Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, September 23, 2012

Pambano la ndondi Oktoba 14 kumuenzi Mwalimu Nyerere

Mabingwa wa uzito wa kati (kilo 72.5) wa Uganda na Tanzania wanaotambuliwa na Tanzania Professional Boxing Organization (TPBO) watapambana tarehe 14 Oktoba mwaka huu Friends Corner Bar, Manzese, Dar es Salaam katika pambano lilioandaliwa kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki zaidi ya miaka 12 iliyopita.

Pambano hilo litawapambanisha bingwa wa Tanzania Thomas Mashali, juu, na bingwa wa Uganda, Med Sebyala, chini.


Mchezo huo utakuwa wa kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki.

Bondia Sebyala ameshawahi kupambana na kushindwa kwa pointi na bondia Francis Cheka, bingwa wa mabara wa Afrika anayetambuliwa na International Boxing Federation (IBF). Aidha, ameshawahi kupambana na Rashidi Matumla na ingawa mapambano yote alishindwa kwa pointi, alitoa upinzani mkali kwa mabondia hao Watanzania.

Bondia Mashali anayo sifa ya kutoa vichapo vikali kwa wapinzani wake na kuwapumzisha kwa knock-out za mapema.

Taarifa kutoka TPBO zinaeleza kuwa kwa kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuthamini juhudi zake za kuendeleza michezo TPBO itaandaa mapambano ya ngumi kwenye kila maadhimisho ya kifo chake tarehe 14 Oktoba.

Friday, September 21, 2012

Twist mpaka chini: harusi za Tanzania zinafanana sana

Sijui ni hisia zangu tu, lakini nahisi kama mtiririko wa ratiba za harusi ninazohudhuria siku hizi zinafanana sana.

Kwenye harusi nilizohudhuria hivi karibuni nimeshuhudia kuna wakati wa kuita kamati iliyoandaa harusi na kila mwanakamati hujitambulisha. Salama ipo kama wanakamati bado hawajachangamka kwa vinywaji vinavyoondoa aibu mbele ya kadamnasi. Lakini kama wanakamati wameshachagamka mambo huwa hayatabiriki.
Mara wanapomaliza kujitambulisha na kueleza mambo waliyofanya kufanikisha harusi, basi muongozaji wa sherehe anaagiza DJ aweke twist ya uhakika.

Na mara zote nimeshuhudia kuwa wimbo unaopigwa ni ule ule. Uchezaji nao ni ule ule, haujabadilika tangu miaka ya hamsini ingawa silalamikii uchezaji nao ubadilike.

Monday, September 17, 2012

Msondo Ngoma bado wanatamba

Wapiga gitaa wa bendi ya Msondo Ngoma Abdul Ridhiwani, kushoto, na Zahoro Bangwe, kulia,
wakiburudisha mashabiki wao hivi karibuni wakati bendi hiyo ilipotumbuiza kwenye ukumbi wa Max Bar, Ilala Bungoni, Dar es Salaam.

Msondo Ngoma ni moja ya bendi kongwe za muziki wa dansi za Tanzania. Zamani ilikuwa inaitwa NUTA Jazz.

Picha na habari zimetolewa na Rajabu Mhamila.

Sunday, September 16, 2012

Mada yangu ya leo: polisi na waandamanaji

Kuna mambo mawili muhimu yanajitokeza baada ya kuuwawa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten wa Iringa, Daudi Mwangosi, tarehe 2 Septemba 2012. Kwanza, Jeshi la Polisi, ambalo mmoja wa askari wake ameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, linahitaji kutoa mafunzo maalum ya namna polisi waliyopo kwenye eneo la maandamano wanavyopaswa kusimamia suala la amani katika maandamano.

Siyo kila tukio la mkusanyiko wa watu linahatarisha mali au maisha ya raia, kwa hiyo ni dhahiri pia kuwa siyo lazima kila mara kutumia nguvu zisizokuwa za lazima dhidi ya raia. Polisi wanafunzi wanapaswa kupewa elimu inayojenga taswira kuwa anaepinga serikali iliyoko madarakani siyo lazima pia awe ni adui wa Taifa au anaetishia usalama wa Taifa.

Picha inayojitokeza baada ya baadhi ya matukio ambapo polisi wameua raia ni kama vile kazi kuu ya polisi ni kuhakikisha kuwa upinzani halali wa kisiasa unaminywa kiasi cha kutosha na kuondoa kabisa uwezekano wa serikali iliyopo madarakani kuondolewa madarakani kwa njia za kidemokrasia.

Polisi wapate mafunzo kuwaelimisha kuwa kazi yao siyo kulinda maslahi ya kisiasa ya serikali iliyopo madarakani, na wafunzwe kukubali uwezekano kuwa chama chochote kilichopo upande wa upinzani kinaweza hatimaye kushinda uchaguzi na kuongoza serikali.

Jambo la pili na ambalo ni muhimu sana ni kuwa sasa waandishi wa habari wapate mafunzo ya namna ya kukusanya habari kwenye maeneo yenye usalama mdogo ili kupunguza tishio kwa usalama na maisha yao. Polisi anafanya kazi kwa amri, na kuna mazingira mengi ya kisheria yanayomruhusu polisi kutumia silaha kwa jinsi ambavyo anaona ni sawa kutokana na mazingira yanayomkabili. Polisi anayefukuzwa na kundi la waandamanaji ambao anaamini wanakusudia kumuua hatasita kutumia silaha yake dhidi ya kundi hilo. Huu ni mfano tu; haya sidhani kama ni mazingira yaliyotokea kwenye tukio lilisobabisha kifo cha Daudi Mwangosi.

Jambo la msingi ni kuwa, hata pale ambapo tunajua tunayo haki, si busara hata kidogo kubishana na mtu ambaye ameshika silaha na anaamini kuwa anatekeleza amri halali aliyopewa na mkubwa wake. Na hili haliwezi kubadilika mpaka itolewe elimu ambayo itambadilisha polisi Mtanzania ili atumie mbinu tofauti kukabiliana na waandamanaji.

Friday, September 14, 2012

Biashara ya vyuma chakavu na ufisidi (ni ufisidi, siyo ufisadi)

Miaka kadhaa iliyopita, mafundi toka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walijenga mnara mdogo wa kumbukumbu kijijini Butiama, sehemu ambapo ilianguka ndege ya kivita aina ya Mig, mara baada ya kuanza vita vya Kagera mwaka 1978.

Ujenzi huo uliambatana na njia ya kupita kwa miguu iliyojengewa mabomba ya chuma kuanzia barabara kuu mpaka sehemu ilipoanguka ndege, umbali wa kama mita 100 hivi.


Manara wa kumbukumbu ilipoanguka ndege ya JWTZ, eneo la Mwitongo, Butiama. Vyuma vyote vilivyo pembeni vimenyofolewa na wachuuzi wa vyuma chakavu.
Haikupita muda mrefu, wachuuzi wa biashara ya vyuma chakavu walikata mabomba yote na kuyapeleka kwa wanunuzi wa vyuma chakavu. Mnunuzi mmoja mkku wa vyuma chakavu yuko Mwanza.

Ni hawa hawa unaweza kuwasikia wakipigia makelele kuwepo kwa ufisidi (ni ufisidi, siyo ufisadi) nchini, wakinyoosha vidole kwa baadhi ya viongozi wetu, wakati hata wao wanayoyafanya hayapishani sana na yale wanayoyakemea.

Thursday, September 13, 2012

Mada yangu ya leo: kufahamu Kiingereza siyo kuwa msomi

Mada yangu leo si ndefu sana, lakini naamini ni muhimu.

Nianze na tukio moja la zamani. Niliwahi kufahamiana na raia mmoja wa Uingereza ambaye aliishi na kufanya kazi Dar es Salaam kwenye miaka ya tisini, akiwa mwajiriwa wa kampuni moja ya ulinzi. Huyu alikuwa mtu mmoja mcheshi, na mchangamfu kwa wengi aliyefahamiana nao ingawa kwa aliyewaongoza kazini alikuwa mkali sana.

Kuna Mtanzania mwenzangu ambaye naye alikuwa akifahamiana naye na alimheshimu sana, siyo tu kama binadamu mwenzake lakini naamini kwa wadhifa wake muhimu wa kuongoza kampuni yenye wafanyakazi wengi wenye jukumu la kulinda mali na makazi ya wateja wa hiyo kampuni.

Miaka kadhaa ilipita na yule Mtanzania mwenzangu siku moja aliniambia: "Unafahamu? Kumbe yule jamaa amesoma mpaka darasa la nne tu!"

Mtanzania mwenzangu, ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu, hakuamini kuwa mtu aliyemdhania ni msomi mwenzake kumbe alikuwa amesoma mapaka darasa le nne tu, pamoja na kupewa jukumu la kuongoza kampuni moja mashuhuri ya Tanzania.

Tatizo nililoliona mimi lilikuwa la lugha. Kwa kipimo cha Mtanzania mwenzangu yule Mwingereza alikuwa anazungumza Kiingereza safi kabisa kuliko ambacho yeye alikuwa anamudu kuongea na kwa mantiki aliyofikia ingekuwa ni dhahiri kuwa yule jamaa alikuwa ni msomi. Kwa sababu tu anaongea Kiingereza kizuri kuliko cha kwake.

Nilimuuliza: "Sasa utamdharau kwa sababu ya ya elimu yake, wakati wote huo ukimwona ni mtu wa maana sana?"

Haya yalitokea zaidi ya miaka 20 iliyopita lakini tatizo la kumpa mtu uzito mkubwa zaidi kwa sababu anaongea Kiingereza vizuri bado lipo mpaka leo.

Jeneral Ulimwengu achangia majadiliano ya katiba mpya

Kwa idhini ya Jenerali Ulimwengu, natoa sehemu ya mada ailiyotoa kwenye kongamano la kujadili katiba mpya lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 15 Januari 2012.

************************************************
Ninavyoangalia jamii ya Tanzania ilivyo sasa hivi, pamoja na mambo yote mema tuliyonayo, tumejaliwa watu wenye kuheshimiana, wenye kupendana,  kwa kiwango kikubwa. Tunaanza kuchukiana chukiana, lakini kwa sababu ya mipangilio mibaya na kujitawala vibaya. Lakini kimsingi, watu wetu ni watu wema. Watawala wao ndiyo waovu.
 
Matokeo yake ni kuwa tumejenga jamii ya watu katika kiwango ambacho kinatisha cha watu wa aina zifuatazo:-
-          Watu wasioaminika
-          Matapeli
-          Wababaishaji
-          Na wapuuzi
Sisi, pamoja na watawala wetu.
 
Watu warushaji katika mahusiano ya kibiashara kiasi kwamba hatuaminiki katika nchi jirani. Mara mafuta yamechakachuliwa; mara ukiuza pamba wameweka mawe. Ali mradi, tumekuwa sisi ni waNigeria wa eneo hili la Afrika.
 
Watu tunaoonea wanyonge. Kuwaibia masikini. Kuwapora wahanga wa ajali, na kuwaua albino kwa imani za kijinga. Washirikina tunaoamini ujinga wakati uthibitisho wa teknolojia tunao mikononi. Kwamba tunaweza ku-Google, search engine ya Google, kutafuta mchawi mahiri yuko wapi.
 
Ujuha wa kiasi hicho. Na wengine sasa wanakwenda bungeni. Watu na jamii fasta fasta. Wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka bila kufanya kazi. Tumekubali wito wa:
-          Kuwa mjanja!
-          Chizika!
-          Pandisha mzuka!
-          Full kujirusha!

 Ambayo yote yametujaza upuuzi wa kibambucha.

Jamii isiyopenda kujifunza. Tumevifanya vitabu ni kama wakwe zetu, tunaogopa kuvifunua wakati tunaona jinsi majirani zetu, kwa mfano, Kenya, vijana wanavyohangaika kujisomea. Ukienda Nairobi, nenda Saritz Centre, uende bookshop ile angalia jinsi wanavyosoma halafu mnaogopa Wakenya watachukuwa nafasi zetu; Wakenya watachukuwa ardhi yetu.

Bora waje Wakenya kuliko kuwa na wajinga wakaharibu nchi hii. 

Watu wakutoa majibu mepesi mepesi kwa maswali mazito. Kwa sababu hatupendi kusumbua akili zetu. Wapiga kura wanaouza kura zao kwa bakuli la kunde, na kisha kulalamika wasipopata uongozi wa kuwafanyia kazi. Watu wasiojua misingi ya haki. Wanaochoma moto mwizi wa kuku, lakini mwizi wanamchagua kumpeleka bungeni.

Kumi, kwa ufupi, watu na jamii iliyopotea.

Jamii hii haiwezi kuandika katiba. Mpaka i-address masuala haya. Mimi naamini kabisa tukienda kuandika katiba sasa hivi, nakubaliana na Issa [Prof. Issa Shivji], kwamba kama hiyo Tume ya Rais itakuwa na watu wanawakilisha makundi mbalimbali, itaanza kuzungumza na hali yenyewe tuliyo nayo ndiyo hii, yaani fanya unavyotaka, hutapata chochote cha maana kwa sababu humu ndani kutakuwa na wezi, wazandiki, matapeli, wababaishaji, wala rushwa. Kila mtu anajaribu kuweka nafasi yake mbele. Na maslahi yake mbele.

Sasa tufanye nini? Yuko Mzee Ibrahim Kaduma hapa. Natumai kuwa kitabu chake kilichozinduliwa juzi kitakuwa hapa. Ili kupambana na haya niliyoyasema, ambayo ni magonjwa makubwa, ni majanga makubwa, na ndiyo yanatawala, hebu turudi kwenye misingi.

Moja: Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote.
Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umasikini, ujinga, maradhi, na dhuluma.
Ongeza na rushwa.
Nne: Rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa.
Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cheo cha mtu mwingine kwa faida yangu.
Hebu niambie ni watu gani ndani ya Serikali wanaweza kusimama hadharani wakasema maneno haya?
(Hadhira: hawapo!)
Sasa tuwafanye wayaseme haya. Katika uandikaji...katika mchakato mzima wa kujadili katiba mpya, tufike mahala tuwalazimishe watu waliomo katika utawala, wasimame mbele yetu waseme hivi: Cheo ni dhamana. Sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa manufaa yangu. Waseme! Halafu tuwapime.
Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya Nchi.
Nyie wasomi hapa chuoni mnasema hiyo? Au? Nasikia wanafunzi wengi sana mnasoma accountancy. Accountancy ni somo zuri lakini sasa sijui mnataka kwenda kufanya kazi wapi?
Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.
Nitasema kweli daima. Fitna kwangu mwiko.
Nitakuwa raia mwema wa Tanzania, Afrika, na Dunia nzima.

Tuyatafakari hayo. Tuwe na muafaka wa kitaifa. Tuwe na maridhiano, tuwe na makubaliano. Tuwe na national charter,  kutokana na hilo sasa ndiyo twende na michakato mingine aliyosema Shivji [Prof. Issa Shivji] ya kujenga misingi ya maelewano nchini na kuandika katiba mpya itakayotuongoza kwa miaka hamsini au mia ijayo. Nawashukuruni sana.

Monday, September 10, 2012

Wageni wa Butiama

Bi Victoria Gilago Bache kutoka Makumbusho ya Taifa alitembelea Butiama hivi karibuni akifanya utafiti juu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Bi Victoria ni msimamizi wa nyumba aliyoishi Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni, Dar es salaa, Mtaa wa Ifunda.
Bi Victoria akiwa ndani ya maktaba yenye mkusanyiko wa vitabu zaidi ya 8,000 vya Mwalimu Nyerere kwenye nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Mwitongo, Butiama.
Utafiti wake ulijikita juu ya maisha ya Mwalimu na familia yake wakati wanaishi kwenye nyumba hiyo ya Magomeni kabla ya uhuru, mwaka 1961.

Saturday, September 8, 2012

Wachawi wa siku hizi

Hii taarifa ni tasfiri ya makala ya lugha ya Kiingereza niliyoiandika mwaka 2005 kwenye gazeti la Sunday News.

Amini au usiamini kuhusu uchawi lakini ukweli unabaki kuwa uchawi ni suala lisiloepukika kwenye jamii za Kiafrika. Butiama nayo haiwezi kukwepa ukweli huu.

Mwezi Mei mtuhumiwa wa uchawi ambaye nitamuita Pepe alitimuliwa Butiama na wanakijiji waliyomtuhumu kufuga na kufanya biashara ya mazuu. Inaaminikia mazuu ni binadamu ambao huzikwa wakiaminika wamekufa lakni hufufuliwa kwa njia za kichawi na hufanyishwa kazi kwenye mashamba na pia kutoa huduma kadhaa za weledi.

Mfanyakazi wa hospitali ambaye mfanyakazi mwenzake aliyekuwa daktari alifariki hivi karibuni amesema kuwa yule mfanyakazi mwenzake, ambaye wote tunajua kuwa ni marehemu, sasa hivi anaendesha hospitali kwenye ulimwengu wa siri wa mazuu. Hospitali hiyo ina upungufu wa wafanyakazi na "mchawi" aliyetimuliwa ndiyo anasadikiwa kupeleka watu wa kuziba nafasi zilizo wazi.

Pepe alijijengea desturi ya kufanya shughuli za kawaida katika mida ambayo siyo ya kawaida. Wanakijiji wenzake wakijiandaa kulala yeye ndiyo kwanza aliwaelekeza mafundi kuendelea na ujenzi wa nyumba yake katika mida ambayo pia inajulikana ndiyo mida wale ambapo wale wanaominika kuwa wasaidizi mahiri wa wachawi, yaani fisi na bundi, wanakuwa na pirika pirika nyingi na mizunguko ya huku na kule.

Jambo moja la kushangaza ni kuwa fundi mmojawapo ambaye alishiriki kwa kipindi kifupi nyakati za usiku kujenga nyumba ya Pepe alikiri kuwa hajaona muda mzuri wa kujenga nyumba kuliko usiku kwa sababu usiku hakuna wale wapiga porojo wa mchana ambao hupunguza kasi ya kazi. Huyo fundi aliacha ujenzi wa nyumba ya Pepe baada ya kupata onyo kali kutoka kwa wazee wa kimila, wanyikura.

Baada ya hapo wanyikura walituma wito kwa Pepe kumtaka aeleze sababu ya kujenga nyumba usiku. Alielekezwa kuendeleza ujenzi wake mchana kama wengine na akafuata kwa muda lakini baadaye akarudia tena ujenzi wa usiku. Alipata wito mwingine kuonana na wanyikura lakini safari hii badala ya kuitika wito, siyo tu hakuhudhuria kikao kilichoitishwa kwa ajili yake, lakini akatuma onyo kwa wazee kuwa wakiendelea kumfuata fuata atawafungulia mashitaka mahakamani na wangeweza kujikuta jela. Kama hii ni kweli basi alikuwa amefanya kosa kubwa sana. Wazee wa jadi ni taasisi muhimu sana ya kimila. Ni dhahiri kuwatishia huku kuliibua tafrani kubwa zaidi.

Wanyikura ni kama serikali. Pepe alikuwa anachochea moto. Kwa kulipiza kisasi wanyikura wakaanza kuweka vikwazo. Hakuna aliyeruhusiwa kuongea naye. Yoyote ambaye angekiuka hiyo amri angeweza kutozwa faini, aghalabu ng'ombe mzima, kutegemea na mazingira ya ukiukwaji uliyofanyika. Athari za ukiukwaji wa aina hii kwenye mazingira ya mjini yanaweza kuwa ni madogo sana, lakini kwenye kijiji, ambapo ushrikiano na wengine ni muhimu sana katika kila nyanja, vikwazo vinaweza kuwa na athari kubwa sana. Nilipata taarifa kuwa mmiliki mmoja wa duka alipewa onyo kali na wazee wa kimila baada ya kumuuzia Pepe vocha za simu.

"Angekubali tu amri ya wazee, akakubali kulipa faini, na kuendela kujenga mchana, angekuwa bado yupo," alisema fundi. Kusingezuka kisingizio cha kumfukuza. Aliwadharau wazee akawapa mwanya wale waliyokuwa wanamshuku kwa uchawi kufanya njama za kumtimua kijijini.

Ukichukulia kuwa mtu yoyote anayeaminiwa kuwa ni mchawi anachukuliwa kuwa hawezi kuwa na woga wa aina yoyote na kuwa ni mkatili mmmoja ambaye hurandaranda usiku akitafuta binadamu wa kuwadhuru akitumia fisi kama usafiri wake, mimi nilifikia uamuzi kuwa Pepe hakufanana asilani na taswira hii. Jioni moja, nilikuwa naendesha gari nikitokea Musoma na nilisimamishwa na kundi la watu waliyokuwa wamesimama pembeni ya gari nyingine ndogo. Miongoni mwao alikuwa Pepe. Alinijulisha kuwa walikuwa wakielekea Musoma lakini baada ya kukuta mawe makubwa yameegeshwa katikati ya barabara niliyopita mimi muda ule ule kabla ya kuwafikia, waligeuza gari haraka wakihofu kushambuliwa na majambazi wenye silaha.

Niliwaambia sikuona mawe yoyote barabarani na kuongeza kuwa yawezekana kuwa baada ya wao kugeuza gari na "majambazi" nao wakatawanyika wakihofia nia yao mbaya imegundulika.

Kutokana na maelezo yangu baadhi ya abiria wa ile gari walifarijika na wakaanza jitihada za kumshawishi dereva apite palepale na kuendelea na safari kwenda Musoma. Mtu pekee aliyeamua kuwa kuendelea na safari ya Musoma ni hatari alikuwa mtuhumiwa wa uchawi, Pepe. Aliniomba lifti tukarudi naye Butiama.

Tuesday, September 4, 2012

Katiba mpya itamke lugha rasmi ya bunge kuwa Kiswahili

Kama kuna kundi liliojijengea utaalamu wa kuvuruga lugha ya Kiswahili, kundi hilo ni la viongozi wa kada mbalimbali hapa Tanzania. Na vinara zaidi wa kuivuruga lugha ya Taifa ni wabunge wetu.

Ukisikiliza mjadala wa Bunge la Muungano ni vigumu kupita dakika kumi bila anayeongea kutumia neno la Kiingereza ndani ya mjadala unaoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya watu wameipachika jina tabia hii ya kuchanganya lugha za Kiingereza na Kiswahili kuwa ni kuongea kiswanglish, neno lisilo rasmi kwenye lugha zote mbili.

Kuna dhana potofu miongoni mwa viongozi wetu wa sasa kuwa unapochanganya mazungumzo kwa kutumia maneno ya Kiingereza kwenye mazungumzo yako, basi wewe unaonekana kuwa ni mtu msomi. Na utakuta viongozi hawa hawa hata kwenye maandishi yao wanaweza kutumia neno la Kiswahili halafu kwenye mabano wanatoa fasili ya neno hilo hilo kwa lugha ya Kiingereza, kama vile kuwakumbusha wale wanaosoma maelezo yao kuwa wasisahau kuwa wao ni wasomi.

Jambo moja dhahiri ni kuwa ni Watanzania wachache sana wanaoelewa hayo maneno ambayo viongozi wetu, katika jitihada za kukogana wao kwa wao, wanayoyatumia kwenye maandishi na matamshi ikiwa ni pamoja na kwenye mijadala, mikutano, na kwenye vyombo vya habari.

Naamini umewadia wakati kwa lugha ya Kiswahili kutamkwa kuwa ndiyo lugha rasmi ya kutumika ndani ya Bunge la Muungano. Haileti mantiki kwa mwananchi aliyepiga kura kumchagua mbunge asielewe anachojadili mbunge wake.

Sunday, September 2, 2012

Dk. Kenneth Kaunda, rais mstaafu wa Zambia

Mwezi Juni 2007 nilialikwa jijini London, Uingereza, kwenye uzinduzi mpya wa Azimio la Arusha na nikafikia kwa wenyeji wangu, Selma James na Nina Lopez, wote ambao hawali nyama. Nikiwa natokea kwenye kabila ambalo ukizungumzia "chakula" ni sawa sawa na kutamka "nyama" na ambapo mboga za majani zinaliwa na mifugo peke yake, zile siku kumi nilizokaa London nikila mboga za majani zilikuwa ni mtihani mkubwa kwangu.

Nilimudu kwa jitihada kubwa kuishi hizo siku kumi bila kula nyama na niliporudi Tanzania watu walioniona walisema kuwa nilionekana kijana kuliko ninavyostahili. Nilihisi kuwa yawezekana kuwa kulishwa mboga za majani kwa siku kumi bila hiari yangu nikiwa London ndiyo kulisababisha mimi kuonekana kijana.

Imani yangu kuwa ulaji wa mboga za majani kwa siku kumi ndiko kulisababisha kupunguza kuzeeka kwangu ilinisukuma kuacha kula nyama na nikaanza jitihada ya kuwa mlaji mboga za majani tu na kuacha kula aina zote za nyama.

Mwaka mmoja baada ya hapo, nikiwa kwenye mkutano jijini Maputo, Msumbiji, nilipata fursa ya kuonana na  Dk. Kenneth Kaunda, rais mstaafu wa Zambia ambaye ni maarufu pia kuwa mtu ambaye hali nyama.
Rais mstaafu wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, kulia.
Aliniambia aliacha kula nyama mwaka 1952 kupinga sera za kibaguzi za serikali ya kikoloni ya Waingereza iloyoelekeza wamiliki wa bucha kuweka madirisha mawili tofauti ya kuwauzia nyama Waafrika na wazungu. Yeye hanywi pombe, kahawa, wala chai lakini anakunywa maji ya matunda kila siku.

Kitendo hicho cha upinzani wa kisiasa kinaelekea kufanikisha kupunguza idadi kubwa ya miaka ya huyu rais mstaafu mwenye umri wa miaka 88. Ni mwingi wa nguvu na mchangamfu sana. Kwenye mkutano Maputo kila alipoitwa kwenye jukwaa alienda kwa mchakamchaka.

Mtanziko mkubwa unaonikabili, mkubwa zaidi kuliko uamuzi wa kuacha kula nyama, ni kipi kitakachofuata kuacha kula kati ya samaki na kuku.