Tuesday, December 19, 2017
Hili sijalielewa hata kidogo
Saturday, November 18, 2017
Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao
Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ni sheria ambayo inaainisha matusi kama mojawapo ya makosa ambayo yanaweza kumtia mtu hatiani kwa yale anayoyaandika au kwa picha anazoweka mtandaoni. Kuna baadhi ya watu, au kwa kutokujua sheria au kwa makusudi, tayari wametiwa hatiani na maandiko ambayo yanaainishwa kuwa makosa kwenye sheria hii.
Na sina shaka kuna wengi wengine watakumbwa na tatizo hilo kwa sababu inaelekea kuna watu wanaamini kuwa akiwa kajibanza pembezoni mwa nchi akarusha matusi kwenye mtandao basi siyo rahisi kupatikana.
Tatizo la kuonana uso kwa uso limenitokea leo baada ya kutembelewa Butiama na Fabian Zegge, "rafiki" wa mtandao ambaye sikutarajia kuonana naye hata siku moja. Alifika Musoma kwenye shughuli zake na akaamua kunitembelea Butiama.
Mara baada ya kusalimiana naye nilimwambia kuwa angekuwa ni mtu ambaye tulirushiana maneno yasiyo na ustaarabu katika mawasiliano yetu kwenye mtandano, leo hii ningeona aibu kujitokeza kusalimiana naye. Ningemwambia amekosea namba ya simu aliponipigia awali kutaka kufahamu iwapo nipo nyumbani.
Kutoka kushoto kwenda kulia: mimi, Fabian Zegge, na mwenyeji wake. |
Pili, na kwa kutambua ukweli huo, nimeone umuhimu kwamba tunapowasiliana na watu mbalimbali kwenye majukwaa kwenye mtandao tunapaswa kuongozwa na ustaarabu kwenye kauli zetu.
Bila kuzingatia hayo tutaumbuliwa na sheria au aibu ya kukutana na tunaowatukana.
Saturday, November 11, 2017
Mimba zisizoisha za Chausiku Suleiman
Nilipoonana naye alikuwa na umri wa miaka 47 na alikuwa na watoto 16 aliyewazaa ndani ya kipindi cha miaka 30. Tatizo lake lilianza alipopata ujauzito wa mtoto wa tano. Majuma matatu baada kujifungua alihisi kuwa alikuwa mjamzito tena. Nilipoonana naye mwaka 2011 alisema kuwa mimba yake wakati huo ilikuwa ina zaidi ya miaka mitatu.
Chausiku Suleiman akiwa na baadhi ya watoto wake, Maji Chai, Arusha. |
Alisema anahisi kuwa madaktari wanaamini kuwa ana imani kuwa na tatizo ambalo halipo.
Saturday, September 2, 2017
Hivi Mwalimu Nyerere alikuwa Yanga au Simba?
Mwaka 2012, nikiwa kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro nikiongozana na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto ya Mwanza, nilipokea simu wakati tukitembea kati ya kambi ya Horombo na kambi ya Kibo.
Aliyenipigia simu alijitambulisha akisema mimi hununua vocha za simu kwenye kibanda chake mjini Musoma.
Alinisimulia kuwa alikuwa anabishana na wenzake, baadhi yao wakisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, wengine wakipinga na kusema siyo kweli. Akaniomba mimi nimalize ubishi wao.
Kwanza, ingawa nilikuwa kwenye njia ya Marangu kuelekea kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, njia ambayo inasemekana kuwa ni moja ya njia rahisi za kufika kileleni, ukweaji Mlima Kilimanjaro wakati wote unampa mtu changamoto za kila aina.
Mawasiliano ya simu za kiganja huwa ni ya kubahatisha kutegemea na sehemu ulipo na kutegemea na hali ya hewa. Mlimani kwenyewe pumzi inavutika kwa kutumia nguvu na jitihada ya ziada. Aidha, kwa sababu ya baridi chaji ya betri ya simu haikai kwa muda mrefu.
Kwa sababu hizo, unapopigiwa simu, unategemea itahusiana na suala la dharura au linalohusiana na kazi au suala lingine la aina hiyo.
Lakini nilielewa kuwa, kwa aliyenipigia simu, kufahamu kama Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga au la ilikuwa muhimu kwake kwa wakati ule.
Nilimwambia kuwa hata mimi husikia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, na wakati fulani wazee wa Yanga walitembelea Butiama nikawauliza swali hilo lakini kwa wakati ule aliponiuliza sikukumbuka walinijibu nini.
Ninachokumbuka ni kusikia mtu akisema kuwa kadi namba 1 ya Dar es Salaam Young Africans huwa haijulikani kapewa nani, na ndiyo hiyo watu wanasema ilikuwa kadi ya Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere mwenyewe aliposimulia kuhusu kuhudhuria mechi za soka alisema ilikuwa muhimu kuwa asikae mtu mbele yake, kwa sababu kila wakati mchezaji alipokaribia kufunga goli naye alikuwa akirusha mguu mbele kupiga mpira hewa.
Bofya kwenye picha hapo chini kusoma taarifa juu ya mechi chache za mpira ambazo Mwalimu Nyerere alihudhuria:
Mwaka 1972, Rais Jaffar El Nimeiry wa Sudan akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye mechi ya soka dhidi ya timu ya taifa ya Sudan. |
http://muhunda.blogspot.com/2013/07/simba-sports-club-wakaribishwa-butiama.html
Friday, August 25, 2017
Umuhimu wa wagombea huru sasa umejidhihirisha
Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2017/07/afrika-tunaibiwa-sana-tena-sana.html
Saturday, August 19, 2017
Simulizi za Samora Machel, rais wa kwanza wa Msumbiji
Katika moja ya hafla zilizoandaliwa na Rais wa Msumbiji wa wakati huo Armando Guebuza, nilipata fursa ya kukaa na mzee mmoja mpiganaji wa zamani wa jeshi la ukombozi la FRELIMO ambaye alishiriki kwenye vita ya ukombozi ya Msumbiji.
Alinisimulia mengi juu ya maisha yao walivyokuwa kwenye kambi za FRELIMO zilizokuwa Tanzania, na baadhi ya matukio katika vita iliyoshiriki.
Alisema kuna wakati Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ilitembelea baadhi ya maeneo yaliyokombolewa ndani ya Msumbiji na kupokelewa na Samora Machel, wakati huo akiwa rais wa FRELIMO aliyeshiriki mwenyewe katika mapambano.
Waliandaa chakula kwa ujumbe ulioyoongozwa na Katibu Mtendaji wa kamati, Hashim Mbita. Lakini walipokuwa tayari kuanza kula tu, hapo hapo ndege za jeshi la Ureno zilianza kushambulia kambi ile na chakula kikaachwa ili kunusuru maisha yao.
Inaelekea jeshi la Ureno lilipata taarifa ya ziara ile.
Mwalimu Nyerere na Samora Machel kwenye moja ya mikutano ya hadhara. |
Niliambiwa kuwa Samora mwenyewe aliongoza mikakati ya kulinda usalama wa ule ujumbe, akiwatanguliza wageni wakikimbia mbele na wakiwa wamezungukwa na ulinzi mkali wa wapiganaji wa FRELIMO. Nikaambiwa Samora mwenyewe alikuwa wa mwisho, nyuma ya kila mtu, akiwa ameshika bastola yake mkononi.
Ni kielelezo cha ushujaa wa baadhi ya viongozi wetu wa zamani. Yule mzee alinitolea simulizi hii huku akicheka kuwa wageni hawakuweza kula siku ile.
Taarifa nyingine ambazo unaweza kupendelea kusoma:
https://muhunda.blogspot.com/2016/12/redio-ya-Mwalimu-Nyerere.html
https://muhunda.blogspot.com/2012/09/wageni-wa-butiama.html
Saturday, August 5, 2017
Baraka Elias, Mtanzania mrefu kuliko Watanzania wote
Friday, July 28, 2017
Afrika tunaibiwa sana, tena sana
Friday, July 21, 2017
Mamlaka ya Mapato Tanzania yawageukia wauza spea
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mamlaka inachunguza bidhaa hizo zilizopo madukani ili kupata uthibitisho wa wenye maduka kuwa wamepata hizo bidhaa kwa njia za halali.
Kwa muda mrefu inaaminika kuwa baadhi ya wenye maduka yanayouza spea za magari wananunua spea hizo kutoka kwa wezi wa magari, au wezi wanaoiba spea kutoka kwenye magari.
Hizi hatua zikiendelea kwa muda mrefu zinaweza kupunguza wizi wa spea za magari, na hata wizi wa magari.
Miaka mingi iliyopita nilipoishi Dar es Salaam niliwahi kuibiwa kioo cha mbele cha gari. Nilipotoa taarifa kituo cha polisi niliambiwa na polisi kuwa wana hakika kuwa kioo changu kitapatikana Gerezani, eneo la Dar es Salaam ambalo huuza bidhaa mbalimbali zilizotumika, nyingi ya hizo zikiwa bidhaa za wizi.
Wezi watapungua |
Cha ajabu ni kuwa wale polisi walinishauri ninunue kioo changu. Bila hivyo walisema sitakipata. Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa kupata mali ya wizi wakati huo.
Bila shaka hizi jitihada mpya za Mamlaka ya Mapato zitapunguza kasi ya wizi, na zitaleta mabadiliko chanya kwa wamiliki wa magari.
Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2016/07/mada-yangu-ya-leo-mwizi-ni-mwizi-tu.html
https://muhunda.blogspot.com/2011/07/maana-sahihi-ya-neno-fisadi.html
Friday, July 14, 2017
Simulizi za Jaffar Idi Amin
Anasema kuna siku alikuwa kwenye matembezi kwenye jiji la Kampala akakuta gari aina ya Volkswagen imeegeshwa na akasimama kwa muda mrefu akiiangalia kwa sababu aliitambua kuwa ilikuwa gari ya zamani ya baba yake.
Akiwa anaiangalia akatokea mtu na kumsalimia na kumuuliza sababu za kukaa muda pale akiangalia ile gari. Mazungumzo yakawa hivi:
"Mbona unaishangaa sana hiyo gari?"
"Ilikuwa gari ya baba yangu."
"Baba yako nani?"
"Idi Amin."
Anasema alivyotamka jina la baba yake yule aliyekuwa anamhoji akashangaa sana na kusema: "Baba yako ndiyo alimuondoa baba yangu nchini!"
Aliyekuwa anaongea naye alikuwa mmoja wa watoto wa Milton Obote, Eddy Engena-Maitum. Serikali ya Rais Obote ilipinduliwa na Idi Amin, wakati huo akiwa kamanda wa jeshi la Uganda, tarehe 25 Januari 1971 wakati Obote akiwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.
Idi Amin alishika madaraka mpaka mwaka 1979 baada ya Rais Nyerere kutangaza vita dhidi ya Uganda kufuatia uvamizi wa eneo la Kagera na majeshi ya Idi Amin. Baada ya kukomboa eneo lililovamiwa vita iliendelea ndani ya ardhi ya Uganda na kuhitimishwa kwa kuangushwa kwa serikali ya Amin.
Jaffar akamwambia Eddy: "Mimi nitakutambulisha kwa mtu ambaye baba yake alimuondoa baba yangu hapa Uganda." Alimaanisha mimi.
Mwalimu Nyerere akiwa na mwenyeji wake, Rais Milton Obote, wakati wa moja ya ziara zake nchini Uganda. Wa pili kutoka kulia ni Idi Amin, na kulia ni Philemon Mgaya, aliyekuwa mpambe wa Rais Nyerere. |
Idi Amin na familia yake walikimbilia nchini Libya, na baadaye kuhamia Saudia Arabia. Milton Obote na familia yake walihamia Tanzania na wakawa majirani zetu Msasani kwa muda mrefu.
Saturday, July 1, 2017
Watoto wa mjini nimewakubali
Nimejifunza siku chache zilizopita kuwa mtoto anayeishi mjini ni tofauti sana na yule anayeishi kijijini. Wa mjini wajanja.
Nilikuwa kwenye mitaa ya Kariakoo hivi karibuni nikaamkiwa na binti mdogo aliyevaa baibui niliyemkadiria kuwa na umri usiozidi miaka saba. Aliniomba msaada wa pesa kwa ajili ya mama mlemavu aliyekuwa kwenye kiti cha walemavu upande wa pili wa barabara.
Nilitoa shilingi 5,000 nikamkabidhi na kumuuliza kama nimsaidie kuvuka barabara ya Livingstone ambayo wakati huo ilikuwa na msululu wa magari. Alinihakikishia atamudu kuvuka mwenyewe. Nikaendelea na kununua miwani kwa machinga na yeye akaondoka.
Dakika 20 baadaye nikamkuta yule mama mlemavu kwenye mtaa wa jirani nikamuuliza kama alipokea zile pesa nilizotoa.
"Pesa gani?"
"Zile elfu tano nilizompa yule binti akuletee?
"Hata sijazipata. Ngoja tumsubiri."
Wakati huo binti alikuwa kwenye duka moja akiendelea kuomba msaada kwa watu mbalimbali.
Binti alivyoniona akatabasamu kwa aibu na kukabidhi zile pesa kwa yule mama, ambaye alinijulisha kuwa ni mjukuu wake.
Nilitafakari kuwa inawezekana wanapozunguka kuomba pesa mjukuu anabaki na pesa nyingi kuliko anazokabidhi kwa bibi yake.
Friday, April 7, 2017
Bila Karume hakuna Tanzania
Nachapisha tena makala iliyochapishwa tarehe 26 Aprili 2016 kwenye safu yangu "Ujumbe toka Muhunda" ndani ya gazeti la Jamhuri. Katika makala hiyo narudia ukweli ambao unasahauliwa, ya kuwa wazo la muungano ni wazo la Sheikh Abedi Amani Karume. Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuuwawa kwake.
Sunday, April 2, 2017
Tumbili wa Mwitongo
Kwa kawaida huogopa binadamu, lakini wanayo hulka ya kuzowea binadamu iwapo hawatishiwi usalama wao. Kwenye video, chini, ni mmoja wa tumbili ambao amepunguza woga kabisa akiniona kiasi cha kuchukua karanga mkononi mwangu.
Wanyama wengine wanaopatikana kwa wingi eneo la Mwitongo ni pimbi,
Tuesday, March 21, 2017
Tanzania ni nchi nzuri sana
Lakini inahitaji fursa ya kutoka sehemu moja na kuzunguka maeneo mbalimbali ya Tanzania ambayo yanavutia kwa mandhari na vivutio mbalimbali vya asili. Ukibaki sehemu moja tu huwezi kufahamu juu ya ukweli huu.
Kama huna hiyo fursa siyo kosa lako, lakini kama unayo fursa na uwezo basi huna budi kuzunguka na kuifahamu vyema nchi yako. Utalii wa ndani unajenga uchumi, na wale ambao tunao uwezo wa kutembelea maeneo ya Tanzania tunapaswa kuchangia kwa kadiri tunavyoweza.
Sunday, March 19, 2017
Unafahamu masuala haya 5 kuhusu Mwitongo?
Mwitongo ni eneo la kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania tarehe 13 Aprili 1922. Aidha, ni eneo alipozikwa tarehe 23 Novemba 1999.
Yafuatayo ni masuala matano ya Mwitongo ambayo pengine huyafahamu.
1. Ajali ya ndege
Mwaka 1978, baada ya majeshi ya Idi Amin Dada kiongozi wa kijeshi wa Uganda kuvamia eneo la mkoa wa Kagera, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianza kampeni ya kuondoa majeshi ya Idi Amin kwenye ardhi ya Tanzania.
Katika harakati za kujiandaa na vita hivyo, kikosi cha anga cha JWTZ kilihamisha baadhi ya ndege zake za kivita kutoka kituo cha Ngerengere na kuzipeleka kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza.
Kwa sababu ya kasi ya hizo ndege, marubani wawili waliorusha hizo ndege walipitiliza Mwanza na kulazimika kuzunguka kuelekea upande wa kaskazini mashariki ili warudi tena kutua Mwanza. Uamuzi huo ukasababisha waruke juu ya anga ya mji wa Musoma.
Askari wa kikosi cha mizinga kilichokuwa kinalinda eneo la Musoma, kwa kukosa taarifa juu ya ndege hizo na kudhania kuwa ni ndege za adui, walizishambulia. Moja ya ndege hizo ilianguka Musoma, na nyingine iliangukia Mwitongo, kwenye msitu wa Muhunda.
Eneo la Mwitongo ilipoanguka ndege ya pili umejengwa mnara wa kumbukumbu.
Mnara wa kumbukumbu ya ajali ya ndege kwenye msitu wa Muhunda. |
Msitu wa Muhunda ni sehemu ya eneo la Mwitongo. Ni msitu ambao, kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, ndiyo makazi ya mzimu wao, Muhunda. Msitu una ukubwa wa ekari 5.
Ni marufuku kukata miti iliyopo ndani ya msitu huo. Inaruhusiwa kukusanya kuni za matawi yaliyoanguka chini tu. Wazee wa kimila hufanya mitambiko ndani ya msitu huo.
Inaaminika kuwa mzimu huo hujibadilisha kuwa mojawapo ya viumbe vifuatavyo: nyani mkubwa, chui, mbuzi mkubwa, au nyoka mkubwa.
3. Mamba Mweusi (Black Mamba)
Mwinuko wa Mwitongo upo ndani ya eneo lililozungukwa na vichaka misitu, na majabali makubwa.
Ni eneo ambalo lina viumbe wadogo wadogo, pamoja na nyoka wa aina mbalimbali. Mojawapo wa nyoka hawa ni mamba mweusi.
Picha ya Mamba Mweusi. Jina lake la kisayansi ni Dendroaspis polylepis. Picha inatumika kwa idhini ya Creative Commons License. Taarifa kamili zipo hapa: http://creativecommons.org/licenses/by-sa/3.0/deed.en |
4. Ziwa Viktoria
Mwitongo ni eneo la mwinuko wa mita 1,405 juu ya usawa wa bahari. Kwa sababu ya mwinuko huo mtu anayesimama Mwitongo anaweza kuona kingo za Ziwa Viktoria zilizopo umbali wa kilomita 40 magharibi mwa Butiama.
Ziwa Viktoria. |
5. Nelson Mandela
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitembelea Mwitongo mwezi Novemba 1999. Alifika Mwitongo kuhani kifo cha Mwalimu Nyerere aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999.
Mzee Mandela aliandaliwa chumba maalum cha kulala wakati wa ziara yake. Kitanda maalum kiliwekwa kwenye chumba hicho. Hata hivyo, ratiba yake haikuruhusu kulala, na akaondoka siku hiyo hiyo kurudi Afrika Kusini. Kitanda kile hakijaondolewa kwenye chumba kile hadi hii leo.