Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, October 31, 2012

Mada yangu ya leo: Jinsi elimu duni inavyohatarisha amani

Nimewahi kuuliza waandishi wa habari wawili, mmoja toka Kenya na mwingine Mtanzania, swali moja: raia wanaamini yuko kiongozi ambaye si mwizi? Mkenya alisema Wakenya wote wanaamini kuwa viongozi wao siyo waaminifu. Mtanzania naye alisema Watanzania wengi zaidi nao wanaamini kuwa viongozi wetu siyo waaminifu.

Madhumuni ya msingi ya kutoa elimu ni kumwezesha mwanafunzi kusoma, kuhesabu, na kuandika. Madhumuni mengine ya muhimu ni kumwezesha mwanafunzi kuwa mdadisi, mchambuzi, mwenye uwezo wa kufikiri, na hata mwenye uwezo ya kupinga kwa hoja yale ambayo anafundishwa. Pengine hili la pili lingeweza kuwa muhimu kuliko lile la kwanza kama isingekuwa haiwezekani kupata uwezo huu wa pili bila kuwa na uwezo wa kusoma, kuhesabu, na kuandika.

Hali duni ya elimu iliyopo sasa inatoa nafasi ndogo sana kwa wanafunzi kuvuka ngazi ya kwanza na kuingia ngazi ya pili. Tunao wanafunzi wa sekondari wasiokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Tunao wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana uwezo wa kuridhisha kulinganisha na wenzao waliosoma miaka ya sitini na ya sabini.
Maisha ya baadaye ya hawa watoto yatakosa amani iwapo mfumo wa elimu hautaboreshwa.
Leo hii wanaopta elimu nzuri ni asilimia ndogo sana ya mamilioni ya Watanzania ambao wanapata elimu hafifu. Kwa sababu hii kila mwaka ongeko la Watanzania wenye uwezo wa kuchambua, kutafakari, kudadisi, na kupinga kwa hoja masuala mbabali mbali wanazidi kupunguka na tena kwa kasi kubwa.

Siasa ya vyama vingi imefanikiwa kifuchua maovu mengi ya siasa za chama kimoja, lakini pia vyama vingi vimejenga pia imani kwa mwananchi wa kawaida kuwa kila mtu ni mwizi. Juzi juzi nimetoka kupanda Mlima Kilimanjaro na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto na nilimsikia mmoja wao akisema kuwa "kila mtu ni mwizi."

Hatuwezi kuacha kulaumu mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ambayo inawafanya raia waamini kuwa viongozi wa umma waaminifu hawapo tena.

Elimu hafifu inapunguza uwezo wa raia wa kuchambua masuala mbali mbali, lakini siasa ya vyama vingi imefanya kazi nzuri ya kumfanya raia ashuku kila kitu na kila mtu. Kwa taratibu za kisheria za mfumo wa sheria unaojulikana kama civil law ni wajibu wa yule anayetuhumiwa kuthibitisha kuwa siyo mwizi, au hafanyi janja janja ya aina fulani anapokuwa kiongozi au mtumishi wa umma.

Hatari ya hali hii ni kuwa hata pale jambo linapokuwa halina mizengwe ni vigumu kwa raia kuamini hivyo. Raia wanapokuwa hawana tena imani na viongozi na mfumo wa utawala, misingi ya amani itaanza kupata nyufa. Na matukio ya miaka ya hivi karibuni yanaashiria kuwa miaka ijayo haitakuwa na amani ambayo Watanzania wamekuwa nayo kwa muda mrefu.

Sunday, October 28, 2012

Kwaya ya Mt. Cecilia ya mjini Singida yatembelea Butiama

Leo jioni wanakwaya wa Kwaya ya Mt. Cecilia ya Kanisa Katoliki mjini Singida wametembelea Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


Wanakwaya hao ambao wako kwenye ziara ya Mkoa wa Mara walipita Butiama wakitokea Musoma na wakiwa njiani kwenda Isenye.

Friday, October 26, 2012

Wazanaki na vitungo

Mzee wa Kizanaki anapokaribia nyumbani kwake baada ya giza kuingia huanza kuimba kwa sauti ya juu wimbo unaojulikana kama kibanziko. Kwa desturi ni wimbo unaoimbwa na mzee ambaye amekunywa pombe kidogo, na madhumuni ya wimbo huu ni kuwafahamisha watu wote watakaomsikia kuwa mzee mwenye nyumba anarudi nyumbani. Mwanaume yoyote ambaye anaweza kuwa nyumbani kwa huyu mzee na ambaye hawezi kutoa maelezo ya kuridhisha kwanini yuko pale atafahamu kuwa ni wakati wa kuondoka haraka. Kila mzee wa Kizanaki ana kibanziko chake.

Mzee wa Kizanaki na heshima zake hawezi kumvizia mkewe kwa madhumuni ya kumfumania. Ni tabia ambayo haikubaliki.

Mzee Ginga Kihanga, mwenye umri wa miaka 93 alinisimulia kuwa wazee hupendelea kuwatisha waviziaji badala ya kujiingiza kwenye makabiliano ambayo yanaweza kusababisha majeraha makubwa au hata kifo.
Hata hivyo haina maana kuwa zama zile watu hawakufumaniwa. Enzi za ukoloni wale walioshikwa kwenye fumanizi walidhalilishwa hadharani kwa kuvuliwa nguo, kuchapwa bakora, na kutozwa faini ya ng'ombe wawili. Tofauti ilikuwa mtemi anapokuwa ndiyo mlalamikaji; yeye aliruhusiwa kupanga faini aliyoona inastahili.

Kibanziko kina madhumuni mengine ya ziada. Mzee Ginga alisema, kwa kawaida, tendo lile haramu lilifanyika kwenye vichaka, mbali na nyumba ya wenye ndoa. Ilikuwa ni fedheha kubwa kwa mwanaume Mzanaki anapofumania nyumbani kwake. Kwa hiyo, kwa namna nyingine, uimbaji wa kibanziko ilikuwa ni njia ya kuzuwia hiyo aibu na kumsababisha huyo 'mwizi' aondoke na kuepusha aibu ndani ya jamii.
Yawezekana kuwa desturi hii ya kuwapa upenyo hawa 'wezi' inatokana na tamaduni ile ya kupanga ndoa. Mzee huyo huyo ambaye jana aliimba kibanziko alipokaribia nyumbani kwake yawezekana alikuwa amepitia kwenye kilabu cha pombe na kufanya makubaliano na mzee mwenzake kuwaoza watoto wao.
Aliporudi nyumbani alimwambia mwanae wa kiume kuwa umewadia wakati wa kufunga ndoa na kuwa ameshamtafutia mchumba anayefaa ambaye anatoka kwenye familia ya wachapakazi hodari ambao hawana historia ya magonjwa ya kurithi, na kuwa siyo wachawi.
Lakini kabla ya kupangiwa hizi ndoa na wazee yawezekana kuwa hao wanandoa watarajiwa walikuwa tayari wana mahusiano na watu tofauti. Na yawezekana kwa kutambua uwezekano huo kuwa mtu anapolazimishwa ndoa ambayo hakuitaka anaweza akawa na mahusiano mengine ya pembeni, basi jamii ya Kizanaki ikaja na kibanziko kama njia ya kuruhusu yale ambayo yalifungwa na ndoa za kupangawa na wazee.
Kuna msemo wa Kizanaki unaoashiria kukubali hali hii unaosema, wiguru na wiyasi, ukimaanisha kuna yule wa juu na yule wa chini; kuna mume, na kuna mviziaji - kune mume (au mke), na kuna kitungo.

Kwa kawaida kitungo ndiyo alikuwa mchumba ambaye angeolewa iwapo kijana angeruhusiwa kuchagua, lakini hakuweza kumuoa huyo kwa sababu ya ndoa ya kupangwa na baba mzazi. Na kwa sababu ndoa aliyopanga mzazi haikuwa na majadiliano kilichotokea ni kuwaunganisha watu wawili ambao walikuwa hawana upendo baina yao.

Matokeo yake ni kuwa walikuwa na mahusiano kama maadui badala ya wanandoa. Mwanaume alimuamrisha mwanamke ndani ya nyumba na mwanamke, kwa hulka, alikuwa mkaidi. Ahueni ilitafutwa kwa kitungo.

Na lugha ya kitungo ilikuwa tamu, ya kubembeleza. Walitumia majina ya wapendanao kama 'Nyababiri', Nyabasasaba' au 'Nyabanane' majina yenye kumaanisha 'wa pili', 'wa saba', 'wa nane' na majina ambayo siyo rahisi kutumika baina ya wanandoa.
  
Kama ilivyo kwa mila na desturi nyingi, kibanziko nacho kinapotea na nyakati. Leo hii vijana wanarudi majumbani mwao bila taarifa. Yawezekana pia kuwa hawana uwezo wa kuimba kama wazee wa Kizanaki.

Thursday, October 25, 2012

Msanii Kingkapita ametoa nyimbo mpya

Msanii wa Hip Hop, Kingkapita, ametoa kibao kipya chenye jina: Shikamoo pesa.



Taarifa aliyoisambaza mwenyewe inaeleza:
"Nilimshirikisha Tash, mzee wa chapia mulemule kutoka Arachuga. Nyimbo imerekodiwa katika studio za Rocanna Basemennt chini ya producer Jimmy Jizze na master kumaliziwa Home Town Record chini ya master Traveller."

Sikiliza kibao hicho hapa: http://www.hulkshare.com/7u4tpclsbwu8

Tuesday, October 23, 2012

Huduma ya bure kufasiri Kiswahili kwa Kiingereza*

*Vigezo na viwango kuzingatiwa: kutokana na kuwa na majukumu mengine naweza kupokea kazi kidogo tu kwa siku.

Nimechunguza kiwango cha watu wengi kumudu uandishi wa lugha ya Kiingereza - na hata lugha yetu ya Kiswahili - na, kwa maoni yangu, picha inayojitokeza ni kuwa kiwango hakiridhishi. Hapa nazungumzia Watanzania wa kada mbali mbali, kuanzia wasomi na wale ambao hawakupata fursa ya kupata elimu ya juu.

Kwa bahati mbaya imejengeka tabia inayohusisha uongo kuwa mtu anayeongea au kuandika kwa lugha ya Kiingereza ndiyo anadhihirisha kuwa ana elimu nzuri. Kwa sababu hii, watu wengi ambao wangeweza kufanya mawasiliano kwa lugha ya Kiswahili hung'ang'ana kuongea au kuandika kwa Kiingereza pasipo kuwepo uwezo mzuri wa kufanya hivyo. Kama ambavyo kutofahamu Kichina haihusiani na kutokuwa na elimu, vivyo hivyo kutofahamu Kiingereza hakuashirii kutokuwa na elimu.

Hata hivyo kuna ukweli kuwa yapo mazingira yanayolazimu mtu kuandika au kuwasilisha mada kwa lugha ya Kiingereza. Hapa naamini naweza kusaidia kutokana na uwezo wangu wa zaidi ya miaka 20 wa uandishi kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili na uandishi kwa ujumla.

Najitolea kufasiri maandishi kutoka lugha ya Kiswahili kwenda kwenye lugha ya Kiingereza iwapo maandishi hayo hayatazidi kurasa moja ya ukubwa wa A-4. Lakini nikiri kuwa nikiona dalili kuwa kazi ni kubwa nitatoza ada kuanzia kurasa ya pili na kuendelea.

Mimi si mtaalamu wa lugha kwa hiyo siwezi kutoa tafsiri rasmi, ila nina uzoefu wa kutosha wa uandishi katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kiasi cha kuweza kutoa tafsiri zinazokidhi viwango vya kuridhisha vya uandishi.

Nitumie maandishi yako kwa barua pepe na nitakurudishia tafsiri siku inayofuata:

kiswahilikwakiingereza@gmail.com

Monday, October 1, 2012

Mwanafunzi wa kidato cha nne afika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Mwanafunzi Placidia Prudence wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto ya jijini Mwanza ambaye alikuwa kwenye msafara wa kukwea Mlima Kilimanjaro amefanikiwa kufika kilele cha mlima huo tarehe 28 Septemba 2012.

Nami nilikuwa kwenye msafara huo ambao ulishirikisha wanafunzi wengine 15 toka shule hiyo pamoja na walimu watatu. Katika wote tulioshiriki ni yeye peke yake alifanikiwa kufika kileleni ambako alifika akiongozana na muongozaji Entold Mpunga.
Placidia Prudence akiwa kwenye kambi ya Horombo baada ya kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Kushoto, juu, unaonekana Mlima Kilimanjaro.
Mwanafunzi Nusra Alkarim, mwalimu wa michezo Isack Katambi, na mimi tulifanikiwa kufika Gillman's Point, mita 5,685 juu ya usawa wa bahari na kiasi cha mwendo wa kama saa moja na nusu toka kilele cha Uhuru alikofika Placidia. Kilele cha Mlima Kilimanjaro kina urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari.

Msafara huo ulipangwa kwa madhumuni ya kuchangisha pesa za mradi wa kuboresha na kufikisha maji safi na salama kwenye shule ya Loreto.

Placidia ana umri wa miaka 20 na ameniarifu anakusudia kuwa mhandisi.