Hili nimeshalisema sana lakini naona kuna umuhimu kulirudia: tofauti na Watanzania wengi tunavyoamini, kufahamu vyema lugha ya Kiingereza
siyo ishara kuwa anayeifahamu vyema lugha hiyo ni mtu aliyesoma kwa kiwango cha
juu. Inasemekana kuwa John Major, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, alikuwa na
elimu ndogo sana lakini hatuna shaka kuwa alifahamu Kiingereza vizuri sana.
Tunang’ang'ania lugha ya Kiingereza tunapoongea au kuandika
kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo tutaonekana ni wasomi sana. Kiingereza ni
lugha kama lugha nyingine: Kichina, Kijapani, Kifaransa, na hata Kizanaki.
Ni kweli mtu anapoongea au kuandika lugha vyema inaashiria
kuwa yeye ni msomi kwa maana ya kwamba yawezekana amekaa kwenye mfumo wa elimu kwa miaka
mingi na bila shaka amejifunza misingi ya hiyo lugha anayoongea. Lakini ukweli
unabaki kuwa hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja kati ya kuongea na
kuandika lugha yoyote kwa ufahasaha na kiwango cha elimu cha mhusika.
Naona mara kadhaa mwenye mitandao ya jamii watu wakijaribu
kujipambanua kuwa waandikaji wazuri wa lugha ya Kiingereza lakini kinachojitokeza
ni kuwa hawana uwezo huo.
Unaweza kujiuliza: kwanini baadhi ya hawa wanaoamini kuwa
kufahamu vyema matumizi ya lugha ya Kiingereza ni ishara ya usomi wasitumie
lugha yao mama, Kiswahili, kwa sababu wengi wanaowaandikia wanafahamu lugha
hiyo? Kama jamii nzima inaamini kuwa kufahamu Kiingereza ndiyo hali ya kujivunia basi ni
vigumu kuona mabadiliko.
Jambo la msingi ingekuwa kwa wale wasiofahamu lugha vyema – siyo Kiingereza tu – wajifunze hizo lugha vyema ili pale wanapoongea au
kuandika basi wafanye hivyo kwa ufasaha na kuweza kuwa walimu wa wengine.
Ukweli ni kuwa kama hufahamu lugha ya Kiswahili vyema ni vigumu kujifunza lugha
nyingine kwa ufasaha.
Lakini kuna suala moja la msingi linajitokeza: iwapo
hufahamu kuwa hufahamu basi tatizo ni kubwa zaidi. Kuna mwanahabari mmoja
mwandamizi aliwahi kuandika makala akisema kuwa ili mtu apate uwezo wa
kufahamu kuwa hafahamu anahitaji kiwango fulani cha elimu. Kwa maana nyingine, inahitaji kuwa msomi kidogo kubaini kuwa huna uwezo na jambo fulani.
Inawezekana kuwa mfumo wetu wa elimu umekuwa duni kwa muda
mrefu sana kiasi ambapo limejengeka tabaka kubwa la Watanzania ambao wako
kwenye kundi hilo la kuwa watu wasiofahamu kuwa hawafahamu na basi hujikuta
wakiandika na kusema vitu ambavyo siyo sahihi kwa Kiingereza wala Kiswahili.
Jambo lingine ambalo linatuangamiza kabisa ni kuwa Watanzania
ni wagumu sana kusahihisha wenzao pale wanapokosea kwenye matamshi na maandishi.
Mkosoaji anaonekana siyo mstaarabu au huonekana anataka kujipambanua kuwa yeye anafahamu zaidi
ya wenzake. Matokeo yake ni kuwa matumizi yasiyo sahihi ya lugha yanaendelea
kushamiri kwenye jamii.
Nimesikiliza mara nyingi tangazo linalosikika hivi karibuni
kwenye vyombo vya habari ambapo binti anatamka namba za simu na anataja “zilo
zilo” akimaanisha “ziro ziro” au “sifuri sifuri.” Hilo tangazo limepitiwa na
wahusika na hawakuona kasoro yake. Matokeo yake mamilioni ya watoto wanalisikiliza
na kuamini kuwa kutamka “zilo” ni sahihi. Najiuliza: hawa wahusika ndiyo wale
wale waliopoteza uwezo wa kutofahamu kuwa hawafahamu, au ndiyo ule ustaarabu
wetu wa kutosahihisha makosa?
Maoni yangu ni kuwa tujifunze Kiswahili vyema kwanza kabla ya
kujaribu kujifunza lugha nyingine. Ni kazi ndogo zaidi kumfundisha Kiswahili
mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama kuliko kumfundisha Kiingereza (au lugha
nyingine) mtu ambaye Kiswahili ni lugha yake mama. Na hili ni kweli hata kwa
yule ambaye Kiswahili ni lugha yake mama na anayetamka “zilo zilo.”
Taarifa zinazofanana na hii:
No comments:
Post a Comment