguzi na hatimaye machafuko na kumwaga damu.


Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si Ufederali au shirikisho. Ndio maana tunayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si Jamhuri ya Shirikisho la Tanzania. Pia Muungano wetu si tenge na mafanikio yake ni makubwa. Hatupaswi kuubeza na kuuita "Tenge". Ndiyo, zipo kero lakini kero hizo hazimaanishi kuwa Muungano ni 'tenge'. Kama ungekuwa tenge kwa maana halisi ya neno tenge basi ungeishavunjika. Leo hii Watanzania tunatembea kifua mbele kwa kujivunia Muungano wetu ambao una faida nyingi kwetu (hii ni mada nyingine).


Serikali za Mitaa
Haya mambo mnayoyataja kuwa yatafanywa na serikali za majimbo tayari yanafanywa na serikali za mitaa nchini. Falsafa ya nguvu ya umma ndiyo msingi mkubwa wa serikali za mitaa. Hoja iwe ni kuziboresha zaidi serikali za mitaa kwa kuzipa mamlaka zaidi ya sasa na si kuziondoa na kuleta serikali za majimbo.


Tuangalie zimeshindwa wapi, kwa nini na nini kifanyike ili ziwahudumie wananchi kwa ufanisi zaidi. Kimsingi kupitia serikali za mitaa ni rahisi zaidi kutoa maamuzi na kusimamia shughuli za maendeleo kuliko katika jimbo litakalokuwa ni kubwa mno na utajikuta unakwama. Mfano katika jimbo la kanda ya ziwa Kagera, Mara na Mwanza kuna watu wenye mahitaji mbali bali. Kwa mfumo wa jimbo si rahisi kuwafikia watu hawa na kutatua matatizo yao. Lakini kwa serikali za mitaa katika kila wilaya ni rahisi zaidi kwani utakuwa unaiongelea Muleba tu na si jimbo zima.


Kimantiki unaliona suala hili kwa uawzi kabisa. Kwanini mambo ya Muleba yaamuliwe katika bunge la jimbo litakalo kuwa pale Mwanza, kwa mfano, badala ya kuamuliwa na baraza la madiwani wa Muleba wanaoijua uzuri Muleba na mahitaji yake? Kwanini niifuate huduma Mwanza badala ya Muleba? Hapa mbona utakuwa unaturudisha kwenye urasimu ule ule ambao serikali ya CCM inauondoa kwa kuzipa serikali za mitaa mamlaka zaidi? Kama hoja ni kuvifuta vyeo vya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na katibu tarafa hili ni suala ambalo linaweza kujadiliwa kwa kuangalia faida na hasara zake kwetu. Lakini uwepo wa viongozi hawa usitumiwe kama hoja ya kutaka serikali za majimbo kwani hakuna uhusiano sisisi wa kimantiki kati ya wakuu hawa na kuwa na serikali za majimbo.


Mzigo Mkubwa
Serikali za majimbo zina utitiri wa viongozi zaidi ya mfumo tulionao sasa. Na huu ndio ukweli. Gharama za kuziendesha serikali za majimbo na shirikisho zitaongeza mzigo mkubwa zaidi kwa wananchi badala ya kuupunguza. Utakuwa na bunge katika kila jimbo na bunge la shirikisho, gavana wa jimbo na mawaziri wake na makatibu wa wizara au idara, wakurugenzi n.k. Msululu ni mrefu mno hadi kuja kufika kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya. Hiyo yote ni pesa ya umma inatafunwa. Hivi kwa nini tupoteze mabilioni yote hayo katika kaunzisha majimbo na kuudurusu upya utendaji wake ili kuuboresha zaidi? Kwanini tuwatwishe wananchi mzigo mkubwa zaidi?


Ikulu Lazima Iongoze Taifa-Nchi
Suala la Ikulu au serikali kuu kuingilia serikali za mitaa lina mapana yake katika kilijadili. Inategemea wanaingilia katika lipi na sheria inasemaje. Hapo ndipo tunapaswa kuziangalia kanuni, taratibu na sheria zetu za mitaa. Kama zina mapungufu tuyaondoe ili seikali za mitaa ziwe huru zaidi. Lakini ni ukweli usio na kificho kuwa Ikulu na serikali kuu ni lazima ziwe na mamlaka ya kiutawala na kiutendaji kwa serikali za mitaa. Kinyume chake Tanzania itakuwa haina serikali kwa maana halisi ya 'serikali ya taifa-nchi' na hivyo basi hakuna sababu ya kuwa na Ikulu. Taifa-nchi ni pamoja na serikali za mitaa.


Sasa tujiulize: Ikulu ni ya nini ikiwa haiwezi kuingilia na kusimamia uendeshaji wa taifa na nchi?


Katika mfumo wetu wa sasa, kwa mfano, kila halmashauri ina vyanzo vyake vya mapato na bajeti. Ni kweli kwamba serikali za mitaa zinapokea pesa kutoka serikali kuu lakini si pesa zote zinazoendesha halmashauri zinatoka Dar es Salaam. Huu ni uwongo na uzushi. Juu ya hayo si kweli kwamba kila jambo katika kila halmashauri linaongozwa na maelekezo ya Ikulu ya Dar es Salaam. Hivi Ikulu inaamua hata ushuru au kodi ya halmashauri itozwe vipi na mapato yatumikeje? Hii ni nguvu ya kuupotosha umma!


(sehemu ya mwisho ya makala ya Amani Millanga itatolewa kesho.

No comments: