Mzee wa Kizanaki anapokaribia nyumbani kwake baada ya giza kuingia huanza kuimba kwa sauti ya juu wimbo unaojulikana kama kibanziko. Kwa desturi ni wimbo unaoimbwa na mzee ambaye amekunywa pombe kidogo, na madhumuni ya wimbo huu ni kuwafahamisha watu wote watakaomsikia kuwa mzee mwenye nyumba anarudi nyumbani. Mwanaume yoyote ambaye anaweza kuwa nyumbani kwa huyu mzee na ambaye hawezi kutoa maelezo ya kuridhisha kwanini yuko pale atafahamu kuwa ni wakati wa kuondoka haraka. Kila mzee wa Kizanaki ana kibanziko chake.
Mzee wa Kizanaki na heshima zake hawezi kumvizia mkewe kwa madhumuni ya kumfumania. Ni tabia ambayo haikubaliki.
Mzee Ginga Kihanga, mwenye umri wa miaka 93 alinisimulia kuwa wazee hupendelea kuwatisha waviziaji badala ya kujiingiza kwenye makabiliano ambayo yanaweza kusababisha majeraha makubwa au hata kifo.
Hata hivyo haina maana kuwa zama zile watu hawakufumaniwa. Enzi za ukoloni wale walioshikwa kwenye fumanizi walidhalilishwa hadharani kwa kuvuliwa nguo, kuchapwa bakora, na kutozwa faini ya ng'ombe wawili. Tofauti ilikuwa mtemi anapokuwa ndiyo mlalamikaji; yeye aliruhusiwa kupanga faini aliyoona inastahili.
Kibanziko kina madhumuni mengine ya ziada. Mzee Ginga alisema, kwa kawaida, tendo lile haramu lilifanyika kwenye vichaka, mbali na nyumba ya wenye ndoa. Ilikuwa ni fedheha kubwa kwa mwanaume Mzanaki anapofumania nyumbani kwake. Kwa hiyo, kwa namna nyingine, uimbaji wa kibanziko ilikuwa ni njia ya kuzuwia hiyo aibu na kumsababisha huyo 'mwizi' aondoke na kuepusha aibu ndani ya jamii.
Yawezekana kuwa desturi hii ya kuwapa upenyo hawa 'wezi' inatokana na tamaduni ile ya kupanga ndoa. Mzee huyo huyo ambaye jana aliimba kibanziko alipokaribia nyumbani kwake yawezekana alikuwa amepitia kwenye kilabu cha pombe na kufanya makubaliano na mzee mwenzake kuwaoza watoto wao.
Aliporudi nyumbani alimwambia mwanae wa kiume kuwa umewadia wakati wa kufunga ndoa na kuwa ameshamtafutia mchumba anayefaa ambaye anatoka kwenye familia ya wachapakazi hodari ambao hawana historia ya magonjwa ya kurithi, na kuwa siyo wachawi.
Lakini kabla ya kupangiwa hizi ndoa na wazee yawezekana kuwa hao wanandoa watarajiwa walikuwa tayari wana mahusiano na watu tofauti. Na yawezekana kwa kutambua uwezekano huo kuwa mtu anapolazimishwa ndoa ambayo hakuitaka anaweza akawa na mahusiano mengine ya pembeni, basi jamii ya Kizanaki ikaja na kibanziko kama njia ya kuruhusu yale ambayo yalifungwa na ndoa za kupangawa na wazee.
Kuna msemo wa Kizanaki unaoashiria kukubali hali hii unaosema, wiguru na wiyasi, ukimaanisha kuna yule wa juu na yule wa chini; kuna mume, na kuna mviziaji - kune mume (au mke), na kuna kitungo.
Kwa kawaida kitungo ndiyo alikuwa mchumba ambaye angeolewa iwapo kijana angeruhusiwa kuchagua, lakini hakuweza kumuoa huyo kwa sababu ya ndoa ya kupangwa na baba mzazi. Na kwa sababu ndoa aliyopanga mzazi haikuwa na majadiliano kilichotokea ni kuwaunganisha watu wawili ambao walikuwa hawana upendo baina yao.
Matokeo yake ni kuwa walikuwa na mahusiano kama maadui badala ya wanandoa. Mwanaume alimuamrisha mwanamke ndani ya nyumba na mwanamke, kwa hulka, alikuwa mkaidi. Ahueni ilitafutwa kwa kitungo.
Na lugha ya kitungo ilikuwa tamu, ya kubembeleza. Walitumia majina ya wapendanao kama 'Nyababiri', Nyabasasaba' au 'Nyabanane' majina yenye kumaanisha 'wa pili', 'wa saba', 'wa nane' na majina ambayo siyo rahisi kutumika baina ya wanandoa.

Kama ilivyo kwa mila na desturi nyingi, kibanziko nacho kinapotea na nyakati. Leo hii vijana wanarudi majumbani mwao bila taarifa. Yawezekana pia kuwa hawana uwezo wa kuimba kama wazee wa Kizanaki.
No comments:
Post a Comment