Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, December 24, 2015

Watu kama sisi

Mwaka jana nilishirikishwa kama mmoja wa waliohojiwa kwenye filamu juu ya albino na adha wanazopata kwenye jamii. Inaelimisha vyema.

Isambaze pia kwa wengine.

Tuesday, December 1, 2015

Kufanikisha falsafa ya Sasa Kazi tu! ni kazi kweli kweli!

Tunajifunza mengi kwa kusikiliza. Leo nimemsikiliza mama wa kijijini Butiama akilalamika kwangu tena kuhusu binti yake kuondoka nyumbani na kuhamia kwa mtu aliyezaa naye.

Tatizo ni kuwa binti mwenyewe ana umri wa miaka 15 tu, na aliyempa ujauzito ni mtu mzima. Alimpa hiyo mimba binti akiwa shuleni, na kwa mujibu wa sheria zilizopo angestahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Hayo hayakutokea.

Nahisi hayakutokea kwa sababu mama wa binti, badala ya kupeleka hilo suala mbele ya sheria, alifikia makubaliano na huyo jamaa na inawezekana kuwa alikuwa anapewa pesa ili kutulia.

Sasa leo kalalamika tena kuwa binti karudi kule kule na akaniambia kuwa sasa anakusudia kufikisha suala hilo polisi. Lakini njia anayotumia haijanyooka vizuri. Kaniambia kuwa ana jirani yake polisi ambaye amemuomba aende kumkamatia yule mhalifu.

Jirani yake kakubali lakini amemwambia ampe shilingi elfu kumi ili amfanyie hiyo kazi. Yeye alisema hana hizo pesa, na akamwambia yule jirani kuwa amfanyie tu hiyo kazi kwa kuwa wanahusiana pia kiukoo. Jirani polisi hakusumbuliwa sana na hoja ya uhusiano wa kiukoo, na amemwambia mlalamikaji atafute angalau shilingi elfu tano ili afanye hiyo kazi.
 
Rais John Magufuli (wa pili kutoka kushoto), akiwa na marais wastaafu (kutoka kushoto kwenda kulia) Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Mrisho Kikwete, na Benjamini William Mkapa. (Picha kwa hisani ya CCM Blog)

Miongoni mwa vielelezo kuwa uongozi ni kazi kubwa ni pamoja na tukio hili. Kwenye ngazi hii ya chini, kujenga imani kuwa falsafa ya Sasa Kazi tu! itafanikiwa ili mradi yupo rais na waziri mkuu wachapa kazi ni ndoto tu. Mabadiliko chanya yatapatikana iwapo wote tutashiriki kwa namna tunavyoweza kuleta mafanikio tunayotarajia.

Wednesday, November 11, 2015

Adha za Mwenge wa Uhuru

Sina tatizo na madhumuni ya mbio za Mwenge wa Uhuru, lakini ninaona kasoro kubwa katika baadhi ya vipengele vya mchakato wa mbio hizo unavyoendeshwa.

Mwenge unapohamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, barabara zote huwa au hazipitiki au zinapitika kwa shida. Barabara zinafungwa mpaka Mwenge upite. Wale wenye shida za dharura wanakuwa hawawezi kutumia usafiri wa barabara kufuatilia shida zao.

Hata mgonjwa mahututi ambaye anapelekwa hospitali au kwenye kituo cha afya anaweza kujikuta ndani ya gari akisubiri Mwenge upite kwanza, ndipo gari alilopanda (kama siyo la kubeba wagonjwa) liweze kuruhusiwa na kuendelea na safari yake.

Gari zikiwa zimesimamishwa eneo la Kisesa, Mwanza, zikisubiri msafara wa Mwenge wa Uhuru upite.
Na isingekuwa vibaya sana iwapo watu wangelazimika kusubiri kwa muda kidogo tu kupisha Mwenge upite. Tatizo ni kuwa wakati mwingine watu husubirishwa kwa muda mrefu sana ili msafara wa Mwenge upite, hata pale ambapo msafara huo unaelekea njia tofauti. Ili mradi tu unapishana nao, basi utalazimika kusimama.

Mwenge wa Taifa ni nembo ya Taifa na nadhani maana ya kusimamishwa watu njiani ni kutoa heshima kwa hiyo nembo ya Taifa. Sijui kama hii ndiyo mantiki ya hatua hizi, lakini inawezekana pia kuwa watu husimamishwa kwa sababu ya kipengele kimoja ambacho nadhani kipo kwenye Sheria ya Usalama Barabarani ambacho kinatamka kuwa msafara rasmi ni lazima upishwe.

Nadhani msafara wa Mwenge unapewa hadhi ya msafara rasmi, kama msafara wa rais au viongozi wengine wa ngazi ya juu. Hatari iliyopo ni kuwa msafara wa Mwenge unaweza kumsubirisha mgonjwa mahututi na asiwahi kupata huduma ya matibabu ambayo inaweza kuokoa maisha yake.

Tuesday, November 10, 2015

Mwalimu Nyerere na nguzo ya uwajibikaji kwa wote katika uongozi

Kwenye kijitabu chake, Ujamaa ni Imani 1: Moyo kabla ya silaha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anasema:

Alinijia Mzanaki mmoja mwaka 1961, mara tu baada ya kupata uhuru. Anataka kazi; anasema, "Mzanaki ndiye Rais, basi sisi Wazanaki tutainuka." Nikamwambia, "Nenda, uko utaratibu wa kupata kazi." Akaniambia, "Na mimi vilevile niende huko?" Nikamwambia, "Kwa nini usiende huko?" Akasema, lazima nije kwako; sasa Mwalimu wewe umekwisha pata, ndugu zako wengine vile vile wapate. Sasa tusipoanza sisi Wazanaki waanze nani? Na wakubwa ndio wa kula, na wakati wa kula umefika; basi tule!"
            (Uk. wa 40)

Yameharibika mengi kwenye nchi hii kwa sababu viongozi wengi wanaamini kuwa uongozi ni sehemu ya kujineemisha wao na familia zao. Na kwa wale ambao hawana ndugu au marafiki kwenye sehemu muhimu za uongozi, uwezekano wa kupata ajira au haupo kabisa au ni finyu sana.
Mwalimu Nyerere

Kurudisha mfumo ambao unatoa fursa sawa kwa wote inawezekana kabisa.

Sunday, November 8, 2015

Yanayotokea niliyatabiri

Kwenye makala yangu ya tarehe 14 April 2015 kwenye gazeti la Jamhuri nilitoa maoni yangu juu ya Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 na kutahadharisha kuwa ni sheria ambayo itawafikisha wengi mahakamani, na hata gerezani.

Na tayari kuna kesi zimeshafikishwa mahakamani dhidi ya watu wanaotuhumiwa kukiuka sheria hii.

Nilitoa hoja kuwa, pamoja na kuwa sheria hii inakusudia kudhibiti uhalifu unaotokea kwa matumizi ya mifumo ya mtandao wa habari na mawasiliano, ni sheria ambayo ina hitilafu kubwa zenye kuhatarisha uhuru wa kusambaza na kutoa maoni mbalimbali ndani ya jamii.

Hakuna raia ambaye analazimishwa kupenda sheria mbalimbali ambazo anaona zina kasoro au hitilafu. Lakini zinabaki kuwa ni sheria na yoyote ambaye hataki, kwa makusudi, kusimama kizimbani kujibu mashtaka ya kukiuka hizo sheria anapaswa kuwa mwangalifu asifike huko.

Njia muafaka ya kuepuka kuishia kubaya ni kuweka mikakati ya pamoja ya kupinga hizi sheria zenye kasoro kwa taratibu zilizopo, za kisheria.

Hoja ya kuwa unawezaje kupinga sheria zenye hitilafu kwa kutegemea serikali ambayo ilipitisha sheria hizi ni hoja yenye nguvu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania chama tawala kimeshinda uchaguzi kwa asilimia ndogo kuliko kwenye chaguzi zote zilizopita. Mimi naamini kuwa ushindi huo mwembamba unaweza kuleta mabadiliko hata kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa tofauti na serikali zake zilizopita, ikawa ni serikali ambayo inasikiliza maoni ya Watanzania na kuanza kupitia upya zile sheria ambazo zinalalamikiwa na watu.

Wasiposikiliza wajiandae kuongeza mahakimu, na kujenga magereza kwa wingi.

Monday, September 21, 2015

Ushauri kwa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza

Nimepiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 1985. Ningeweza kupiga kura mwaka 1980 lakini sikuwa nchini wakati huo, nilikuwa masomoni. Naamini kuna vijana wengi ambao watakuwa wanapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka huu na naomba nitoe ushauri mdogo kwao.
Nikiwa na Mwalimu wangu, Godian Muikza (kushoto) ambaye ni diwani anayemaliza muda wake wa Kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini.

Kwanza lipo suala muhimu la kuchambua ahadi. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1985 nilimpa kura ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi na ya ubunge nilimpa Kapteni Ukiwaona Ditopile Ramadhani Mwinshehe Mzuzuri. Siku zile sikuwahi kuhudhuria mkutano wowote wa kampeni za uchaguzi kwa hiyo kura yangu ya ubunge sikupiga kutumia kigezo kikubwa zaidi ya kufurahishwa na jina la mgombea. Sikumbuki hata alikuwa anagombea nafasi ile dhidi ya nani, lakini nakumbuka ilikuwa wanawania nafasi ya ubunge wa jimbo la Ilala. Mgombea urais, Mzee Mwinyi, alikuwa ana fursa ya kusikika zaidi ya wagombea ubunge kwenye vyombo vya habari kwa hiyo yeye tulimsikia zaidi ya wagombea ubunge.

Hata mwaka huu naamini kuna wapiga kura wengi watajitokeza wa aina yangu, kama nilivyokuwa mimi mwaka 1985 na kupiga kura kwa kufurahishwa na jina la mtu tu bila hata kuchambua kwa makini sera anazowakilisha mgombea huyo. Mwaka 1985 hatukuwa na vyama vingi, lakini sasa vipo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya msingi ya mpiga kura yoyote kuacha kuweka sera za vyama kwenye mizania na kuamua chama kipi kitapata kura yake. Hatuna uhakika kuwa yanayoahidiwa yatatekelezwa, lakini bado ni muhimu kuchambua sera tofauti. Akishinda mtu wako na asipotekeleza ilani yake angalau unayo sehemu ya kuanzia kumhoji. Kama ulimchagua kwa mkumbo tu hutakuwa na kigezo cha kuamua kuwa hajatimiza ahadi zake.
Wapiga kura wa Butiama wakipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010


Pili, nazungumzia wale ambao wana uhakika mkubwa wa matokeo ya ushindi kwa wanaowaunga mkono, ikiwa ni vyama vya siasa au mgombea mmoja mmoja. Kusikiliza na kuamini na kauli kama “ushindi ni lazima” ni mwanzo wa kukaribisha vurugu. Kama kiongozi anatumia kauli hiyo kuhamasisha tu wafuasi wake ili waweke juhudi kubwa kwenye kampeni inaweza kuwa haina madhara. Lakini kauli hiyo inaweza kufasiriwa kuwa “tumeshashinda hata kabla ya kupiga kura na mtu yoyote atakayesema kuwa hatujashinda ni muongo na ametuibia kura.” Hapo tunakaribisha vurugu.

Mwaka 2010 niliteuliwa wakala wa mgombea ubunge na nilijifunza kitu kimoja cha msingi. Kama wakala wa mgombea yuko makini, siyo rahisi kuibiwa kura. Sikulala siku hiyo mpaka matokeo yalipothibitishwa na msimamizi wa uchaguzi alfajiri ya siku iliyofuata. Wanaoibiwa kura ni wale ambao wameweka mawakala ambao siyo waaminifu au ambao hawakuwa makini. Mtu akitaka kuibiwa, ataibiwa.
Kulia ni Mhe. Vincent Nyeerere, Mbunge wa Musoma Vijijini kupita Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) anayemaliza kipindi chake cha ubunge aliyeniteua kusimamia kura zake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kushoto ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kapteni Godfrey Ngatuni.
Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi tumesikia shutuma kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo wataalamu wa kuiba kura. Kama hizo shutuma ni za kweli, sioni sababu yoyote ya kutoana roho kwa sababu sasa hivi Mhe. Edward Lowassa amehamia upande wa pili. Yeye amekulia na kujifunza siasa ndani ya CCM na, kwa vyovyote vile, atakuwa amehama na uelewa uliobobea wa mbinu zinazotumika kuiba kura na atakuwa anafahamu mbinu za kutumika kuzuwia wizi huo. Mwizi hawezi kumuibia mwizi.
Mwanachama wa Chama cha wananchi (CUF) akielekea kwenye mkutano wa kampeni jijini Mwanza mwaka 2010.

Kwa sababu hii sioni kabisa busara ya mtu yoyote kutamka kuwa kaibiwa kura kama yeye mwenyewe hataki kuibiwa kura. Labda atumie kauli hiyo kama kisingizio cha kupinga matokeo. Tunao wajibu wa kujenga mazingira yenye kulinda amani, lakini tunao pia uwezo wa kuweka mazingira yanayobomoa amani.

Uchaguzi huu umeibua ushindani mkubwa kati ya CCM na vyama vinavyowakilishwa na UKAWA. Kwa bahati mbaya, ushindani unaonyesha dalili za uhasama na muelekeo kuwa kipindi hiki cha kampeni kitaibua matukio ya kuvunjika kwa amani. Lakini amani itavunjika tu iwapo wapiga kura tutakubali ivunjike. Na amani inapovunjika hutasikia hata siku moja kuwa Mhe. John Magufuli au Mhe. Edward Lowassa kavunjika mguu kwa sababu ya vurugu za kisiasa.


Bado sijaona sababu ya msingi ya kuvunjika kwa amani kutokana na uchaguzi. Usikubali kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani.

Thursday, September 10, 2015

Mada yangu ya leo: Hii siyo siasa

Tuawasikia baadhi ya viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakimtaka mgombea urais wa UKAWA akubali wakutane kwenye mdahalo ili waeleze maovu yake. Yeye anasema kama wana ushahidi kuhusu maovu yake waende mahakamani. Hii siyo siasa.

Nionavyo mimi, siasa ingekuwa hivi:

1. Kama una tuhuma dhidi ya mgombea urais husubiri awe rais kwanza. Unasema yale unayoyafahamu. Akisha kuwa rais halafu utafanya nini? Utaomba mdahalo?

2. Mpiga kura ana haki ya kufahamu taarifa zote muhimu juu ya wagombea kabla hajafikia uamuzi wa kumchagua yule ambaye anaona anafaa. Kuamua kuwa taarifa hizo ni kama mali adimu haina tofauti na kujifanya mtaalamu wa bishara (au taaluma nyingine) ambaye ametumia muda mwingi kupata elimu na uzoefu kwenye taaluma yake halafu anaamua, kwa haki kabisa, kuwa taarifa hizo hazitoki mpaka kwa masharti yanayomnufaisha yeye, au kwa pesa au kwa njia nyingine atakayoamua. Ni wajibu wa kiongozi yoyote makini kumpa mpiga kura taarifa sahihi, hasa wakati wa uchaguzi.

3. Mpaka sasa, tumemsikia mtuhumiwa akisema kuwa hana tuhuma yoyote na, kwa mantiki hiyo, anaposema nendeni mahakamani ni sawa kabisa. Wale wenye taarifa hizo wakaziibue mahakamani. Watuhumiwa wachache sana hukubali kosa nje ya mahakama.

Kwa hayo machache, sisemi kuwa tuhuma ni za uongo.

Ninachoona ni kundi moja ambalo limekosa ujasiri wa kutamka wanalotaka kutamka na badala yake kuwafanya wapiga kura kubaki wanabishana wenyewe kwa wenyewe na ujinga wao* (kama ujinga huo upo kweli) bila kuwapa taarifa ambazo zinaweza kuwasaidia kufanya chaguo sahihi.

Kama huo ujasiri unakosekana, basi ni bora kunyamaza tu. Kuwafanya wapiga kura kuwa wajinga mara ya pili ni hatari kisiasa.

Huo ndiyo ujumbe wango leo hii.

*Wale ambao mtakimbilia kwenye Tume ya Mawasiliano kunilalamikia kuhusu kutumia neno "ujinga" ni kwamba siyo tusi, ni hali ya kutofahamu tu.

Wednesday, August 12, 2015

Lugha yetu Kiswahili: Kiswahili kinasambaa toka Scotland mpaka Butiama

Wanafunzi 12 toka Chuo Kikuu cha Edinburgh wapo kijijini Butiama kujifunza Kiswahili kwa mwezi mmoja.

Mafunzo yao ni sehemu ya mpango wa Chuo Kikuu cha Edinburgh kuvutia wanafunzi kutoka nje ya Scotland kujiunga na masomo mbalimbali katika chuo hicho maarufu, ambacho mmoja wa wanafunzi wake mashuhuri ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wanafundishwa Kiswahili na walimu Watanzania watatu.
Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh wakiwa Butiama, pamoja na walimu wao wa lugha ya Kiswahili.
Kuwepo kwa wanafunzi wa lugha ya Kiswahili kutoka Edinburgh hapa Butiama kwa Mwalimu Nyerere, ambaye pia anatambuliwa kama mmoja wa viongozi wa Tanzania ambao walitoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ni suala la fahari kubwa kwa mmoja wa waratibu wa mafunzo haya ya Kiswahili, Dk. Thomas Molony, ambaye mwaka jana alichapisha kitabu juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere kinachoitwa Nyerere: The Early Years.

Akiwa Butiama wakati akifanya utafiti wa kitabu chake, nilipata fursa ya kuchangia kwa kiwango kidogo taarifa ambazo hatimaye alizitumia kwenye kitabu hicho.

Na mimi nakubaliana naye. Naamini kuwa Mwalimu Nyerere angekuwa hai angefurahi sana kushuhudia wanafunzi kutoka chuo chake cha zamani wakiwa Butiama kujifunza lugha ambayo yeye mwenyewe aliipenda na aliyoshiriki kuiimarisha.

Tuesday, July 14, 2015

Kwenye mchakato huu, dozi ya politiki ilizidi kiwango

Nafikiri ni General Defao aliyeimba: "umekalia politiki tu, kazi hufanyi". Katika kipindi ambacho Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiendelea na mchakato wa kupata mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, hali hiyo ya kukalia politiki tu imekuwa kweli kwa watu wengi.

Wengi tunatambua umuhimu wa mchakato wowote wa kisiasa kama jambo muhimu katika jamii na jambo la msingi ni kupata viongozi wanaosimama kuwakilisha matakwa ya wengi. Na bila shaka ni suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulifuatilia kwa karibu sana.

Lakini mchakato huo unapotufanya tuache kila kitu, hata zile kazi ambazo zinatulipa ajira, basi suala la siasa linakuwa limezidi dozi ya kawaida. Kuna watu wengi tu ambao hawakuwa na nafasi yoyote katika vikao vya maamuzi vya CCM vilivyokaa Dodoma kumpitisha John Magufuli ambao walienda Dodoma kufuatilia mchakato huo.

Baadhi ya ambao hatukuwa Dodoma tulikaa muda wote tukisikiliza taarifa kwenye vyombo vya habari kufuatilia mchakato. Wengine wengi walitumia muda wao kujibishana na wenzao kwenye mitandao ya jamii. Dozi haikuwa ndogo hata kidogo.
"I've always been and will continue to be a proud member of the ruling party CCM...I'm happy with all the five candidates and know that we'll get a great President to lead our beautiful nation...All the best....God Bless Tanzania󾍛....#ccm #chamachamapinduzi #januarymakamba #membe #magufuli #migiro #amina #umojaniushindi #tanzania"
Baadhi ya watia nia waliofikia hatua za mwisho za mchakato wa kupata mgombea urais wa CCM
Naamini watafiti wanaweza kubaini kushukua kwa uzalishaji katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita.

Tushukuru kuwa mchakato huu wa CCM umeisha na labda watu watarejea kwenye maisha yao na majukumu yao ya kila siku.

Monday, June 22, 2015

Utamaduni wa utoaji majina miongoni mwa kabila la walango wa Uganda

Nimepata fursa hivi karibuni ya kuonana tena na mmoja wa watoto wa kiume wa rais wa zamani wa Uganda, Apollo Milton Obote na tuliongelea utamaduni wa kutoa majina kwa kabila lao la walango.

Nilipenda kufahamu kwa nini jina lake halina ubini wa baba yake, Obote. Yeye anaitwa Eddy Engena-Maitum, na ni askofu wa kanisa la Bright Morningstar Ministry. Alinijibu kuwa kwa mila na desturi za kabila lao, kila mtoto anayezaliwa anapewa majina yake bila kuweka jina la baba mzazi. Alifafanua kuwa majina yote ya baba yake ni yake, hakutumia ya baba yake (babu yake Eddy).

Mdogo wake naye anafuata utaratibu huo huo: ni Jimmy Akena, ambaye ni mwanasiasa na rais wa chama cha Uganda Peoples' Congress. Aidha, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika 2017. Alipomuoa mbunge mwenzake Betty Amongi mwaka 2013 Rais Yoweri Museveni alihudhuria harusi hiyo.

Mimi (kulia), nikiwa pamoja na Askofu Eddy Engena-Maitum jijini Kampala hivi karibuni.
Eddy anafafanua kuwa zipo faida na hasara za kutotumia ubini wa baba yao. Wakati mwingine akijitambulisha kama mtoto wa Milton Obote wale wasiomfahamu humtilia shaka wanapoona kuwa jina lake kamili halina jina la baba yake. Faida ni kuwa pale inapokuwa siyo lazima kujitambulisha hivyo inampa fursa ya kubaki bila utambulisho huo ambao, kwa watoto ambao wazazi ni wanasiasa inaweza kuwa ni jambo linalozua hisia tofauti kwa wanaobaini hali hiyo. Inaweza kutokea kubebeshwa kesi ambayo siyo yako.

Monday, April 13, 2015

Hapa ndipo alipozaliwa Mwalimu Nyerere

Hapa ndipo miaka 93 iliyopita alizaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kijijini Butiama.
Ni eneo la Mwitongo alipoishi baba yake Mtemi Nyerere Burito wa kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, na mama yake, Mgaya wa Nyang'ombe, aliyekuwa mke wa tano kati ya wake 22 wa Mtemi Nyerere.

Leo eneo hili ni sehemu inayotembelewa na mamia ya wageni kila mwezi kutoka sehemu mbalimbali.

Saturday, March 14, 2015

Mahojiano yangu kuhusu wagombea urais

Majuma kadhaa yaliyopita nilihojiwa na mwandishi wa habari wa Mwanza kuhusu maoni yangu juu ya wagombea urais waliojitokeza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

Sehemu ya mahojiano hayo imechapishwa hapa.

Saturday, January 24, 2015

Waheshimiwa wengi sana Tanzania

Neno mheshimiwa limekosa heshima inayokusudiwa kwa maoni yangu.Sababu kubwa ni kuwa Tanzania ina waheshimiwa wengi sana.

Sizungumzii wale watu ambao nafasi zao katika jamii zinatulazimu kuwaita "waheshimiwa", kwa mfano mahakimu, majaji, na wabunge. Nazungumzia tabia iliyojengeka ya matumizi ya "mheshimiwa" kwa kila raia anayezungumza Kiswahili. 

Mimi nilidhani kuwa madhumuni ya kutumia "mheshimiwa" haina tofauti sana na kumuita mtu daktari. Madhumuni ni kumpambanua kama mtu mwenye nafasi muhimu katika jamii ambayo inahitaji kuweka mipaka ya namna watu wengine wanavyowasiliana nae, au kubainisha kuwa ni mtu ambaye anayo taaluma maalum. Kwa upande wa majaji na mahakimu ni viongozi ambao wana majukumu muhimu ndani ya jamii na wanapata upendeleo fulani kwa namna wanavyochukuliwa na jamii. Kwa kuwapa huo upendeleo jamii pia inategemea kuwa waheshimiwa watakuwa watu wanaojiheshimu mbele ya jamii.

Sasa cheo hiki anapopewa kila mtu kuna hatari ya kukigawa kwa watu ambao hawajiheshimu hata chembe na ambao wataharibu maana halisi ya uheshimiwa. Kwa maoni yangu waheshimiwa wanaosimamia kesi mahakamani ndiyo wanastahili zaidi kuitwa waheshimiwa.

Sisi tuliobaki tungerudia kuitana ndugu, ingawa wengi wanaamini undugu unahusiana na siasa ya Ujamaa peke yake. Siyo kweli. Tumsikilize Rais Mstaafu Mkapa, akizungmuza kwenye semina ya Muafaka ya Vyama vya Siasa, Zanzibar, tarehe 7 Machi 2005:

"Ndugu siyo neno la kiitikadi tu, linahusu pia utamaduni wetu. Mtaniwia radhi nikiwaita "Ndugu wanasemina."

Wewe ni ndugu au mheshimiwa?

Sunday, January 11, 2015

Kandambili, rangi mbili

Sehemu nyingi za Tanzania, hasa kwenye miji midogo, ukiingia kwenye gesti au hoteli basi kama umewekewa kandambili chumbani utakuta kila moja ina rangi tofauti.
Sababu kubwa ni kuwa baadhi ya wateja wanaoingia kwenye sehemu hizi siyo waaminifu na wanapoondoka huamua kuondoka na kandambili. Inaaminiwa kuwa zikiwa zina rangi mbili tofauti basi mwenye kusudio la kuziiba ataacha kufanya hivyo. Sina hakika kama inasaidia kuzuwia wizi.