Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, January 6, 2011

Amani Millanga bado anahoji Sera ya Majimbo ya CHADEMA (sehemu ya pili na ya mwisho)

Sehema ya kwanza ya makala ya Amani Millanga juu ya sera ya majimbo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) niliitoa hapa kwenye wavuti hii tarehe 31 Oktoba 2010. Niliahidi kutoa sehemu ya pili na ya mwisho, kesho yake, yaani tarehe 1 Novemba 2010. Naomba radhi kuwa sikuweza kutimiza ahadi hiyo mpaka leo hii.
 -----------------------------------------------------------
Sera za Majimbo: Utaifa na Hatima ya Amani Yetu (sehemy ya pili na ya mwisho)
Na Amani Millanga


Viongozi wawajibikaji
Suala la kiongozi kuwajibika kwa watu msingi wake mkuu ni demokrasia, utawala wa sheria unaoheshimu na kuzingatia haki, na uadilifu. Ukiwa na mfumo wa sheria unaofanya kazi vizuri na watu wenye uelewa wa haki zao, viongozi watawajibika. Ni hoja nzuri meya kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi lakini hii haimaanishi kuwa atawajibika kwao. Mifano tunayo kila pembe ya dunia ya viongozi kuchaguliwa na watu lakini wasiwajibike kwa waliowachagua. Wapo wakuu wa nchi na serikali ambao hawachaguliwi na wananchi moja kwa moja hasa katika mfumo wa serikali za mabunge kama Uingereza, India, Australia, n.k. Hata rais wa Marekani hachaguliwi moja kwa moja na wananchi. Lakini viongozi wa nchi hizi wanawajibika kwa wananchi wao kama ambavyo meya anavyowajibika kwenye halmashauri yake. Suala la kuhumiza hapa ni uongozi bora unaoheshimu haki, utu, na sheria. Hiyo ndiyo dawa mujarabu na si serikali za majimbo. Serikali ya CCM inaongoza kwa mujibu wa sheria na viongozi wake wanawajibika kwa umma wa Watanzania.

Tanzania inaongozwa na misingi ya demokrasia hivyo basi waliopewa dhamana ya kuongoza wanayo haki ya kutoa maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya taifa na kufuata matakwa ya wananchi. Pamoja na kuwa demokrasia yetu bado ni changa lakini upo ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika masuala yote yanayohusu nchi yetu katika kila ngazi ya uongozi kuanzia mtaa hadi taifa. Tuna mfumo mzuri wa uwakilishi; kubwa ni kuuboresha zaidi na kazi hiyo inafanywa na serikali ya CCM. Kusema kwamba "CCM haifanyi chochote" si kuitendea haki. Yapo mambo mengi mazuri ambayo CCM imeyafanya. Hii ni mada tofauti, inataka wakati wake muafaka kuijadili.

Majimbo si dawa ya rushwa
Mwandishi amegusia suala la rushwa na ufisadi na kwamba serikali za majimbo ndiyo suluhisho. Nigeria ina utitiri wa majimbo lakini inaongoza kwa rushwa. India na Afrika Kusini pia zinanuka rushwa. Hata Marekani kuna rushwa na ufisadi (fuatilia gavana wa Illinois alivyotaka kukiuza kiufisadi kiti cha useneta alichokiacha [Barack] Obama). Hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa serikali za majimbo ni dawa mujarabu ya rushwa na ufisadi. Hii ni dhana isiyokuwa na uzito wowote. Rushwa na ufisadi dawa yake uongozi bora, utawala wa sheria, maadili na miiko ya uongozi si serikali za majimbo.

Tanzania haijagawanywa kimakabila
Mwandishi anasema wilaya za Tanzania zimegawanywa kikabila. Si kweli kwamba wilaya zimegawanywa kwa misingi ya makabila. Kwa hili ni kumkosea heshima Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyefanya kila jitihada za kuondoa ukabila katika nchi yetu kwani wilaya nyingi zilianzishwa wakati wa uongozi wake. Wilaya ya Muleba iliyoanzishwa mwaka 1975 kwa mfano ina Wahaya wengi, lakini katika maeneo ya Kimwani kuna Wakara, Wakerewe, Wasukuma, Wazinza, na Wasubi. Ikitokea mfano Wilaya ya Bukoba ikawa na Wahaya peke yake hilo ni suala la kabila hilo kuwa sehemu hiyo na si kugawanywa kimakabila. Sengerema na Geita zina Wasukuma, Wasumbwa, na Wazinza, n.k. Mkoa wa Mara una makabila mengi sana kuliko mkoa wowote Tanzania na si Wakurya na Wajaluo tu. Kuna Wajita, Wasukuma, Wasimbiti, Waikizu, n.k. Lengo kuu la kuundwa kwa wilaya na mikoa mipya ni kurahisisha kufikisha huduma kwa wananchi. Hizi tafsiri nyingine kwamba wilaya na mikoa inaundwa kwa misingi ya kikabila ni tofauti na malengo ya serikali. Kwa kweli tafsiri kama hizi haziwezi kuijenga Tanzania.

Hivi kwa nini mnataka tuigawe Tanzania kwa mafungu ya makabila katika majimbo? Mtaweka wapi mpaka kwamba hapa ndipo mwisho wa Wasukuma na huu ni mwanzo wa Wanyamwezi? Kwamba hapa ni mwisho wa Waha na huu ni mwanzo wa Wahangaza? Mkianza kufanya hivi mtapanda mbegu ya "sisi na wao" kama alivyowahi kuonya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Na mkifika hatua hii ya "sisi na wao" hilo jimbo litakuwa limegawanyika katika "sisi ni Waziba, wao ni Wanyaihangiro, Wahamba, Wayoza, au Wanyambo, n.k." Kumbe mnakuwa hamna jimbo tena. Mkiwa hamna jimbo ina maana hamna utaifa. Hamna UTANZANIA. Matokeo yake ni nini? Tanzania inakuwa kama Nigeria au hata Somalia. Msipande mbegu chafu ya kutugawa kwani madhara yake ni makubwa sana kwetu. Hakika sera ya majimbo ni nguvu ya kuangamiza umma na utaifa!

Ajira na raslimali za kimajimbo: utengano si ushindani
Katika suala la ajira mwandishi anamaanisha kuwa Muhaya hatatoka kwenda kufanya kazi Mbeya au Mtwara. Maana yake nyingine ni kuwa jimbo fulani likiwa ni tajiri basi yale majimbo maskini yasiyo na vivutio vya ajira yataendelea kuwa nyuma daima kwani hata wale wachache wazuri walionao watachukuliwa na majimbo mengine tajiri. Huku ni kuiua Tanzania tukiwa tunaona. Hivi ni sababu gani ya msingi ya kutufanya tujigawe hivi? Mwandishi pia anaamini katika kanuni mwitu ambayo msingi wake mkuu ni mwenye nguvu, makucha na meno makali huwatafuna wadogo. Kwa mantiki hiyo sehemu zile ambazo ziko nyuma kimaendeleo zitamezwa na zile ambazo ziko mbele kimaendeleo katika mfumo wa serikali za majimbo. Hii ni dhuluma kwa umma!

Hakuna ushahidi wa kitakwimu katika nchi zenye majimbo kuwa uwepo wa serikali za majimbo umeongeza ushindani maradufu katika ajira au biashara. Ushindani ndani ya nchi haujengwi kwa majimbo. Ushindani unajengwa kwa kuweka mfumo mzuri wa elimu, ajira, biashara, na miundombinu. Ushindani hauletwi na jimbo kwa jimbo kushindana. Na kushindana katika lipi hasa ili hali vyanzo vya uchumi na ajira vinatofautiana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu? Sioni hoja za msingi katika dhana ya ushindani kati ya majimbo kama msingi wa kuweka utamaduni wa ushindani nchini. Hivyo dhana ya ushindani kwa mnasaba wa majimbo si sahihi.

Pamoja na kwamba Tanzania ina raslimali kila mahali si busara hata kidogo kusema kwamba raslimali za mkoa au jimbo kwa mtizamo wako zitumike kwa jimbo hilo peke yake. Nchi ni yetu sote. Haki aliyonayo Msukuma wa Geita kwa dhahabu iliyoko pale ni sawa na aliyonayo Mmakonde kwa dhahabu hiyo. Kwa hiyo tuongelee ajira na rasilimali za taifa na si majimbo. Kunufaika zaidi kwa Dar es Salaam au miji mikubwa na rasilimali za taifa ni suala la kujadiliwa na kufanyiwa kazi ili mapato ya taifa yafike kila pembe ya nchi lakini si kigezo cha kuhalalisha umajimbo. Pia sheria kama hiyo ya kukataza kuvuta sigara haihitaji mpaka uwe na serikali za majimbo. Hili ni suala la serikali kuu kupitia bunge kupitisha sheria ya kupiga marufuku kuvuta sigara katika maeneo mbalmbali yatakayotajwa katika sheria hiyo.

Hitimisho
Ndugu yangu, suluhisho la matatizo yetu liko katika kuwa na uongozi bora, utawala wa sheria unaoheshimu haki za binadamu, demokrasia ya kweli, na elimu bora kwa wote. Suluhisho haliko katika serikali za majimbo.

Umesema Tanzania ya sasa imeanza kuonyesha matabaka kati ya mtu na mtu. Je, mkiongeza tabaka la majimbo si ndiyo mtatumaliza kabisaaaa? Tabaka la jimbo na jimbo ambalo linaambatana na tabaka la umkoa, ukabila, nu udini, n.k. Hivi kweli hii ndiyo nguvu ya umma au nguvu ya kutugawanya? Hatuyahitaji mabadiliko ya kisera yasiyotoa kipaumbele kwa umoja, amani, na utaifa wetu. Mabadiliko haya yatatuvuruga badala ya kutujenga. Kwanini tufike hatua ya kutumia jeshi ili hali tunaweza kuimarisha umoja wetu zaidi kupitia mfumo tulionao sasa wa serikali za mitaa badala ya kujikaribishia matatizo kwa sera za maangamizi za majimbo?

Nakukumbusha kuwa hoja za Mwalimu bado ni hai na zenye manufaa kwa utaifa wetu na maendeleo yetu. Kubwa ni kuzitekeleza kwa umakini na uadilifu. Mafanikio makubwa ya Mwalimu [Nyerere] yako katika kuujenga utaifa wetu, kuulinda umoja wetu, maendeleo ya watu na kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani. Haya yote yalifanikiwa kwa sababu ya Tanzania kuwa taifa lisiloendeshwa kwa misingi ya ukabila, udini, na umkoa, au umajimbo. Mnataka kuturudisha kwenye nchi bila utaifa. Naamini Watanzania wanajua athari za siasa za majimbo na hawazitaki. Huu ndio ukweli unaotamalaki.

Kongamano la katiba mpya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
Academic Staff Assembly

JUMUIYA YA WANATAALUMA CHUO KIKUU CHA
DAR ES SALAAM (UDASA)

inawaletea:

KONGAMANO LA KATIBA

MADA KUU: MCHAKATO NA MAUDHUI YA KATIBA MPYA
WAZUNGUMZAJI WAKUU:

1. PROFESA ISSA SHIVJI
2. NDG JENERALI ULIMWENGU

TAREHE: 

JUMAMOSI, 15 JANUARI 2011
UKUMBI: NKRUMAH, CHUO KIKUU CHA DSM
MUDA:
SAA 4:00 ASUBUHI HADI SAA 8:00 MCHANA
WOTE MNAKARIBISHWA

Sunday, January 2, 2011

Sherehe za Mwaka Mpya Butiama

Wakazi wa kijiji cha Butiama walikarubisha Mwaka Mpya, 2011, kwa sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika kwenye bwalo la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), eneo la Mwitongo. Picha hizi zinaonyesha mambo yalivyokuwa:
Nashon Jirabi, kulia, akisubiri Mwaka Mpya, muda mchache kabla ya Mwaka Mpya kuanza

Kutoka kushoto - kulia: Nashon Jirabi, Charles John, na Frank Peter

Mduara pia ulichezwa

Mpiga picha mashuhuri wa Butiama, Masumbuko Joseph, akipumzika baada ya kupiga picha nyingi kwenye sherehe

Pongezi za Mwaka Mpya kwa wageni wa meza kuu